Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • “Hakuna Hata Mmoja Wenu Atakayepotea”
    “Kutoa Ushahidi Kamili” Kuhusu Ufalme wa Mungu
    • SURA YA 26

      “Hakuna Hata Mmoja Wenu Atakayepotea”

      Paulo avunjikiwa meli, aonyesha imani kubwa na upendo kwa watu

      Matendo 27:1–28:10

      1, 2. Paulo anaelekea wapi, na huenda anafikiria nini?

      “UTAENDA kwa Kaisari.” Bado mtume Paulo anakumbuka maneno hayo ya Gavana Festo. Paulo amekaa gerezani kwa miaka miwili, kwa hiyo safari ndefu ya kwenda Roma, angalau itampa nafasi ya kuona mazingira mapya. (Mdo. 25:12) Hata hivyo, Paulo anakumbuka mengi zaidi kuhusu safari zake nyingi za baharini mbali na upepo mwanana wenye kuburudisha na maji mengi ya bahari yanayofikia upeo wa macho. Kwa kuwa wakati huu anapelekwa kwa Kaisari, huenda anajiuliza maswali mengi.

      2 Paulo amekuwa katika “hatari baharini” mara nyingi, mara tatu ameokoka baada ya meli kuvunjika. Hata wakati fulani alikaa usiku na mchana baharini. (2 Kor. 11:25, 26) Isitoshe, safari hii ni tofauti kabisa na safari zake za umishonari alipokuwa huru. Wakati huu atasafiri akiwa mfungwa, tena anaenda mbali, kilomita zaidi ya 3,000, kutoka Kaisaria hadi Roma. Je, atafika salama? Hata ikiwa atafika salama, je, atahukumiwa kifo? Kumbuka kwamba anaenda kuhukumiwa na serikali kuu katika ulimwengu wa Shetani wakati huo.

      3. Paulo aliazimia kufanya nini, nasi tutazungumzia nini katika sura hii?

      3 Kutokana na habari ambazo umesoma kuhusu Paulo, unafikiri atakata tamaa na kujihurumia akifikiria mambo yatakayompata? Hapana! Anajua atakabili hali nyingi ngumu, ijapokuwa hajui ni hali gani hususa zitakazompata. Kwa nini apoteze shangwe ya huduma yake kwa sababu ya kuhangaikia mambo asiyoweza kubadili? (Mt. 6:27, 34) Paulo anajua mapenzi ya Yehova ni kwamba atumie kila nafasi anayopata kuhubiri habari njema ya Ufalme wa Mungu, hata mbele ya watawala wa serikali. (Mdo. 9:15) Paulo aliazimia kutimiza mgawo wake, hata hali ziweje. Hilo ndilo linalopaswa kuwa azimio letu pia. Hivyo basi, acheni tuandamane na Paulo katika safari hiyo ya pekee tukifikiria jinsi tunavyoweza kufuata mfano mzuri aliotuwekea.

      “Pepo Zilizokuwa Zikivuma Kinyume Nasi” (Mdo. 27:1-7a)

      4. Paulo alianza safari yake katika meli ya aina gani, na ni nani waliosafiri pamoja naye?

      4 Paulo na wafungwa wengine walitiwa mikononi mwa ofisa Mroma anayeitwa Yulio. Ofisa huyo aliamua wapande meli ya kibiashara iliyokuwa imefika Kaisaria. Ilikuwa imetoka Adramitiamu, bandari iliyo upande wa magharibi wa pwani ya Asia Ndogo, ng’ambo ya jiji la Mitilene katika kisiwa cha Lesbos. Meli hiyo ingesafiri kuelekea kaskazini kisha kuelekea magharibi, ikitua sehemu mbalimbali ili kupakua na kupakia shehena. Meli hizo hazikukusudiwa kubeba abiria, hasa wafungwa. (Ona sanduku lenye kichwa “Safari za Baharini na Njia Zilizotumiwa na Wafanyabiashara.”) Jambo linalotia moyo ni kwamba Paulo hakuwa Mkristo pekee katikati ya kikundi hicho cha wahalifu. Waamini wengine wawili, Aristarko na Luka, walikuwa pamoja naye. Luka ndiye aliyeandika masimulizi hayo. Hatujui iwapo waandamani hao wawili walilipa nauli ili kusafiri au walikuwa watumishi wa Paulo.​—Mdo. 27:1, 2.

      SAFARI ZA BAHARINI NA NJIA ZILIZOTUMIWA NA WAFANYABIASHARA

      Katika ulimwengu wa kale, meli zilitumiwa kusafirisha mizigo si abiria. Watu waliotaka kusafiri walilazimika kutafuta meli ya wafanyabiashara inayoelekea katika eneo wanaloenda. Kisha, wangekubaliana nauli ya usafiri na kusubiri hadi meli itakapoondoka.

      Maelfu ya meli zilisafiri katika Bahari ya Mediterania zikisafirisha vyakula na bidhaa nyingine. Wengi waliosafiri katika meli hizo walilazimika kulala kwenye sitaha, labda katika vibanda walivyotengeneza kila jioni na kubomolewa kila asubuhi. Pia, walihitaji kujibebea vitu walivyohitaji kama vile chakula na vitu vya kulalia.

      Muda ambao safari ingechukua ulitegemea upepo. Kwa sababu ya hali mbaya ya hewa wakati wa majira ya baridi kali, meli hazikusafiri kuanzia katikati ya Novemba mpaka katikati ya Machi.

      Meli ya kale na sehemu zake kuu nne kuanzia kwenye tezi mpaka omo. 1. Makasia. 2. Tanga kuu. 3. Nanga. 4. Tanga la mbele.

      5. Paulo alifurahia ushirika gani alipokuwa Sidoni, nasi tunajifunza nini?

      5 Baada ya kukaa siku nzima baharini, wakiwa wamesafiri kilomita 110 hivi kuelekea upande wa kaskazini, meli hiyo ilitia nanga Sidoni, katika pwani ya Siria. Yaonekana Yulio hakumtendea Paulo kama alivyokuwa akiwatendea wafungwa, huenda ni kwa sababu Paulo alikuwa raia wa Roma naye hakuwa ameshtakiwa na kuthibitishwa kuwa na hatia. (Mdo. 22:27, 28; 26:31, 32) Yulio alimruhusu Paulo ashuke na kwenda kuwatembelea Wakristo wenzake. Lazima ndugu na dada hao waliliona kuwa pendeleo kubwa kumsaidia mtume huyo baada ya kufungwa kwa muda mrefu! Je, kuna pindi zozote unazoweza kuonyesha ukarimu kama huo kwa upendo nawe utiwe moyo pia?​—Mdo. 27:3.

      6-8. Safari ya Paulo kutoka Sidoni hadi Kinido ilikuwaje, na huenda alipata nafasi gani ya kuhubiri?

      6 Kisha, meli ikang’oa nanga kutoka Sidoni, na kusafiri kandokando ya pwani, ikapita Kilikia, karibu na Tarso, jiji la nyumbani kwa Paulo. Luka hataji vituo vingine, ijapokuwa anataja hali ya anga ambayo haikuwa shwari, anaposema ‘pepo zilikuwa zikivuma kinyume nasi.’ (Mdo. 27:4, 5) Haikosi Paulo alitumia kila nafasi ili kuhubiri habari njema. Bila shaka aliwahubiria wafungwa wenzake na wengine waliokuwa kwenye meli hiyo, kutia ndani mafundi wa mitambo na askari, na pia watu wengine wowote aliokutana nao meli ilipotia nanga katika bandari mbalimbali. Je, sisi hutumia kila nafasi tunayopata ili kuhubiri?

      7 Baada ya muda, meli hiyo ilifika Mira, bandari iliyo katika pwani ya kusini ya Asia Ndogo. Huko Paulo na wenzake walipanda meli nyingine, ambayo ingewafikisha Roma. (Mdo. 27:6) Siku hizo, Misri ilikuwa ghala ya Roma, na meli za nafaka kutoka Misri zilikuwa zikitia nanga Mira. Yulio alipata mojawapo ya meli hizo na kuwapandisha askari na wafungwa. Lazima meli hiyo ilikuwa kubwa zaidi kuliko ile ya kwanza. Ilikuwa na shehena kubwa ya ngano na abiria 276—mafundi wa mitambo, wafungwa, na huenda watu wengine waliokuwa wakielekea Roma. Bila shaka, katika meli hiyo, Paulo alipata eneo jipya la kuhubiri, naye hakusita kufanya hivyo.

      8 Kituo kilichofuata ni Kinido, kusini magharibi mwa Asia Ndogo. Kwa kawaida meli zingeweza kusafiri umbali huo kwa siku moja ikiwa hali ya hewa ni shwari. Hata hivyo, kama Luka anavyoripoti, “baada ya kusafiri polepole kwa siku kadhaa, tukafika kwa shida huko Kinido.” (Mdo. 27:7a) Bahari ilizidi kuchafuka. (Ona sanduku lenye kichwa “Pepo Hatari za Mediterania.”) Wazia hali ya watu waliokuwa katika meli hiyo huku wakikabili pepo zenye nguvu na bahari iliyochafuka.

      PEPO HATARI ZA MEDITERANIA

      Safari za meli za biashara katika Bahari ya Mediterania, inayoitwa pia Bahari Kuu, zilitegemea sana pepo na majira. Katika upande wa mashariki wa bahari hiyo, kwa kawaida pepo zilikuwa zikivuma kutoka magharibi kuelekea mashariki kuanzia Juni hadi Septemba. Kwa sababu hiyo, ilikuwa rahisi kusafiri kuelekea upande wa mashariki, kama ilivyokuwa wakati Paulo alipokuwa akirudi kutoka katika safari yake ya tatu ya umishonari. Yeye na wenzake walikuwa katika meli iliyotoka Mileto, ikapitia Rode, na kutia nanga Patara. Kisha meli hiyo ilisafiri moja kwa moja hadi Tiro, katika pwani ya Foinike. Luka anasema kwamba walipita kisiwa cha Kipro, kilichokuwa upande wao wa kushoto, ikimaanisha kwamba walikuwa wakisafiri kuelekea upande wa kusini wa Kipro.​—Mdo. 21:1-3.

      Namna gani safari za kuelekea magharibi? Meli zingeweza kuelekea upande wa magharibi zikifuata njia hiyohiyo iwapo pepo zingeruhusu. Lakini wakati mwingine haikuwezekana. Kitabu The International Standard Bible Encyclopedia kinasema hivi: “Wakati wa majira ya baridi kali, hali ya anga hubadilika badilika sana na vimbunga vikali huvuma kuelekea upande wa mashariki wa Mediterania, na kusababisha mvua nyingi au hata theluji.” Kulikuwa na hatari nyingi sana kwa sababu ya hali hizo.

      Katika majira yoyote, vyombo vilivyokuwa karibu na ufuo vingeweza kusafiri kuelekea kaskazini kandokando ya pwani ya Palestina na kuendelea na safari hadi Pamfilia. Mwishoni mwa safari hiyo, upepo mwanana kutoka nchi kavu na mikondo inayoelekea magharibi ilirahisisha safari za meli. Ndivyo ilivyokuwa katika sehemu ya kwanza ya safari ya Paulo kuelekea Roma akiwa mfungwa. Hata hivyo, nyakati nyingine pepo zingebadili mwelekeo na kuwa hatari. (Mdo. 27:4) Inawezekana kwamba meli ya nafaka inayotajwa sana katika masimulizi ya Luka ilisafiri kuelekea upande wa kaskazini kutoka Misri, kisha ikazunguka na kuingia bahari iliyokuwa salama kati ya Kipro na Asia Ndogo. Kutoka Mira, kapteni wa meli alikusudia kuendelea na safari kuelekea upande wa magharibi—azunguke chini ya Ugiriki, kisha apande kuelekea upande wa magharibi wa Italia. (Mdo. 27:5, 6) Hata hivyo, pepo na majira yalibadili kabisa safari hiyo!

      “Tukirushwarushwa kwa Nguvu na Dhoruba” (Mdo. 27:7b-26)

      9, 10. Ni hali gani ngumu zilizotokea karibu na Krete?

      9 Kapteni wa meli hiyo alipanga kuendelea na safari kuelekea upande wa magharibi kutoka Kinido, hata hivyo, Luka anasema “upepo ulituzuia kusonga mbele.” (Mdo. 27:7b) Meli ilipoanza kwenda mbali na nchi kavu, ilipoteza mkondo, kisha upepo mkali kutoka kaskazini magharibi ukaisukuma, huenda kwa kasi sana. Kama vile meli hiyo ilivyolindwa na kisiwa cha Kipro awali kutokana na pepo zilizokuwa zikivuma kinyume, ililindwa pia na kisiwa cha Krete. Baada ya meli hiyo kupita rasi ya Salmone upande wa mashariki wa Krete, kukawa na utulivu kiasi. Kwa nini? Kwa sababu meli hiyo ilikuwa upande wa kusini wa kisiwa hicho, na hivyo ililindwa kutokana na zile pepo kali. Wazia furaha ya muda waliokuwa nayo watu katika meli hiyo! Hata hivyo, maadamu meli bado ilikuwa baharini, mafundi wa mitambo hawangeweza kupuuza majira ya baridi kali yaliyokuwa yakikaribia. Walikuwa na wasiwasi.

      10 Luka anasema hivi kwa usahihi: “Tukasafiri kwa shida kandokando ya pwani [ya Krete], tukafika mahali panapoitwa Bandari Nzuri.” Hata hivyo, bado haikuwa rahisi kuendesha meli hiyo. Mwishowe, walitia nanga katika ghuba ndogo inayodhaniwa kuwa ilikuwa katika eneo la pwani, kabla tu ya kugeuka kuelekea kaskazini. Walikaa hapo muda gani? Luka anasema walikaa “muda mrefu,” hata hivyo, hawakuwa na wakati wa kupoteza, kwa sababu Septemba na Oktoba ni miezi hatari kusafiri.​—Mdo. 27:8, 9.

      11. Paulo aliwapa wenzake ushauri gani, hata hivyo waliamua kufanya nini?

      11 Huenda abiria fulani walimwomba Paulo ushauri kwa sababu alikuwa na uzoefu wa kusafiri katika Bahari ya Mediterania. Alipendekeza wasitishe safari, kwa kuwa ikiwa wangeendelea, wangepatwa na “madhara na hasara kubwa,” na huenda baadhi yao wangepoteza uhai. Hata hivyo, nahodha na mwenye meli walitaka kuendelea na safari, huenda kwa kuwa walitaka kufika haraka mahali salama zaidi. Walimsadikisha Yulio, na wengi wao wakakubaliana wajaribu kufika Feniki, bandari iliyokuwa mbali kidogo katika pwani hiyo. Huenda ilikuwa bandari kubwa na nzuri zaidi, mahali ambapo wangeweza kukaa wakati wa majira ya baridi kali. Kwa hiyo, upepo mwanana ulipoanza kupunga kutoka upande wa kaskazini, meli ikang’oa nanga.​—Mdo. 27:10-13.

      12. Baada ya kuondoka Krete, meli ilikumbwa na nini, nao mafundi wa mitambo walifanya nini ili kujaribu kuepuka msiba?

      12 Kisha mambo yakawa mabaya zaidi: kukazuka “upepo mkali” kutoka kaskazini mashariki. Kwa muda fulani, walifichwa na “kisiwa kidogo kinachoitwa Kauda,” kilomita 65 hivi kutoka Bandari Nzuri. Hata hivyo, bado meli hiyo ilikuwa hatarini, ingeweza kusukumwa upande wa kusini na kugonga ukingo wa bahari kwenye pwani ya Afrika. Wakihofia hali hiyo, mabaharia hao wakaivuta mashua ndogo iliyokuwa ikikokotwa na meli yao. Haikuwa rahisi kwa sababu inawezekana ilikuwa imejaa maji. Kisha wakajaribu kuikaza meli isivunjike, wakipitisha kamba au minyororo chini yake ili kushikilia mbao zake pamoja. Kisha wakashusha vifaa vya kuendeshea, tanga na kamba za mlingoti, na kung’ang’ana kuielekeza meli hiyo katika upepo huo hadi dhoruba ipite. Wazia jinsi tukio hilo lilivyokuwa lenye kuogopesha! Hata baada ya kufanya yote hayo, bado meli hiyo iliendelea ‘kurushwarushwa kwa nguvu na dhoruba.’ Siku ya tatu, wakatupa ayari majini, huenda ili kuiwezesha meli hiyo kuelea vizuri.​—Mdo. 27:14-19.

      13. Hali ilikuwaje katika meli ya Paulo wakati wa dhoruba?

      13 Wote walikuwa na hofu kubwa. Hata hivyo, Paulo na wenzake walijipa moyo. Bwana alikuwa amemhakikishia Paulo kwamba atatoa ushahidi Roma, na baadaye malaika akamthibitishia ahadi hiyo. (Mdo. 19:21; 23:11) Hata hivyo, dhoruba hiyo iliendelea kwa majuma mawili, usiku na mchana. Kwa sababu ya mvua iliyokuwa ikinyesha daima na mawingu mazito yaliyozuia nuru ya jua na nyota, kapteni wa meli hangeweza kuona mbali wala kujua wako wapi. Wasafiri hata hawakuweza kula chakula. Isitoshe, ni nani angeweza kula katika mazingira hayo ya baridi, mvua, kichefuchefu, na woga?

      14, 15. (a) Alipokuwa akizungumza na wasafiri wenzake, kwa nini Paulo aliwakumbusha ushauri wake wa awali? (b) Tunaweza kujifunza nini kutokana na ujumbe wa tumaini ambao Paulo alitangaza?

      14 Paulo akasimama. Akawakumbusha ushauri aliowapa ijapokuwa hakuwa akiwalaumu na kusema, ‘Si niliwaambia.’ Hata hivyo, mambo yaliyowapata yalionyesha wazi kwamba hawapaswi kamwe kupuuza maneno yake. Kisha akasema: “Sasa ninawahimiza mjipe moyo, kwa maana hakuna hata mmoja wenu atakayepotea, meli tu ndiyo itakayopotea.” (Mdo. 27:21, 22) Lazima maneno hayo yaliwasisimua sana waliokuwa wakimsikiliza! Bila shaka Paulo pia alifurahi sana kwa kuwa Yehova alimpa ujumbe wenye tumaini wa kuwaambia wengine. Tunapaswa kukumbuka kwamba Yehova anajali uhai wa kila mtu. Kila mtu ni mwenye thamani machoni pake. Mtume Petro aliandika: “Yehova . . . hataki yeyote aangamizwe bali hutaka wote wafikie toba.” (2 Pet. 3:9) Hivyo basi, tunapaswa kuwatangazia watu wengi iwezekanavyo ujumbe wa tumaini wa Yehova! Uhai wa watu uko hatarini.

      15 Inaelekea Paulo aliwahubiria wengi katika meli hiyo kuhusu “tumaini la ahadi iliyotolewa na Mungu.” (Mdo. 26:6; Kol. 1:5) Sasa, meli yao ikikaribia kuvunjika, Paulo angeweza kutoa msingi thabiti wa tumaini lililo karibu zaidi. Aliwaambia: “Usiku huu malaika wa Mungu ambaye mimi ni mali yake . . . , alisimama kando yangu akasema, ‘Usiogope, Paulo. Utasimama mbele ya Kaisari, na, tazama! Mungu amekupa wale wote wanaosafiri pamoja nawe.’” Kisha Paulo akawahimiza: “Basi jipeni moyo, kwa maana ninamwamini Mungu kwamba itakuwa kama nilivyoambiwa. Hata hivyo, ni lazima tutupwe kwenye ufuo wa kisiwa fulani.”​—Mdo. 27:23-26.

      “Wote Wakafika Salama Kwenye Nchi Kavu” (Mdo. 27:27-44)

      Paulo akisali katika meli ya mizigo iliyojaa watu. Baadhi ya abiria waliochoka wameinamisha vichwa vyao huku wengine wakiwaangalia. Kuna mikate juu ya baadhi ya masanduku.

      “Akamshukuru Mungu mbele yao wote.”—Matendo 27:35

      16, 17. (a) Paulo alitumia nafasi gani kutoa sala, na matokeo yalikuwa nini? (b) Mambo aliyotabiri Paulo yalitimiaje?

      16 Baada ya majuma mawili yenye kutia hofu, na baada ya meli kusukumwa na upepo kilomita 870 hivi, mabaharia hao walianza kuona ishara za mabadiliko, huenda hata walianza kusikia mawimbi yakigonga nchi kavu. Walishusha nanga kutoka kwenye tezi ili wasichukuliwe na mawimbi nao wakaanza kuielekeza meli nchi kavu endapo wangeweza kuifikisha pwani. Kisha, wakajaribu kuondoka melini lakini wakazuiwa na askari. Paulo akamwambia ofisa wa jeshi pamoja na askari hao: “Watu hawa wasipobaki katika meli, ninyi hamwezi kuokoka.” Sasa, meli ikiwa imara kiasi, Paulo aliwahimiza wale chakula, akiwahakikishia tena kwamba wataokoka. Kisha Paulo “akamshukuru Mungu mbele yao wote.” (Mdo. 27:31, 35) Kwa kutoa sala hiyo ya shukrani, Paulo aliwawekea mfano mzuri Luka, Aristarko, na Wakristo wa leo. Je, sala unazotoa mbele za wengine ni zenye kutia moyo na kuwafariji wengine?

      17 Baada ya Paulo kutoa sala, “wote wakajipa moyo, nao pia wakaanza kula.” (Mdo. 27:36) Kisha, wakaanza kupunguza uzito kwa kutupa baharini shehena ya ngano, na hivyo kuiwezesha meli kuelea zaidi inapokaribia pwani. Kulipopambazuka, wakakata nanga, wakafungua amari za makasia ya mtambo wa usukani, na kutweka tanga la mbele ili waweze kuiongoza meli hadi pwani. Omo ya meli ikakwama, huenda katika mchanga au matope, nayo tezi ikaanza kuvunjika kwa sababu ya mawimbi. Askari fulani walitaka kuwaua wafungwa ili yeyote kati yao asitoroke, lakini Yulio akaingilia kati na kuwazuia. Akawahimiza wote waogelee au kuelea juu ya mbao hadi nchi kavu. Aliyotabiri Paulo yakatimia—wote 276 wakaokoka. Ndiyo, “wote wakafika salama kwenye nchi kavu.” Hata hivyo, walikuwa wapi?​—Mdo. 27:44.

      “Fadhili Zinazopita za Kawaida” (Mdo. 28:1-10)

      18-20. Watu wa Malta walionyesha jinsi gani “fadhili zinazopita za kawaida,” na Mungu alifanya muujiza gani kupitia Paulo?

      18 Waokokaji hao walijikuta katika kisiwa cha Malta, upande wa kusini wa Sisili. (Ona sanduku lenye kichwa “Kisiwa cha Malta Kilikuwa Wapi?”) Watu wa kisiwa hicho wanaozungumza lugha ya kigeni walionyesha “fadhili zinazopita za kawaida.” (Mdo. 28:2) Waliwasha moto kwa ajili ya watu hao wasiowajua waliofika pwani wakiwa wamelowa na kutetemeka kwa sababu ya baridi. Moto huo uliwasaidia kujipasha joto. Hali hiyo pia ilitokeza muujiza.

      19 Paulo alijitolea kusaidia kazi. Alikusanya kuni kadhaa, na kuzitia motoni. Alipokuwa akifanya hivyo, nyoka mwenye sumu akatokea, akamuuma, na kujifunga mkononi mwake. Wenyeji hao wa Malta walidhani ni adhabu kutoka kwa Mungu.a

      20 Wenyeji waliomwona nyoka huyo akimuuma Paulo walifikiri “atavimba.” Kulingana na kitabu kimoja, neno la lugha ya awali linalotumiwa hapa ni “neno la kitiba.” Haishangazi kuona “Luka, daktari mpendwa” akitumia neno hilo katika masimulizi yake. (Mdo. 28:6; Kol. 4:14) Vyovyote vile, Paulo alimkung’uta nyoka huyo, naye hakupatwa na madhara yoyote.

      21. (a) Ni habari gani hususa, au sahihi, tunazopata katika masimulizi ya Luka? (b) Paulo alifanya miujiza gani, nayo ilikuwa na matokeo gani kwa wenyeji wa Malta?

      21 Publio, tajiri mwenye mashamba alikuwa akiishi katika eneo hilo. Huenda alikuwa mwakilishi mkuu wa Roma katika kisiwa cha Malta. Luka anamwita “mkuu wa kisiwa hicho,” akitumia jina la cheo linalopatikana katika vitabu viwili vya Kimalta. Aliwakaribisha Paulo na wenzake kwa siku tatu. Hata hivyo, baba ya Publio alikuwa mgonjwa. Kwa mara nyingine tena, Luka anafafanua hali yake kwa usahihi. Anataja ugonjwa hususa aliokuwa nao akisema kwamba “alikuwa amelala kitandani akiugua homa na ugonjwa wa kuhara damu.” Paulo alisali na kuweka mikono yake juu yake, naye akapona. Wakiwa wamevutiwa sana na muujiza huo, wenyeji wa kisiwa hicho wakaleta wagonjwa wengine waponywe, nao wakaleta zawadi kwa ajili ya mahitaji ya Paulo na wenzake.​—Mdo. 28:7-10.

      22. (a) Profesa mmoja amesema nini kuhusu masimulizi ya Luka ya safari ya kwenda Roma? (b) Tutazungumzia nini katika sura inayofuata?

      22 Habari kuhusu safari ya Paulo tuliyozungumzia kufikia sasa ni sahihi na kweli. Profesa mmoja alisema: “Masimulizi ya Luka . . . ni mojawapo ya masimulizi yaliyo wazi zaidi katika Biblia nzima. Mambo mbalimbali yanayotajwa kuhusu safari za baharini katika karne ya kwanza ni sahihi kabisa na hali zinazozungumziwa za upande wa mashariki wa Mediterania ni sahihi kabisa,” hivi kwamba lazima ziliandikwa kwa kutegemea daftari ya matukio ya kila siku ya mtu aliyekuwa katika safari hiyo. Yawezekana kwamba Luka alinakili mambo hayo alipokuwa akisafiri na mtume Paulo. Ikiwa alifanya hivyo, basi Luka alikuwa na mengi ya kuandika katika sehemu inayofuata ya safari hiyo. Paulo angepatwa na nini baada ya kufika Roma? Tutaona katika sura inayofuata.

      KISIWA CHA MALTA KILIKUWA WAPI?

      Visiwa mbalimbali vimedhaniwa kuwa “Malta,” ambako meli ya Paulo ilivunjikia. Watu fulani wanakisia kwamba ni kisiwa fulani karibu na Corfu, katika pwani ya magharibi ya Ugiriki. Makisio ya wengine yanategemea neno “Malta” linalotumiwa katika kitabu cha Matendo. Katika Kigiriki, neno hilo ni Me·liʹte. Kwa hiyo, wanafikiri kisiwa hicho ni Melite Illyrica, ambacho sasa kinaitwa Mljet, kilicho katika Bahari ya Adriatiki, karibu na pwani ya Kroatia.

      Ni kweli kwamba andiko la Matendo 27:27 linataja “Bahari ya Adria,” hata hivyo katika siku za Paulo, “Adria” ilitia ndani eneo kubwa zaidi kuliko Bahari ya Adriatiki ya leo. Ilitia ndani Bahari ya Ionia na bahari zilizo upande wa mashariki wa Sisili na upande wa magharibi wa Krete, hivyo ikitia ndani bahari iliyo karibu na eneo ambalo leo linaitwa Malta.

      Meli ambayo Paulo alipanda ililazimika kuelekea upande wa kusini kutoka Kinido kuelekea Krete. Kwa sababu ya pepo za dhoruba hiyo, haielekei kwamba meli hiyo iligeuka na kusafiri kuelekea kaskazini mpaka Mljet au kisiwa kingine karibu na Corfu. Kwa hiyo, uwezekano mkubwa ni kwamba kisiwa cha Malta kilikuwa upande wa magharibi. Ikiwa ndivyo, kisiwa cha Malta kingekuwa upande wa kusini wa Sisili, mahali ambapo huenda ndipo meli inayozungumziwa ilivunjikia.

      a Kwa kuwa wenyeji waliwajua nyoka hao, yaonekana kwamba nyoka hao walikuwako katika kisiwa cha Malta nyakati hizo. Leo, hawapatikani huko. Huenda sababu ikawa kwamba kadiri ambavyo miaka imepita, kumekuwa na mabadiliko ya mazingira. Au nyoka hao waliisha kwa sababu ya ongezeko la watu kwenye kisiwa hicho.

  • “Kutoa Ushahidi Kamili”
    “Kutoa Ushahidi Kamili” Kuhusu Ufalme wa Mungu
    • SURA YA 27

      “Kutoa Ushahidi Kamili”

      Paulo afungwa Roma, aendelea kuhubiri

      Matendo 28:11-31

      1. Paulo na wenzake wana uhakika gani, na kwa nini?

      MELI yenye sanamu ya “Wana wa Zeu,” ambayo huenda ni meli kubwa ya nafaka, inasafiri kutoka kisiwani Malta katika Bahari ya Mediterania kwenda Italia. Ni mwaka wa 59 hivi W.K. Mtume Paulo—mfungwa aliye chini ya ulinzi wa askari—pamoja na Wakristo wenzake, Luka na Aristarko, wako katika meli hiyo. (Mdo. 27:2) Tofauti na mafundi wa mitambo wa meli hiyo, waeneza injili hao hawahitaji ulinzi wa ndugu pacha Castor na Pollux, wana wa Zeu, mungu wa Wagiriki. (Mdo. 28:11) Paulo na wenzake ni waabudu wa Yehova, aliyetabiri kwamba Paulo atatoa ushahidi kuhusu ile kweli jijini Roma na kwamba atasimama mbele ya Kaisari.​—Mdo. 23:11; 27:24.

      2, 3. Meli ya Paulo inaelekea wapi, na anategemezwa jinsi gani katika safari yake?

      2 Siku tatu baada ya kutia nanga Sirakusa, jiji lenye kupendeza la Sisili na maarufu kama Athene na Roma, meli yang’oa nanga na kuelekea Regiamu katika rasi ya Italia. Kisha, ikisukumwa na upepo wa kusi, meli hiyo yasafiri umbali wa kilomita 320 hadi bandari ya Italia inayoitwa Puteoli (karibu na mahali panapoitwa Naples leo), na kufika huko siku ya pili, haraka kuliko ilivyo kawaida.​—Mdo. 28:12, 13.

      3 Sasa, Paulo anaanza sehemu ya mwisho ya safari ya kuelekea Roma, ambapo atasimama mbele ya Maliki Nero. Katika safari yake yote, “Mungu wa faraja yote” amekuwa pamoja na Paulo. (2 Kor. 1:3) Kama tutakavyoona, Yehova hakumwacha kamwe; naye Paulo hakupunguza bidii yake akiwa mmishonari.

      “Paulo. . . Akamshukuru Mungu na Kujipa Moyo” (Mdo. 28:14, 15)

      4, 5. (a) Ni ukarimu gani ambao Paulo na wenzake walionyeshwa walipofika Puteoli, na kwa nini Paulo alipewa uhuru mwingi? (b) Hata wanapofungwa gerezani, Wakristo wanaweza kunufaikaje kutokana na mwenendo wao mzuri?

      4 Walipofika Puteoli, Paulo na wenzake ‘waliwakuta akina ndugu huko, wakawasihi wakae pamoja nao kwa siku saba.’ (Mdo. 28:14) Huo ni mfano mzuri sana wa ukarimu wa Kikristo! Bila shaka ndugu hao wakarimu walibarikiwa hata zaidi kwa kuwa Paulo na wenzake waliwatia moyo kiroho. Hata hivyo, mfungwa anayelindwa angewezaje kupata uhuru mwingi hivyo? Huenda kwa sababu walinzi hao Waroma walimwamini kabisa mtume huyo.

      5 Vivyo hivyo leo, watumishi wa Yehova, wanapokuwa katika magereza na kambi za mateso, mara nyingi hupewa uhuru zaidi na kuruhusiwa kufanya mambo ambayo wafungwa wengine hawawezi kwa sababu wakiwa Wakristo, ni wanyoofu na wenye kutegemeka. Kwa mfano, nchini Romania, mtu aliyehukumiwa kifungo cha miaka 75 kwa kosa la wizi, alianza kujifunza Neno la Mungu na kufanya mabadiliko makubwa maishani. Kwa sababu ya mabadiliko aliyokuwa amefanya, wenye mamlaka gerezani walimpa kazi ya kwenda mjini—akiwa peke yake—na kununua vitu vinavyohitajiwa gerezani! Zaidi ya yote, mwenendo wetu mzuri humtukuza Yehova.​—1 Pet. 2:12.

      6, 7. Akina ndugu wa Roma walionyeshaje ukarimu wa pekee?

      6 Kutoka Puteoli, yawezekana kwamba Paulo na wenzake walitembea kwa miguu kilomita 50 hivi hadi Kapua kwenye Njia ya Apio, inayoenda Roma. Ikiwa imetandazwa kwa mawe, njia hiyo maarufu ilikuwa na mandhari zenye kuvutia za nchi ya Italia, na mtu akiwa sehemu fulani katika njia hiyo, angeweza hata kuiona Bahari ya Mediterania. Pia, njia hiyo ilipitia Pontine Marshes, eneo lenye majimaji, kilomita 60 hivi kutoka Roma, ambapo Soko la Apio lilikuwa. Ndugu wa Roma “waliposikia habari zetu,” aandika Luka, baadhi yao walikuja mpaka Soko la Apio, na wengine wakasubiri mahali pa kupumzika panapoitwa Mikahawa Mitatu, umbali wa kilomita 50 hivi kutoka Roma. Walimpenda sana Paulo.​—Mdo. 28:15.

      7 Soko la Apio halikuwa mahali pa kustarehesha, hasa kwa wasafiri waliohitaji kupumzika baada ya safari ndefu yenye kuchosha. Horace, mshairi Mroma, anataja kwamba soko hilo lilikuwa “limesongamana na wenye mashua na wenye mikahawa wajeuri.” Aliandika kwamba “maji yalikuwa yenye kuchukiza.” Naye hata alikataa kula mahali hapo! Bila kujali yote hayo, akina ndugu kutoka Roma walimngoja Paulo na wenzake ili kuwasindikiza katika sehemu ya mwisho ya safari yao.

      8. Kwa nini Paulo alimshukuru Mungu “alipowaona” ndugu zake?

      8 “Alipowaona” ndugu zake, masimulizi yanasema, “Paulo . . . akamshukuru Mungu na kujipa moyo.” (Mdo. 28:15) Ndiyo, alipowaona tu ndugu hao wapendwa, ambao huenda mtume huyo aliwajua baadhi yao kibinafsi, alihisi kwamba amepata nguvu mpya na kufarijiwa. Kwa nini Paulo alimshukuru Mungu? Alijua kwamba upendo usio na ubinafsi ni sehemu ya tunda la roho. (Gal. 5:22) Leo pia, roho takatifu huwachochea Wakristo kujitoa kwa ajili ya wengine na kuwafariji wenye uhitaji.​—1 The. 5:11, 14.

      9. Tunaweza kuigaje roho iliyoonyeshwa na ndugu waliokuja kumpokea Paulo?

      9 Kwa mfano, roho takatifu huwachochea akina ndugu kuwaonyesha ukarimu waangalizi wa mzunguko, wamishonari, na watumishi wengine wa wakati wote, ambao wengi wao wamejinyima mengi ili kumtumikia Yehova kikamili zaidi. Jiulize: ‘Kuna lolote ninaloweza kufanya ili kutegemeza ziara ya mwangalizi wa mzunguko, labda kwa kumwonyesha ukarimu yeye na mke wake ikiwa ameoa? Ninaweza kupanga kuhubiri pamoja nao?’ Ukifanya hivyo utapata baraka nyingi. Kwa mfano, wazia shangwe ambayo ndugu wa Roma walipata walipokuwa wakimsikiliza Paulo na wenzake wakisimulia mambo mengi waliyojionea yenye kujenga imani.​—Mdo. 15:3, 4.

      “Yanasemwa Vibaya Kila Mahali” (Mdo. 28:16-22)

      10. Hali ya Paulo ilikuwaje huko Roma, na mtume huyo alifanya nini mara tu baada ya kufika huko?

      10 Mwishowe, kikundi hicho cha wasafiri kilipoingia Roma, “Paulo aliruhusiwa kukaa peke yake akiwa na mwanajeshi aliyemlinda.” (Mdo. 28:16) Kwa kawaida, wafungwa wa makosa madogo walizuiliwa kwa kufungwa kwa minyororo pamoja na askari walinzi. Hata hivyo, kwa kuwa Paulo alikuwa mtangazaji wa Ufalme, minyororo hiyo haikumfunga kinywa. Kwa hiyo, baada ya kupumzika kwa siku tatu, akawaita wakuu wa Wayahudi waliokuwa Roma ili ajitambulishe na kuwatolea ushahidi.

      11, 12. Alipokuwa akizungumza na Wayahudi wenzake, Paulo alijaribu jinsi gani kuondoa chuki yoyote ambayo huenda walikuwa nayo kumwelekea?

      11 Paulo akasema hivi: “Wanaume, akina ndugu, ingawa sikuwa nimefanya jambo lolote kinyume cha watu au desturi za mababu zetu, nilikabidhiwa nikiwa mfungwa kutoka Yerusalemu na kutiwa mikononi mwa Waroma. Na baada ya kufanya uchunguzi, walitaka kuniacha huru, kwa maana hawakuwa na sababu yoyote ya kuniua. Lakini Wayahudi walipopinga, nililazimika kukata rufaa kwa Kaisari, lakini si kwa sababu nilikuwa na shtaka lolote dhidi ya taifa langu.”​—Mdo. 28:17-19.

      12 Kwa kuwaita Wayahudi hao “ndugu,” Paulo alijaribu kujenga urafiki na kuondoa chuki yoyote ambayo huenda ilikuwa kati yao. (1 Kor. 9:20) Pia, aliwajulisha wazi kwamba hakuja kuwalaumu Wayahudi wenzake, bali ili kukata rufaa kwa Kaisari. Hata hivyo, Wayahudi hao walishangaa kusikia kwamba amekuja kukata rufaa. (Mdo. 28:21) Kwa nini Wayahudi wa Yudea hawakuwajulisha lolote? Kitabu kimoja kinasema: “Inaonekana kwamba meli ya Paulo ilikuwa miongoni mwa meli za kwanza kufika Italia baada ya majira ya baridi kali, nao wawakilishi wa wenye mamlaka miongoni mwa Wayahudi wa Yerusalemu hawakuwa wamefika, wala barua zozote kuhusu kesi hiyo hazikuwa zimewasili.”

      13, 14. Paulo alianzaje kuzungumzia Ufalme, na tunawezaje kuiga mfano wake?

      13 Kisha, Paulo akaanza kuzungumza kuhusu Ufalme. Alianza kwa kutaja jambo ambalo bila shaka liliamsha hamu ya Wayahudi waliokuwa wamekuja. Alisema: “Kwa sababu hii niliomba kuwaona na kuzungumza nanyi, kwa maana nimefungwa mnyororo huu kwa sababu ya tumaini la Israeli.” (Mdo. 28:20) Tumaini hilo lilitegemea Masihi na Ufalme wake uliokuwa ukitangazwa na kutaniko la Kikristo. Wazee hao Wayahudi wakamjibu: “Tunaona inafaa kusikia kutoka kwako maoni yako, kwa maana kwa kweli kuhusu madhehebu haya, tunajua yanasemwa vibaya kila mahali.”​—Mdo. 28:22.

      14 Tunapopata nafasi ya kutangaza habari njema, tunaweza kufuata mfano wa Paulo kwa kutumia maneno yanayoamsha hamu ya wasikilizaji wetu. Tunaweza kupata mapendekezo mazuri katika vitabu kama vile Kutoa Sababu kwa Kutumia Maandiko, Faidika na Elimu ya Shule ya Huduma ya Kitheokrasi na Boresha Uwezo Wako wa Kusoma na Kufundisha. Je, unavitumia vizuri vitabu hivyo vya kujifunzia Biblia?

      “Kutoa Ushahidi Kamili”​—Mfano Tunaoweza Kufuata (Mdo. 28:23-29)

      15. Ni mambo gani manne yanayojitokeza wazi kuhusiana na njia ya Paulo ya kuhubiri?

      15 Siku iliyopangwa, Wayahudi wenyeji “wakaja wakiwa wengi hata zaidi,” mahali alipoishi Paulo. Naye akawafafanulia jambo hilo “kuanzia asubuhi mpaka jioni . . . na kutoa ushahidi kamili kuhusu Ufalme wa Mungu, ili kuwashawishi kumhusu Yesu kwa kutumia Sheria ya Musa na pia Manabii.” (Mdo. 28:23) Mambo manne yanajitokeza wazi kuhusiana na njia ya Paulo ya kuhubiri. Kwanza, alikazia Ufalme wa Mungu. Pili, alijitahidi kuchochea mioyo ya wasikilizaji wake kwa kuwashawishi. Tatu, alijadiliana nao kwa kutumia Maandiko. Nne, alijitolea kwa nafsi yote, akiwahubiria “kuanzia asubuhi mpaka jioni.” Alituwekea mfano mzuri sana! Alipata matokeo gani? “Baadhi yao wakaanza kuamini,” lakini wengine hawakuamini. Mgawanyiko ukazuka, nao watu “wakaanza kuondoka,” asema Luka.​—Mdo. 28:24, 25a.

      16-18. Kwa nini kutoitikia kwa Wayahudi wa Roma hakukumshangaza Paulo, na tunapaswa kuhisije ujumbe wetu unapokataliwa?

      16 Hilo halikumshangaza Paulo, kwa kuwa lilipatana na unabii wa Biblia, isitoshe haikuwa mara ya kwanza kwake kujionea hilo. (Mdo. 13:42-47; 18:5, 6; 19:8, 9) Kwa hiyo, Paulo akawaambia wale waliokuwa wakiondoka: “Kwa kufaa roho takatifu ilisema kupitia Isaya nabii kwa mababu zenu, ikisema, ‘Nenda kwa watu hawa uwaambie: “Kwa kweli mtasikia lakini hamtaelewa kamwe, na kwa kweli mtatazama, lakini hamtaona kamwe. Kwa maana mioyo ya watu hawa imekuwa migumu.”’” (Mdo. 28:25b-27) Neno la lugha ya awali linalotafsiriwa “mgumu” hurejelea moyo “mnene” au “wenye mafuta mengi,” hivi kwamba ujumbe wa Ufalme haungeweza kupenya. (Mdo. 28:27) Ilikuwa hali yenye kusikitisha sana!

      17 Tofauti na Wayahudi hao, Paulo alisema kwamba, ‘mataifa wangesikiliza.’ (Mdo. 28:28; Zab. 67:2; Isa. 11:10) Bila shaka, mtume huyo angeweza kusema hivyo akiwa na uhakika, kwa sababu alijionea Watu wa Mataifa wakikubali ujumbe wa Ufalme!—Mdo. 13:48; 14:27.

      18 Kama Paulo, hatupaswi kuvunjika moyo watu wanapokataa habari njema. Tayari tunajua kwamba ni wachache watakaoipata barabara inayoongoza kwenye uzima. (Mt. 7:13, 14) Pia, watu wenye mwelekeo unaofaa wanapojiunga na ibada ya kweli, tunapaswa kufurahi na kuwakaribisha kwa moyo wote.​—Luka 15:7.

      “Akiwahubiria Ufalme wa Mungu” (Mdo. 28:30, 31)

      19. Ni kwa njia gani Paulo alitumia hali zake vizuri?

      19 Luka anamalizia masimulizi yake kwa jambo lenye kutia moyo sana. Anasema hivi: “[Paulo] akakaa huko kwa miaka miwili kamili katika nyumba yake ya kukodi, naye alikuwa akiwakaribisha kwa fadhili wale wote waliomtembelea, akiwahubiria Ufalme wa Mungu na kuwafundisha kumhusu Bwana Yesu Kristo kwa uhuru mwingi wa kusema, bila kizuizi.” (Mdo. 28:30, 31) Hicho ni kielelezo kizuri sana cha ukarimu, imani, na bidii!

      20, 21. Taja watu mbalimbali walionufaika na huduma ya Paulo katika jiji la Roma.

      20 Mmoja wa watu waliopokewa na Paulo kwa fadhili ni Onesimo, mtumwa aliyetoroka Kolosai. Paulo alimsaidia Onesimo kuwa Mkristo, naye Onesimo akawa “ndugu . . . mwaminifu na mpendwa” kwa Paulo. Paulo anamwita “mwanangu . . . ambaye nimekuwa baba yake.” (Kol. 4:9; Flm. 10-12) Bila shaka Onesimo alimtia moyo sana Paulo!a

      21 Wengine pia walinufaika na mfano mzuri wa Paulo. Aliwaandikia hivi Wafilipi: “Hali yangu kwa kweli imesaidia kuendeleza habari njema, hivi kwamba vifungo vyangu vya gereza kwa ajili ya Kristo vimejulikana wazi kati ya Walinzi wote wa Mfalme na watu wengine wote. Sasa akina ndugu wengi katika Bwana wamekuwa na uhakika kwa sababu ya vifungo vyangu vya gereza, nao wanaonyesha uhodari mwingi wa kulisema neno la Mungu bila woga.”​—Flp. 1:12-14.

      22. Paulo alitumia wakati wake jinsi gani alipokuwa mfungwa jijini Roma?

      22 Paulo alitumia wakati wake akiwa mfungwa jijini Roma kuandika barua muhimu ambazo sasa ni sehemu ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo.b Barua hizo walizoandikiwa Wakristo wa karne ya kwanza, ziliwanufaisha sana. Sisi pia tunanufaika na barua za Paulo kwa sababu ushauri aliotoa ulioongozwa na roho unatufaa leo pia.​—2 Tim. 3:16, 17.

      BARUA TANO ALIZOANDIKA PAULO ALIPOFUNGWA ROMA MARA YA KWANZA

      Mtume Paulo aliandika barua tano mwaka wa 60-61 hivi W.K., alipofungwa jijini Roma mara ya kwanza. Katika barua yake kwa Filemoni, mwabudu mwenzake, Paulo anaeleza kwamba Onesimo, aliyekuwa mtumwa wa Filemoni lakini akatoroka, amekuwa Mkristo. Paulo alikuwa baba yake wa kiroho, naye alikuwa akimtuma mtumwa huyo ambaye ‘zamani hakufaa kitu’ arudi kwa bwana wake akiwa ndugu Mkristo.​—Flm. 10-12, 16.

      Katika barua yake kwa Wakolosai, Paulo anataja kwamba Onesimo alikuwa ‘anatoka kwao.’ (Kol. 4:9) Onesimo na Mkristo mwenzake Tikiko, walikuwa na pendeleo la kupeleka barua hizo mbili pamoja na barua ambayo Paulo aliwaandikia Waefeso.​—Efe. 6:21.

      Anapowaandikia Wafilipi, Paulo anataja ‘vifungo vyake vya gereza,’ kisha anataja hali ya ndugu aliyepeleka barua hiyo, Epafrodito. Wafilipi walikuwa wamemtuma Epafrodito akamsaidie Paulo. Lakini Epafrodito akawa mgonjwa karibu kufa. Pia, alikuwa amehuzunika sana kwa sababu Wafilipi ‘walisikia alikuwa mgonjwa.’ Kwa sababu hiyo, Paulo aliwaambia wawaheshimu sana “watu wa namna hiyo.”​—Flp. 1:7; 2:25-30.

      Barua kwa Waebrania iliandikwa kwa ajili ya Wakristo Waebrania waliokuwa Yudea. Ingawa barua yenyewe haitaji mwandikaji ni nani, uthibitisho unaonyesha kwamba Paulo ndiye aliyeiandika. Mtindo wa kuandika ni wake. Paulo anatuma salamu kutoka Italia, na anamtaja Timotheo, ambaye alikuwa pamoja naye Roma.​—Flp. 1:1; Kol. 1:1; Flm. 1; Ebr. 13:23, 24.

      23, 24. Kama Paulo, Wakristo wengi leo wamedumishaje shangwe yao na kuendelea kuhubiri ijapokuwa wamefungwa isivyo haki?

      23 Kufikia wakati ambapo alifunguliwa, ijapokuwa hautajwi katika kitabu cha Matendo, Paulo alikuwa amekaa gerezani miaka minne—miwili Kaisaria na miwili Roma.c (Mdo. 23:35; 24:27) Hata hivyo, hakupoteza shangwe, bali aliendelea kufanya yote aliyoweza katika utumishi wa Mungu. Vivyo hivyo pia, watumishi wengi wa Yehova leo, ijapokuwa wanatiwa gerezani isivyo haki kwa sababu ya imani yao, wao huendelea kuwa na shangwe na kuendelea kuhubiri. Fikiria mfano wa Adolfo, aliyefungwa huko Hispania kwa sababu ya kukataa kujiunga na jeshi. “Unatushangaza,” akasema ofisa mmoja. “Tumekuwa tukifanya maisha yako yawe magumu, na kadiri tunavyozidi ndivyo unavyozidi kutabasamu na kuzungumza nasi kwa fadhili.”

      24 Baada ya muda, Adolfo aliaminika kiasi cha kwamba mlango wa chumba chake cha gereza ulikuwa ukiachwa wazi. Askari walikuwa wakija kumuuliza maswali ya Biblia. Hata mlinzi mmoja alikuwa akiingia katika chumba cha Adolfo ili kuisoma Biblia, huku Adolfo akimlinda asikamatwe. Kwa hiyo, mfungwa akawa “akimlinda” mlinzi! Mfano mzuri wa Mashahidi kama hao na utuchochee kuonyesha “uhodari mwingi wa kulisema neno la Mungu bila woga,” hata chini ya hali ngumu.

      25, 26. Paulo alijionea utimizo wa unabii gani miaka isiyozidi 30 baadaye, na hali hiyo inalingana jinsi gani na siku zetu?

      25 Mtume wa Kristo aliye katika kifungo cha nyumbani “akiwahubiria Ufalme wa Mungu” wote wanaomtembelea—mwisho wenye kutia moyo sana wa kitabu cha Matendo! Katika sura ya kwanza, tulisoma kuhusu mgawo ambao Yesu aliwapa wafuasi wake aliposema: “Roho takatifu itakapokuja juu yenu mtapokea nguvu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, katika Yudea yote na Samaria, na mpaka sehemu ya mbali zaidi ya dunia.” (Mdo. 1:8) Sasa, miaka isiyozidi 30 baadaye, tayari ujumbe wa Ufalme ulikuwa umehubiriwa “katika uumbaji wote chini ya mbingu.”d (Kol. 1:23) Huo ni ushahidi mkubwa wa nguvu za roho ya Mungu!—Zek. 4:6.

      26 Leo, roho hiyo imewawezesha ndugu za Kristo na waandamani wao, “kondoo wengine,” kuendelea “kutoa ushahidi kamili kuhusiana na ufalme wa Mungu” katika nchi zaidi ya 240! (Yoh. 10:16; Mdo. 28:23) Je, unashiriki kikamili katika kazi hiyo?

      MAISHA YA PAULO BAADA YA MWAKA WA 61 W.K.

      Inaonekana kwamba katika mwaka wa 61 hivi W.K., Paulo alifikishwa mbele ya Maliki Nero, ambaye yaelekea alikata kauli kwamba Paulo hana hatia. Hatujui mengi kuhusu shughuli za mtume huyo baada ya hapo. Ikiwa alifunga safari aliyopanga ya kwenda Uhispania, basi huenda alienda wakati huo. (Rom. 15:28) Paulo alisafiri “katika sehemu za mbali za [Magharibi],” akaandika Clement wa Roma mwaka wa 95 hivi W.K.

      Tunaposoma barua tatu za Paulo alizoandika wakati huo baada ya kufunguliwa—barua ya 1 na ya 2 ya Timotheo na Tito—ni wazi kwamba Paulo alienda Krete, Makedonia, Nikopoli, na Troa. (1 Tim. 1:3; 2 Tim. 4:13; Tito 1:5; 3:12) Huenda alikamatwa tena alipokuwa Nikopoli, Ugiriki. Vyovyote vile, mwaka wa 65 hivi W.K., alifungwa tena gerezani jijini Roma. Hata hivyo, wakati huo Nero hakumwonyesha rehema. Kulingana na Tasito, mwanahistoria Mroma, moto ulipoteketeza jiji hilo mwaka wa 64 W.K., Nero aliwalaumu Wakristo kwa uwongo kwamba walianzisha moto huo, naye akaanza kampeni kali ya kuwatesa.

      Katika barua yake ya pili kwa Timotheo, Paulo, akitazamia kuuawa karibuni, aliwaomba Timotheo na Marko waje kwake upesi. Inapendeza kuona ujasiri wa Luka na Onesiforo, waliohatarisha uhai wao ili kumfariji Paulo. (2 Tim. 1:16, 17; 4:6-9, 11) Wakati huo, ikiwa mtu angekiri hadharani kuwa Mkristo, angekamatwa na hata kuuawa kikatili. Yaelekea kwamba Paulo aliuawa kwa sababu ya imani yake muda mfupi baada ya kuandika barua yake ya mwisho kwa Timotheo mwaka wa 65 hivi W.K. Inasemekana kwamba Nero mwenyewe aliuawa kikatili miaka mitatu hivi baada ya Paulo kuuawa.

      HABARI NJEMA “ILIHUBIRIWA KATIKA UUMBAJI WOTE”

      Mwaka wa 61 hivi W.K., mtume Paulo akiwa bado gerezani jijini Roma, aliandika kwamba “habari njema . . . ilihubiriwa katika uumbaji wote chini ya mbingu.” (Kol. 1:23) Alimaanisha nini?

      Inaonekana Paulo alikuwa akieleza kwa ujumla jinsi “habari njema” ilivyokuwa imeenea sana. Kwa mfano, Aleksanda Mkuu alikuwa ameingia Asia hadi mipaka ya India katika karne ya nne K.W.K. Kaisari Yulio alikuwa amevamia Uingereza mwaka wa 55 K.W.K., naye Klaudio alikuwa ameteka sehemu ya kusini ya kisiwa hicho na kukifanya kuwa sehemu ya Milki ya Roma katika mwaka wa 43 W.K. Eneo la Mashariki ya Mbali lilijulikana pia, kwa sababu hariri nzuri ilikuwa ikipatikana huko.

      Je, habari njema ilikuwa imehubiriwa Uingereza, China, na Mashariki ya Mbali? Haielekei. Paulo alipowaandikia Wakolosai, hakuwa ametimiza mradi wake alioweka mwaka wa 56 hivi W.K., lengo la kuhubiri Uhispania, ambako wakati huo lilikuwa “eneo ambalo halijaguswa.” (Rom. 15:20, 23, 24) Hata hivyo, kufikia mwaka wa 61 hivi W.K., ujumbe wa Ufalme ulikuwa umejulikana sana. Angalau ulikuwa umefika maeneo ya Wayahudi na wageuzwa imani waliobatizwa wakati wa Pentekoste, mwaka wa 33 W.K., na pia katika nchi ambazo mitume wa Yesu walitembelea.​—Mdo. 2:1, 8-11, 41, 42.

      a Paulo alitaka Onesimo akae naye, lakini hilo lingevunja sheria za Roma na vilevile haki za Mkristo Filemoni, bwana mkubwa wa Onesimo. Kwa hiyo, Onesimo akarudi kwa Filemoni, akiwa na barua kutoka kwa Paulo iliyomhimiza Filemoni ampokee kwa fadhili, kama ndugu yake wa kiroho.​—Flm. 13-19.

      b Ona sanduku lenye kichwa “Barua Tano Alizoandika Paulo Alipofungwa Roma Mara ya Kwanza.”

      c Ona sanduku lenye kichwa “Maisha ya Paulo Baada ya Mwaka wa 61 W.K.”

      d Ona sanduku lenye kichwa “Habari Njema ‘Ilihubiriwa Katika Uumbaji Wote.’”

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki