Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 8/22 kur. 16-18
  • Kuudhiwa Kingono—Naweza Kujilindaje?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuudhiwa Kingono—Naweza Kujilindaje?
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Njia za Kuepusha Kuudhiwa
  • Ikiwa Unakabiliwa
  • Naweza Kupambanaje na Kusumbuliwa Kingono?
    Amkeni!—2000
  • Kusumbuliwa Kingono—Jinsi Unavyoweza Kujikinga
    Amkeni!—1996
  • Naweza Kujilinda Jinsi Gani Shuleni?
    Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazi, Buku la 2
  • Nifanye Nini Nikisumbuliwa Kingono?
    Vijana Huuliza
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 8/22 kur. 16-18

Vijana Huuliza...

Kuudhiwa Kingono—Naweza Kujilindaje?

ANITA ni mwenye umri wa miaka 16 mchangamfu na mwenye kutabasamu kwa urahisi. Ingawa hivyo, yeye akunja uso anapofafanua matukio ya majuzi kwenye shule yake. “Kijana mmoja mashuhuri alinikabili ukumbini na kuanza kunipapasa kwa njia isiyofaa,” yeye akumbuka. “Wasichana kadhaa hawakupinga vitendo vyake—walishawishika na matendo yake, lakini haikuwa hivyo nami! Kumwomba kwa njia nzuri aache kunipapasa hakukuwa na matokeo. Hakufikiri nilimaanisha hivyo kwelikweli.”

Tatizo la Anita kwa hakika si jambo lisilo la kawaida. Kuudhiwa kingono yaonekana kulikuwa kwa kawaida katika nyakati za Biblia. (Linganisha Ruthu 2:8, 9, 15.) Na kumeenea kwa njia yenye kutisha leo. “Wanaume fulani kazini wametoa maelezo machafu kuhusu mwili wangu,” asema msichana mmoja tineja. Lakini nyakati nyingi kuudhiwa huhusisha zaidi ya maneno tu. “Wengine wamejaribu kunipapasa au kunibaka,” yeye aongeza. Msichana tineja aitwaye René aliambia Amkeni! hivi: “Kuudhiwa kuliendelea kuwa kubaya sana kazini hivi kwamba ilinilazimu kuacha kazi.”

Uchunguzi mmoja wa hivi majuzi uliripoti kwamba asilimia 81 ya wanafunzi katika darasa la nane hadi kidato cha tatu walisema kwamba walikuwa wameudhiwa kingono angalau mara moja. “Kati ya hao,” laripoti U.S.News & World Report, “asilimia 65 ya wasichana na asilimia 42 ya wavulana walisema kwamba walikuwa wamepapaswa, kubakwa au kufinywa kwa njia ya kingono.” Ndiyo, wavulana na vilevile wasichana ni majeruhi. Kama mzazi wa mmoja wa vijana matineja akumbukavyo: “Nimeshtuliwa na jinsi wasichana walivyo washupavu kwenye shule ya mwana wangu. Kutoka wakati alipokuwa na umri wa miaka 12 hivi, tumepata simu zisizokoma, mialiko ya kufanya miadi ya kijinsia, madokezo ya kufanya mambo yasiyofaa—na kadhalika.”

Ni rahisi kuchukulia kivivi hivi tabia yenye kuudhi. Kijana mmoja alitoa maelezo hivi: “Nyakati nyingine hufanywa katika namna ya mzaha.” Lakini si mzaha kwa Wakristo! Wao wanajua kwamba kuudhiwa kingono mara nyingi ni jaribio la kushawishi mtu kuingia katika ukosefu wa adili katika ngono, jambo ambalo Yehova Mungu hushutumu. (1 Wakorintho 6:9, 10) Zaidi ya hilo, Neno la Mungu huamrisha kwamba wanawake vijana watendewe kwa “usafi wote.” (1 Timotheo 5:2) Hilo pia hukataza “mzaha wenye aibu.” (Waefeso 5:3, 4, NW) Kwa hivyo vijana Wakristo hawapaswi kuvumilia kuudhiwa kingono! Swali ni, Je, waweza kujilindaje kutokana na kuwa jeruhi wa kuudhiwa kingono? Acheni tuzungumze kuhusu hatua za kuzuia.

Njia za Kuepusha Kuudhiwa

Sitawisha sifa ya mwenendo wa Kikristo. “Nuru yenu na iangaze mbele ya watu,” akahimiza Yesu. (Mathayo 5:16) Kushiriki yale unayoamini pamoja na wanashule wenzako na wafanyakazi wenzako ni njia moja ya kufanya hili. Unapojulikana kuwa mtu ambaye ana usadikisho na viwango vya juu vya adili, yamkini hautakuwa sana shabaha ya kuudhiwa.

