Kusumbuliwa Kingono—Jinsi Unavyoweza Kujikinga
“HAKUNA mwanamke apaswaye kusumbuliwa kingono kila siku,” asema mhariri wa gazeti aitwaye Gretchen Morgenson, “wala si kusababu kuzuri kwa wanawake kutarajia mazingira safi kazini yasiyo na tabia ya kukosa adabu.” Jambo la kupongezwa ni kwamba jitihada za waajiri na za mahakama za kufanya kazini kuwa mahali salama zaidi zimepata matokeo kadhaa mazuri. Kwa kielelezo, hatari ya kushtakiwa imefanya waajiri na waajiriwa ulimwenguni pote wajaribu kuboresha mazingira ya kazi. Makampuni mengi yameanzisha taratibu zao yenyewe za kushughulikia kuudhiwa kazini. Mikutano na semina hufanywa ili kufunza waajiriwa tabia ifaayo kazini.
Bila shaka, ni jambo la kupatana na akili kujua na kufuata sera za kampuni na sheria za hapo. (Warumi 13:1; Tito 2:9) Wakristo pia wamepata manufaa kwa kutumia kanuni za Biblia. Kufuata miongozo hiyo iliyopuliziwa katika shughuli zako na wafanyakazi wenzako kwaweza kukusaidia sana kuepuka kusumbuliwa kingono—au kusumbua wengine kingono.
Mwenendo Uwafaao Wanaume
Fikiria jinsi wanaume wanavyopaswa kuwatendea wanawake. Wastadi wengi hutahadharisha dhidi ya kugusa watu wa jinsia tofauti. Wao huonya kwamba kupiga mtu mgongoni kirafiki kwaweza kueleweka vibaya. “Mabaraza ya mahakama huchukua mguso kwa uzito sana,” asema wakili Frank Harty. Yeye anadokeza nini? “Kama ni zaidi ya kusalimiana kwa mkono, usikubali.” Kweli, Biblia haitoi sheria ya ujumla juu ya jambo hili.a Lakini kwa kufikiria hali ya sasa ya kisheria na kiadili, yafaa kujihadhari—hasa kwa wale ambao wana mwelekeo wa kugusa-gusa bila kutambua wanapoongea na wengine.
Ni kweli kwamba si rahisi sikuzote kufuata shauri kama hilo. Kwa mfano, Glen amelelewa katika utamaduni wa Kihispania. “Nitokako,” yeye asema, “watu huelekea zaidi kukukumbatia kuliko hapa Marekani. Katika familia yetu mara nyingi sisi husalimia marafiki kwa busu, lakini hapa tulitahadharishwa tusiwe wepesi kufanya hivyo.” Hata hivyo, kanuni za Biblia huthibitika kuwa zenye msaada kwa habari hii. Mtume Paulo alimwambia kijana Timotheo: “Watendee wanaume wachanga kama ndugu, wanawake wazee kama mama, na wanawake wachanga kama dada, kwa utakato kamili.” (1 Timotheo 5:1, 2, New International Version) Je, hilo halingeondosha kabisa mguso wa kingono, wa kutongoza, au usiotakikana?
Kanuni iyo hiyo yaweza kutumika pia kwa usemi. Kwa kufaa, Biblia husema: “Uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi.” (Waefeso 5:3, 4) Wakili wa masuala ya kusumbuliwa kingono Kathy Chinoy adokeza kwamba kabla ya kusema jambo fikiria swali moja: “Je, ungetaka mama yako, dada yako, au binti yako asikie usemi huo?” Usemi mchafu wenye kudokeza ngono hushusha hadhi ya msemaji na ya msikiaji vilevile.
Kuzuia Kusumbuliwa
Mtu aweza kujaribuje kuepuka kusumbuliwa? Shauri ambalo Yesu aliwapa wanafunzi wake alipowatuma kwenye mgawo wao wa kwanza wa kuhubiri labda laweza kutumika katika muktadha huu: “Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa-mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua.” (Mathayo 10:16) Vyovyote vile, Mkristo ana msaada. Biblia hutuhakikishia hivi: ‘Hekima iingiapo moyoni mwako, busara itakulinda; ufahamu utakuhifadhi.’ (Mithali 2:10, 11) Basi, ebu tuchunguze baadhi ya kanuni za Biblia ziwezazo kukusaidia kujilinda.
