Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • yb14 kur. 26-35
  • Ripoti ya Mambo ya Kisheria

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ripoti ya Mambo ya Kisheria
  • 2014 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehovah
  • Habari Zinazolingana
  • Ripoti ya Mambo ya Kisheria
    2015 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
  • Matukio Muhimu ya Mwaka Uliopita
    2013 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
  • Ripoti ya Mambo ya Kisheria
    2016 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
  • Matukio Muhimu ya Mwaka Uliopita
    2012 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
Pata Habari Zaidi
2014 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehovah
yb14 kur. 26-35
Picha katika ukurasa wa 27

MATUKIO MUHIMU YA MWAKA ULIOPITA

Ripoti ya Mambo ya Kisheria

Mtume Paulo aliwahimiza hivi Wakristo: “Wakumbukeni wale walio katika vifungo vya gereza kana kwamba ninyi mmefungwa pamoja nao.” (Ebr. 13:3) Tukiwa waabudu wa Yehova, tunaendelea kuwakumbuka ndugu na dada zetu waaminifu na kusali kwa ajili ya “wale wote walio katika cheo cha juu; ili tuendelee kuishi maisha shwari na matulivu pamoja na ujitoaji-kimungu kamili na kuchukua mambo kwa uzito.”​—1 Tim. 2:1, 2, Efe. 6:18.

Vifuatavyo ni baadhi ya visa ambavyo Mashahidi wa Yehova wamekabiliana navyo mwaka uliopita:

Ndugu zetu nchini Urusi wanaendelea “bila kuacha kufundisha na kutangaza habari njema” licha ya jitihada za Kanisa Othodoksi la Urusi na baadhi ya maofisa wa serikali kuzuia kazi yetu. (Mdo. 5:42) Wenye mamlaka nchini Urusi wanatumia vibaya sheria isiyo wazi kuhusu watu wenye msimamo mkali wa kidini ili kuzuia machapisho yetu na kuwanyanyasa ndugu zetu. Sheria hiyo ilitungwa hasa ili kukabiliana na ugaidi. Matokeo ni kwamba Mahakama za Urusi zimesema kwamba machapisho yetu 70 hivi yana maneno yanayochochea watu kuwa na msimamo mkali, na serikali imeyaongeza kwenye orodha ya taifa ya machapisho yaliyopigwa marufuku kwa sababu ya msimamo mkali. Wakidai kwamba machapisho hayo ni hatari, baadhi ya maofisa wa serikali wanavamia Majumba ya Ufalme na nyumba za ndugu zetu ili kutafuta machapisho hayo. Polisi wanawakamata, wanawapiga picha, na kisha kuwachukua alama za vidole Mashahidi wengi kwa sababu ya kushiriki katika utumishi wa shambani. Mara nyingi wao hujaribu kuwatisha ndugu zetu wanapowazuia kwenye kituo cha polisi.

Kuanzia Mei 2013, ndugu na dada 16 jijini Taganrog walishtakiwa kwa kosa la kupanga, kuhudhuria mikutano ya Kikristo, na kushiriki katika kazi ya kuhubiri. Hii ni mara ya kwanza tangu kuanguka kwa Muungano wa Sovieti kwa Mashahidi kushtakiwa kwa sababu ya kushiriki katika mambo yanayohusiana na imani yao. Wenye mamlaka katika maeneo mengine ya Urusi wanajaribu kuzishinikiza mahakama zitangaze machapisho yetu kuwa yenye “msimamo mkali,” na kuwashtaki ndugu zetu kwa kosa la kuchochea chuki ya kidini.

Hali ya ndugu na dada zetu nchini Eritrea haijabadilika. Kufikia Julai 2013, Mashahidi 52 walikuwa gerezani, kutia ndani ndugu nane wenye umri wa miaka 70 hivi na dada sita. Ndugu watatu, Paulos Eyassu, Isaac Mogos, na Negede Teklemariam, wamefungwa gerezani tangu Septemba 24, 1994, kwa sababu ya kukataa kujiunga na jeshi.

