Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kimbelembele Hutokeza Aibu
    Mnara wa Mlinzi—2000 | Agosti 1
    • Kimbelembele Hutokeza Aibu

      “Je, kimbelembele kimekuja? Basi aibu itakuja; lakini hekima i pamoja na wenye kiasi.”—MITHALI 11:2, NW.

      1, 2. Kimbelembele ni nini, na kimetokeza misiba katika njia zipi?

      MLAWI mmoja mwenye husuda aongoza umati wenye kuasi dhidi ya watu waliopewa mamlaka na Yehova. Mwana-mfalme mmoja mwenye tamaa ya makuu atunga hila ya kunyakua utawala wa babake. Mfalme asiye na subira apuuza maagizo ya wazi ya nabii wa Mungu. Waisraeli hao watatu walikuwa na sifa moja: kimbelembele.

      2 Kimbelembele ni tabia ya moyoni ambayo ni tisho kubwa kwa wote. (Zaburi 19:13) Mtu mwenye kimbelembele huamua tu kufanya mambo bila kibali. Mara nyingi kufanya hivyo hutokeza msiba. Kimbelembele hata kimewaangamiza wafalme na kuangusha milki nyingi. (Yeremia 50:29, 31, 32; Danieli 5:20) Kimbelembele hata kimewanasa watumishi fulani wa Yehova na kuwaangamiza.

      3. Tunaweza kujifunzaje hatari za kuwa wenye kimbelembele?

      3 Biblia ina sababu nzuri inaposema: “Je, kimbelembele kimekuja? Basi aibu itakuja; lakini hekima i pamoja na wenye kiasi.” (Mithali 11:2, NW) Biblia inatupa mifano inayothibitisha ukweli wa mithali hiyo. Kuchunguza baadhi ya mifano hiyo kutatusaidia kuona hatari ya kuvuka mipaka iliyowekwa. Basi, ebu tuchunguze jinsi husuda, tamaa ya makuu, na kukosa subira kulivyowafanya wale watu watatu waliotajwa hapo mwanzoni watende kwa kimbelembele, na kuaibika.

      Kora—Mwasi Mwenye Husuda

      4. (a) Kora alikuwa nani, na yaelekea alishiriki katika matukio gani makuu? (b) Katika miaka yake ya baadaye, Kora alichochea tendo gani baya?

      4 Kora alikuwa Mlawi wa Kohathi na pia binamu ya Musa na Aroni. Inaonekana kwamba alikuwa mwaminifu-mshikamanifu kwa Yehova kwa miaka mingi. Kora alikuwa na pendeleo la kuwa miongoni mwa wale waliookolewa kimuujiza walipovuka Bahari Nyekundu, na yaelekea alishiriki kutekeleza hukumu ya Yehova dhidi ya Waisraeli walioabudu ndama kwenye Mlima Sinai. (Kutoka 32:26) Lakini, hatimaye Kora aliongoza maasi dhidi ya Musa na Aroni, maasi ambayo yaliwahusisha Dathani, Abiramu, na Oni, wa kabila la Reubeni, pamoja na wakuu 250 wa Israeli.a “Ninyi inawatosha,” wakamwambia Musa na Aroni, “kwa kuwa mkutano wote ni mtakatifu, kila mmoja miongoni mwao, BWANA naye yu kati yao; n’nini basi kujitukuza juu ya mkutano wa BWANA?”—Hesabu 16:1-3.

      5, 6. (a) Kwa nini Kora aliasi dhidi ya Musa na Aroni? (b) Kwa nini inaweza kusemwa kwamba yaelekea Kora hakuthamini mahali pake katika mpango wa Mungu?

      5 Kwa nini Kora aliasi baada ya kuwa mwaminifu kwa miaka mingi? Hakika Musa hakuongoza Israeli kwa dhuluma, kwa sababu “alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi.” (Hesabu 12:3) Hata hivyo, inaonekana Kora aliwahusudu Musa na Aroni na kuchukia umashuhuri wao, na hilo likamfanya aseme—isivyo kweli—kwamba walikuwa wamejitukuza kwa ubinafsi juu ya mkutano.—Zaburi 106:16.

      6 Yaelekea tatizo moja la Kora ni kwamba hakuthamini mapendeleo yake mwenyewe katika mpango wa Mungu. Ni kweli kwamba Walawi wa Kohathi hawakuwa makuhani, lakini walikuwa walimu wa Sheria ya Mungu. Pia walibeba vyombo vya tabenakulo wakati vyombo hivyo vilipohitaji kusafirishwa. Huo ulikuwa mgawo mkubwa, kwa sababu vyombo hivyo vitakatifu vilipasa kubebwa tu na watu safi kidini na kiadili. (Isaya 52:11) Hivyo, Musa alipomkabili Kora, ni kama alikuwa akimwuliza, Je, unaona mgawo wako kuwa kitu kidogo sana hivi kwamba ni lazima pia uwe kuhani? (Hesabu 16:9, 10) Kora hakutambua kwamba heshima kubwa zaidi ni kumtumikia Yehova kwa uaminifu kulingana na mpango wake—wala si kupata hadhi au cheo fulani cha kipekee.—Zaburi 84:10.

      7. (a) Musa alishughulikaje na Kora na wafuasi wake? (b) Maasi ya Kora yalimalizwaje kwa msiba?

      7 Musa akawaambia Kora na watu wake wakusanyike kwenye hema la kukutania kesho yake asubuhi wakiwa na chetezo na uvumba. Kora na wafuasi wake hawakuruhusiwa kufukiza uvumba kwa sababu hawakuwa makuhani. Kama wangekuja na chetezo na uvumba, ingekuwa wazi kwamba watu hao bado waliona wana haki ya kuwa makuhani—hata baada ya kuwa na fursa ya kulifikiria jambo hilo usiku kucha. Walipojitokeza asubuhi iliyofuata, kwa haki Yehova alionyesha hasira yake ya kisasi. Kwa habari ya wana wa Reubeni, ‘nchi ilifunua kinywa chake, ikawameza.’ Waliosalia, kutia ndani Kora, waliteketezwa kwa moto kutoka kwa Mungu. (Kumbukumbu la Torati 11:6; Hesabu 16:16-35; 26:10) Kimbelembele cha Kora kilimfanya apate aibu hatimaye—akakataliwa na Mungu!

      Kinza “Mwelekeo wa Kuhusudu”

      8. “Mwelekeo wa kuhusudu” unaweza kujitokezaje miongoni mwa Wakristo?

      8 Simulizi hilo la Kora ni onyo kwetu. Kwa kuwa “mwelekeo wa kuhusudu” umo katika wanadamu wasiokamilika, unaweza kujitokeza hata katika kutaniko la Kikristo. (Yakobo 4:5) Kwa mfano, huenda ikawa tunatamani wadhifa. Kama Kora, huenda tukawahusudu wale ambao wana mapendeleo tunayotamani. Au huenda tukawa kama yule Mkristo wa karne ya kwanza aitwaye Diotrefesi. Alichambua sana mamlaka ya mitume, kwa sababu inaonekana alitaka kuongoza. Yohana akaandika kwamba Diotrefesi “hupenda kuwa na mahali pa kwanza.”—3 Yohana 9.

      9. (a) Tunahitaji kuepuka mtazamo gani kuhusu mapendeleo katika kutaniko? (b) Ni maoni gani yanayofaa kuhusu fungu letu katika mpango wa Mungu?

      9 Si vibaya kwa mwanamume Mkristo kujitahidi kufikilia mapendeleo katika kutaniko. Paulo hata alipendekeza jambo hilo. (1 Timotheo 3:1) Lakini, hatupaswi kuona mapendeleo ya utumishi kuwa ishara ya kwamba tumestahili heshima fulani, kana kwamba kwa kuyapata, tumepanda kile kiitwacho eti cheo cha ukubwa. Kumbuka kwamba Yesu alisema: “Yeyote yule atakaye kuwa wa kwanza miongoni mwenu lazima awe mtumwa wenu.” (Mathayo 20:26, 27) Ni wazi kwamba si vizuri kuwahusudu wale ambao wana madaraka zaidi, kana kwamba thamani yetu mbele za Mungu hutegemea “cheo” tulicho nacho katika tengenezo lake. Yesu alisema: “Nyinyi nyote ni akina ndugu.” (Mathayo 23:8) Ndiyo, tuwe wahubiri au mapainia, tuwe tumebatizwa majuzi au tuwe washika uaminifu-maadili wa muda mrefu—sote tunaomtumikia Yehova kwa moyo wote tunathaminiwa katika mpango wake. (Luka 10:27; 12:6, 7; Wagalatia 3:28; Waebrania 6:10) Ni baraka kwelikweli kufanya kazi bega kwa bega na mamilioni ya watu ambao wanajaribu kufuata shauri hili la Biblia: “Jifungeni hali ya akili ya kujishusha chini kuelekea mtu na mwenzake.”—1 Petro 5:5.

      Absalomu—Laghai Mwenye Tamaa ya Makuu

      10. Absalomu alikuwa nani, na alijaribuje kujipendekeza kwa wale waliokuwa wakimwendea mfalme ili wapate hukumu?

      10 Maisha ya mwana wa tatu wa Mfalme Daudi, Absalomu, yanatupa somo kuhusu tamaa ya makuu. Mwana huyo laghai na mwenye hila alijaribu kujipendekeza kwa watu ambao walikuwa wakimwendea mfalme ili wapate hukumu. Kwanza alidokeza kwamba Daudi hakujali mahitaji yao. Kisha akaacha ujanja na kutaja waziwazi kusudi lake. “Laiti mimi ningewekwa kuwa mwamuzi katika nchi hii,” Absalomu akasema, “ili kila mtu mwenye neno au dawa aje kwangu, nimpatie haki yake!” Absalomu alitumia ujanja mwingi sana. “Alipokaribia mtu ye yote kumsujudia,” Biblia inasema, “hunyosha mkono wake, na kumshika, na kumbusu. Hivyo ndivyo Absalomu alivyowatendea Israeli wote, waliomwendea mfalme ili wapate hukumu.” Matokeo yakawa nini? “Absalomu akawadanganya watu wa Israeli.”—2 Samweli 15:1-6.

      11. Absalomu alijaribuje kunyakua ufalme wa Daudi?

      11 Absalomu aliazimia kunyakua utawala wa babake. Miaka mitano awali, aliagiza mwana mkubwa wa Daudi, Amnoni, auawe eti alipize kisasi kwa sababu ya kubakwa kwa dadake, Tamari. (2 Samweli 13:28, 29) Lakini, huenda hata wakati huo Absalomu alikuwa akitamani kiti cha ufalme, akiona kumwua Amnoni kuwa njia nzuri ya kuondoa mpinzani.b Kwa vyovyote vile, wakati ulipowadia, Absalomu alichukua hatua. Akaagiza itangazwe kotekote nchini kwamba amekuwa mfalme.—2 Samweli 15:10.

      12. Eleza jinsi kimbelembele cha Absalomu kilivyomwaibisha.

      12 Kwa muda fulani, Absalomu alifanikiwa, kwa kuwa “fitina yao ikawa na nguvu; maana watu waliokuwa pamoja na Absalomu wakazidi kuwa wengi.” Baada ya muda, Mfalme Daudi alilazimika kutoroka ili kuokoa uhai wake. (2 Samweli 15:12-17) Lakini punde tu baadaye, maasi ya Absalomu yakakatizwa alipouawa na Yoabu, akatupwa shimoni, na kufunikwa kwa mawe. Ebu wazia—mtu huyo mwenye tamaa ya makuu aliyetaka kuwa mfalme hata hakuzikwa kwa heshima alipokufa!c Kwa kweli kimbelembele kilimfanya Absalomu apate aibu.—2 Samweli 18:9-17.

      Epuka Tamaa ya Makuu Yenye Ubinafsi

      13. Roho ya kutamani makuu inaweza kukuaje katika moyo wa Mkristo?

      13 Kuinuka kwa Absalomu kunyakua ufalme na kuanguka kwake kunatufundisha somo fulani. Katika ulimwengu wa leo wenye ushindani mkali, ni kawaida kwa watu kuwarairai wakubwa wao, wakijipendekeza kwao ili tu waonekane au labda wapate pendeleo fulani au kupandishwa cheo. Wakati uo huo, wanaweza kujisifu kwa wale walio chini yao, wakitumaini kupata upendeleo wao na kuungwa mkono. Tusipojihadhari, roho hiyo ya kutamani makuu inaweza kukua katika mioyo yetu. Inaonekana jambo hilo lilitokea miongoni mwa wengine katika karne ya kwanza, ikiwalazimu mitume wawaonye vikali.—Wagalatia 4:17; 3 Yohana 9, 10.

      14. Kwa nini tuepuke roho ya kutamani makuu na ya kujitukuza?

      14 Yehova hataki katika tengenezo lake watu wenye kujitutumua na wenye hila wanaojaribu ‘kutafuta utukufu wao wenyewe.’ (Mithali 25:27) Hata Biblia inaonya hivi: “BWANA ataikata midomo yote ya kujipendekeza, nao ulimi unenao maneno ya kiburi [“makuu,” NW].” (Zaburi 12:3) Absalomu alikuwa na midomo ya kujipendekeza. Aliwarairai wale aliotaka kujipendekeza kwao—ili tu apate mamlaka aliyotamani sana. Kinyume cha hali hiyo, sisi tumebarikiwa kama nini kuwa miongoni mwa udugu ambao hufuata shauri hili la Paulo: “[Msifanye] jambo lolote kwa ugomvi au kwa majisifu ya bure, bali kwa hali ya akili ya kujishusha chini mkifikiria kwamba wengine ni wakubwa kuliko nyinyi.”—Wafilipi 2:3.

      Sauli—Mfalme Asiye na Subira

      15. Pindi moja Sauli alijionyeshaje kuwa mwenye kiasi?

      15 Pindi moja Sauli, ambaye baadaye alipata kuwa mfalme wa Israeli, alikuwa mtu mwenye kiasi. Kwa mfano, ebu fikiria jambo lililotendeka alipokuwa angali kijana. Samweli, nabii wa Mungu, aliposema maneno mazuri kumhusu, Sauli alijibu hivi kwa unyenyekevu: “Je! mimi si Mbenyamini, mtu wa kabila iliyo ndogo kuliko kabila zote za Israeli? na jamaa yangu nayo si ndogo kuliko jamaa zote za kabila la Benyamini? Kwa nini basi, kuniambia hivyo?”—1 Samweli 9:21.

      16. Ni katika njia gani Sauli alikosa subira?

      16 Lakini, baadaye Sauli akakosa kuwa mwenye kiasi. Alipokuwa akipigana na Wafilisti, alirudi Gilgali, ambako alitazamiwa amngojee Samweli aje amsihi Mungu kwa dhabihu. Samweli alipochelewa kufika kwa wakati uliopangwa, kwa kimbelembele Sauli mwenyewe akatoa dhabihu ya kuteketezwa. Alipomaliza tu, Samweli akafika. “Umefanya nini?” Samweli akamwuliza. Sauli akajibu: “Ni kwa sababu naliona ya kuwa watu wanatawanyika mbali nami, na wewe hukuja siku zile zilizonenwa . . . Kwa hiyo nalijishurutisha, nikatoa sadaka ya kuteketezwa.”—1 Samweli 13:8-12.

      17. (a) Ukitazama kijuujuu tu, kwa nini matendo ya Sauli huenda yakaonekana kuwa yalifaa? (b) Kwa nini Yehova alimkemea Sauli kwa kukosa subira?

      17 Ukitazama kijuujuu tu, huenda matendo ya Sauli yakaonekana kuwa yalifaa. Kwani, watu wa Mungu walikuwa “katika dhiki,” na ‘kufadhaishwa,’ wakitetemeka kwa sababu ya hali mbaya waliyokabili. (1 Samweli 13:6, 7) Si vibaya kuchukua hatua ikihitajika.d Lakini, kumbuka kwamba Yehova anaweza kusoma mioyo na kutambua nia zetu za ndani kabisa. (1 Samweli 16:7) Kwa hiyo, huenda aliona mambo fulani kuhusu Sauli ambayo hayatajwi moja kwa moja katika masimulizi hayo ya Biblia. Kwa mfano, huenda Yehova aliona kwamba Sauli alikosa subira kwa sababu ya kiburi. Labda Sauli alikasirika sana kwamba yeye—mfalme wa Israeli yote—ati amngoje mtu ambaye alimwona kuwa nabii aliyezeeka, mwenye kuchelewa-chelewa! Kwa vyovyote vile, Sauli alihisi kwamba kuchelewa kwa Samweli kulimpa haki ya kujifanyia mambo mwenyewe na kupuuza maagizo ya wazi ambayo alikuwa amepewa. Matokeo yakawaje? Samweli hakumsifu Sauli kwa hatua aliyochukua. Badala yake, alimkemea akisema: “Ufalme wako hautadumu . . . kwa sababu wewe hukulishika neno lile BWANA alilokuamuru.” (1 Samweli 13:13, 14) Kwa mara nyingine tena, kimbelembele kilitokeza aibu.

      Jihadhari Usije Ukakosa Subira

      18, 19. (a) Eleza jinsi kukosa subira kunavyoweza kumfanya mtumishi wa Mungu wa wakati huu atende kwa kimbelembele. (b) Tunapaswa kukumbuka nini kuhusu utendaji wa kutaniko la Kikristo?

      18 Masimulizi ya tendo la kimbelembele la Sauli limeandikwa katika Neno la Mungu kwa manufaa yetu. (1 Wakorintho 10:11) Ni rahisi sana tukasirikie kutokamilika kwa ndugu zetu. Kama Sauli, huenda tukakosa subira, tukihisi kwamba tukitaka mambo yafanywe vizuri, ni lazima tuyafanye sisi wenyewe. Kwa mfano, tuseme ndugu fulani ana ustadi mkubwa wa kufanya mambo fulani kwa utaratibu. Hachelewi kufanya mambo, anajua vizuri jinsi mambo yanavyopasa kufanywa kutanikoni, na ana kipawa cha kusema na kufundisha. Vilevile anatambua kwamba wengine si waangalifu kama yeye, na kamwe hawafanyi mambo kwa njia bora kama ambavyo angependa. Je, hiyo imfanye akose subira? Je, awachambue ndugu zake, labda akidokeza kwamba kama si kwa sababu ya jitihada zake mambo hayangefanywa nalo kutaniko lingeathirika? Hicho kingekuwa kimbelembele!

      19 Kwa kweli, ni nini kinachofanya kutaniko la Wakristo liwe na muungano? Je, ni ustadi katika usimamizi? uwezo wa kufanya mambo kwa njia bora? ujuzi mwingi? Ni kweli kwamba mambo hayo yanafaa ili kutaniko liendeshwe vizuri. (1 Wakorintho 14:40; Wafilipi 3:16; 2 Petro 3:18) Lakini, Yesu alisema kwamba wafuasi wake wangetambuliwa hasa kwa upendo wao. (Yohana 13:35) Hiyo ndiyo sababu wazee wenye kujali, ingawa wana utaratibu, wanatambua kwamba kutaniko si kampuni inayohitaji usimamizi mkali; badala yake, ni kundi linalohitaji kutunzwa kwa wororo. (Isaya 32:1, 2; 40:11) Kupuuza kwa kimbelembele kanuni kama hizo mara nyingi hutokeza ugomvi. Tofauti na hiyo, utaratibu wa kimungu hutokeza amani.—1 Wakorintho 14:33; Wagalatia 6:16.

      20. Tutazungumzia nini katika makala ifuatayo?

      20 Masimulizi ya Biblia kuhusu Kora, Absalomu, na Sauli yanaonyesha wazi kwamba kimbelembele hutokeza aibu, kama inavyotajwa kwenye Mithali 11:2. Lakini, mstari uo huo waongezea kusema: “Hekima i pamoja na wenye kiasi.” Kiasi ni nini? Kuna mifano gani katika Biblia ambayo inaweza kutusaidia kuelewa sifa hii, na tunawezaje kuonyesha kiasi leo? Maswali haya yatazungumziwa katika makala ifuatayo.

      [Maelezo ya Chini]

      a Kwa kuwa Reubeni ndiye aliyekuwa mzaliwa wa kwanza wa Yakobo, huenda wazao wake waliochochewa na Kora kuasi walichukia mamlaka ya Musa juu yao kwa sababu Musa alikuwa wa uzao wa Lawi.

      b Kileabu, mwana wa pili wa Daudi, hatajwi baada ya kuzaliwa. Huenda alikufa wakati fulani kabla ya maasi ya Absalomu.

      c Katika nyakati za Biblia kuzika maiti kulikuwa jambo muhimu sana. Kwa hiyo, kutozikwa kulikuwa jambo la msiba na mara nyingi kulionyesha kukataliwa na Mungu.—Yeremia 25:32, 33.

      d Kwa mfano, Finehasi alichukua hatua ya haraka ili kukomesha pigo ambalo lilikuwa limeua makumi ya maelfu ya Waisraeli, naye Daudi aliwatia moyo watu wake wenye njaa sana wale pamoja naye mikate ya wonyesho katika “nyumba ya Mungu.” Mungu hakuyashutumu matendo hayo mawili kuwa kimbelembele.—Mathayo 12:2-4; Hesabu 25:7-9; 1 Samweli 21:1-6.

  • “Hekima I Pamoja na Wenye Kiasi”
    Mnara wa Mlinzi—2000 | Agosti 1
    • “Hekima I Pamoja na Wenye Kiasi”

      “BWANA anataka nini kwako, ila . . . kwenda kwa unyenyekevu [“kiasi,” “NW”] na Mungu wako!”—MIKA 6:8.

      1, 2. Kiasi ni nini, na kinatofautianaje na kimbelembele?

      MTUME mashuhuri akataa kujitukuza. Mwamuzi mmoja mjasiri wa Israeli ajiita mdogo katika nyumba ya babake. Mtu mkuu zaidi aliyepata kuishi akiri kwamba hana mamlaka kamili. Kila mmoja wao anaonyesha kiasi.

      2 Kiasi ni kinyume cha kimbelembele. Mtu mwenye kiasi anafahamu vizuri uwezo wake na ustahili wake na hana kiburi wala majisifu. Badala ya kuwa mwenye kiburi, mwenye kujisifu, au mtaka makuu, nyakati zote mtu mwenye kiasi hutambua udhaifu wake. Kwa hiyo, yeye hustahi na kujali hisia za wengine na maoni yao.

      3. Ni katika njia gani hekima “i pamoja na wenye kiasi”?

      3 Kwa sababu nzuri Biblia inasema hivi: “Hekima i pamoja na wenye kiasi.” (Mithali 11:2, NW) Mtu mwenye kiasi ana hekima kwa sababu yeye hufuata mwendo ambao Mungu anakubali, naye huepuka roho ya kimbelembele ambayo huleta aibu. (Mithali 8:13; 1 Petro 5:5) Hekima ya kuwa mwenye kiasi inathibitishwa na maisha ya watumishi kadhaa wa Mungu. Ebu tufikirie ile mifano mitatu ambayo imetajwa katika fungu la kwanza.

      Paulo—Mtu ‘wa Chini’ na ‘Msimamizi-Nyumba’

      4. Paulo alipata mapendeleo gani ya kipekee?

      4 Paulo alikuwa mashuhuri miongoni mwa Wakristo wa mapema, na kwa sababu nzuri. Katika huduma yake, alisafiri maelfu ya kilometa baharini na barani, na alianzisha makutaniko mengi. Na zaidi, Yehova alimbariki Paulo kwa kumpa maono na uwezo wa kusema lugha za kigeni. (1 Wakorintho 14:18; 2 Wakorintho 12:1-5) Pia Yehova alimpulizia Paulo aandike barua 14 ambazo sasa ni sehemu ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo. Kwa wazi, inaweza kusemwa kwamba kazi za Paulo zilizidi kazi za wale mitume wengine.—1 Wakorintho 15:10.

      5. Paulo alionyeshaje kwamba alikuwa na maoni yenye kiasi juu yake mwenyewe?

      5 Kwa kuwa Paulo alikuwa katika mstari wa mbele katika utendaji wa Kikristo, huenda wengine wangetarajia kumwona akifurahia kutukuzwa, hata akiringia mamlaka yake. Lakini, haikuwa hivyo, kwa kuwa Paulo alikuwa mwenye kiasi. Alijiita “mdogo zaidi sana kati ya wale mitume,” akiongezea: “Nami sistahili kuitwa mtume, kwa sababu nililinyanyasa kutaniko la Mungu.” (1 Wakorintho 15:9) Kwa kuwa aliwanyanyasa Wakristo zamani, Paulo hakusahau kamwe kwamba ni kupitia tu fadhili isiyostahiliwa ya Mungu angeweza kuwa na uhusiano na Mungu, sembuse kufurahia mapendeleo ya kipekee ya utumishi. (Yohana 6:44; Waefeso 2:8) Kwa hiyo, Paulo hakuhisi kwamba mafanikio yake ya ajabu katika huduma yalimfanya awe bora kuliko wengine.—1 Wakorintho 9:16.

      6. Paulo alionyeshaje kiasi aliposhughulika na Wakorintho?

      6 Jinsi Paulo alivyoshughulika na Wakorintho inadhihirisha sana kwamba alikuwa mwenye kiasi. Inaonekana kwamba baadhi yao walivutiwa na wale ambao walifikiri kuwa waangalizi mashuhuri, kutia ndani Apolo, Kefa, na Paulo mwenyewe. (1 Wakorintho 1:11-15) Lakini Paulo hakutafuta sifa kwa Wakorintho wala hakutumia vibaya heshima aliyopewa na wengine. Alipowazuru, yeye hakujitokeza ‘na usemi wenye kupita kiasi wala hekima.’ Badala yake, Paulo alisema hivi juu yake mwenyewe na waandamani wake: “Acheni mtu atukadirie sisi hivyo kama walio chini ya Kristo na wasimamizi-nyumba wa siri takatifu za Mungu.”a—1 Wakorintho 2:1-5; 4:1.

      7. Paulo alionyeshaje kiasi hata alipokuwa akitoa ushauri?

      7 Paulo hata alionyesha kiasi alipolazimika kutoa ushauri mkali na mwongozo. Badala ya kutumia mamlaka yake akiwa mtume, Paulo aliwasihi Wakristo wenzake “kwa huruma za Mungu” na “Msingi wa upendo.” (Waroma 12:1, 2; Filemoni 8, 9) Kwa nini Paulo alifanya hivyo? Kwa sababu kwa kweli alijiona kuwa ‘mfanyakazi mwenzi’ wa ndugu zake, wala hakujiona kuwa ‘bwana-mkubwa juu ya imani yao.’ (2 Wakorintho 1:24) Inaelekea kwamba sifa ya Paulo ya kiasi ndiyo iliyomfanya apendwe sana na makutaniko ya karne ya kwanza.—Matendo 20:36-38.

      Maoni Yenye Kiasi Kuhusu Mapendeleo Yetu

      8, 9. (a) Kwa nini tuwe na maoni yenye kiasi juu yetu wenyewe? (b) Wale ambao wana madaraka fulani wanaweza kuonyeshaje kiasi?

      8 Paulo aliwawekea Wakristo wa leo mfano mzuri. Hata tuwe tumepewa mapendeleo gani, hatupaswi kuhisi kwamba sisi ni bora kuliko wengine. “Ikiwa yeyote afikiri yeye ni kitu wakati yeye si kitu,” Paulo aliandika, “anadanganya akili yake mwenyewe.” (Wagalatia 6:3) Kwa nini? Kwa sababu “wote wamefanya dhambi na hupungukiwa na utukufu wa Mungu.” (Waroma 3:23; 5:12) Ndiyo, hatupaswi kusahau kwamba sisi sote tumerithi dhambi na kifo kutoka kwa Adamu. Mapendeleo ya pekee hayatuondolei hali yetu ya chini yenye dhambi. (Mhubiri 9:2) Kama Paulo, ni kwa fadhili tu isiyostahiliwa kwamba wanadamu wanaweza kuwa na uhusiano wowote pamoja na Mungu, sembuse kumtumikia katika pendeleo fulani la kipekee.—Waroma 3:12, 24.

      9 Akitambua jambo hilo, mtu mwenye kiasi hajivunii mapendeleo yake wala hajisifii mafanikio yake. (1 Wakorintho 4:7) Anapotoa mashauri au mwelekezo, anafanya hivyo kama mfanyakazi mwenzi—wala si kama bwana-mkubwa. Hakika, ingekuwa makosa kwa mtu ambaye hufanya mambo fulani kwa njia bora kutafuta sifa au kutumia vibaya heshima anayopewa na waamini wenzake. (Mithali 25:27; Mathayo 6:2-4) Sifa pekee inayofaa hutoka kwa wengine—na haipaswi kutafutwa. Na tukisifiwa, jambo hilo halipasi kutufanya tujifikirie kuliko ilivyo lazima.—Mithali 27:2; Waroma 12:3.

      10. Eleza jinsi wengine wanaoonekana kuwa wa hali ya chini wanavyoweza kuwa “matajiri wa imani” kwelikweli.

      10 Tunapokabidhiwa madaraka fulani, kuwa wenye kiasi kutatusaidia kuepuka kujifikiria mno, tukitokeza wazo la kwamba kutaniko linastawi kwa sababu ya jitihada zetu na uwezo wetu. Kwa mfano, huenda tuna kipawa cha kufundisha. (Waefeso 4:11, 12) Lakini, tukiwa wenye kiasi ni lazima tutambue kwamba baadhi ya mambo makubwa zaidi tunayojifunza kwenye mikutano ya kutaniko hayafundishwi kutoka jukwaani. Kwa mfano, je, hutiwi moyo unapoona mzazi ambaye hana mwenzi akija kwa ukawaida kwenye Jumba la Ufalme akiambatana na watoto wake? Au mtu ambaye ameshuka moyo anayehudhuria mikutano japo hisia zenye kudumu za kujiona kuwa hafai? Au kijana ambaye anazidi kufanya maendeleo ya kiroho japo mavutano mabaya shuleni na kwingineko? (Zaburi 84:10) Watu hawa huenda wasiwe mashuhuri. Mara nyingi majaribu ya uaminifu-maadili wanayokabili hayaonwi na wengine. Lakini, huenda wao ni “matajiri wa imani” kama tu wale ambao ni mashuhuri. (Yakobo 2:5) Kwani hatimaye, uaminifu ndio humfurahisha Yehova.—Mathayo 10:22; 1 Wakorintho 4:2.

      Gideoni—“Mdogo” Katika Nyumba ya Baba Yake

      11. Gideoni alionyeshaje kiasi alipokuwa akizungumza na malaika wa Mungu?

      11 Gideoni, kijana hodari wa kabila la Manase, aliishi wakati wa mvurugo katika historia ya Israeli. Kwa miaka saba, watu wa Mungu walikuwa wameumia kwa kudhulumiwa na Wamidiani. Lakini, sasa wakati ulikuwa umewadia wa Yehova kuwakomboa watu wake. Basi, malaika akamtokea Gideoni, akasema: “BWANA yu pamoja nawe, Ee shujaa.” Gideoni alikuwa mwenye kiasi, kwa hiyo hakujitutumua kwa sababu ya kusifiwa huko ambako hakutarajia. Badala yake, akamwambia malaika huyo kwa staha: “Ee Bwana wangu, ikiwa BWANA yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata?” Malaika huyo akamweleza Gideoni mambo kwa wazi: ‘Utawaokoa Israeli na mkono wa Midiani.’ Gideoni alijibuje? Badala ya kuchukua mgawo huo kwa hamu nyingi akiuona kuwa fursa ya kuwa shujaa katika taifa lote, Gideoni alijibu: “Ee Bwana, nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani? Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase, na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu.” Alionyesha sifa ya kiasi iliyoje!—Waamuzi 6:11-15.

      12. Gideoni alionyeshaje busara alipotekeleza mgawo wake?

      12 Kabla ya kumtuma Gideoni aende vitani, Yehova alimjaribu. Kwa njia gani? Gideoni aliambiwa aharibu madhabahu ya babake ya kuabudia Baali na aikatekate Ashera iliyokuwa kando yake. Mgawo huo ulihitaji ujasiri, lakini Gideoni pia alionyesha kiasi na busara katika njia aliyoutimiza. Badala ya kufanya mambo aliyoagizwa hadharani, Gideoni alifanya kazi hiyo usiku ambapo yaelekea hangeonekana. Isitoshe, Gideoni alitimiza mgawo wake kwa tahadhari iliyohitajika. Alichukua watumishi kumi—labda ili baadhi yao wawe walinzi na waliobaki wamsaidie kuharibu madhabahu na Ashera.b Kwa vyovyote vile, kwa baraka za Yehova, Gideoni alitekeleza mgawo wake, na baadaye akatumiwa na Mungu kukomboa Israeli kutoka kwa Wamidiani.—Waamuzi 6:25-27.

      Kuonyesha Kiasi na Busara

      13, 14. (a) Tunaweza kuonyeshaje kiasi tunapopata pendeleo fulani la utumishi? (b) Ndugu A. H. Macmillan aliwekaje mfano mzuri wa kuwa mwenye kiasi?

      13 Tunaweza kujifunza mengi kutokana na jinsi Gideoni alivyoonyesha kiasi. Kwa mfano, inakuwaje tunapopokea pendeleo fulani la utumishi? Je, kwanza tunafikiria umashuhuri au sifa zitakazotokezwa na pendeleo hilo? Au kwa kiasi na kwa sala tunafikiria kama tunaweza kutimiza matakwa ya mgawo huo? Ndugu A. H. Macmillan, aliyemaliza mwendo wake wa duniani mwaka wa 1966 aliweka mfano mzuri kwa habari hiyo. Pindi moja C. T. Russell, msimamizi wa kwanza wa Watch Tower Society, alimwomba Ndugu Macmillan atoe maoni yake kuhusu mtu ambaye angesimamia kazi Ndugu Russell asipokuwapo. Katika mazungumzo yaliyofuata, Ndugu Macmillan hakujipendekeza hata kidogo, ijapokuwa ingekuwa rahisi sana kwake kufanya hivyo. Mwishowe, Ndugu Russell alimwomba Ndugu Macmillan afikirie kukubali mgawo huo. “Niliduwaa pale nilipokuwa nimesimama,” Ndugu Macmillan akaandika miaka mingi baadaye. “Nilifikiria jambo hilo kwa uzito sana, na kusali juu yake kwa muda fulani kabla ya kumwambia hatimaye kwamba ningefurahi kufanya yote niwezayo ili kumsaidia.”

      14 Baadaye kidogo, Ndugu Russell akafa, na ikawa kwamba Watch Tower Society haina msimamizi. Kwa kuwa Ndugu Macmillan ndiye aliyekuwa msimamizi wakati Ndugu Russell alipokuwa katika safari ya mwisho ya kuhubiri, ndugu fulani alimwambia hivi: “Mac, kuna uwezekano mkubwa kwamba ni wewe utakuwa msimamizi. Ulikuwa mwakilishi wa pekee wa Ndugu Russell wakati alipokuwa ameenda, na alituambia sisi sote tufanye yale unayotuambia. Sasa, alienda na hakurudi. Inaonekana ni wewe utaendeleza kazi hii.” Ndugu Macmillan akajibu: “Ndugu, hupaswi kufikiria mambo hayo hivyo. Hii ni kazi ya Bwana na wadhifa pekee unaopokea katika tengenezo la Bwana ni ule ambao Bwana anaona unafaa akupe; na nina hakika mimi sistahili kufanya kazi hiyo.” Kisha Ndugu Macmillan akapendekeza mtu mwingine achukue wadhifa huo. Kama Gideoni, yeye alikuwa na maoni yenye kiasi juu yake mwenyewe—na ni vizuri tusitawishe maoni kama hayo.

      15. Tunaweza kutumia ufahamu katika njia zipi zinazofaa tunapowahubiria wengine?

      15 Sisi pia tunapaswa kuwa wenye kiasi katika njia ambayo tunatekeleza mgawo wetu. Gideoni alikuwa mwenye busara, na alijaribu kutowakasirisha wapinzani wake bila sababu. Vivyo hivyo, katika kazi yetu ya kuhubiri, tunapaswa kuwa wenye kiasi na wenye busara kuhusu jinsi tunavyozungumza na wengine. Ni kweli kwamba tunapigana vita ya kiroho ya kupindua “mambo yaliyotiwa kwa nguvu sana katika mahandaki” na “mawazowazo.” (2 Wakorintho 10:4, 5) Lakini hatupaswi kuzungumza kwa kuwadharau wengine au kuwafanya wawe na sababu yoyote halali ya kuudhika na ujumbe wetu. Badala yake, ni lazima tustahi maoni yao, tukazie mambo tunayokubaliana nao, kisha tuzingatie mambo yafaayo ya ujumbe wetu.—Matendo 22:1-3; 1 Wakorintho 9:22; Ufunuo 21:4.

      Yesu—Mfano Bora wa Kuonyesha Kiasi

      16. Yesu alionyeshaje kwamba alikuwa na maoni ya kiasi juu yake mwenyewe?

      16 Yesu Kristo ni mfano bora wa mtu mwenye kiasi.c Licha ya uhusiano wa karibu sana na Baba yake, Yesu hakusita kukiri kwamba hakuwa na mamlaka juu ya mambo mengine. (Yohana 1:14) Kwa mfano, mama ya Yakobo na Yohana alipoomba kwamba wana wake wawili waketi kando ya Yesu katika ufalme wake, Yesu alisema: “Huku kuketi kwenye mkono wangu wa kuume na kwenye mkono wangu wa kushoto si kwangu mimi kutoa.” (Mathayo 20:20-23) Pindi nyingine, Yesu alikiri waziwazi hivi: “Mimi siwezi kufanya kitu chochote kwa uanzisho wangu . . . natafuta sana, si mapenzi yangu mwenyewe, bali mapenzi yake aliyenituma mimi.”—Yohana 5:30; 14:28; Wafilipi 2:5, 6.

      17. Yesu alionyeshaje kiasi aliposhughulika na wengine?

      17 Kwa kila njia, Yesu alikuwa mkuu kuliko wanadamu wasiokamilika, na Yehova Baba yake alimpa mamlaka kubwa kuliko mwanadamu yeyote yule. Lakini, Yesu alishughulika na wafuasi wake kwa kiasi. Yeye hakuwalemea kwa wonyesho mkubwa wa ujuzi mwingi. Aliwajali wengine na kuwaonea huruma naye aliyafikiria mahitaji yao ya kibinadamu. (Mathayo 15:32; 26:40, 41; Marko 6:31) Kwa hiyo, ingawa Yesu alikuwa mkamilifu, yeye hakuwa mwenye kudai ukamilifu kwa wengine. Yeye hakuwataka wanafunzi wake wafanye mengi zaidi ya uwezo wao, wala hakuwapa mambo ambayo wasingeweza kuyahimili. (Yohana 16:12) Si ajabu kwamba aliwaburudisha wengi!—Mathayo 11:29.

      Iga Mfano wa Yesu wa Kiasi

      18, 19. Tunaweza kuigaje kiasi cha Yesu kwa (a) jinsi tunavyojiona, na (b) jinsi tunavyowatendea wengine?

      18 Ikiwa mtu mkuu zaidi aliyepata kuishi alionyesha kiasi, namna gani sisi. Mara nyingi wanadamu wasiokamilika hawakubali kwa urahisi kwamba hawana mamlaka kamili. Lakini, kwa kumwiga Yesu, Wakristo hujitahidi kuwa wenye kiasi. Wao si wenye kiburi mno wasiwape madaraka wale ambao wamestahili kuyapokea; wala wao si wenye kujivuna na wasiotaka kukubali mwelekezo kutoka kwa wale ambao wamepewa mamlaka. Wakionyesha roho ya kushirikiana, wao huacha mambo yote kutanikoni yatendeke kwa “adabu na kwa mpango.”—1 Wakorintho 14:40.

      19 Pia sifa ya kiasi itatufanya tuyafikirie mahitaji ya wengine na kutokuwa wenye kudai mno katika mambo tunayowatarajia wafanye. (Wafilipi 4:5) Huenda tukawa na uwezo fulani na nguvu fulani ambazo huenda wengine hawana. Lakini, tukiwa wenye kiasi, hatutawatarajia wengine sikuzote wafanye mambo kama ambavyo tungependa wafanye. Tukijua kwamba kila mtu ana udhaifu wake, tutaonyesha sifa ya kiasi kwa kutozingatia kasoro za wengine. Petro aliandika: “Juu ya mambo yote, iweni na upendo wenye juhudi nyingi nyinyi kwa nyinyi, kwa sababu upendo hufunika wingi wa dhambi.”—1 Petro 4:8.

      20. Tunaweza kufanya nini ili kushinda mwelekeo wowote wa kukosa kiasi?

      20 Kama ambavyo tumejifunza, kwa kweli hekima i pamoja na wenye kiasi. Lakini, namna gani ukitambua kwamba una mielekeo ya kukosa kiasi au ya kuwa na kimbelembele? Usivunjike moyo. Badala yake, fuata mfano wa Daudi, aliyesali hivi: “Umzuie mtumishi wako asitende mambo ya kiburi [“kimbelembele,” NW], yasinitawale mimi.” (Zaburi 19:13) Kwa kuiga imani ya watu kama Paulo, Gideoni, na—zaidi ya wote—Yesu Kristo, sisi binafsi tutaona ukweli wa maneno haya: “Hekima i pamoja na wenye kiasi.”—Mithali 11:2, NW.

      [Maelezo ya Chini]

      a Neno la Kigiriki lililotafsiriwa “walio chini” linaweza kurejezea mtumwa ambaye alipiga makasia katika sehemu ya chini ya meli kubwa. Kwa kutofautisha, huenda “wasimamizi-nyumba” wakakabidhiwa mapendeleo zaidi, labda ya kutunza nyumba nyingi. Hata hivyo, machoni pa wakubwa wengi, msimamizi-nyumba alipaswa kuwa mtiifu kama tu mtumwa mwenye kupiga makasia katika sehemu ya chini ya meli.

      b Busara na tahadhari za Gideoni hazipasi kuonwa kuwa woga. Badala yake, ujasiri wake unathibitishwa na andiko la Waebrania 11:32-38, ambapo Gideoni ameorodheshwa miongoni mwa watu ‘waliofanywa kuwa wenye nguvu’ na ‘kuwa mashujaa katika vita.’

      c Kwa kuwa sifa ya kiasi hutia ndani kutambua udhaifu wako, Yehova hawezi kusemwa kwa haki kuwa mwenye kiasi. Lakini yeye ni mnyenyekevu.—Zaburi 18:35.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki