-
Jeuri Iathiripo NyumbaniAmkeni!—1993 | Februari 8
-
-
Jeuri Iathiripo Nyumbani
“Jeuri ya kibinadamu—iwe ni kuchapwa kofi au kusukumwa,kudungwa kisu au kupigwa risasi—hutukia mara nyingi zaidi miongoni mwa washiriki wa familia kuliko mahali penginepo katika jamii yetu.”—Behind Closed Doors.
TEMBEA katika barabara yoyote katika Amerika. Katika kila nyumba moja kati ya mbili, namna fulani ya jeuri ya nyumbani itatukia angalau mara moja mwaka huu. Na katika nyumba 1 kati ya 4, itatukia mara nyingi. Kwa kushangaza, wengi ambao huogopa kutembea barabarani usiku wamo katika hatari kubwa zaidi wawasilipo nyumbani.
Lakini jeuri ya nyumbani haitukii katika Amerika peke yake. Inatukia ulimwenguni kote. Kwa mfano, katika Denmarki mauaji ya kimakusudi 2 kati ya 3 hutukia katika familia. Utafiti katika Afrika huonyesha kwamba mauaji yote ya kimakusudi yale yatukiayo ndani ya familia hutofautiana kati ya asilimia 22 hadi 63, ikitegemea nchi. Na katika Latini Amerika watu wengi, hasa wanawake, hushushiwa heshima, hupigwa, au kuuawa na wanaume wajivuniao nguvu zao za kiume.
Katika Kanada wanawake wapatao mia moja huuawa na waume zao au wanaume waishio nao. Katika United States, ikiwa na watu karibu mara kumi ya idadi ya watu wa kanada, kila mwaka wanawake wapatao 4,000 huuawa na waume au wanaume rafiki zao. Zaidi ya hilo, kila mwaka watoto wapatao 2,000 huuawa na wazazi wao, na idadi hiyohiyo ya wazazi huuawa na watoto wao.
Hivyo, ulimwenguni kote, waume hupiga wake zao, wake hugonga waume zao, wazazi huchapa watoto wao, watoto hushambulia wazazi wao, na watoto ni wenye jeuri kuelekeana. Hasira na jeuri iliyo nyingi zaidi ambayo huwapata watu wazima katika maisha zao ni kutoka au kuelekea watu wenye uhusiano wa damu,” chashikilia kitabu When Families Fight, “na hasira hiyo ni kali zaidi ya ipatwayo katika uhusiano mwingine wowote.”
Familia Yapigana
Kumtendea vibaya mwenzi wa ndoa: Mara nyingi mno, waume hukiona cheti cha ndoa kuwa cheti cha ruhusa ya kupiga wake zao. Ingawa wanawake hupiga wanaume, dhara kwa kawaida si kubwa kama lile liwapatalo wanawake wakati wanaume wanapowapiga wake zao. Gazeti Parents huripoti hivi: “Zaidi ya asilimia 95 ya visa viripotiwavyo vya kutendwa vibaya [sana] kwa mwenzi wa ndoa huhusisha mwanamume akimpiga mwanamke.”
Mwanasheria wa wilaya katika New York ataarifu hivi: “Jeuri dhidi ya wanawake inaenea kwa kadiri kubwa katika jamii ya Kiamerika. FBI [Shirika la Upelelezi] limekadiria kwamba . . . wanawake wengi kama milioni 6 hupigwa kila mwaka.” Ingawa idadi ya visa hutofautiana nchi na nchi, ripoti huonyesha kwamba kupigwa kwa wanawake na wanaume huenea pote katika mabara mengi ikiwa si yale mengi zaidi.
Katika United States, inakadiriwa kwamba “mmoja kati ya wanawake 10 atashambuliwa vikali (apigwe, apigwe mateke, aumwe au atendwe jambo baya zaidi) na mume wake wakati fulani katika wakati wa ndoa yake.” Visa visivyo vibaya kama hivyo vitiwapo ndani, gazeti Family Relations hutaarifu, “mmoja kati ya wanawake wawili katika United States atapatwa na jeuri ya nyumbani.”
Kwa kweli, mwanasheria mmoja wa wilaya katika New York asema kwamba imeonyeshwa kwamba kupiga wake husababisha kwa wanawake majeraha mengi zaidi yenye kutaka walazwe hospitalini kuliko visa vyote vya kunajisiwa, kushambuliwa na wakora na aksidenti za magari vikijumlishwa pamoja.”
Dakt. Lois G. Livezey aandika hivi: “Ni wazi kwamba jeuri dhidi ya wanawake na jeuri ndani ya familia iko kila mahali, na kwamba watendaji . . . ni watu wa kawaida. . . . Ni tatizo zito miongoni mwa tabaka zote na jamii zote na idadi zote za watu.”
Nyakati nyingine watendwa vibaya hujilaumu wenyewe kwa kutendwa vibaya, ikitokeza hali ya kutojiheshimu sana. Gazeti Parents hueleza hivi: “Mwanamke akosaye kujitumaini na ambaye hajiheshimu sana hujifanya awe lengo la kutendwa vibaya. . . . Mfano wa mwanamke aliyetendwa vibaya ni yeye ambaye huhofu kupanga na kutenda kwa manufaa yake mwenyewe.”
Jeuri ya kindoa huwa pia na matokeo mabaya kwa watoto. Wao hujifunza kwamba jeuri yaweza kutumiwa ili kutumia wengine kujifaidi. Baadhi ya akina mama hata huripoti kwamba watoto wao hutumia vitisho dhidi yao, kama vile “Nitamwambia baba akupige,” ili kupata watakayo.
Kuwatenda watoto vibaya: Kila mwaka mamilioni ya watoto hukabili adhabu ya kimwili yenye kupita kiasi ambayo ingeweza kuwajeruhi, kuwalemaza, au kuwaua. Inakadiriwa kwamba kwa kila kisa cha kutendwa vibaya kiripotiwacho, visa 200 haviripotiwi. “Kwa watoto, mara nyingi nyumbani ndipo mahali hatari kupita pengine pote pa kuwa,” chadai kitabu Sociology of Marriage and the Family.