Zaidi ya nusu ya waliofungwa wako katika gereza la Meiter, lililoko jangwani kaskazini ya mji mkuu, Asmara. Kuanzia Oktoba 2011 hadi Agosti 2012, wenye mamlaka waliwaadhibu ndugu zetu 25 kwa kuwaweka kwenye jengo la mabati lililokuwa limefukiwa nusu ardhini. Wakati wa majira ya joto, askari wanawatoa nje wafungwa wakati wa mchana ili wasiumizwe na joto. Hata hivyo, hawapati chakula na maji ya kutosha, jambo linalofanya afya yao izorote sana. Inasikitisha kwamba Ndugu Yohannes Haile, mwenye umri wa miaka 68 alikufa Agosti 2012 kwa sababu ya mateso hayo, na Ndugu Misghina Gebretinsae pia alikufa mwaka wa 2011 kwa sababu hiyohiyo.

Wakataa Utumishi Unaounga Mkono Vita kwa Sababu ya Dhamiri

Ona Isaya 2:4 na Yohana 18:36.

ARMENIA

Novemba 27, 2012, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) ilifikia uamuzi unaofaa katika kesi ya Khachatryan and Others v. Armenia (Khachatryan na Wengine Dhidi ya Armenia). Serikali iliwashtaki kinyume cha sheria Mashahidi 17 kwa kuwa walikataa kufanya utumishi wa kiraia uliokuwa ukisimamiwa na jeshi. Serikali ya Armenia imewalipa fidia Mashahidi hao na pia imelipia gharama zote za kesi hiyo kwa tendo hilo lililokiuka sheria.

Licha ya uamuzi huo mzuri uliofikiwa katika kesi ya Khachatryan na uamuzi mkubwa wa kihistoria uliofikiwa mapema katika kesi ya Bayatyan v. Armenia (Bayatyan Dhidi ya Armenia), na pia uamuzi mbalimbali uliotolewa na ECHR, serikali ya Armenia iliendelea kuwafungulia mashtaka na kuwahukumu Mashahidi waliokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Hata hivyo, Juni 8, 2013, serikali ilifanyia marekebisho Sheria Kuhusu Utumishi wa Kiraia, na inaonekana kwamba jeshi halitasimamia utumishi wa kiraia. Mashahidi wote waliokuwa gerezani kwa sababu ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri walikuwa wameachiliwa huru kufikia Novemba 12, 2013, na vijana Mashahidi wanaoomba kufanya utumishi wa kiraia wanakubaliwa kufanya hivyo.

KOREA KUSINI

Kufikia Oktoba 31, 2013, kulikuwa na ndugu 602 gerezani. Tangu mwaka wa 1950, serikali ya Korea Kusini imewahukumu Mashahidi wa Yehova 17,605 jumla ya miaka 34,184 gerezani kwa kuwa walikataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

Kwa muda mrefu, Mashahidi wengi wamefungiwa ndani ya chumba kimoja na wahalifu, kutia ndani wahalifu waliofanya makosa makubwa. Hata hivyo, akina ndugu walimtembelea mkuu wa magereza nchini Korea na kumwomba awaamuru wasimamizi wa magereza wawatenganishe ndugu zetu na wafungwa wengine. Wasimamizi wa magereza waliwatoa mara moja wengi wa ndugu zetu kutoka vyumba vilivyokuwa na wahalifu, hivi kwamba kufikia Aprili 2013, angalau asilimia 75 ya ndugu zetu walikuwa wakikaa wanne au watano katika chumba kimoja cha gereza. Badiliko hilo limekuwa na matokeo gani kwa ndugu zetu?

Ndugu mmoja alisema hivi, “Sasa tuko mbali na mambo yasiyofaa kama vile upotovu wa maadili na matusi.” Mwingine alisema, “Sasa tunaweza kutiana moyo na pia tunaweza kufanya mikutano yote mitano kila juma.”