Angalia jinsi unavyovaa na kujipamba. Katika nyakati za Biblia mavazi fulani yalimtambulisha mwanamke kuwa asiye na adili. (Linganisha Mithali 7:10.) Vivyo hivyo leo, huenda mitindo yenye kuchochea kingono ikakufanya uwe mashuhuri kwa marika wako, lakini ingeweza kutoa maoni mabaya. Unaweza kujikuta ukivuta uangalifu usiofaa, wa kingono kutoka kwa mtu wa jinsia tofauti. Tatizo linalofanana na hilo laweza kuzuka ikiwa msichana ajipamba kwa virembeshi katika njia ya kwamba ajifanya kuonekana mwenye umri mkubwa kuliko alivyo kikweli. Shauri la Biblia ni kwamba ‘mjirembe wenyewe katika mavazi yenye mpangilio mzuri, pamoja na kiasi na utimamu wa akili.’—1 Timotheo 2:9, NW.

Chagua washiriki wako kwa uangalifu. (Mithali 13:20) Viwavyo vyote, watu wataamua ulivyo kulingana na washiriki wako. Na ikiwa washiriki wako wanajulikana kutumia wakati mwingi sana wakizungumza kuhusu watu wa jinsia tofauti, watu wanaweza kukuelewa isivyofaa.—Linganisha Mwanzo 34:1, 2.

Epuka kucheza kimahaba. Ni kweli kwamba hakuna ubaya kuwa mwenye urafiki, hata hivyo kutazama na kugusa kwaweza kwa urahisi kueleweka vibaya na mtu wa jinsia tofauti. Si lazima kugusa mtu ili kuendeleza mazungumzo. Jizoeze Kanuni Bora na utendee watu wa jinsia tofauti kama utakavyo kutendewa—kwa usafi na kwa staha. (Mathayo 7:12) Epuka kujaribu kuvuta uangalifu wa mtu wa jinsia tofauti kwa ajili ya raha tu. Kufanya hivyo kwaweza kuwa si ukosefu wa fadhili na tendo la kupotosha tu bali pia jambo hatari. “Je, mtu aweza kutia moto kifuani pake, na nguo zake zisiteketezwe?” yauliza Biblia kwenye Mithali 6:27.

Ikiwa Unakabiliwa

Bila shaka, hata ikiwa mabadiliko katika mavazi yako, kujipamba, au mwenendo yana mpangilio mzuri, wengine hawana haki ya kukugusa kimahaba au kukutolea madokezo ya kufanya yasiyofaa. Na hata vijana fulani ambao wamekuwa wenye kielelezo chema katika sura na mwenendo wameudhiwa. Wapaswa kufanya nini jambo hili likikupata? Haya ni baadhi ya madokezo.

Kataa kwa uthabiti. Inajulikana sana kwamba watu fulani watasema la kwa madokezo ya kingono wakati ambapo kwelikweli wanamaanisha ndiyo. Kwa hivyo huenda washambuliaji wadhanie kwamba kusema la kwa moyo nusu kwamaanisha kikweli ndiyo—au angalau kuna uwezekano—hadi uwasadikishe kwamba sivyo. Shauri la Yesu kwamba la yenu imaanishe la ni lenye kutumika katika jambo hili. (Mathayo 5:37) Usicheke kipumbavu au kujifanya mwenye haya-haya. Wala haupaswi kuruhusu ishara zako za mwili, sauti, au wonyesho wa uso upinge maneno yako.

Tokeza fujo. Washambuliaji wa kingono mara nyingi hutegemea ukosefu wa utayari wa kukinza wa majeruhi wao. Ingawa hivyo, katika nyakati za Biblia, wanawake Waisraeli walipewa haki, kwa kweli wajibu, wa kukinza shambulizi la kingono. (Kumbukumbu la Torati 22:23, 24) Vivyo hivyo leo, Mkristo hapaswi kuhisi kwamba kuguswa isivyofaa au kukumbatiwa si tatizo zito sana. Ni kosa, shambulizi kwa heshima yako ukiwa mtu na ukiwa Mkristo. Hauhitaji kukubali bila kukinza! “Lichukieni lililo ovu” yahimiza Biblia!—Warumi 12:9.

Njia moja yenye matokeo ya kusimamisha huo ukosefu wa tabia ni kutokeza fujo na kumwaibisha mwenye kuudhi; labda ataacha. Kumbuka ono la Anita, aliyetajwa hapo mwanzo. Kumwomba kwa upole mshambulizi wake aache kumpapasa hakukuwa na matokeo. Anita atueleza hivi: “Ilibidi nimwaibishe mbele ya rafiki zake kwa kumwambia kwa sauti kubwa ASINIGUSE katika njia hiyo!” Matokeo yalikuwa nini? “Rafiki zake wote walimchekelea. Alikuwa asiye na huruma kwa muda, lakini siku chache baadaye, aliomba radhi kwa tabia yake na baadaye hata alinitetea wakati mtu mwingine alijaribu kunisumbua.”

Maneno yasipokuwa na matokeo, huenda ikakulazimu kwenda zako tu—au hata kukimbia—kutoka kwenye hilo shambulizi. Na ikiwa kutoroka hakuwezekani, una haki ya kutumia njia yoyote ya lazima ili kuondosha kutendwa vibaya. Msichana mmoja Mkristo alitumia waziwazi maneno haya: “Mvulana alipojaribu kunishika, nilimpiga konde kwa nguvu zangu zote, na kukimbia!” Bila shaka, hili halimaanishi kwamba mwenye kuudhi hatajaribu tena. Kwa hiyo yaelekea utahitaji kupata msaada.

Mwambie mtu fulani. “Hilo ndilo mwishowe nililazimika kufanya,” akiri Adrienne mwenye umri wa miaka 16. “Niliwaomba wazazi wangu shauri juu ya hali wakati mvulana ambaye nilimfikiria kuwa rafiki mzuri alikuwa akiendelea kuniudhi kingono bila kukoma. Kadiri nilivyompinga, ndivyo alivyozidi kuendelea, kama kwamba ulikuwa mchezo.” Wazazi wa Adrienne walikuwa na shauri lenye kutumika ambalo lilimsaidia kukabiliana na hilo tatizo kwa matokeo zaidi.

Wazazi wako pia wanaweza kukusaidia kushughulika na matokeo yoyote ya kihisia-moyo ambayo huenda yakatokea kutokana na kukabiliwa na tatizo la kuudhiwa kingono, kama vile fedheha, hofu, au aibu. Wanaweza kukuhakikishia kwamba hilo shambulizi halikuwa kosa lako. Wanaweza pia kuchukua hatua zitakazokusaidia katika wakati ujao.

Kwa kielelezo, huenda wakaamua kwamba ni jambo lenye faida kumjulisha mwalimu wako au maofisa wa shule kuhusu hilo tatizo. Shule nyingi katika Marekani hufikiria malalamiko kwa uzito na zina sera zilizofafanuliwa wazi za kushughulikia kuudhiwa kingono miongoni mwa wanafunzi.

Ni kweli, si maofisa wote wa shule walio na hisia-mwenzi. “Katika shule yangu,” asema Earlisha mwenye umri wa miaka 14, “nyakati fulani walimu hukosa adabu na hutenda vibaya mno zaidi ya watoto. Haujui ugeukie wapi kwa ajili ya msaada.” Haishangazi basi, kwamba aliporipoti kwamba alikuwa akiudhiwa kingono, alilaumiwa kwa kuwa mnyetivu kupita kiasi. Ingawa hivyo, Earlisha hakukata tamaa. Walikusanyana yeye na wasichana wengine sita waliokuwa wamefinywa na kukumbatiwa na mvulana yuleyule. “Ilituchukua watu sita kumsadikisha mwalimu mkuu kwamba kulikuwa na tatizo halisi,” yeye asema. Mwishowe, alifaulu kufanya huo utovu wa tabia uachishwe.

Mgeukie Mungu kwa ajili ya utegemezo. Ikiwa kuwa shuleni nyakati fulani hufanya uhisi kama umenaswa katika tundu la simba, kumbuka kwamba Yehova Mungu alimlinda nabii Danieli katika tundu halisi la simba. (Danieli 6:16-22) Yehova aweza kukusaidia wewe pia. Yeye anafahamu misongo unayokabili shuleni. Na hali iwapo ngumu, waweza kumwomba msaada—kwa sauti kuu ikihitajika! Usiogope au kuona haya kujulikana kuwa mtumishi wa Mungu wa kweli. Biblia huahidi watumishi waaminifu wa Yehova hivi: “Huwalinda nafsi zao watauwa wake, na kuwaokoa na mkono wa wasio haki.”—Zaburi 97:10.

Hili halihakikishi kuokolewa kimuujiza. Lazima ufanye kile uwezacho ili kujilinda. Fuata kanuni za Biblia. Uwe mwenye kiasi katika usemi wako na sura. Jizoeze busara katika kushughulika na mtu wa jinsia tofauti. Kwa kufanya hivyo, unaweza kufanya mengi ili kujilinda kutokana na kuudhiwa kingono.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Usiwe na moyo nusu unapokataa madokezo yasiyofaa; acha la yako imaanishe la!

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki