Nusu Karne Chini ya Utawala wa Kiimla
Kama ilivyosimuliwa na Lembit Toom
Katika mwaka wa 1951, nilihukumiwa kifungo cha miaka kumi cha kazi ngumu katika Siberia. Tulisafirishwa maelfu ya kilometa hadi kwenye kambi iliyokuwa mbali zaidi ya Mzingo wa Aktiki. Kazi ilikuwa yenye kuchosha, halihewa ilikuwa mbaya sana, na hali za maisha zilikuwa mbaya ajabu. Acheni nieleze jinsi ambavyo nilijikuta huko na kwa nini kuteseka kwetu hakukuwa bure.
BABA yangu alionwa kuwa msomi katika Estonia, nchi ya Baltiki nilikozaliwa Machi 10, 1924. Ingawa hivyo, katika miaka yake ya baadaye, alilima shamba la familia huko Järvamaa sehemu ya kati ya Estonia. Familia yetu kubwa ya Kilutheri ilikuwa na watoto tisa na mimi nlikuwa kitindamimba. Baba yangu alikufa nilipokuwa na umri wa miaka 13. Mwaka uliofuata nilihitimu kutoka shule ya msingi. Mnamo Septemba 1939, Vita ya Ulimwengu ya Pili ilipozuka, kaka yangu Erich aliitwa kutumikia jeshini, na sikuweza kuendelea na masomo yangu. Kisha, katika mwaka wa 1940, Estonia ilifanywa kuwa sehemu ya Muungano wa Sovieti, na mwaka mmoja baadaye Wajerumani waliitwaa Estonia. Walimtia Erich gerezani lakini akaachiliwa na kurudi Estonia mnamo Agosti 1941. Mnamo 1942, niliweza kuhudhuria shule ya kilimo.
Nilipokuwa nimetembea nyumbani kutoka shuleni kwa ajili ya Krismasi mwaka wa 1943 dada yangu Leida alinitajia kwamba daktari aliyekuwa akitibu familia yetu alizungumza naye kuhusu Biblia. Alikuwa amempa vijitabu fulani vilivyochapishwa na Watch Tower Bible and Tract Society. Nilivisoma na upesi nikamtafuta Dakt. Artur Indus, ambaye baadaye alijifunza Biblia pamoja nami.
Nalazimika Kuamua
Wakati huo, vita kati ya Ujerumani na Muungano wa Sovieti ilipamba moto. Kufikia Februari 1944, Warusi walikuwa wamesonga na kukaribia mpaka wa Estonia. Erich aliitwa kwenye jeshi la Ujerumani, pia mimi nikapokea hati za kujiandikisha. Niliamini kwamba Mungu hukataza kuua binadamu wenzetu, na Dakt. Indus alisema kwamba angenisaidia kutafuta nahapi pa kujificha hadi vita iishe.
Siku moja konstebo mmoja na kiongozi wa kikundi cha hapa cha ulinzi wa raia waliwasili shambani kwetu. Walikuwa wamepewa amri ya kunikamata kwa kushukiwa kwamba nilikuwa nikijaribu kukwepa utumishi wa kijeshi. Wakati huo nilijua kwamba ningehitaji kutoroka nyumbani la sivyo nifungwe kwenye kambi ya mateso ya Ujerumani.
Nilipata kimbilio kwenye shamba la mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Ili niimarishe imani yangu nilipokuwa mafichoni, nilisoma Biblia sana na vichapo vingi vya Watch Tower Society kwa kadiri nilivyoweza. Usiku mmoja nilinyemelea na kurudi nyumbani ili kuchukua kiasi fulani cha chakula. Nyumba ilijaa askari-jeshi Wajerumani, kwa kuwa ndugu yangu Erich alikuwa amerudi na baadhi ya marafiki wake kwa likizo ya siku chache. Niliweza kuzungumza na Erich kisiri kwenye sakafu ya kupuria usiku huo. Ilikuwa mara ya mwisho niliyopata kumwona. Kuponea Chupuchupu Usiku huohuo, baada ya kurudi kwenye shamba hilo nilipokuwa nimejificha, shamba hilo lilivamiwa. Konstebo wa mahali hapo na wanaume kutoka kikundi cha ulinzi wa raia walikuwa wakifanya uchunguzi kufuatia ripoti kwamba mtu fulani alikuwa akijificha kwenye shamba hilo. Niliponyoka na kuingia ndani ya nafasi ya kutambaa chini ya sakafu, na kwa muda mfupi nilisikia sauti ya njumu juu ya kichwa changu. Akimtisha mkulima kwa bunduki, ofisa huyo alipaza sauti: “Kuna mtu anayejificha ndani ya nyumba hii! Tunaweza kuingiaje ndani ya nafasi ya kutambaa chini ya sakafu?” Ningeweza kuona mwali wa mwanga ukizunguka-zunguka kutoka kwenye tochi zao. Nilijongea nyuma kidogo na kulala hapo na kusubiri. Walipoondoka, nilikaa kwenye nafasi ya kutambaa kwa muda fulani ili kuhakikisha kwamba hatari ilikuwa imekwisha.
Kabla hakujapambazuka niliondoka katika nyumba hiyo, nikimshukuru Yehova kwamba sikupatikana. Ndugu Wakristo walinisaidia kupata maficho mengine, ambapo nilikaa mpaka mwisho wa umiliki wa Wajerumani. Baadaye nilipata habari kwamba konstebo huyo na kiongozi wa mahali hapo wa kikundi cha ulinzi wa raia walikuwa wameuawa, yaelekea na wazalendo wa Urusi. Mnamo Juni 19, 1944, nilidhihirisha wakfu wangu kwa Mungu kwa ubatizo wa maji, na dada yangu Leida pia akawa mmoja wa Mashahidi wa Yehova.
Mnamo Juni 1944 Wasovieti waliiteka tena Estonia, na miezi michache baadaye, nilikuwa huru kurudi nyumbani ili kusaidia katika kazi za shambani. Lakini katika Novemba, muda mfupi baada ya kurudi, niliamriwa nipige ripoti kwenye jeshi la Urusi. Nikiwa na ushujaa mwingi, nilihubiria kamati ya kuandikisha askari kwa ujasiri. Waliniambia kwamba mfumo wa Sovieti haukupendezwa na itikadi zangu na kwamba lazima kila mtu atumikie jeshini. Hata hivyo, kwa muda wote ambao vita iliendelea, niliweza kubaki huru, na nikajitoa kusaidia kuandaa fasihi za Biblia kwa Mashahidi wenzangu.
Utendaji Baada ya Vita
Vita ilipoisha mwezi wa Mei 1945 na msamaha ukatolewa kwa wenye kukataa vita kwa sababu ya dhamiri zao, nilirudi shuleni. Kufikia mwanzoni mwa mwaka wa 1946, nilikata kauli kwamba singeweza kutegemea ukulima katika Estonia, kwa kuwa mfumo wa Sovieti wa ujamaa ulikuwa umechukua mahali pa sekta ya kibinafsi. Hivyo, niliacha shule na kuanza kushiriki kikamili katika kazi ya kuhubiri Ufalme.
Chini ya utawala wa Sovieti, huduma yetu haingeweza kuendelezwa peupe. Kwa kweli, mawasiliano na Watch Tower Society yalikuwa yamekatishwa wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili. Kwa hiyo, nikiwa na mashine nzee ya kurudufu, nilisaidia kutoa nakala za fasihi ambazo tulikuwa tumehifadhi. Pia tulijitahidi vilivyo kufanya mikutano ya kutaniko.
Kunyanyaswa kwa Mashahidi wa Yehova na KGB (Halmashauri ya Usalama wa Kitaifa ya Sovieti) kulianza Agosti 1948. Watano miongoni mwa wale waliokuwa wakisimamia kazi walikamatwa na kutiwa gerezani, na upesi ikawa dhahiri kwamba wapelelezi wa KGB walitaka kukamata kila mtu. Halmashauri ya watu wanne kati yetu iliundwa ili kupanga kazi ya kuhubiri, kuwatia moyo ndugu zetu Wakristo, na kusaidia walio gerezani. Kwa kuwa nilikuwa na uhuru wa kiasi fulani wa kusafiri, nilitumiwa kuwasiliana na Mashahidi wenzetu.
Hati rasmi ya kuteta ya Septemba 22, 1948, ilipelekwa kwa maofisa wa Sovieti katika Estonia. Ilifafanua tengenezo letu na kusudi la kazi yetu, na ikadai waamini wenzetu waliofungwa gerezani waachiliwe. Itikio lilikuwaje? Kukamatwa zaidi. Mnamo Desemba 16, 1948, tulipeleka hati nyingine ya kuteta kwa Baraza Kuu la Kimahakama la Estonia SSR tukidai ndugu zetu wafunguliwe. Nakala za hati hii na maombi mengineyo yangali kwenye faili katika hifadhi za nyaraka za jiji la Tallinn. Ilikuwa hatari kusafiri, kwa kuwa hatungeweza kupata hati zinazofaa. Na bado, tulizuru makutaniko katika Aravete, Otepää, Tallinn, Tartu, na Võru kwa kutumia pikipiki yenye injini kubwa iliyo na gari lililojengwa kando iliyokuwa imenunuliwa kutoka kwa ofisa Mrusi. Tulipenda kuiita Gari.
Twateta Dhidi ya Stalin
Mnamo Juni 1, 1949, ombi jingine lilipelekwa kwa mamlaka kuu zaidi ya Jamhuri ya Kisoshalisti ya Estonia na vilevile kwa Nikolay Shvernik, mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Sovieti ya USSR. Hati hii, ambayo nakala yake ilipatikana kutoka kwa hifadhi za nyaraka za Tallinn, ina muhuri wa Nikolay Shvernik, unaoonyesha kwamba aliipokea na kupeleka nakala kwa Joseph Stalin, kiongozi wa serikali ya Muungano wa Sovieti. Sehemu ya mwisho ya ombi hilo inasema hivi
“Tunadai kwamba Mashahidi wa Yehova waachiliwe huru kutoka gerezani na kwamba mnyanyaso dhidi yao ukomeshwe. Tengenezo la Yehova Mungu, kupitia kwa Watchtower Bible and Tract Society, lapasa kuruhusiwa kuhubiri, bila kupingwa, habari njema za Ufalme wa Yehova kwa wakazi wote wa Muungano wa Sovieti; kama sivyo, Yehova ataangamiza kabisa Muungano wa Sovieti na Chama cha Kikomunisti.
Tunadai jambo hili kwa jina la Yehova Mungu na Mfalme wa Ufalme wake, Yesu Kristo, na pia kwa jina la waamini wote waliotiwa gerezani.
“Imetiwa sahihi: Mashahidi wa Yehova katika Estonia (Juni 1, 1949).”
Mnyanyaso Wapamba Moto
Mapema mwaka wa 1950, tulipokea matoleo matatu ya Mnara wa Mlinzi kutoka kwa mtu fulani aliyekuwa akirudi kutoka Ujerumani. Kusudi ndugu zetu wote Wakristo wafaidike na chakula hiki cha kiroho, iliamuliwa kwamba tungepanga kuwe na kusanyiko mnamo Julai 24, 1950, katika ghala ya nyasi kavu ya mwanafunzi mmoja wa Biblia karibu na kijiji cha Otepää. Hata hivyo, kwa njia fulani, wapelelezi wa KGB walipata habari kuhusu mipango yetu, na wakapanga kukamata watu wengi sana.
Lori mbili zilizojaa askari-jeshi zilisimamishwa kwenye kituo cha reli katika Palupera, mahali ambapo akina ndugu wangeshukia. Kwa kuongezea, askari-jeshi aliyekuwa na redio ya kuwasiliana alisimama akisubiri kandokando ya barabara ya Otepää/Palupera, mwendo mfupi kutoka sehemu ambayo kusanyiko lingefanyiwa. Ndugu fulani tuliokuwa tukitazamia wawasili mapema walipokosa kufika kwa wakati, tulishuku kwamba mipango yetu ilikuwa imegunduliwa.
Nilimchukua Shahidi mwenzi Ella Kikas na kuendesha pikipiki kasi hadi kwenye kituo cha garimoshi kilicho vituo viwili kabla ya kufika Palupera. Garimoshi lilikuwa limewasili tu, hivyo mimi na Ella tulilipanda kutoka miisho yote miwili na kukimbia ndani ya mabehewa tukipaza sauti ili wote washuke. Mashahidi waliposhuka, tulifanya mipango ya kuwa na kusanyiko letu katika ghala nyingine siku iliyofuata. Hivyo mpango wa wapelelezi wa KGB wa kuwakamata Mashahidi wengi sana ulitibuka. Hata hivyo, miezi miwili baada ya kusanyiko hilo, Mashahidi walianza kukamatwa kwa wingi. Nilikamatwa ili kuhojiwa mnamo Septemba 22, 1950, na pia wale watatu waliokuwa katika halmashauri iliyosimamia kazi ya kuhubiri katika Estonia. Tulitiwa katika gereza la wapelelezi wa KGB kwa miezi minane katika Tallinn kwenye Barabara ya Pagari. Baadaye, tulihamishwa hadi gereza kuu lililoko Barabara ya Kalda, ambalo liliitwa Betri. Tulizuiliwa humo kwa miezi mitatu. Kwa kulinganishwa na gereza la wapelelezi wa KGB ambapo tulikuwa tumewekwa ndani ya shimo lililo chini ya nyumba, hili la Bahari ya Baltiki lilikuwa kama mahali pa mapumziko.
Maisha Magumu Katika Siberia
Baadaye kidogo, nilihukumiwa miaka kumi ndani ya kambi katika Noril’sk iliyo mbali sana, Siberia, pamoja na Harri Ennika, Aleksander Härm, Albert Kose, na Leonhard Kriibi. Huko jua halishuki kwa miezi miwili wakati wa kiangazi, na wakati wa kipupwe halichomozi kwa miezi kwa miezi miwili.
Mwezi wa Agosti 1951, tulianza mkondo wa kwanza wa safari yetu kutoka Tallinn hadi Noril’sk kwa garimoshi. Tulisafiri kilometa zipatazo 6,000, kwa kutumia njia ya Pskov, St. Petersburg (zamani ilikuwa Leningrad), Perm’, Yekaterinburg (zamani ilikuwa Sverdlovsk), Novosibirsk, na Krasnoyarsk, kwenye Mto Yenisey. Hatimaye, mapema mwezi wa Oktoba, tulipanda tishali huko Krasnoyarsk na kuvutwa kuelekea kaskazini zaidi ya kilometa 1,600. Majuma mawili baadaye tulifika mji wa Dudinka, juu kabisa ya Mzingo wa Aktiki. Huko Dudinka tuliingia garimoshi tena ili kuendelea na mkondo wa kilometa 120 wa safari ya kuelekea Noril’sk. Kutoka kituo cha Noril’sk, tulitembea kilometa 15 zilizobakia kuelekea kambi ya kazi nje ya mji juu ya barafu nyingi.
Kwa kuwa mavazi yangu ya kujikinga baridi yalikuwa yameibwa tulipokuwa kwenye tishali, nilikuwa tu na koti la majira ya kiangazi la kuvaa juu ya nguo nyingine, chepeo, na makubazi. Tulikuwa tumedhoofishwa na safari ya majuma mengi kutoka Tallinn, na hatukuwa tumepewa chakula chetu cha kila siku ambacho kilikuwa kiasi kidogo. Kwa hiyo wafungwa fulani walizirai. Tuliwasaidia mpaka farasi walipoletwa, na kisha tukawapandisha kwenye sleji zinazokokotwa na farasi.
Tulipowasili kwenye kambi, tuliandikishwa, tukapelekwa kwenye bafu ya mvuke, na kupewa kiasi chetu cha chakula cha siku hiyo. Kambi zilikuwa na joto, na upesi nikalala usingizi mzito. Hata hivyo, katikati ya usiku, niliamka nikiwa na maumivu makali yaliyosababishwa na uvimbe katika masikio yangu. Ilipofika asubuhi nilitibiwa na kukubaliwa nisifanye kazi. Lakini maofisa wa gereza walikasirika kwa kuwa singeweza kufanya kazi na hivyo wakanichapa. Niliwekwa kwenye kifungo cha upweke kwa mwezi mmoja, kwa kuwa walisema kwamba nilikuwa “nikivuruga amani kambini.” Kwa shukrani, dawa kutoka kwenye zahanati ziliandaliwa, na muda niliotumia nikiwa peke yangu ulinipa fursa ya kurudia afya yangu.
Majira ya kwanza ya kipupwe kwenye kambi yalitokeza magumu mengi zaidi. Kazi, ambayo mara nyingi tuliifanya katika machimbo ya nikeli, ilikuwa yenye kuchosha, na chakula kidogo tulichopokea kilikuwa duni. Wengi walipoonyesha dalili za kiseyeye, tulidungwa sindano zenye vitamini C ili kutuliza maradhi hayo. Hata hivyo, kwa kufurahisha, tulikutana na Mashahidi wenzetu katika kambi, waliotoka Moldova, Poland, na Ukrainia.
Mabadiliko Katika Maisha Gerezani
Katika masika ya mwaka wa 1952, wafungwa walianza kupokea mshahara mdogo, ulioturuhusu kununua chakula ili kuongezea mlo wetu. Pia, Mashahidi fulani walianza kupokea chakula ndani ya masanduku ambayo sehemu za chini zilikuwa bandia na ambapo fasihi za Biblia zilifichwa humo. Wakati mmoja Shahidi kutoka Moldova alipokea mkebe wa chakula kilichotiwa mafuta ya nguruwe. Chakula hicho kilipokuwa kinaliwa, bitana ya utumbo wa nguruwe ilitokea. Ndani yake kulikuwa na matoleo matatu ya Mnara wa Mlinzi!
Stalin alipokufa, Machi 5, 1953, maisha gerezani yalibadilika kwa njia yenye kutazamisha. Mwanzoni, migomo na maasi vilizuka huku wafungwa wakidai waachiliwe. Vikosi vya wanajeshi vilitumwa vije kukandamiza mambo haya. Katika Noril’sk, wafungwa 120 waliuawa katika maasi; lakini Mashahidi hawakuhusika, na hakuna mmoja wao aliyeuawa wala kujeruhiwa. Katika kiangazi cha mwaka wa 1953, kazi katika machimbo ya nikeli ilikoma kwa majuma mawili. Baadaye, maisha ya gerezani yakawa nafuu. Wafungwa fulani waliachiliwa huru, na wengine wakapunguziwa vifungo vyao.
Shahidi Mwaminifu
Baada ya wakati huu wa msukosuko katika kambi, nilihamishwa katika kambi iliyo upande wa kusini karibu na jiji la Tayshet, katika mkoa wa Irkutsk. Huko nilikutana na Artur Indus, ambaye hapo mwanzoni alijifunza Biblia pamoja nami. Alikuwa amekataa kufanya kazi ya udaktari kambini, badala yake akakubali kazi yenye kuhitaji nguvu za kimwili zaidi. Alieleza: “Dhamiri yangu haikuniruhusu niidhinishe likizo ya ugonjwa kwa wafungwa wenye afya waliokuwa wamepewa nyadhifa za madaraka, huku walio wagonjwa kikweli wakilazimishwa kufanya kazi.”
Wakati huo Ndugu Indus alikuwa amedhoofika na kuwa mgonjwa, kwa kuwa hakuwa amefanya kazi nyingi yenye kuhitaji nguvu za kimwili awali. Na bado aliniambia kwamba kuteseka kwake kulikuwa kumetakasa moyo wake katika maana ya kiroho. Tulikuwa pamoja kwa karibu majuma matatu. Kisha akapelekwa kwenye hospitali ya kambi, ambapo alikufa Januari 1954. Kaburi lake lisilo na jina lapatikana mahali fulani kwenye msitu mkubwa sana wa sehemu ya chini ya Aktiki. Alikufa akiwa Mkristo mwaminifu na anangojea ufufuo.
Kuachiliwa na Safari ya Kurudi Nyumbani
Katika mwaka wa 1956 Tume ya Kamati Kuu ya Muungano wa Sovieti ilitumwa kwenye kambi yetu ili kupitia faili za wafungwa. Nilipoletwa mbele ya tume hiyo, jenerali aliyekuwa akiisimamia aliuliza: “Utafanya nini baada ya kufunguliwa?”
“Tutajua wakati ukifika,” nikamjibu.
Niliruhusiwa kutoka nje ya chumba hicho, na nilipoalikwa ndani tena, jenerali huyo alisema: “Wewe ndiye adui mkubwa zaidi wa Muungano wa Sovieti—wewe ni adui wa itikadi.” Na bado aliongezea: “Tutakuachilia huru, lakini tutakufuata.” Niliachiliwa huru mnamo Julai 26, 1956.
Kwa siku mbili nikiwa pamoja na Mashahidi wa Ukrainia nilizuru Suyetikha, kijiji kilicho karibu na Tayshet, ambapo walikuwa wametekwa katika mwaka wa 1951. Halafu nilisimama kwa siku nne katika wilaya ya Tomsk, karibu na mahali ambapo Mama alikuwa amehamishwa. Kutoka kwenye kituo cha reli, nilitembea kilometa 20 hadi kijiji cha Grigoryevka. Huko nilipata hali zilizokuwa mbaya hata zaidi ya tulizopata katika kambi! Dada yangu Leida alikuwa ameachiliwa huru kutoka kambi ya gereza katika Kazakhstan na alikuwa amekuja katika eneo hilo miezi michache mapema kukaa na Mama. Lakini kwa kuwa pasipoti yake ilikuwa imetwaliwa, bado hakuwa ameweza kurudi Estonia.
Chini ya Mkazo Estonia
Baada ya muda, niliwasili nyumbani Estonia na kwenda moja kwa moja kwenye shamba la wazazi wangu. Kama vile uvumi ulivyokuwa umeenea katika Siberia, niligundua kwamba serikali ilikuwa imebomoa majengo yetu yote! Siku chache baadaye, nilishikwa na ugonjwa wa kupooza. Nilikaa hospitalini kwa muda mrefu na kuendelea na matibabu baadaye. Hadi leo, mimi hutembea nikichechemea.
Upesi nikaajiriwa kazi na kampuni iliyokuwa imeniajiri wakati wa kiangazi cha mwaka wa 1943, Kampuni ya Lehtse Peat. Kampuni hiyo ilinipa nyumba, na wakati Mama na Leida waliporudi kutoka uhamishoni Desemba 1956, walikuja kuishi nami katika Lehtse. Mnamo Novemba 1957, nilifunga ndoa na Ella Kikas, ambaye pia alikuwa amerejea tu kutoka kambi ya gereza katika Siberia. Miezi miwili baadaye tulihamia Tartu, ambapo tulipata chumba kidogo katika nyumba ya faragha. Hatimaye niliweza kupata kazi ya udereva kwenye Ushirika wa Wanunuzi wa Wilaya ya Tartu.
Nilipokuwa Siberia nilikuwa nimetafsiri makala kumi za funzo la Mnara wa Mlinzi kutoka Kirusi hadi Kiestonia na nilikuwa nimezileta nyumbani. Baadaye, tulipokea kitabu Kutoka Paradiso Iliyopotea Mpaka Paradiso Iliyopatikana, ambacho pia tulikitafsiri katika lugha ya Kiestonia. Kisha tulifanya nakala zilizopigwa chapa za kitabu hicho. Wakati huohuo, wapelelezi wa KGB waliendelea na uchunguzi wao. Kwa kuwa tulifahamu mbinu zao za kutafuta watu, sikuzote tulikuwa macho na waangalifu, kama wanyama wanaowindwa.
Shabaha ya Wapelelezi wa KGB
Mapema miaka ya 1960, wapelelezi wa KGB walianzisha kampeni ya uchongezi dhidi ya Mashahidi. Mimi na mke wangu tulikuwa shabaha kubwa. Magazeti ya habari yalianza kuchapisha makala zenye uchongezi, na tukakemewa kwenye redio na televisheni. Wapelelezi wa KGB walifanya mikutano ya hadhara mahali pangu pa kazi mara mbili. Pia, tamthiliya yenye kuchekesha iliyonihusu ilichezwa na waigizaji wataalamu kwenye Jumba la Maonyesho la Estonia katika Tallinn. Hali hiyo ilinikumbusha maneno ya Daudi: “Waketio langoni hunisema, na nyimbo za walevi hunidhihaki.”—Zaburi 69:12.
Jitihada hizi za kutufedhehesha ziliendelea hadi mwaka wa 1965 mkutano wa mwisho ulipofanywa, kwenye Jengo la Afya ya Umma katika Tartu. Mimi na Ella tulikuwako, pamoja na maajenti wa KGB na umati uliojaa. Mara nyingi ambapo Ella alihojiwa, wasikilizaji waliitikia kwa makofi. Ilikuwa wazi kwamba wasikilizaji walituunga mkono. Maajenti wa KGB walitamaushwa na kukasirishwa na matokeo hayo.
Njaa ya Kiroho Yatoshelezwa
Hata ingawa Wakomunisti walijaribu kuzuia kutawanywa kwa fasihi zetu, baada ya mwaka wa 1965 hivi tuliweza kuwaandalia ndugu zetu Wakristo ugavi wa kutosha. Hata hivyo, kazi ya kutafsiri na kuchapisha kisiri ilihitaji wakati na nguvu nyingi. Akirejezea utendaji wangu wa siri na njia ya kusafirisha fasihi, wakati mmoja ajenti wa KGB aliniambia hivi: “Wewe, Toom, uko kama sanduku ambalo sehemu yake ya chini ni bandia.”
Bila shaka, mikutano yetu, ilihitaji kufanywa kwa siri na katika vikundi vidogo-vidogo. Na tulihubiri kivivi-hivi. Ndugu zetu walihitaji kutayarishwa kwa misako ambayo ingefanywa katika nyumba zao wakati wowote. Hivyo fasihi za Watch Tower Society zilihitaji kufichwa kwa njia ya uangalifu sana. Na bado, hata chini ya hali hizi, wengi waliopenda kweli ya Biblia walipatikana na wakachukua msimamo wa kuunga mkono Ufalme.
Waziri Mkuu wa Sovieti Mikhail Gorbachev alipoanza marekebisho yake katika miaka ya 1980, tulipata uhuru zaidi wa kumtumikia Mungu. Hatimaye, mwaka wa 1991, Muungano wa Sovieti uliporomoka, na Mashahidi wa Yehova wakatambuliwa kisheria. Kwa sasa tuna makutaniko manne katika Tartu, na karibuni ujenzi wa Jumba la Ufalme letu wenyewe ulimalizika. Sasa kuna Mashahidi zaidi ya 3,800 wanaoshiriki huduma katika Estonia, wakilinganishwa na labda Mashahidi 40 au 50 nilipoanza kuhubiri zaidi ya nusu karne iliyopita.
Maisha ya Kikristo Yenye Kuridhisha
Sijawahi kutilia shaka kamwe kwamba nilifanya uamuzi unaofaa nilipoamua kumtumikia Yehova. Mimi hutafakari kwa moyo uliojaa uradhi mwingi, nikifurahia kuona kwamba tengenezo la Yehova lazidi kusonga mbele kwa nguvu na kwamba bado kuna wengi zaidi na zaidi wanaotaka kumtumikia Yehova.
Namshukuru sana Yehova kwa kuwa upendo na ulinzi wake umenitegemeza pamoja na mke wangu kwa miaka mingi ambayo imepita. Kukumbuka kwamba mfumo wenye uadilifu wa Yehova unakaribia sana kumetupatia nguvu za kiroho. Hapana shaka, tunapofikiria ukuzi wa kustaajabisha katika idadi ya wale wanaomwabudu Yehova, tunasadikishwa kwamba kuteseka kwetu hakujawa bure.—Waebrania 6:10; 2 Petro 3:11, 12.
[Ramani katika ukurasa wa 12, 13]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Ramani inayoonyesha safari ndefu ya miezi miwili kutoka Tallin hadi kwenye kambi yenye sifa mbaya ya Noril’sk
Tallinn
Pskov
St. Petersburg
Perm’
Yekaterinburg
Novosibirsk
Krasnoyarsk
Dudinka
Noril’sk
MZINGO AKTIKI
[Hisani]
Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 14]
Artur Indus, Mkristo hodari mfia-imani
[Picha katika ukurasa wa 14]
Wafungwa katika Siberia, mwaka wa 1956. Mimi ni wa nne kutoka upande wa kushoto safu ya nyuma
[Picha katika ukurasa wa 15]
Nikiwa na mke wangu, mbele ya makao makuu ya zamani ya wapelelezi wa KGB ambapo mara nyingi tulihojiwa