Profesa wa chuo kikuu John E. Bates asema kwamba kutendwa vibaya ndio uvutano wenye nguvu zaidi wa nyumbani uathirio jinsi mtoto atakavyojiendesha baadaye maishani. Dakt. Susan Forward asema hivi: “Mimi nimeona kwamba hakuna tukio jingine maishani ambalo hutia makovu sana hali ya kujiheshimu kwa watu au kuwafanya waelekee kuwa na magumu makubwa ya kihisiamoyo katika utu mzima.” Ishara za tabia ya jeuri katika hali ngumu zaweza kuonekana hata katika watoto kuanzia umri wa miaka minne hadi mitano. Kadiri wakuavyo, watoto hao huwa na viwango vya juu zaidi vya kutumia vibaya dawa za kulevya, kutumia vibaya kileo, tabia ya uhalifu, masumbufu ya kiakili, na ukuzi uliokawia.
Kwa kueleweka, watoto wengi waliotendwa vibaya huwa na hasira kuelekea awatendaye vibaya, lakini mara nyingi huwa na hasira pia ku-elekea yule mzazi asiyewatenda vibaya kwa kuruhusu jeuri iendelee. Katika akili ya mtoto, yule mzazi aonaye akitendwa vibaya asizuie huenda akaonwa kuwa mshiriki wa kutenda vibaya.
Kuwatenda vibaya watu wa umri mkubwa: Ikadiriwayo kuwa asilimia 15 ya watu wenye umri mkubwa wa Kanada hutendwa vibaya kimwili na kiakili na watoto wao walio watu wazima. Daktari mmoja atabiri kwamba “hali itazidi tu kuwa mbaya huku idadi kubwa zaidi ya watu iwapo yenye umri mkubwa zaidi, na mizigo yenye kulemea kifedha na kihisiamoyo kwa watoto wao iongezekavyo.” Hofu kama hizo huhisiwa ulimwenguni pote.
Mara nyingi, wenye umri mkubwa huwa hawana nia ya kuripoti kutendwa vibaya. Huenda wakawa wanamtegemea mwenye kuwatenda vibaya na hivyo wakachagua kuendelea kuishi chini ya hali mbaya. “Wakati mwingine” ndilo jibu alilotoa daima mwanamke mwenye umri mkubwa alipoulizwa angewaripoti mwana na binti mkwe wake wakati gani kwa wenye mamlaka. Walikuwa wamempiga vibaya sana hivi kwamba alilazwa hospitalini kwa mwezi mmoja.
Kutendeana vibaya kwa watoto: Hii ni namna ya jeuri ya nyumbani yenye kuenea sana. Baadhi ya watu huifanya kuwa jambo dogo, wakisema, “Hiyo ni kawaida ya wavulana.” Hata hivyo, zaidi ya nusu ya watoto waliokuwa katika uchunguzi mmoja walikuwa wametenda vitendo vilivyokuwa vibaya sana kiasi cha kutosha kushtakiwa kwa uhalifu kama vitendo hivyo vingalikuwa vimeelekezwa dhidi ya mtu fulani nje ya familia.
Wengi huhisi kwamba kutendeana vibaya kwa watoto hutokeza kigezo ambacho huendelezwa hadi utu mzima. Kwa wengine hiyo huenda hata ikawa sababu ya kutenda vibaya mwenzi wa ndoa baadaye badala ya kuwa kwamba wameona jeuri kati ya wazazi wao.
Mahali Hatari pa Vita
Mchunguzi mmoja wa kisheria alikadiria wakati mmoja kwamba polisi waliitwa washughulikie mapambano ya familia mara nyingi zaidi ya visa vyote vingine vya uhalifu vikijumlishwa pamoja. Alidai pia kwamba polisi wengi zaidi waliuawa walipokuwa wameenda kushughulikia tatizo la kinyumbani kuliko wakati walipokuwa wakishughulikia ombi la namna nyingine yoyote. “Angalau kwa habari ya wizi wa kutumia nguvu unajua la kutazamia,” akasema polisi mmoja. “Lakini ingia ndani ya nyumba ya mtu fulani . . . hujui litakalotukia.”
Baada ya uchunguzi mwingi wa jeuri ya nyumbani, kikundi kimoja cha uchunguzi katika Amerika kilifikia mkataa kwamba, familia ilikuwa ndicho kikundi cha kijamii chenye jeuri zaidi, isipokuwa tu jeshi katika wakati wa vita.
Ni nini hutokeza jeuri ya familia? Je! itakwisha wakati wowote? Je! Kuna wakati wowote inapostahili? Makala ifuatayo itachunguza maswali hayo.
-
-
Ni Nini Husababisha Jeuri ya Nyumbani?Amkeni!—1993 | Februari 8
-
-
Ni Nini Husababisha Jeuri ya Nyumbani?
“Badala ya kuwa kimbilio kutoka kwenye mikazo, shida, vitendo visivyo vya kiakili vya jamii iliyo nje, familia mara nyingi huonekana ikionyesha au hata kukuza shida hizo.”—The Intimate Environment—Exploring Marriage and the Family.
UTAFITI juu ya jeuri ya familia ni jitihada ya karibuni kwa kulinganisha. Uchunguzi mwingi umefanywa tu wakati wa miongo ya karibuni. Matokeo ya uchunguzi huo mwingi huenda yasipatane sikuzote, lakini mambo fulani ya msingi yenye kuchangia jeuri ya nyumbani yamegunduliwa. Acheni tufikirie baadhi yayo.
Historia ya Familia Huwa na Fungu Gani?
Idadi fulani ya watafiti walisema hivi kuhusu mambo waliyogundua: “Kadiri wenzi wa ndoa waliohojiwa walivyo wajeuri zaidi kwa mmoja na mwenzake, ndivyo watoto wao walivyo wajeuri zaidi kwa mmoja na mwenzake, na kwa wazazi wao.”
Kuona tu jeuri ya familia kuna matokeo makubwa kwa mtoto. “Mtoto aonaye mama yake akipigwa ni sawa na mtoto kupigwa,” asema daktari wa tiba ya therapia John Bradshaw. Kijana mmoja aitwaye Ed alichukia kuona baba yake akimpiga mama yake. Hata hivyo, ijapokuwa huenda akawa hakujua hivyo, alikuwa akifunzwa kuamini kwamba wanaume hudhibiti wanawake na kwamba ili kufanya hivyo, wanaume lazima wawaogopeshe, wawaumize, na kuwavunjia heshima. Alipopata kuwa mtu mzima, Ed alitumia mbinu hizo za jeuri, za kumtenda vibaya mke wake.
Baadhi ya wazazi hukataza watoto wao kwa tahadhari wasitazame jeuri katika televisheni, na hilo ni jambo zuri. Lakini wazazi wapaswa kuwa wenye tahadhari hata zaidi inapohusu kuangalia tabia yao wenyewe wakiwa violezo vya kuigwa na watoto wao wenye kuathiriwa na mambo hayo kwa urahisi sana.
Mkazo Huwa na Fungu Gani?
Uchukuaji mimba, ukosefu wa kazi ya kuajiriwa, kifo cha mzazi, kuhama, ugonjwa, na matatizo ya kifedha huleta mkazo, kama yafanyavyo mambo mengine. Watu wengi zaidi hushughulikia mkazo bila kufanya jeuri. Hata hivyo, kwa wengine, mkazo waweza kutokeza jeuri, hasa ukichanganywa na mambo mengine. Kwa mfano, kutunza mzazi mwenye umri mkubwa—hasa mzazi akiwa mgonjwa—mara nyingi kumeongoza kwenye kumtenda vibaya wakati mtunzaji amelemewa na madaraka mengine ya familia.
Kulea watoto hutokeza mkazo. Kama tokeo, uwezekano wa kumtenda mtoto vibaya huongezeka kadiri familia izidivyo kuwa kubwa. Watoto huenda wakaleta ongezeko la kutendwa vibaya kwa mwenzi wa ndoa pia, maana “kutopatana juu ya watoto ndiko huonekana zaidi kukifanya wenzi wa ndoa waanze kupigana,” laripoti Behind Closed Doors.
Maoni Yasiofaa Juu ya Jinsia Tofauti
Dan Bajorek ambaye husimamia kikundi cha kushauri katika Kanada, husema kwamba wanaume wenye kutumia jeuri juu ya wanawake huwa na maoni mabaya juu ya wanawake: “Hata wawe watoka utamaduni gani, wamelelewa kuamini kwamba wanaume ni Namba 1.” Hamish Sinclair, ambaye husimamia programu ya tiba kwa ajili ya wanaume wenye kutumia jeuri juu ya wanawake, husema kwamba wanaume wamezoezwa kuamini kwamba wao ni bora kuliko wanawake na kwamba ni haki yao “kuwaadhibu, kuwatia nidhamu au kuwaogopesha.”
Katika mabara mengi mwanamume huonwa kuwa ana haki ya kumtendea mke wake kama kitu tu, kama kisehemu kingine cha mali yake. Udhibiti na utawala wake juu ya mke wake humfanya aonwe kuwa mwanamume na aheshimiwe. Mara nyingi wake hupigwa vibaya sana na kutendwa vibaya vinginevyo, na mifumo ya kisheria haifanyi lolote hata kidogo juu ya jambo hilo kwa sababu hiyo ndiyo sheria katika mabara hayo. Mwanamume ni bora, na mwanamke ni wa chini; lazima atoe utii kamili kwake bila kujali kama yeye ni mwenye kudharaulika, mjeuri, mpotovu, au mwenye ubinafsi kadiri gani.
Morley Safer ripota wa televisheni ya CBS aliripoti juu ya nchi moja ya Amerika Kusini: “Hakuna mahali katika Latini Amerika ambapo ibada ya kujivunia nguvu za kiume huonekana wazi zaidi . . . Huienea jamii yote, kutia na mahakama ambamo katika kutetea heshima yake ya kiume aweza hata kuua kimakusudi bila hofu ya kuadhibiwa, hasa ikiwa mwenye kuuawa ni mke au kimada wake.” Alishikilia kwamba “hakuna mahali duniani ambapo wanawake huvunjiwa heshima” kama ifanywavyo katika nchi hiyo. Lakini utawala wa wanaume juu ya wanawake na kuvunjia heshima wanawake ni mambo ambayo yameenea pote. Si jambo la bara moja, hata liwe baya kadiri gani humo.
Minna Schulman, mkurugenzi wa idara ya jeuri ya nyumbani na kufikiliza sheria katika New York, alitaarifu kwamba jeuri ni chombo ambacho wanaume hutumia ili kudumisha udhibiti na kuonyesha nguvu na mamlaka yao juu ya wanawake. Aliongeza hivi: “Sisi huona jeuri ya nyumbani kuwa matumizi mabaya ya nguvu na udhibiti.”
Baadhi ya wapiga wake husumbuliwa na hali ya kutojiheshimu, tabia ileile ambayo wao hutia katika wale wapigao. Wakifanya hivyo basi kujiheshimu kwao kutatoshelezwa, nao watahisi kadiri fulani ya kuwa bora na kuwa na udhibiti juu ya binadamu mwingine. Wao huhisi kwamba wanathibitisha uanaume wao kwa njia hiyo. Hata hivyo, je, kweli wafanya hivyo? Kwa kuwa wao hufanya jeuri yao juu ya mwanamke aliye dhaifu zaidi, je, hilo lathibitisha kwamba kwelikweli wao wana nguvu, au badala ya hivyo, halithibitishi kwamba wao hawatumii akili? Je! kweli ni jambo la kiume kwa mwanamume mwenye nguvu zaidi kumpiga mwanamke dhaifu zaidi, asiye na nguvu zaidi? Mwanamume wa tabia yenye nguvu zaidi ya kiadili angeonyesha ufikirio na huruma kwa yule aliye dhaifu zaidi na asiye na nguvu zaidi, si kumtumia isivyo haki kwa manufaa yake mwenyewe.
Wonyesho mwingine wa kufikiri kusiko kwa akili kwa mtumiaji jeuri juu ya wanawake ni uhakika wa kwamba mara nyingi yeye humlaumu mke wake kwa kuchochea mapigo hayo. Huenda akadokeza, au hata akamwambia, mambo kama vile: ‘Hukufanya hili vizuri. Ndiyo sababu ninakupiga.’ Au: ‘Chakula kilichelewa, hivyo wapata tu ustahilicho.’ Katika akili ya mfanya jeuri, ni kosa la mwanamke. Hata hivyo, hakuna kosa la mwanamke linalostahilisha pigo.
Je! Kileo Huleta Tofauti?
Kwa kuwa kileo hupunguza kujidhibiti na huzidisha uwezekano wa kutenda bila kufikiri, haishangazi kwamba wengine huhisi kwamba kinaweza kutokeza utumiaji wa jeuri. Mara nyingi mtu huweza kudumisha udhibiti juu ya hisia zenye jeuri wakati amelevuka, lakini baada ya vinywaji vichache vyenye kileo, huwa mwenye kutumia jeuri. Kileo kimepunguza uwezo wake mbalimbali wa kiakili na kupunguza uwezo wake wa kudhibiti hasira.
Hata hivyo, wengine hudai kwamba tatizo hutokezwa sana-sana na mkazo wala si kileo chenyewe. Wao husema kwamba mtu atumiaye kileo ili kuuweza mkazo ni mtu wa aina ileile ambayo ingeweza kutumia jeuri kwa kusudi hilo. Hilo lamaanisha kwamba mnywaji aweza kuwa mwenye kutumia jeuri akiwa amelevuka kama vile wakati amelewa. Vyovyote iwavyo, hata sababu iwe nini kwa habari hii, hakika kileo hakisaidii kudhibiti hisia za mtu bali kwa kawaida kitafanya jambo lililo kinyume.
Jinsi Vyombo vya Habari Huathiri Vitendo vya Watu
Wengine hudai kwamba televisheni pamoja na sinema hutia moyo maoni ya kujivunia nguvu za kiume na hufundisha kwamba jeuri ni njia halali ya kushughulikia matatizo na hasira. “Mimi nilivutiwa na itikio langu mwenyewe lenye nguvu kwa sinema Rambo,” akiri mshauri mmoja wa familia. “Ingawa katika akili na hisia zangu za mtu mzima ninagutushwa na mauaji mengi ya Rambo, hisia zangu za kitoto humtia moyo aendelee kuua.”
Kwa kuwa watoto wengi wanatumia maelfu ya saa wakitazama televisheni kukiwa na vitendo visivyohesabika vya jeuri, kunajisiwa, na kuvunjiwa heshima kwa wanadamu wengine, hasa wanawake, si ajabu kwamba wengi hukua na kutenda wengine vitendo hivyohivyo vyenye kudhuru kijamii. Na si watoto peke yao wanaoathiriwa bali hata watu wazima pia.
Pia, hasa katika miaka ya karibuni, kiwango kimeongezeka sana cha vitendo vilivyo wazi sana vya jeuri, vya ukosefu wa adili kingono, na vya kuvunjia heshima wanawake kama vionyeshwavyo katika televisheni na sinema. Hakika hilo lazima lifanye tamasha ya jeuri ya nyumbani kuwa mbaya zaidi. Kama vile kikundi kimoja cha uchunguzi kilivyoona, kuna “uhusiano . . . ulio wazi kati ya kutazama televisheni na sinema na mwenendo wenye jeuri.”
Matokeo ya Upweke
Kwa wengi leo maisha hayahusishi watu wengine na ni yenye upweke. Maduka makubwa-makubwa yamechukuwa mahali pa maduka ya ujirani ambayo wenyewe walijua wateja wao kwa majina na walikuwa wenye urafiki kwao. Programu za kujenga upya majengo duni ya viungani, matatizo ya kiuchumi, na ukosefu wa kazi za kuajiriwa hulazimisha familia kuwa zenye kuhama-hama. Kadiri kubwa ya jeuri ya nyumbani huonekana miongoni mwa wale wasio na mawasiliano yenye nguvu ya kijamii.
James C. Coleman, katika kitabu chake Intimate Relationships, Marriage, and the Family, aeleza kwa nini yeye afikiri ndivyo ilivyo. Yeye ahisi kwamba kuwa mpweke hupunguza mazungumzo yenye maana na hufanya iwe vigumu kwa mtumiaji jeuri kuona hali yake ifaavyo na kutafuta msaada kutoka kwa rafiki mwenye kutumainiwa. Kwa kutokuwa na marafiki na jamaa za karibu wawezao kutenda kama nguvu ya kupunguza jeuri humwezesha mtu kuonyesha ubinafsi wake kwa urahisi zaidi, kwa kuwa kufikiri kwake kwenye makosa hakuzuiwi kila siku na wengine walio karibu naye. Ni kama vile Mithali 18:1 isemavyo: “Ajitengaye na wenzake hutafuta matakwa yake mwenyewe; hushindana na kila shauri jema.”
Msaada kwa Familia Yenye Jeuri
Tumezungumzia kisehemu tu cha maelezo yatolewayo kwa sababu za jeuri ya nyumbani. Kuna mengine. Tukiisha kutambua baadhi ya visababishi, sasa twahitaji kuchunguza utatuzi. Ikiwa mtu yumo katika familia yenye jeuri, kigezo cha jeuri chaweza kukomeshwaje? Ni nini maoni ya Biblia? Je! jeuri ya familia itakwisha wakati wowote? Makala ifuatayo kwenye ukurasa wa 10 itazungumzia maswali hayo.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]
Jeuri ya Kihisiamoyo—Kupiga Sana kwa Maneno
KATIKA jeuri ya kutumia nguvu za mwili shambulio hufanywa kwa ngumi; katika jeuri ya kihisiamoyo shambulio hufanywa kwa maneno. Tofauti pekee ni chaguo la silaha. Ni kama Mithali 12:18 isemavyo: “Kuna anenaye bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga; bali ulimi wa mwenye haki ni afya.”
Jeuri ya kihisiamoyo ni yenye hatari kadiri gani, kutia huko “kuchoma kwa upanga”? Dakt. Susan Forward aandika hivi: “Matokeo ni yaleyale [kama ya jeuri ya kutumia nguvu za mwili]. Unaogopa jinsi ileile, unahisi kuwa hoi jinsi ileile, na hupatwa na maumivu jinsi ileile,” kunena kihisiamoyo.
Jeuri ya kihisiamoyo kuelekea mwenzi wa ndoa: “Jeuri ya kindoa si ya kutumia nguvu za mwili tu. Sehemu kubwa, labda iliyo kubwa zaidi, ni ya maneno na kihisiamoyo,” akasema mwanamke mmoja aliyefanyiwa jeuri kwa muda mrefu. Jeuri hiyo huenda ikatia ndani kuita mtu majina mabaya, kupiga kelele, kuchambua daima, matukano yenye kumvunjia mtu heshima, na vitisho vya kufanyiwa jeuri ya kutumia nguvu za mwili.
Maneno yenye kuumiza ambayo humfanya mtu ajione kuwa si wa maana, yenye kushusha, au kuogopesha yaweza kufanya madhara makubwa. Kama maji yenye kutona-tona juu ya mwamba, huenda mwanzoni maneno yenye kumvunjia mtu heshima yakaonekana kuwa bila madhara. Lakini upesi hali ya mtu ya kujiheshimu huharibiwa polepole. “Kama ningelazimika kuchagua kati ya jeuri ya kutumia nguvu za mwili na ya kutumia maneno, ningependelea kupigwa wakati wowote,” akasema mwanamke mmoja. “Waweza kuona alama,” akaeleza, “hivyo angalau watu wakusikitikia. Jeuri ya kutumia maneno hukuudhi tu kupita kiasi. Makovu hayaonekani. Hakuna anayejali.”
Jeuri ya kihisiamoyo kuelekea mtoto: Huenda hiyo ikatia ndani kuchambua daima na kudharau sura, akili, uwezo wa kufanya mambo, au thamani ya mtoto akiwa mtu. Hasa maneno yenye kuumiza ni yenye kudhuru sana. Mara nyingi watoto huyaelewa maneno yenye kuumiza jinsi yalivyo, bila kupambanua kati ya yale yasemwayo kwa uzito na yale yasemwayo kwa “ucheshi.” Daktari wa tiba ya therapia Sean Hogan-Downey asema hivi: “Mtoto huhisi akiumia, lakini kila mtu anacheka, hivyo hujifunza kutotumaini hisia zake.”
Hivyo, katika visa vingi zaidi, kuna kweli katika yale ambayo mwanahistoria na mtungaji wa insha Mskotlandi Thomas Carlyle alisema wakati mmoja: “Sasa naona maneno yenye kuumiza kuwa, kwa ujumla, lugha ya Ibilisi; kwa sababu hiyo, tangu muda mrefu, nimeikataa kabisa.”
Joy Byers, mtaalamu wa kutibu watoto waliofanyiwa jeuri, asema hivi: “Jeuri ya kutumia nguvu za mwili huenda ikamuua mtoto, lakini waweza pia kuua roho [tabia na nia ya mtoto], na hivyo ndivyo kigezo cha daima cha maneno ya mzazi yenye kuvunja moyo yawezavyo kufanya.” Gazeti FLEducator hutoa maelezo haya: “Tofauti na machubuko ambayo yaweza kutambulikana na kwisha, jeuri ya kihisiamoyo hutokeza mabadiliko yasiyoonekana katika akili na utu wa mtoto ambayo hubadili kwa njia yenye kudumu hali yake ya kuona jinsi mambo yalivyo kikweli na uhusiano wake na wengine.”
[Picha katika ukurasa wa 7]
Kuona jeuri kuna matokeo yenye nguvu juu ya mwenendo wa baadaye wa mtoto
-
-
Mwisho wa Jeuri ya NyumbaniAmkeni!—1993 | Februari 8
-
-
Mwisho wa Jeuri ya Nyumbani
“Ule uzuiaji wa jeuri nyumbani na upunguzaji wa jeuri
ya familia huhusisha mabadiliko makubwa katika
muundo na kigezo cha jamii na familia pia.”—Behind Closed Doors.
UUAJI wa kimakusudi wa kwanza katika historia ya kibinadamu ulihusu ndugu wawili. (Mwanzo 4:8) Muda wote wa mileani tangu hapo, mwanadamu amesumbuliwa na namna zote za jeuri ya nyumbani. Hata ingawa utatuzi mwingi umedokezwa, mwingi una vizuizi.
Mathalani, urekebishaji tabia huwafikia wakosaji wale tu wakirio tatizo lao. Mwanamume mmoja aliyekuwa akirekebishwa tabia yake ya zoea la kumtendea mke wake kijeuri aliomboleza hivi: “Kwa kila mmoja wetu [sisi wenye kurekebishwa tabia], kuna wanaume watatu huko nje wasemao, ‘yakupasa umdhibiti mke.’” Hivyo mtenda kijeuri huhitaji kujifunza kushughulika na hali yake mwenyewe. Ni kwa nini amekuwa mtenda kijeuri? Kwa kupata msaada ili kusahihisha makosa yake, huenda hatimaye akashinda tatizo hilo.
Lakini programu za kijamii zina wafanyakazi wachache mno. Hivyo, inakadiriwa kwamba katika asilimia 90 ya visa vya kuua kimakusudi watoto katika United States, hali yenye hatari ya familia ilikuwa imeripotiwa kabla ya mauaji kutukia. Kwa sababu hiyo, programu za kijamii na mashirika ya polisi yaweza kufanya machache tu. Kuna jambo jingine lihitajiwalo sana.
“Utu Mpya”
“Linalohitajiwa si jingine ila kubadili muundo na kigezo cha mahusiano kati ya washiriki wa familia,” chasema kikundi kimoja cha uchunguzi. Jeuri ya nyumbani si tatizo tu la kutumia ngumi; sana-sana ni tatizo la akili. Hutokana na jinsi washiriki wa familia—mwenzi wa ndoa, mtoto, mzazi, ndugu au dada—huwaona wenzao. Kubadili mahusiano hayo humaanisha kuvaa kile ambacho Biblia hukiita “utu mpya.”—Waefeso 4:22-24; Wakolosai 3:8-10.
Acheni tuchunguze baadhi ya kanuni za Biblia zinazohusu familia ambazo hutusaidia kuvaa ule utu mpya kama ule wa Kristo uwezao kuleta uhusiano bora miongoni mwa washiriki wa familia.—Ona Mathayo 11:28-30.
Maoni juu ya watoto: Mengi zaidi yahusika katika kuwa mzazi kuliko tu kuzaa mtoto. Ingawa hivyo, kwa kuhuzunisha wengi leo huona watoto wao kuwa mzigo wenye kulemea na kwa hiyo hukosa kujiona kuwa na sharti katika daraka lao la kuwa mzazi. Hao ndio wawezao kuwatendea watoto kijeuri.
Biblia huita watoto “urithi wa BWANA [Yehova, NW]” na “thawabu.” (Zaburi 127:3) Wazazi wana daraka mbele za Muumba la kutunza urithi huo. Wale waonao watoto kuwa mzigo wenye kulemea wahitaji kusitawisha utu mpya kuhusiana na jambo hilo.a
Matarajio yenye akili juu ya watoto: Uchunguzi mmoja ulifunua kwamba akina mama wengi wenye kuwatendea watoto kijeuri hutarajia vitoto vitofautishe mema na mabaya kufikia wakati mtoto ana umri wa mwaka mmoja. Theluthi moja ya waliochunguzwa walitaja waziwazi miezi sita.
Biblia huonyesha kwamba kila mtu huzaliwa akiwa si mkamilifu. (Zaburi 51:5; Warumi 5:12) Haidai kwamba utambuzi hupatikana wakati wa kuzaliwa. Badala ya hivyo, inasema kwamba “kwa kutumiwa,” uwezo wa mtu wa utambuzi ‘huzoezwa kupambanua mema na mabaya.’ (Waebrania 5:14) Na zaidi, Biblia hunena juu ya “mambo ya kitoto,” “ujinga” wa utoto, na “ubatili” wa ujana. (1 Wakorintho 13:11; Mithali 22:15; Mhubiri 11:10) Lazima wazazi waelewe vizuizi hivyo, wasitarajie mengi zaidi ya yafaayo umri na uwezo wa mtoto.
Kuwatia watoto nidhamu: Katika Biblia neno la Kigiriki litafsiriwalo “nidhamu” humaanisha “elimisha.” Kwa hiyo, kwanza kabisa, mradi wa nidhamu si kusababisha uchungu, bali kuzoeza. Mengi yayo yaweza kutimizwa bila kuchapa, ingawa huenda hilo likahitajiwa nyakati fulani. (Mithali 13:24) Biblia husema: “Sikieni mafundisho [nidhamu, NW], mpate hekima, wala msiikatae.” (Mithali 8:33) Vilevile, Paulo aliandika kwamba mtu apaswa kujiweka mwenyewe katika hali ya ‘kutokuwa mgomvi.’ akitoa karipio kwa ‘uvumilivu.’ (2 Timotheo 2:24; 4:2) Hilo hukataza mifoko ya hasira na kutumia nguvu kupita kiasi hata wakati kuchapa kunapohitajiwa.
Kwa kufikiria kanuni hizo za Biblia, jiulize hivi: ‘Je! nidhamu yangu hufundisha, au hudhibiti tu kwa kuumiza? Je! nidhamu yangu hukaza ndani ya moyo kanuni zifaazo au hofu tu?’
Mipaka ya tabia kwa Watu Wazima: Mtendea mke kijeuri mmoja alidai kwamba alikuwa tu “ameshindwa kujidhibiti” akampiga mke wake. Mshauri alimuuliza mwanamume huyo kama amepata kamwe kumdunga kisu mke wake. “Singeweza kamwe kufanya hivyo!” mwanamume huyo akajibu. Mwanamume huyo alisaidiwa kuona kwamba alikuwa akitenda ndani ya mipaka fulani aliyojiwekea, lakini tatizo lilikuwa kwamba haikuwa mipaka ifaayo.
Mipaka yako imewekwa wapi? Je! wewe huacha kabla ya kutopatana kusitawi na kuwa jambo la kijeuri? Au wewe hupandwa na hasira na hatimaye kuanza kupiga kelele, kutumia matusi, kusukuma, kurusha vitu, au kumpiga mwenzi?
Ule utu mpya una mipaka yenye masharti makali, imewekwa kwa njia isiyoruhusu kutumia jeuri ya kiakili au ya kutumia nguvu za mwili. “Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu,” yasema Waefeso 4:29. Mstari wa 31 huongeza hivi: “Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya.” Neno la Kigiriki litafsiriwalo “ghadhabu” huonyesha “asili itendayo bila kufikiri.” Kwa kupendeza, kitabu Toxic Parents husema kwamba tabia ya kawaida miongoni mwa wenye kuwatendea watoto kijeuri ni “ukosefu mbaya sana wa kudhibiti hali ya kutenda bila kufikiri.” Utu mpya huweka mipaka imara juu ya kutenda bila kufikiri, kimwili na kwa maneno.
Bila shaka, utu mpya hutumika kwa wake na kwa waume pia. Mke apaswa kufanyia kazi kutomchokoza mwenzi wake wa ndoa, akionyesha uthamini kwa jitihada zake za kutunza familia, akishirikiana na mume wake. Na wote wawili wapaswa kutotaka kutoka kwa mwingine kile ambacho hakuna yeyote wao awezaye kutokeza—ukamilifu. Badala ya hivyo, wote wawili wapaswa kutumia 1 Petro 4:8: “Zaidi ya yote iweni na juhudi nyingi katika kupendana; kwa sababu upendano husitiri wingi wa dhambi.”
Kuwastahi wenye umri mkubwa: “Onyesha staha kwa watu wazee na kuwaheshimu,” yasema Mambo ya Walawi 19:32. (Today’s English Version) Huenda hilo likawa tatizo wakati mzazi mwenye umri mkubwa awapo mgonjwa na labda mwenye kudai mengi mno. Timotheo wa Kwanza 5:3, 4 hunena juu ya kuwapa ‘heshima’ na “kuwalipa” wazazi. Hilo laweza kutia ndani maandalizi ya kifedha na staha pia. Kwa kufikiria yale yote ambayo wazazi wetu walitufanyia tulipokuwa vitoto vilivyo hoi, twapaswa kuwapa ufikirio kama huo uhitajiwapo.
Shinda ushindani wa ndugu na dada: Kabla ya uhasama wa Kaini kumwongoza katika kumuua ndugu yake Abeli, alishauriwa hivi: “Dhambi inakuotea mlangoni pako. Inataka kukutawala, lakini lazima uishinde.” (Mwanzo 4:7, TEV) Hisia zaweza kudhibitiwa. Jifunzeni kuwa na subira kuelekeana, “Mkichukuliana kwa ukarimu kwa sababu mwapendana.”—Waefeso 4:2, Phillips.
Kujifunza Kumtobolea Rafiki Siri
Wengi watendewao kijeuri nyumbani hawamwambii yeyote juu ya jeuri hiyo. Lakini Dakt. John Wright ahimiza hivi: “Wanawake wapigwao na wenzao wa ndoa wapaswa kutafuta ulinzi wa kihisiamoyo na wa kimwili kutoka kwa mtu mwingine.” Na ndivyo ilivyo kwa habari ya mshiriki yeyote wa familia atendewaye kijeuri.
Nyakati nyingine atendewaye kijeuri huona vigumu kumtobolea siri mtu mwingine. Kwa vyovyote vile, utumainifu ndani ya kikundi cha kijamii cha karibu zaidi—familia—umetokeza maumivu. Hata hivyo, “Yuko rafiki aambatanaye na mtu kuliko ndugu,” yasema Mithali 18:24. Kupata rafiki huyo na kujifunza kumtobolea siri kwa busara ni hatua ya maana katika kupata usaidizi uhitajiwao. Bila shaka, mtendaji kijeuri ahitaji msaada pia.
Kila mwaka mamia ya maelfu ya watu huwa Mashahidi wa Yehova. Hao hukubali kushinda ugumu wa kuvaa ule utu mpya. Miongoni mwao wamo wale waliokuwa hapo zamani watendaji wa jeuri ya nyumbani. Ili kupinga mwelekeo wowote wa kurudia, lazima waendelee kuruhusu Biblia ‘iwafae kwa mafundisho, kwa kuwaonya makosa yao, na kwa kuwaongoza.’—2 Timotheo 3:16.
Kwa hao Mashahidi wapya, kuvaa utu mpya ni tendo lenye kuendelea, kwa maana Wakolosai 3:10 husema ‘unafanywa mpya.’ Kwa hiyo jitihada yenye kuendelea yahitajiwa. Shukrani ni kwamba, Mashahidi wa Yehova wana utegemezo wa ‘ndugu na dada na akina mama na watoto’ wengi wa kiroho.—Marko 10:29, 30; ona pia Waebrania 10:24, 25.
Halafu, pia, katika makundi yote yapatayo 70,000 ya Mashahidi wa Yehova ulimwenguni kote, mna waangalizi wenye upendo ambao ni kama “mahali pa kujificha na upepo, na mahali pa kujisitiri na dhoruba.” “Macho na masikio yao yatafunguliwa kuona mahitaji ya watu.” (Isaya 32:2, 3, TEV) Kwa hiyo Mashahidi wa Yehova wapya, na pia wale wa zamani, wana chemchemi nzuri ya msaada upatikanao katika kundi la Kikristo wafanyiapo kazi kuvaa utu mpya.
Waangalizi Wenye Huruma
Watu wawajiapo waangalizi Wakristo katika makundi ya Mashahidi wa Yehova ili wapate shauri, waangalizi hao wamezoezwa kuwasikiliza wote bila upendeleo. Wao hutiwa moyo waonyeshe kila mmoja huruma kubwa na uelewevu, hasa watendewao kijeuri vibaya sana.—Wakolosai 3:12; 1 Wathesalonike 5:14.
Mathalani, mke mwenye kupigwa huenda akawa aliumizwa kinyama. Katika mabara mengi leo, kama mtu mwingine nje ya familia angalipigwa jinsi hiyohiyo, mtendeaji kijeuri huyo angalitiwa gerezani hatimaye. Hivyo mtendewa kijeuri ahitaji kutendewa kwa fadhili isiyo ya kawaida, kama watendewavyo watendewa kijeuri wa aina nyingine zozote, kama vile kutendewa kijeuri kingono.
Zaidi ya hilo, wahalifu dhidi ya sheria za Mungu wahitaji kuadhibiwa. Kwa njia hiyo kundi linawekwa likiwa safi, na watu wengine wasio na hatia wanalindwa. Na la maana zaidi, utiririkaji wa roho ya Mungu hauzuiwi.—1 Wakorintho 5:1-7; Wagalatia 5:9.
Maoni ya Mungu Juu ya Ndoa
Watu wanapokuwa Mashahidi wa Yehova, wao hukubali kufuata kanuni za maisha ya Kikristo zipatikanazo katika Neno la Mungu. Wanajifunza kwamba mwanamume alikusudiwa kuwa kichwa cha familia, kuiongoza katika ibada ya kweli. (Waefeso 5:22) Lakini ukichwa haumpi mamlaka kamwe ya kumpiga kinyama mke wake, akiponda utu wake, au kupuuza matakwa yake.
Tofauti na hivyo Neno la Mungu huelewesha wazi kwamba waume wapaswa ‘kuwapenda wake zao, kama naye Kristo alivyolipenda Kanisa akajitoa kwa ajili yake. Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza.’ (Waefeso 5:25, 28, 29) Kwelikweli, Neno la Mungu husema waziwazi kwamba wake wapaswa kupewa “heshima.”—1 Petro 3:7; ona pia Warumi 12:3, 10; Wafilipi 2:3, 4.
Hakika hakuna mume Mkristo awezaye kutoa hoja kwa kweli kwamba ampenda mke wake kikweli au amheshimu ikiwa yeye humtendea kijeuri kwa maneno au kwa kutumia nguvu za mwili. Huo ungekuwa unafiki, kwa maana Neno la Mungu hutaarifu hivi: “Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao.” (Wakolosai 3:19) Hivi karibuni, hukumu za Mungu zijapo dhidi ya mfumo huu mbovu kwenye Har–Magedoni, wanafiki watapatwa na hukumu ileile itakayowapata wapinzani wa utawala wa Mungu.—Mathayo 24:51.
Mume mwenye kumhofu Mungu apaswa kumpenda mke wake kama mwili wake mwenyewe. Je! angepiga mwili wake mwenyewe, ajipige ngumi usoni, au avute nywele zake mwenyewe kijeuri? Je! angejivunjia heshima kwa dharau na kwa maneno machungu mbele ya wengine? Anayefanya mambo kama hayo hakika angefikiriwa kuwa hana akili timamu.
Mwanamume Mkristo akimpiga mke wake, hilo hubatilisha kazi nyingine zote za Kikristo machoni pa Mungu. Kumbuka, “mpiga watu” hastahili kuwa na mapendeleo katika kundi la Kikristo. (1 Timotheo 3:3; 1 Wakorintho 13:1-3) Bila shaka, mke yeyote amtendeaye mume wake vivyo hivyo anahalifu sheria za Mungu pia.
Wagalatia 5:19-21 huweka miongoni mwa kazi zishutumiwazo na Mungu “uadui, ugomvi, hasira,” na kutaarifu kwamba “watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.” Hivyo, si haki kamwe kumpiga mwenzi wa ndoa au watoto. Kwa kawaida jambo hilo hupingana na sheria ya nchi na hakika lapingana na sheria ya Mungu.
Mnara wa Mlinzi, gazeti litangazwalo na Mashahidi wa Yehova, limetoa maoni ya Kimaandiko juu ya jambo hilo, likisema hivi juu ya wale wadaio kuwa Wakristo na bado ni wapigaji wake: “Mtu ye yote ajiitaye Mkristo, anayehamaki-hamaki bila kutubu aweza kutengwa na ushirika,” aondoshwe.—Januari 15, 1978, ukurasa 22; linganisha 2 Yohana 9, 10.
Linaloruhusiwa na Sheria ya Mungu
Mwishoni kabisa Mungu atahukumu wale wahalifuo sheria zake. Lakini kwa sasa, Neno lake hufanya uandalizi gani kwa wale wenzi wa ndoa Wakristo ambao wamepigwa vibaya sana na hali mtendaji kijeuri habadiliki lakini huendelea na kumpiga vibaya mke wake? Je! Watendewao kijeuri wasio na hatia wawajibika kuendelea kuhatirisha afya yao ya kimwili, ya kiakili, na ya kiroho, labda hata uhai wao?
Mnara wa Mlinzi, ukitoa maelezo juu ya jeuri ya nyumbani, husema jambo ambalo Neno la Mungu huruhusu. Linataarifu hivi: “Mtume Paulo hushauri hivi: ‘Mke asiachane na mumewe; lakini, ikiwa ameachana naye, na akae asiolewe, au apatane na mumewe; tena mume asimwache mkewe.’” Makala hiyo husema zaidi hivi: “Ikitukia kwamba kutendwa vibaya kunakuwa kusikovumilika, au uhai wenyewe wahatirishwa, mwenzi wa ndoa aaminiye aweza kuchagua ‘kumwacha mumewe.’ Lakini jitihada yapasa kuwa ‘kupatana tena’ baada ya wakati. (1 Wakorintho 7:10-16) Walakini, ‘kuachana’ kwenyewe hakuandai msingi wa Kimaandiko wa talaka na kufunga ndoa tena; hata hivyo, talaka au kutengana kisheria kwaweza kuandaa kadiri fulani ya ulinzi kutokana na kutendewa vibaya zaidi.”—Machi 15, 1983 (Kiingereza), kurasa 28-9; ona pia toleo la Novemba 1, 1988, kurasa 22-3.
Lile ambalo mtendewa kijeuri achagualo kufanya katika hali hizo lazima liwe uamuzi wa kibinafsi. “Kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe.” (Wagalatia 6:5) Hakuna mwingine yeyote awezaye kufanyia mke uamuzi kama huo. Na hakuna mwingine yeyote apaswaye kujaribu kumsonga arudi kwa mume mtendaji kijeuri ambapo afya, uhai, na hali yake ya kiroho vinahatirishwa. Huo lazima uwe uchaguzi wake mwenyewe, wa hiari yake mwenyewe, si kwa sababu wengine wanajaribu kumtwika nia yao.—Ona Filemoni 14.
Mwisho wa Jeuri ya Nyumbani
Mashahidi wa Yehova wamejifunza kwamba jeuri ya nyumbani ni mfano wa yaliyotabiriwa na Biblia kwa hizi siku za mwisho, ambazo katika hizo wengi wangekuwa “wenye kutendea vibaya,” “wasio na shauku ya kiasili,” “wakali.” (2 Timotheo 3:2, 3, The New English Bible) Mungu huahidi kwamba kufuatia hizi siku za mwisho, yeye ataleta ulimwengu mpya wenye amani ambao katika huo watu “watakaa salama salimini, wala hapana atakayewatia hofu.”—Ezekieli 34:28.
Katika ulimwengu huo mpya wa ajabu, jeuri ya nyumbani itakuwa milele jambo la wakati uliopita. “Wapole watairithi nchi, watajifurahisha kwa wingi wa amani.”—Zaburi 37:11.
Twakuhimiza ujifunze zaidi juu ya ahadi za Biblia kwa ajili ya wakati ujao. Kwelikweli, waweza kuvuna manufaa hata sasa kwa kutumia kanuni za Biblia katika mazingira ya familia yako.
-