Wakati huohuo, wanaume 56 walioruhusiwa kuondoka jeshini na kuwa wanajeshi wa akiba, ambao sasa ni Mashahidi wamekuwa wakishtakiwa, wakipigwa faini, na kufungwa kwa sababu ya kukataa mwito wa kwenda kuzoezwa kama wanajeshi wa akiba. Kwa kuwa wanaitwa mara kadhaa kwa mwaka, kwa kipindi cha miaka minane, imekuwa vigumu sana kukabiliana na ukosefu huo wa haki.

SINGAPORE

Licha ya kuomba mara kwa mara kufanya utumishi wa kiraia badala ya kwenda jeshini, ndugu zetu 12 wamefungiwa katika Kambi za Kijeshi, na kila mmoja wao anatumikia kifungo cha miezi 39. Ndugu mwingine anatumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani kwa sababu ya kukataa kutumikia katika kikosi cha wanajeshi wa akiba.

TURKMENISTAN

Ndugu zetu tisa wamefungwa kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, na sasa wanatumikia kifungo cha mwaka mmoja na nusu hadi miaka miwili gerezani na mara nyingi wanapigwa vibaya sana na askari-magereza na wanajeshi. Mashahidi hao wanapoachiliwa huru, serikali huwashtaki tena isivyo haki kwa kosa lilelile na kuwawekea sheria kali gerezani. Mawakili wa Mashahidi kumi ambao wamekataa kujiunga na jeshi wametuma malalamishi yao kwa Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa.

Wakataa Kushiriki Katika Sherehe za Kizalendo kwa Sababu ya Dhamiri

Ona Danieli 3:16-18.

Picha katika ukurasa wa 32

Tanzania: Baada ya kuondolewa mashtaka, Mashahidi hawa walirudi tena shuleni

TANZANIA

Mahakama ya Rufaa jijini Dar es Salaam, ambayo ndiyo mahakama kuu zaidi nchini Tanzania, ilikubaliana kwa kauli moja kwamba uamuzi wa kamati ya shule wa kuwafukuza wanafunzi watano na kuwasimamisha kwa muda wengine 122 kwa sababu ya kukataa kuimba wimbo wa taifa unapingana na sheria. Katika uamuzi uliofikiwa Julai 12, 2013, mahakama ilitambua unyofu wa imani ya Mashahidi hao na kwamba kulingana na katiba, uhuru wao wa dhamiri na uhuru wa kuabudu ulipaswa kulindwa. Azimio la vijana hao la kubaki washikamanifu kwa Mungu lilileta ushindi ambao unalitukuza jina la Yehova na kutusaidia tuabudu kwa uhuru nchini Tanzania.

Uhuru wa Kusema

Ona Matendo 4:19, 20.

KAZAKHSTAN

“Uchunguzi wa wataalamu” uliofanywa na Wizara ya Mambo ya Kidini ya Mkoa uliorodhesha baadhi ya machapisho yetu kuwa miongoni mwa machapisho yenye “msimamo mkali,” ukidai kwamba yanachochea migawanyiko ya kijamii na kidini. Aprili 6, 2013, polisi katika jiji la Karabalyk walivamia kinyume cha sheria mkutano wa kutaniko uliokuwa ukifanywa katika nyumba moja na kuchukua machapisho. Julai 3, 2013, Mahakama ya Uchumi jijini Astana iliunga mkono uamuzi wa kupiga marufuku machapisho yetu kumi, na hivyo kuendelea kudhibiti na kuzuia machapisho yetu yasiingizwe nchini. Zaidi ya yote, mnamo Desemba 2012, maofisa wa serikali walianza kuwakamata na kuwafunga jela ndugu zetu kwa madai ya kwamba walikuwa wakifanya kazi ya umishonari kinyume cha sheria. Machi 28, 2013, Shirika la Masuala ya Dini liliagiza Kituo Kikuu cha Kidini cha Mashahidi wa Yehova nchini Kazakhstan kiwataarifu Mashahidi wa Yehova nchini humo kwamba ni kinyume cha sheria kuhubiri nje ya maeneo yao ya ibada yaliyosajiliwa. Kufikia Julai 2013, serikali ilikuwa imewafungulia mashtaka ndugu na dada 21.

Uhuru wa Kukusanyika Pamoja

Ona Waebrania 10:24, 25.

AZERBAIJAN

Mnamo Januari 2010 Kamati ya Kitaifa ya Kazi na Mashirika ya Kidini ilikataa kusajili upya Shirika la Kidini la Mashahidi wa Yehova kwa sababu ya makosa madogo sana waliyodai yalifanywa katika fomu ya maombi. Licha ya Mashahidi wa Yehova kujitahidi kurekebisha makosa hayo, bado wenye mamlaka wanakataa kuwasajili upya. Julai 31, 2012, ndugu zetu walipeleka kesi hiyo katika mahakama ya Ulaya (ECHR), wakidai kwamba kwa kukataa kutusajili upya kuwa shirika la kidini, serikali ilikuwa imekiuka haki yetu ya uhuru wa kuabudu bila msingi wowote wa kisheria. Wasiposajiliwa upya, ndugu zetu hawatatambuliwa kisheria.

Uhuru na Usalama wa Mtu na Mali

Ona Wafilipi 1:7.

UKRAINIA

Ingawa Mashahidi wa Yehova nchini Ukrainia wanafurahia uhuru wa kuabudu, bado wanapigwa, Majumba yao ya Ufalme yanachomwa, na mengine kuharibiwa. Polisi hawafanyii uchunguzi visa hivyo na kuwakamata wanaohusika. Haishangazi kwamba jambo hilo huwafanya wapinzani wahisi wanaweza kufanya lolote bila kuchukuliwa hatua. Kwa sababu hiyo, matendo ya kihalifu dhidi ya ndugu zetu yameongezeka katika mwaka wa 2012 na 2013. Visa 5 vya kuchomwa au kuharibiwa kwa Majumba ya Ufalme vilivyoripotiwa katika mwaka wa 2010 viliongezeka na kufikia 15 katika mwaka wa 2011, mwaka wa 2012 kulikuwa na visa 50, na katika miezi mitano ya kwanza ya mwaka wa 2013, kulikuwa na visa 23. Ofisi ya tawi imewasilisha malalamishi yake kuhusu ukosefu huo wa haki kwa Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa.

Picha katika ukurasa wa 28

Ukrainia: Ndugu zetu wanajitayarisha kujenga upya Jumba la Ufalme lililochomwa

Uhuru wa Kujifanyia Uamuzi

Ona Matendo 5:29 na Matendo 15:28, 29.

ARGENTINA

Mwaka wa 2012, Pablo Albarracini alipigwa risasi kadhaa na watu waliokuwa wakijaribu kuiba katika eneo fulani. Alikimbizwa hospitalini akiwa amepoteza fahamu. Alikuwa ametia sahihi kadi ya mamlaka ya kudumu ya uwakilishi (DPA) na kukataa matibabu yanayohusisha matumizi ya damu. Ingawa hospitali ilikuwa tayari kuheshimu uamuzi wake, mshiriki wa familia yake ambaye si Shahidi alitafuta agizo la mahakama ili Ndugu Albarracini atiwe damu mishipani, akidai kwamba damu hiyo ingeokoa uhai wake. Hata hivyo, Mahakama Kuu nchini Argentina ilifikia uamuzi uliomuunga mkono Ndugu Albarracini, na kuheshimu haki yake ya kujifanyia uamuzi kuhusiana na mambo ya kitiba ingawa alikuwa amepoteza fahamu. Hakutiwa damu mishipani na alipona kabisa. Anamshukuru sana Yehova kwa kumsaidia kuendelee kudumisha utimilifu wake katika jambo hilo muhimu.

Wabaguliwa kwa Sababu ya Dini

Ona Luka 21:12-17.

KYRGYZSTAN

Aprili 16, 2013, mahakama ilifikia uamuzi uliowaunga mkono ndugu zetu mjini Toktogul, baada ya wakazi wa eneo hilo kuharibu Jumba la Ufalme mara mbili. Mahakama hiyo iliwahukumu wakosaji hao na kuwaamuru walipe fidia. Kesi dhidi ya wale waliohusika hasa katika shambulio la kwanza bado inaendelea, na hilo linatupa tumaini kwamba matatizo katika eneo hilo yatakwisha. Hata hivyo, makutaniko yatajenga upya Jumba hilo la Ufalme.

Picha katika ukurasa wa 38

Kyrgyzstan: Wakazi waliliharibu mara mbili Jumba hili la Ufalme

Ushindi Mkubwa wa Kisheria

  1. Suala: Je, ni lazima kikundi cha kidini kipate kibali cha kufanya makusanyiko na mikutano ya kutaniko?

    Uamuzi: Desemba 5, 2012, Mahakama ya Katiba ya Shirikisho la Urusi ilipitisha uamuzi kuwa Katiba ya Urusi inawapa raia uhuru wa ibada, na iliamua kwamba ndugu zetu wanaweza kufanya mikutano ya kidini bila kutoa taarifa au kupata kibali cha serikali.

  2. Suala: Je, raia wana haki ya kukataa rekodi zao za kitiba kukaguliwa bila idhini yao? Historia fupi: Mnamo 2007 naibu wa mwendesha-mashtaka wa jiji la St. Petersburg, Urusi, aliagiza vituo vyote vya afya jijini humo viwasilishe kwenye ofisi ya mwendesha-mashtaka majina ya Mashahidi wa Yehova wanaokataa kutiwa damu mishipani, bila kumjulisha mgonjwa. Mahakama za Urusi ziliposhindwa kutetea haki ya faragha ya wagonjwa, akina ndugu walipeleka kesi hiyo kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR).

    Uamuzi: Juni 6, 2013, Mahakama hiyo ilitoa uamuzi kwamba agizo la mwendesha-mashtaka lilivunja haki za msingi za kutoingilia mambo ya faragha na kuthibitisha kwamba hakuna “sababu za msingi au za kutosha” za kutoa habari za siri kwa maofisa wa serikali. Hatimaye uamuzi wa mwisho ulifikiwa Oktoba 7, baada ya Baraza Kuu la Mahakama hiyo kukataa rufaa ya Urusi.​—Kesi ya Avilkina and Others v. Russia (Avilkina na Wengine Dhidi ya Urusi).

Habari za Karibuni Kuhusu Ripoti za Kisheria Zilizotolewa Katika Kitabu cha Mwaka Uliopita

Serikali ya Ufaransa imekubali kulipa pesa ilizoamuriwa kulipa na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) Julai 5, 2012 kwa sababu ya kutoza kodi isivyo haki. Serikali hiyo imerudisha pesa ilizochukua pamoja na riba, na pia imelipa gharama zote za kesi hiyo, na kurudisha mali ya ofisi ya tawi iliyokuwa imechukua. Kitabu cha Mwaka​—2013, ukurasa wa 34.

Mashahidi wa Yehova nchini India wanaendelea kukabiliana na upinzani katika sehemu mbalimbali za nchi hiyo. Hata hivyo, hawajazuiliwa au kufunguliwa mashtaka ya uwongo kama ilivyokuwa hapo zamani. Kwa sasa, kesi 20 hivi zimewasilishwa mahakamani ili kushughulikia makosa ambayo ndugu zetu wametendewa.​—Kitabu cha Mwaka​—2013, ukurasa wa 35.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki