Kusumbuliwa Kingono—Tatizo la Duniani Pote
KAZI ilikuwa imekuwa ogofyo kwa karani mmoja mchanga aitwaye Rena Weeks. Ni kweli kwamba kampuni ya sheria iliyomwajiri ilikuwa mashuhuri nayo ilikuwa na ofisi katika zaidi ya nchi dazani mbili. Lakini, yeye alimfanyia kazi mwanamume mmoja ambaye, kulingana na dai lake, hangeweza kuacha kumkamata-kamata na kumshika-shika. Hayo mashambulizi yenye kumwaibisha yaliandamana na usemi mchafu wenye kudokeza ngono.
Miaka mingi iliyopita, wanawake waliokuwa katika hali kama hii hawakuwa na namna—ila tu labda waache kazi. ‘Neno [la mwanamke] dhidi ya [mwanamume]’ halingekuwa kesi. Na hata wale walioelekea kuamini yale ambayo mwanamke alisema labda wangepuuza tu tatizo hilo kwa kusema, ‘Si jambo kubwa.’ Lakini nyakati zimebadilika. Rena Weeks alifanya zaidi ya kukasirika tu na kuacha kazi. Yeye alishtaki.
Baraza la mahakama la Marekani liliamuru apewe ridhaa ya dola 50,000 kwa sababu ya kufadhaika kihisia-moyo, pamoja na dola 225,000 za ziada ili kuadhibu yule aliyekuwa mkubwa wake wa kazi. Kisha katika hatua iliyonasa uangalifu wa makampuni ya biashara na ya sheria ulimwenguni pote, hilo baraza la mahakama liliamuru kampuni hiyo ilipe kiasi kikubwa sana cha pesa cha dola milioni 6.9 za ziada kikiwa adhabu ya kukosa kurekebisha hilo tatizo!
Bila shaka kesi ya Weeks si kisa cha pekee cha aina hiyo. Shtaka jingine la majuzi lilihusu kampuni moja ya kitaifa (Marekani) yenye maduka mengi ya kuuza bidhaa kwa bei iliyopunguzwa. Mwajiriwa mmoja aitwaye Peggy Kimzey alidai kwamba msimamizi wake wa kazi alikuwa amemwambia maneno machafu mengi ya kingono. Katika 1993, Peggy Kimzey alijiuzulu kazi yake na kushtaki. Iliamriwa alipwe dola 35,000 kwa sababu ya kuaibishwa na masumbufu ya kiakili pamoja na dola 1 ya mfano kwa kupoteza mshahara. Baraza la mahakama liliamua pia kwamba aliyekuwa mwajiri wake alikuwa amefanyiza mazingira mabaya ya kazi kwa kuachilia kusumbuliwa kwake. Adhabu ikawa nini? Alitozwa Dola milioni 50!
Gazeti Men’s Health lasema: “Kesi za kusumbuliwa kingono zimekuwa zikiongezeka sana. Katika 1990, EEOC [Tume ya Fursa Sawa ya Kuajiriwa] ilishughulikia malalamiko kama hayo 6,127; kufikia mwaka uliopita [1993] jumla ya mwaka mzima ilikuwa karibu maradufu kufikia 11,908.”
Kutumia Mamlaka Vibaya
Huku amri za mabaraza ya mahakama zikiwa habari kuu za vyombo vya habari, ukweli ni kwamba ni visa vichache tu ambavyo hupelekwa mahakamani. Wengi wanaosumbuliwa huugua kimya-kimya—wakiwa wadhulumiwa wa tendo baya la kutumia vibaya mamlaka na matisho linalofanywa katika ofisi, barabarani, katika basi, kwenye kaunta za chakula cha mchana, na katika viwanda. Nyakati nyingine, kuna ushurutisho wa kufanya ngono. Ingawa hivyo, mara nyingi udhia huwa matendo ya hila, yenye kuchokoza yasiyo na aibu: miguso isiyotakikana au isiyofaa, maneno machafu, na kutazamwa kwa tamaa ya kingono.
Ni kweli kwamba wengine hukataa kutaja kwamba tabia hiyo ni kusumbuliwa, wakibisha kwamba ni jaribio tu la kijinga kwa upande wa wanaume fulani kuvutia uangalifu wa watu wa jinsia tofauti. Lakini wengi, kama mwandikaji Martha Langelan, hukataa majaribio kama hayo ya kutolea udhuru tabia mbaya. Yeye aandika: “Hiyo si kutafuta uchumba kijinga, au kutafuta uchumba kusiko na adabu, au kutafuta uchumba kimzaha, au kutafuta uchumba ‘kunakoeleweka vibaya.’ Haikusudiwi ivutie wanawake; hiyo ni tabia yenye kusudi jingine kabisa. Kama kulala kinguvu, kusumbua kingono kumekusudiwa kushurutisha wanawake, si kuwavutia. . . . [Huko] ni wonyesho wa mamlaka.” Ndiyo, mara nyingi kutendwa vibaya kwa njia hiyo ni njia nyingine tu iliyo katili ambayo “mutu ana uwezo juu ya mwenzake kwa kumwumiza.”—Muhubiri 8:9, Zaire Swahili Bible; linganisha Mhubiri 4:1.
Mara nyingi wanawake hawafurahii kusumbuliwa kingono nao huitikia wakiwa na hisia kama machukizo na hasira hadi kushuka moyo na kuaibishwa. Mmoja aliyedhulumiwa akumbuka: “Hiyo hali ilinimaliza kabisa. Nilipoteza utumainifu wangu, uhakika wangu, kujistahi kwangu, na tamaa zangu za kazi-maisha. Utu wangu ukabadilika mara moja. Nilikuwa mtu mwenye furaha maishani. Nikawa mwenye uchungu, mpweke, na mwenye aibu.” Na wakati mdhulumu ni mwajiri au mtu mwingine mwenye mamlaka, kusumbuliwa hasa huwa kubaya hata zaidi.
Basi, si ajabu kwamba mahakama zimeanza kuadhibu wakosaji na kuamuru wadhulumiwa walipwe ridhaa. Tangu Mahakama Kuu ya Marekani ifafanue kutendwa vibaya kwa njia hiyo kuwa ukiukaji wa haki za raia, waajiri wamezidi kuwa na daraka la kisheria la kudumisha mazingira ya kazi ambayo si “mabaya au yenye kuudhi.”
Makampuni yaachiliayo kusumbuliwa kingono yaweza kupatwa na hali ya wafanyakazi kukosa motisha ya kazi, wengi kukosa-kosa kufika kazini, matokeo ya chini, na kuajiriwa kwa wafanyakazi wengi wanaochukua mahali pa wengine wanaoacha—bila kutaja hasara za kifedha wadhulumiwa wakiamua kushtaki.
Kumeenea Kiasi Gani?
Kusumbuliwa kingono kumeenea kwa kiasi gani hasa? Uchunguzi mbalimbali waonyesha kwamba zaidi ya nusu ya wanawake wanaofanya kazi Marekani wamesumbuliwa kingono. Hivyo kitabu kimoja chadai: “Kusumbuliwa kingono ni tatizo lililoenea sana. Hupata wanawake katika kila aina ya kazi tokea wahudumu wa hoteli hadi wakuu wa mashirika. Hutukia katika kila ngazi ya usimamizi wa mashirika na katika kila aina ya biashara na viwanda.” Hata hivyo, tatizo hilo haliko Marekani pekee. Kitabu Shockwaves: The Global Impact of Sexual Harassment, cha Susan L. Webb, chataja takwimu zifuatazo:a
KANADA: “Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba wanawake 4 kati ya 10 waliripoti kuwa walisumbuliwa kingono wakiwa kazini.”
JAPANI: “Uchunguzi wa Agosti 1991 ulionyesha kwamba asilimia 70 ya wanawake waliokubali kuhojiwa walisumbuliwa” kazini. “Asilimia 90 walisema kwamba walisumbuliwa kingono wakati wa kwenda na kutoka kazini.”
AUSTRIA: “Uchunguzi wa 1986 ulionyesha kwamba karibu asilimia 31 ya wanawake waliripoti visa vibaya vya kusumbuliwa.”
UFARANSA: “Katika 1991 uchunguzi mmoja . . . uligundua kwamba asilimia 21 ya wanawake 1,300 waliohojiwa walisema kwamba wao binafsi walikuwa wamepata kusumbuliwa kingono.”
UHOLANZI: Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba “asilimia 58 ya wanawake waliokubali [kuhojiwa] walisema kwamba wao binafsi walipata kusumbuliwa kingono.”
Ishara ya Nyakati
Bila shaka, kuudhiwa na kusumbuliwa kazini si mambo mapya. Wanawake—na nyakati nyingine wanaume—walitendwa vibaya kwa njia hiyo hata huko nyuma katika nyakati za Biblia. (Mwanzo 39:7, 8; Ruthu 2:8, 9, 15) Lakini tabia hiyo mbaya yaonekana imeenea hasa leo. Kwa nini?
Jambo moja ni kwamba katika miaka ya majuzi wanawake wengi sana wameanza kufanya kazi. Basi, wanawake wengi wamejipata katika hali ambazo wanaweza kutendwa vibaya. Hata hivyo, la muhimu hata zaidi ni unabii wa Biblia uliotabiriwa zamani sana: “Kumbuka hili! Kutakuwa na nyakati zilizo ngumu katika siku za mwisho. Watu watakuwa wenye ubinafsi, wenye pupa, wenye kujisifu, na hila; watakuwa wenye kutukana . . . ; watakuwa wasio na fadhili, wasio na huruma, wachongezi, wenye jeuri, na wakali.” (2 Timotheo 3:1-3, Today’s English Version) Kuenea kwa kusumbuliwa kingono ni mojawapo tu uthibitisho wenye kutokeza kwamba maneno hayo yanatimizwa leo. Kwa kupendeza, makala moja katika gazeti Men’s Health yasema kwamba “ongezeko la madai ya kusumbuliwa kingono limeandamana na kupunguka sana kwa adabu kwa ujumla. Tabia mbaya zipo kila mahali.”
Kuenea kwa kusumbuliwa kingono pia kwaonyesha ile “adili mpya,” ambayo ilienea sana katika ulimwengu wakati wa miaka ya 1960. Kuvunjwa kwa maadili ya kidesturi kumeandamana na hali ya kushangaza sana ya kutojali haki na hisia za wengine. Hata chanzo kiwe nini, kusumbuliwa kingono ni jambo la kuogofya litokealo kazini. Wanaume na wanawake wanaweza kufanya nini ili kujilinda? Je, kutapata kuwa na wakati ambapo mahali pa kazi hapatakuwa na kusumbuliwa?
[Maelezo ya Chini]
a Takwimu huelekea kutofautiana, kwa kuwa watafiti hutumia njia na ufafanuzi tofauti-tofauti wa kusumbuliwa kingono.
[Sanduku katika ukurasa wa4]
Kusumbuliwa Kingono—Ngano Dhidi ya Mambo ya Hakika
Ngano: Kusumbuliwa kingono huripotiwa kupita kiasi sana. Ni jambo jingine tu la kupita, tokeo la kutiliwa chumvi na kichaa la vyombo vya habari.
Hakika: Sanasana, mwanamke hupata hasara sana kuliko faida kwa kuripoti juu ya kudhulumiwa. Kwa kweli, ni wanawake wachache tu (asilimia 22 kulingana na uchunguzi mmoja) ambao hupata kuambia mtu yeyote kwamba wamesumbuliwa. Hofu, haya, kujilaumu, kuvurugika akili, kutojua haki zao za kisheria hufanya wanawake wengi wanyamaze. Hivyo, wastadi wengi huamini kwamba tatizo hilo sanasana haliripotiwi!
Ngano: Wanawake wengi hufurahia kuelekezewa fikira. Wale ambao hudai kwamba wamesumbuliwa ni wenye kuitikia mambo kupita kiasi.
Hakika: Uchunguzi mbalimbali waonyesha kwa kudumu kwamba wanawake huudhikia kutendwa kwa njia isiyo ya adabu kama hiyo. Katika uchunguzi mmoja, “zaidi ya wanawake wawili kati ya kila watano walisema waliudhika sana na karibu thuluthi moja wakasema walikasirika.” Wengine waliripoti walihisi wasiwasi, kuumizwa, na kushuka moyo.
Ngano: Wanaume husumbuliwa sawa tu na wanawake.
Hakika: Watafiti wa Shirika la Kitaifa la Wanawake Wafanyao Kazi (Marekani) waripoti kwamba “visa vipatavyo asilimia 90 vya kusumbuliwa huhusu wanaume ambao wamesumbua wanawake, asilimia 9 ni visa vya watu wa jinsia moja . . . , na asilimia 1 huhusu wanawake ambao wamesumbua wanaume.”
[Picha katika ukurasa wa 5]
Kusumbuliwa kingono hakuhusu ngono pekee