1. Chunga mwenendo wako pamoja na wafanyakazi wenzako. Hili halimaanishi kuwa baridi au mkali, kwa kuwa Biblia hutuhimiza ‘tujitahidi kuishi kwa amani na watu wote.’ (Waebrania 12:14, Habari Njema kwa Watu Wote; Warumi 12:18) Lakini kwa kuwa Biblia hutahadharisha Wakristo ‘waenende kwa hekima mbele yao walio nje,’ basi lapatana na akili kudumisha tabia ya uzito, hasa unaposhughulika na watu wa jinsia tofauti. (Wakolosai 4:5) Kitabu Talking Back to Sexual Pressure, cha Elizabeth Powell, huhimiza wafanyakazi “wajifunze tofauti iliyo kati ya mtazamo wenye kufurahisha unaofaa hali yao na aina ya urafiki ambayo yaweza kudokeza kwamba unakubali mambo ya kingono.”
2. Vaa kwa kiasi. Unachovaa huwapa wengine ujumbe. Huko nyuma katika nyakati za Biblia, kuvaa mitindo fulani ya mavazi kulionyesha ikiwa mtu alikuwa mkosa-adili au mfanya ngono ovyo-ovyo. (Mithali 7:10) Na mara nyingi ndivyo ilivyo leo; mavazi yenye kubana, ya madoido, au yenye kuonyesha uchi yaweza kuvutia uangalifu usiofaa. Ni kweli kwamba wengine waweza kuhisi wana haki ya kuvaa chochote watakacho. Lakini kama mwandikaji Elizabeth Powell anavyosema, “ukifanya kazi miongoni mwa watu ambao wanaamini si kosa kuiba pesa, ningekuambia usiweke kibeti chako cha pesa katika mfuko wako wa nyuma. . . . Ni lazima utambue udhaifu wa . . . mitazamo ya jamii na kujaribu kujilinda usidhulumiwe nayo.” Hivyo, shauri la Biblia ni la kisasa. Hilo huonya wanawake kwa upole “wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi.” (1 Timotheo 2:9) Vaa kwa kiasi, na huenda usielekezewe sana usemi au matendo machafu.
3. Chunga mashirika yako! Biblia hutuambia juu ya mwanamke mchanga aitwaye Dina aliyeshambuliwa kingono. Yaonekana alivutia uangalifu wa mshambulizi wake kwa sababu kwa ukawaida ‘alikuwa akitoka kuwaona binti za nchi’ ya Kanaani—wanawake waliojulikana kufanya ngono ovyo-ovyo! (Mwanzo 34:1, 2) Leo vilevile, ukiwa na mazoea ya kuzungumza na—au kuwasikiliza—wafanyakazi wenzako ambao hujulikana kuongea juu ya habari zenye kuamsha tamaa, basi wengine huenda wakaamua kwamba unaweza kukubali madokezo ya kingono.
Hili halimaanishi kwamba ni lazima uepuke wafanyakazi wenzako. Lakini mazungumzo yakija kuwa machafu, mbona usiondoke? Kwa kupendeza, wengi wa Mashahidi wa Yehova wamepata kwamba kuwa na viwango vya juu vya kiadili huwalinda kutokana na kusumbuliwa.—1 Petro 2:12.
4. Epuka hali zinazoweza kukufanya uridhiane. Biblia hueleza jinsi mwanamume kijana aitwaye Amnoni alivyofanya hila abaki peke yake na mwanamke mchanga aitwaye Tamari ili amtumie vibaya kingono. (2 Samweli 13:1-14) Leo vilevile wasumbuaji wanaweza kutenda kwa njia hiyo, labda kwa kualika mfanyakazi wa cheo cha chini kushiriki kunywa kileo au kubaki kazini baada ya saa za kawaida za kufunga kazi bila sababu yoyote nzuri. Jihadhari na mialiko kama hiyo! Biblia husema: “Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha.”—Mithali 22:3.
Ukisumbuliwa
Bila shaka wanaume fulani watafanya madokezo yasiyofaa hata kama mwanamke anajiendesha vizuri. Unapaswa kutendaje ukifanyiwa madokezo hayo? Wengine wamependekeza kushughulikia jambo hilo bila kukasirika! ‘Mambo ya kingono ofisini ni kichangamshi cha maisha!’ asema mwanamke mmoja. Hata hivyo, badala ya kuona uangalifu kama huo usiofaa kuwa wenye kuchekesha au wa kusifusifu, Wakristo wa kweli huchukizwa nao. Wao ‘huchukia lililo ovu’ na kutambua kwamba kusudi la miendo hiyo mara nyingi ni kumshawishi mtu aingie katika ukosefu wa adili kingono. (Warumi 12:9; linganisha 2 Timotheo 3:6.) Huo mwenendo mchafu huvunja adhama yao ya Kikristo. (Linganisha 1 Wathesalonike 4:7, 8.) Unaweza kushughulikiaje hali hizo?
1. Chukua msimamo! Biblia hutuambia jinsi mtu mmoja mwenye kumhofu Mungu aitwaye Yosefu alivyoitikia mapendekezo yasiyo ya adili: “Ikawa baada ya mambo hayo, mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala nami.” Je, Yosefu alipuuza tu mapendekezo yake, akitumaini kwamba tatizo hilo lingeisha lenyewe tu? Tofauti kabisa! Biblia husema kwamba alikataa kijasiri mwendo wake, akisema: “Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu?”—Mwanzo 39:7-9.
Hatua alizochukua Yosefu hutuwekea kielelezo kizuri sisi sote wanaume na wanawake. Kupuuza—au jambo baya zaidi, kutishwa na—usemi wenye kudokeza ngono au tabia ya kutumia nguvu ni nadra sana iondoe tatizo; badala ya hivyo, hofu au kusitasita yaweza kufanya hali izidi kuwa mbaya! Mshauri wa jinsi ya kuepuka kulalwa kinguvu Martha Langelan atahadharisha kwamba watu ambao hulala wengine kinguvu mara nyingi hutumia kusumbua wengine kingono kuwa “njia ya kupima uwezekano wa mwanamke kujitetea akishambuliwa; ikiwa yeye ni mpole na mwoga anaposumbuliwa, wao hudhani kwamba mwanamke huyo atakuwa mpole na kuhofishwa ashambuliwapo.” Basi ni jambo muhimu uchukue msimamo mara moja unaposumbuliwa. Kulingana na mwandikaji mmoja, “kukataa mara moja na kwa njia ya wazi mara nyingi hutosha kumfanya msumbuaji aache tabia yake mbaya.”
2. La yako na iwe la! Yesu alisema hilo katika Mahubiri yake ya Mlimani. (Mathayo 5:37) Taarifa yake hufaa katika pindi hizi, kwa kuwa mara nyingi wasumbuaji hawakomi. Unahitaji kuwa thabiti kwa kadiri gani? Hilo hutegemea hali na itikio la msumbuaji. Tumia kadiri yoyote ile ya uthabiti inayotakikana ili kudhihirisha msimamo wako. Katika visa fulani, taarifa sahili ya moja kwa moja kwa sauti tulivu itatosha. Mtazame kwa macho. Wastadi hudokeza yafuatayo: (a) Taja jinsi unavyohisi. (“Sipendi kamwe . . .”) (b) Taja kihususa tabia hiyo inayoudhi. (“. . . unapotumia usemi mbaya, mchafu . . . ”) (c) Umwambie wazi unalotaka afanye. (“Nataka ukome kunizungumzia kwa njia hiyo!”)
“Hata hivyo,” Langelan atahadharisha, “mkabiliano usipite kiasi kamwe hata kufikia hatua ya kuwa mkali. Kuwa mkali pia (kutukana, kutisha, na kutumia maneno yenye kuumiza, kurusha ngumi, kumtemea mate msumbuaji) hakuna matokeo. Jeuri ya mdomo ni hatari, na hakuna haja ya kutumia nguvu ila tu kama umeshambuliwa kihalisi na unahitaji kujikinga.” Shauri kama hilo lenye kutumika hupatana na maneno ya Biblia kwenye Warumi 12:17: “Msimlipe mtu ovu kwa ovu.”
Vipi ikiwa kusumbuliwa kwaendelea japo jitihada zako zote kukukomesha? Makampuni fulani yameanzisha taratibu za kushughulikia kusumbuliwa kingono. Mara nyingi tisho tu la kupeleka malalamiko kwa kampuni litafanya msumbuaji wako akome. Na tena huenda asikome. Kwa kusikitisha, kupata msimamizi wa kazi mwenye kusikiliza si rahisi sikuzote kwa wanawake au kwa wanaume. Glen, adaiye alisumbuliwa na mfanyakazi wa kike, alijaribu kulalamika. Yeye akumbuka: “Nilipomwambia mkubwa wa kazi kuhusu tatizo hilo, hakunisaidia hata kidogo. Kwa kweli yeye aliona hilo kuwa jambo la kuchekesha sana. Nililazimika tu kuchunga mwanamke huyo na kumwepa.”
Wengine wamejaribu kushtaki kisheria. Lakini zile hukumu kubwa-kubwa unazosoma katika vyombo vya habari si kawaida hata kidogo. Isitoshe, kitabu Talking Back to Sexual Pressure huonya: “Utatuzi wa kisheria dhidi ya kusumbuliwa huhitaji nguvu nyingi sana za kihisia-moyo na wakati; huo hutokeza mkazo wa kimwili na kiakili.” Basi, kwa sababu nzuri Biblia huonya: “Usiharakishe kufanya mashtaka ya kisheria.” (Mithali 25:8, New World Translation) Baada ya kuhesabu gharama za kihisia-moyo na kiroho ya hatua ya kisheria, wengine wameonelea watafute kazi nyingine.
Mwisho wa Kusumbuliwa
Kusumbuliwa kingono si jambo jipya. Kumeenea ulimwenguni pote kama moyo wa kibinadamu usiokamilika, wenye pupa na hila. Tume za uchunguzi na kesi za mahakama hazitapata kamwe kuondolea jamii hali ya kusumbuliwa kingono. Kuondoa hali ya kusumbuliwa kingono huhitaji badiliko kubwa la moyo katika watu.
Leo, Neno la Mungu na roho yake hutokeza badiliko hilo katika watu ulimwenguni pote. Ni kana kwamba mbwa-mwitu na simba wanajifunza kutenda kama wana-kondoo na ndama, kama ilivyotabiriwa na nabii Isaya. (Isaya 11:6-9) Kwa kujifunza Biblia pamoja na watu, kila mwaka Mashahidi wa Yehova husaidia maelfu mengi ya wale ambao zamani walikuwa “mbwa-mwitu” kufanya mabadiliko ya utu ya kudumu na ya kina sana. Watu hao hutii amri ya Kimaandiko ya ‘kuvua kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani’ na kuubadili na “utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli.”—Waefeso 4:22-24.
Siku moja dunia itajawa na wanaume na wanawake ambao hushikilia viwango vya Biblia. Watu wenye kumhofu Mungu hungoja kwa tamaa siku hiyo, ambapo aina zote za kutendwa vibaya hazitakuwapo. Mpaka wakati huo, wao hukabiliana kwa kadiri wawezavyo na matendo mabaya ya leo.
[Maelezo ya Chini]
a Tahadhari ya Paulo kwenye 1 Wakorintho 7:1 ya ‘kutomgusa mwanamke’ yaonekana yarejezea kugusa kingono, bali si mguso wa kawaida. (Linganisha Mithali 6:29.) Katika huo muktadha, Paulo anahimiza useja na kuonya dhidi ya kujiingiza katika ukosefu wa adili kingono.—Ona “Maswali Kutoka kwa Wasomaji” katika Mnara wa Mlinzi la Januari 1, 1973, la Kiingereza.
[Blabu katika ukurasa wa 7]
“Je, ungetaka mama yako, dada yako, au binti yako asikie usemi huo?”
[Picha katika ukurasa wa 8]
Tabia ya uzito na mavazi ya kiasi hulinda sana mtu asisumbuliwe
[Picha katika ukurasa wa 10]
Wakristo wa kweli leo hujifunza kutendeana kwa njia ya heshima