-
Uhai Ulianzaje?Je, Kuna Muumba Anayekujali?
-
-
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 36, 37]
Ni Mazuri Lakini Yatilika Shaka
Majaribio ya Stanley Miller mnamo 1953 mara nyingi hutajwa kuwa uthibitisho wa kwamba uhai ungaliweza kujitokeza wenyewe katika wakati uliopita. Lakini, maelezo yake yanategemea dhana ya kwamba anga la awali la dunia lilikuwa “likipunguka.” Hiyo ikimaanisha kwamba anga lilikuwa na kiwango kidogo tu cha oksijeni safi. Kwa nini anga lilikuwa hivyo?
Kitabu The Mystery of Life’s Origin: Reassessing Current Theories chasema kwamba ikiwa oksijeni nyingi sana ilikuwapo, ‘hakuna asidi-amino hata moja ambayo ingalifanyizwa, na ikiwa zingefanyizwa kwa nasibu, hizo zingeharibika haraka.’a Je, dhana ya Miller kuhusu lile liitwalo eti anga la kale ina msingi thabiti kwa kadiri gani?
Katika hati bora iliyochapishwa miaka miwili baada ya majaribio yake, Miller aliandika: “Bila shaka, mawazo hayo ni makisio, kwa kuwa hatujui kama Dunia ilikuwa na anga lenye kupunguka ilipofanyizwa. . . . Hakuna uthibitisho wa moja kwa moja ambao umepatikana.”—Journal of the American Chemical Society, Mei 12, 1955.
Je, uthibitisho uliwahi kupatikana? Miaka 25 baadaye, mwandikaji wa sayansi Robert C. Cowen aliripoti: “Wanasayansi wanalazimika kufikiria tena dhana zao. . . . Hakuna uthibitisho ambao umetokea wa kuunga mkono wazo la anga lenye kujaa hidrojeni na linalopunguka kwa kasi, lakini uthibitisho mwingine wapinga jambo hilo.”—Technology Review, Aprili 1981.
Na tangu wakati huo? Mnamo 1991, John Horgan aliandika katika Scientific American: “Katika mwongo mmoja uliopita, dhana za Urey na Miller kuhusu anga zimetokeza shaka. Majaribio yaliyofanywa katika maabara na kule kufanyizwa tena kwa anga katika kompyuta . . . yanadokeza kwamba mnururisho wa miale ya urujuani-mno kutoka kwenye jua, ambao leo umekingwa na hewa ya ozoni ya anga, ungaliharibu molekuli za hidrojeni katika anga. . . . Anga kama hilo la [kaboni dioksidi na nitrojeni] halingetokeza hali nzuri ya kufanyizwa kwa asidi-amino na vitu vingine vilivyokuwapo kabla ya uhai kutokea.”
Basi, ni kwa nini watu wengi wangali wanasisitiza kwamba anga la awali la dunia lilikuwa likipunguka, likiwa na oksijeni kidogo? Katika kitabu Molecular Evolution and the Origin of Life, Sidney W. Fox na Klaus Dose wajibu: Ni lazima anga lilikosa oksijeni kwa sababu, kwanza, “majaribio katika maabara yaonyesha kwamba mageuzi ya kemikali . . . yangezuiwa kabisa na oksijeni” na kwa sababu vitu kama asidi-amino “si thabiti wakati wa kufanyizwa kwa miamba ikiwa kuna oksijeni.”
Je, huko si kusababu kwa kutegemea matokeo tu? Inasemekana kwamba anga la awali lilikuwa linapunguka kwa sababu kama sivyo uhai haungejitokeza wenyewe. Lakini, hakuna uthibitisho wa kwamba lilikuwa likipunguka.
Kuna jambo jingine dogo muhimu: Katika yale majaribio ya Miller, ikiwa ule mchanganyiko wa hewa unawakilisha anga, cheche za umeme zikiwakilisha radi, na maji yenye kuchemka kuwakilisha bahari, ni nini au nani anayewakilishwa na mwanasayansi anayepanga na kufanya majaribio hayo?
[Maelezo ya Chini]
a Oksijeni ni hewa yenye utendaji sana. Kwa mfano, hiyo hujichanganya na chuma na kufanyiza kutu au kujichanganya na hidrojeni na kufanyiza maji. Ikiwa kungalikuwa na oksijeni nyingi zaidi katika anga wakati asidi-amino zilipokuwa zikifanyizwa, ingejichanganya haraka na asidi-amino na kuharibu molekuli wakati zingekuwa zikiendelea kufanyizwa.
-
-
Uhai Ulianzaje?Je, Kuna Muumba Anayekujali?
-
-
Mwanasayansi Stanley L. Miller, akifanya majaribio katika maabara ya Harold Urey, alichukua hidrojeni, amonia, methani, na mvuke (akidhani ya kwamba anga la awali lilifanyizwa kwa hewa hizo), akafunika hewa hizo katika chupa ambayo ilikuwa na maji yenye kuchemka upande wa chini (ili kuwakilisha bahari), na kupitisha umeme (uwe kama radi) kwenye mchanganyiko uliokuwa ndani ya chupa. Katika juma moja, kulikuwa na dalili za umajimaji fulani mzito ulio mwekundu-mwekundu, na ambao Miller aliuchunguza na kupata kuwa una asidi-amino nyingi sana—yaani protini nyingi. Huenda umepata kusikia juu ya majaribio haya kwa sababu kwa miaka mingi yametajwa katika vitabu vya mafundisho ya sayansi na katika mitaala ya shule kana kwamba majaribio hayo yanaeleza juu ya jinsi uhai ulivyoanza duniani. Lakini, je, kweli majaribio hayo yanaeleza jinsi uhai ulivyoanza?
Kwa hakika, manufaa ya majaribio ya Miller yanatiliwa shaka sana leo. (Ona “Ni Mazuri Lakini Yatilika Shaka,” ukurasa wa 36-37.)
-
-
Uhai Ulianzaje?Je, Kuna Muumba Anayekujali?
-
-
Baada ya Miller na wengine kufanyiza zile asidi-amino, wanasayansi walitaka kutengeneza protini na DNA, ambazo zote ni lazima ziwepo ili kuwe na uhai duniani. Baada ya kufanya maelfu ya majaribio katika zile zionwazo kuwa hali zilizokuwapo kabla ya uhai, matokeo yalikuwa nini? Kichapo The Mystery of Life’s Origin: Reassessing Current Theories chasema: “Kuna tofauti kubwa kati ya mafanikio ya kufanyiza asidi-amino na kushindwa daima kufanyiza protini na DNA.” Jitihada hizo za kufanyiza protini na DNA “zote ziliambulia patupu.”
-
-
Uhai Ulianzaje?Je, Kuna Muumba Anayekujali?
-
-
[Sanduku katika ukurasa wa 35]
“[Bakteria ndogo sana] inafanana sana na watu kuliko ule mchanganyiko wa kemikali uliofanyizwa na Stanley Miller, kwa sababu tayari hiyo bakteria ina uhai. Kwa hiyo kupiga hatua ya kutoka kwa bakteria hadi watu ni afadhali kuliko kupiga hatua kutoka mchanganyiko wa asidi-amino hadi bakteria.” —Profesa wa Biolojia Lynn Margulis
-