Sura Ya Tatu
Uhai Ulianzaje?
DUNIA yetu imejaa viumbe. Tokea Aktiki yenye theluji hadi msitu wa mvua wa Amazoni, tokea Jangwa la Sahara hadi bwawa la Everglades, tokea sakafu za bahari zenye giza hadi vilele vya milima vyenye kung’aa—viumbe vimejaa tele. Navyo viumbe vina mambo mengi ya kutustaajabisha.
Kuna viumbe vya aina mbalimbali vyenye ukubwa mbalimbali, navyo ni vingi ajabu. Kuna aina milioni moja ya wadudu wanaopuruka na kuvuma katika dunia yetu. Kuna samaki zaidi ya aina 20,000 katika maji yanayotuzingira—wengine wakiwa wadogo kama punje ya mchele, wengine wakiwa warefu kama lori. Kuna angalau aina 350,000 za mimea—mingine ni ya ajabu-ajabu, na mingine ni maridadi sana—ambazo zimetanda dunia. Na zaidi ya aina 9,000 za ndege hupaa juu. Viumbe hivi vyote, kutia ndani na wanadamu, hufanyiza mandhari na upatano ambao sisi huuita uhai.
Lakini jambo lenye kushangaza hata zaidi kuliko unamna-namna wenye kupendeza wa uhai unaotuzunguka ni ule upatano wao mkubwa. Wataalamu wa biolojia na kemia, ambao huchunguza viumbe vya dunia kwa makini, hueleza kwamba viumbe vyote vinavyoishi—viwe ni vijidudu vidogo sana au wanadamu—hutegemea upatano wenye kustaajabisha sana: yaani ule ushirikiano kati ya asidi za kiini cha chembe (ziitwazo DNA na RNA) na molekuli za protini. Utaratibu wa hali ya juu sana unaohusu asidi za kiini cha chembe na molekuli za protini hutukia katika karibu chembe zote za mwili wa binadamu, kama unavyofanya katika chembe za ndege, simba, na nyangumi. Mwingiliano huo wenye kupatana hutokeza aina nyingi zenye kuvutia za viumbe. Upatano huo wa uhai ulipataje kuwapo? Kwa kweli, uhai ulianzaje?
Yaelekea unakubali kwamba wakati fulani hakukuwa na uhai duniani. Sayansi inakubali jambo hilo, na hata vitabu vingi vya kidini pia vinakubali. Lakini, huenda unatambua kwamba mambo hayo mawili—sayansi na dini—yatofautiana yanapofafanua jinsi uhai ulivyoanza duniani.
Mamilioni ya watu wenye viwango mbalimbali vya elimu waamini kwamba Muumba mwenye akili, Mbuni wa awali, alitokeza uhai duniani. Kwa kutofautisha, wanasayansi wengi wasema kwamba uhai ulianza kutokana na kitu kisicho na uhai, kisha kwa nasibu tu uhai ukapiga hatua moja baada ya nyingine ya kikemikali. Je, uhai uliumbwa, au uhai ulijitokeza wenyewe tu?
Hatupaswi kufikiri kwamba suala hili halituhusu wala halihusu kutafuta kwetu maisha yenye umaana zaidi. Kama ambavyo tayari imetajwa, mojawapo ya maswali makubwa zaidi ambayo wanadamu wametafuta jibu lake ni, Sisi tukiwa wanadamu wanaoishi, tulitoka wapi?
Masomo mengi ya sayansi hukazia kubadilikana na kuokoka kwa aina fulani za wanyama badala ya kukazia swali kuu la chanzo chenyewe cha uhai. Huenda ikawa umeona kwamba majaribio ya kufafanua jinsi uhai ulivyotokea mara nyingi hayaelezi mambo wazi, kama vile: ‘Zaidi ya mamilioni fulani ya miaka, molekuli zilizogongana zilitokeza uhai.’ Lakini, je, hilo ni jibu lenye kuridhisha kweli? Hilo lingemaanisha kwamba wakati nishati kutoka kwenye jua, radi, au volkeno zilipokuwapo, kitu fulani kisicho na uhai kilisonga, kikajipanga kwa utaratibu, na hatimaye kikaanza kuishi—yote hayo bila kuongozwa kamwe. Hilo lingekuwa badiliko la ajabu kama nini! Tokea kitu kisicho na uhai hadi chenye uhai! Je, kweli uhai ungalitokea kwa njia hiyo?
Huko nyuma katika Enzi za Kati, hakungekuwa na tatizo la kukubali wazo kama hilo kwa sababu wakati huo wengi waliamini kwamba uhai ulianza kutokana na kitu kisicho na uhai. Hatimaye, katika karne ya 17, tabibu mmoja Mwitalia Francesco Redi alithibitisha kwamba mabuu walitokea katika nyama iliyooza baada tu ya nzi kuitagia mayai. Mabuu hawakutokea katika nyama ambayo nzi hawangeweza kufikia. Ikiwa wadudu wadogo kama nzi hawakujitokeza wenyewe, vipi kuhusu vijidudu ambavyo daima hutokea kwenye chakula—kiwe kimefunikwa au hakijafunikwa? Ingawa majaribio ya baadaye yalionyesha kwamba vijidudu havikutokana na kitu kisicho na uhai, suala hilo liliendelea kubishaniwa. Ndipo yakaja majaribio ya Louis Pasteur.
Watu wengi hukumbuka kazi ya Pasteur ya kutatua matatizo yanayohusu kuchacha kwa vitu na vilevile maradhi ya kuambukiza. Yeye pia alifanya majaribio ya kujaribu kuthibitisha ikiwa ni kweli kwamba viumbe vidogo-vidogo vingeweza kujitokeza vyenyewe. Kama ambavyo huenda umepata kusoma, Pasteur alithibitisha kwamba hata bakteria ndogo kabisa haikujifanyiza katika maji safi kabisa ambayo yalikingwa yasichafuliwe. Mnamo 1864 alitangaza: “Fundisho la uhai kujitokeza kutokana na kitu kisicho na uhai limemalizwa na pigo kubwa la jaribio hili sahili.” Taarifa hiyo ingali kweli. Hakuna jaribio lolote lile ambalo limeweza kutokeza uhai kutokana na kitu kisicho hai.
Basi, uhai uliweza kutokeaje duniani? Majaribio ya wakati huu ya kujibu swali hilo yalianza karibu miaka ya 1920 kwa nadharia ya mtaalamu Mrusi wa biolojia na kemia, Aleksanda I. Oparin. Yeye pamoja na wanasayansi wengine tangu wakati huo wametokeza kitu kama drama yenye maonyesho matatu inayoonyesha kile ambacho wao wanadai kuwa kilitukia kwenye sayari Dunia. Onyesho la kwanza laonyesha elementi za dunia, au vitu ambavyo vimefanyiza dunia, zikigeuzwa kuwa vikundi vya molekuli. Kisha onyesho la pili latokeza ule mruko wa kufikia molekuli zilizo kubwa. Na onyesho la mwisho la drama hii latokeza hatua ya kufikia chembe ya kwanza iliyo hai. Lakini, kweli hivyo ndivyo mambo yalivyotokea?
Jambo la msingi la drama hiyo ni kueleza kwamba anga la awali la dunia lilikuwa tofauti sana na vile lilivyo sasa. Nadharia moja inawazia kwamba ni kama oksijeni haikuwapo na kwamba zile elementi za nitrojeni, hidrojeni, na kaboni zilifanyiza amonia na methani. Wazo ni kwamba radi na nuru ya urujuani-mno zilipogonga angahewa lililofanyizwa kwa hewa hizo na mvuke, sukari na asidi-amino zilitokezwa. Hata hivyo, kumbuka kwamba hiyo ni nadharia tu.
Kulingana na drama hii ya kuwaziwa, mifanyizo kama hiyo ya molekuli ilipelekwa hadi baharini au kwenye maji mengineyo. Baada ya muda mrefu, sukari, asidi, na vitu vinginevyo vikajikusanya vikawa mchanganyiko wa “umajimaji uliotangulia uhai” ambamo ndani yake asidi-amino ziliungana pamoja ili kuwa protini. Kwa kuendeleza mambo hayo ya kuwaziwa, vitu vingine vinavyoitwa nukleotidi vilifanyiza miunganisho na kuwa asidi ya kiini cha chembe, kama vile DNA. Yasemekana kwamba mambo hayo yote yalitayarisha onyesho la mwisho katika drama hii ya molekuli.
Mtu aweza kuona hili onyesho la mwisho, ambalo halijathibitishwa, kuwa kama hadithi ya mapenzi. Molekuli za protini na molekuli za DNA zilitukia kukutana, zikatambuana, na kukumbatiana. Kisha, kabla tu ya mwisho wa onyesho hilo, chembe ya kwanza iliyo hai ikazaliwa. Kama ungalikuwa unatazama drama hii, ungalijiuliza, ‘Je, hili ni jambo halisi la maisha au limebuniwa tu? Je, kweli uhai duniani ungalitokea kwa njia hiyo?’
Je, Uhai Unaweza Kufanyizwa Katika Maabara?
Mapema katika miaka ya 1950, wanasayansi walitaka kujaribu ile nadharia ya Alexander Oparin. Ilikuwa imethibitishwa kwamba uhai hutokana tu na uhai, lakini wanasayansi walisema kwamba ikiwa hali zilikuwa tofauti katika wakati uliopita, basi huenda uhai ulitokea polepole kutokana na kitu kisicho hai. Je, jambo hilo lingeweza kuthibitishwa? Mwanasayansi Stanley L. Miller, akifanya majaribio katika maabara ya Harold Urey, alichukua hidrojeni, amonia, methani, na mvuke (akidhani ya kwamba anga la awali lilifanyizwa kwa hewa hizo), akafunika hewa hizo katika chupa ambayo ilikuwa na maji yenye kuchemka upande wa chini (ili kuwakilisha bahari), na kupitisha umeme (uwe kama radi) kwenye mchanganyiko uliokuwa ndani ya chupa. Katika juma moja, kulikuwa na dalili za umajimaji fulani mzito ulio mwekundu-mwekundu, na ambao Miller aliuchunguza na kupata kuwa una asidi-amino nyingi sana—yaani protini nyingi. Huenda umepata kusikia juu ya majaribio haya kwa sababu kwa miaka mingi yametajwa katika vitabu vya mafundisho ya sayansi na katika mitaala ya shule kana kwamba majaribio hayo yanaeleza juu ya jinsi uhai ulivyoanza duniani. Lakini, je, kweli majaribio hayo yanaeleza jinsi uhai ulivyoanza?
Kwa hakika, manufaa ya majaribio ya Miller yanatiliwa shaka sana leo. (Ona “Ni Mazuri Lakini Yatilika Shaka,” ukurasa wa 36-37.) Hata hivyo, mafanikio yake ya wazi yalifanya majaribio mengine yafanywe ambayo hata yalitokeza vitu vingine vinavyopatikana katika asidi za kiini cha chembe (DNA au RNA). Wataalamu wa mambo hayo (ambao nyakati nyingine huitwa wanasayansi wa chanzo cha uhai) walikuwa na uhakika, kwa kuwa ilionekana kana kwamba walikuwa wamefaulu kuiga lile onyesho la kwanza la ile drama ya molekuli. Na ilionekana kana kwamba majaribio ya maabara ya yale maonyesho mengine mawili yanayobaki yangefanywa. Profesa mmoja wa kemia alidai hivi: “Hivi karibuni tutagundua jinsi uhai wa kwanza ulivyotokea kupitia mageuzi.” Na mwandikaji mmoja wa sayansi alionelea hivi: “Wataalamu walidhani kwamba wanasayansi, kama yule Dakt. Frankenstein katika kitabu cha Mary Shelley, wangetokeza vijiumbe vilivyo hai katika maabara yao na hivyo basi kuthibitisha kinaganaga jinsi mwanzo ulivyotokea.” Wengi wakadhani ya kwamba lile fumbo la uhai kuanza wenyewe tu lilikuwa limetatuliwa.—Ona “Mkono wa Kulia, Mkono wa Kushoto,” ukurasa wa 38.
Maoni ya Wanasayansi Yabadilika —Maswali Yenye Kutatanisha Yabaki Vilevile
Hata hivyo, katika miaka ambayo imepita tangu wakati huo matazamio yao yametoweka. Miongo mingi imepita, na siri za chanzo cha uhai bado hazijagunduliwa. Miaka ipatayo 40 baada ya majaribio yake, Profesa Miller aliliambia hivi gazeti Scientific American: “Tatizo la chanzo cha uhai limekuwa gumu sana kuliko jinsi watu wengi walivyowazia kutia na mimi.” Wanasayansi wengine vilevile wamebadili maoni yao. Kwa mfano, huko nyuma katika mwaka wa 1969, Profesa wa Biolojia Dean H. Kenyon alishiriki kutunga kitabu Biochemical Predestination. Lakini hivi karibuni zaidi yeye alikata kauli ya kwamba “haiwezekani kabisa kwamba kitu kisicho na uhai pamoja na nishati zilijipanga zenyewe kwa utaratibu na kuwa hai bila kusaidiwa kwa njia yoyote.”
Kwa hakika, majaribio ya maabara yanaunga mkono uchanganuzi wa Kenyon wa kwamba kuna “kasoro fulani ya msingi katika nadharia zote zinazosema kwamba uhai ulianza kikemikali.” Baada ya Miller na wengine kufanyiza zile asidi-amino, wanasayansi walitaka kutengeneza protini na DNA, ambazo zote ni lazima ziwepo ili kuwe na uhai duniani. Baada ya kufanya maelfu ya majaribio katika zile zionwazo kuwa hali zilizokuwapo kabla ya uhai, matokeo yalikuwa nini? Kichapo The Mystery of Life’s Origin: Reassessing Current Theories chasema: “Kuna tofauti kubwa kati ya mafanikio ya kufanyiza asidi-amino na kushindwa daima kufanyiza protini na DNA.” Jitihada hizo za kufanyiza protini na DNA “zote ziliambulia patupu.”
Kwa uhalisi, fumbo hilo lahusisha zaidi tu ya jinsi molekuli za protini ya kwanza na asidi ya kiini cha chembe (DNA au RNA) zilivyokuja kuwako. Latia ndani jinsi zinavyoshirikiana pamoja. “Uhai Duniani wakati huu wategemea ushirikiano tu wa molekuli hizo mbili,” chasema The New Encyclopædia Britannica. Lakini kitabu hicho chaonyesha kwamba jinsi ushirikiano huo uwezavyo kutukia labaki “kuwa tatizo kubwa ambalo halijatatuliwa kuhusu chanzo cha uhai.” Huo ni ukweli mtupu.
Nyongeza ya A, “Ushirikiano wa Molekuli Wenye Kuendeleza Uhai” (ukurasa wa 45-47), yapitia baadhi ya mambo madogo-madogo ya msingi juu ya jinsi protini na asidi za kiini cha chembe zinavyoshirikiana kwa njia ya kushangaza sana. Hata kuona tu utendaji wa chembe za mwili wetu hutufanya tustaajabie sana kazi ya wanasayansi wa mambo hayo. Wao wameonyesha utendaji mwingi wenye kutatanisha ajabu ambao ni watu wachache sana huufikiria lakini ambao huendelea kufanyika daima katika maisha yetu. Hata hivyo, kutokana na maoni mengine, utaratibu huo wenye kutatanisha na ambao unatenda kwa usahihi unaohitajika kabisa na kwa njia ya kustaajabisha sana kwaturudisha kwenye lile swali, Mambo haya yote yalitokeaje?
Huenda ikawa unajua kwamba wanasayansi wa chanzo cha uhai hawajakoma kubuni matukio yenye kukubalika katika ile drama kuhusu jinsi uhai ulivyoanza. Hata hivyo, maandishi yao mapya hayasadikishi. (Ona Nyongeza ya B, “Je, Uhai Ulitokana na RNA au Ulitoka Kwenye Anga la Nje?” ukurasa wa 48.) Kwa mfano, Klaus Dose wa Taasisi ya Kemia na Biolojia katika Mainz, Ujerumani, alisema hivi: “Kwa wakati huu mazungumzo yote juu ya nadharia hiyo na majaribio makubwa kuhusu suala hili ama hukosa kufikia uamuzi ama hushindwa kabisa.”
Hata katika Mkutano wa Kimataifa wa 1996 Juu ya Chanzo cha Uhai, hakuna utatuzi uliopatikana. Badala yake, jarida la Science liliripoti kwamba wanasayansi wapatao 300 ambao walikuwa wamekusanyika “walikuwa wameng’ang’ana na fumbo la jinsi molekuli za [DNA na RNA] zilivyotokea mara ya kwanza na jinsi zilivyogeuka na kuwa chembe zenye kujizalisha zenyewe.”
Akili na elimu ya juu zilihitajika ili kuchunguza na hata kujaribu kufafanua kile ambacho hutukia katika molekuli zilizo katika chembe zetu. Je, inafaa kuamini kwamba hatua zenye kutatanisha zilitokea kwanza zenyewe tu katika “umajimaji uliotangulia uhai,” bila kuelekezwa, na kwa nasibu? Au kuna mambo mengi yaliyohusika?
Kwa Nini Kuna Maswali Yenye Kutatanisha?
Leo, mtu aweza kuwaza juu ya yale makisio na maelfu ya majaribio ambayo yamefanywa kwa nusu-karne hivi na ambayo yalijaribu kuthibitisha kwamba uhai ulianza wenyewe. Mtu akifanya hivyo, ingekuwa rahisi kukubaliana na mshindi wa tuzo la Nobeli Francis Crick. Akizungumza juu ya nadharia za chanzo cha uhai, Crick alisema kwamba kuna “makisio mengi sana yanayotegemea mambo machache sana ya hakika.” Basi inaeleweka kwamba baadhi ya wanasayansi wanaochunguza mambo hukata kauli ya kwamba uhai ni tata sana hivi kwamba hauwezi kutokea wenyewe tu hata katika maabara ambapo mambo yamepangwa kwa utaratibu, sembuse mazingira yaliyokaa kiholela.
Ikiwa sayansi ya hali ya juu haiwezi kuthibitisha kwamba uhai unaweza kujianzisha wenyewe, ni kwa nini wanasayansi fulani huendelea kushikilia nadharia kama hizo? Miongo michache iliyopita, Profesa J. D. Bernal alitaja mambo fulani ya busara katika kitabu The Origin of Life: “Kwa kutumia kanuni kali za sayansi kwa habari hii [ya uhai kujitokeza wenyewe], inawezekana kudhihirisha ifaavyo katika sehemu nyingi ya ile hadithi, jinsi ambavyo uhai haungaliweza kujitokeza wenyewe; jambo hilo ni kama haliwezekani kabisa, na uwezekano wa uhai kutokea ni kidogo mno.” Aliongezea hivi: “Kutokana na maoni hayo, inasikitisha kwamba uhai upo Duniani katika namna zake nyingi na utendaji wake mwingi na hoja kuhusu jinsi uhai ulivyotokea ni lazima zibadilishwe ili kuunga mkono mawazo ya jinsi uhai ulivyotokea.” Na hali hiyo haijaboreka.
Ebu fikiria jambo la msingi la kusababu kwa njia hiyo. Ni kama kusema: ‘Kulingana na sayansi, ni kweli kusema kwamba uhai haungeweza kujianzisha wenyewe. Lakini uhai kujitokeza wenyewe ni uwezekano mmoja tu ambao tutazungumzia. Basi, inafaa kubadili hoja za kuunga mkono mawazo ya kwamba uhai ulijianzisha wenyewe.’ Je, unaridhika na mawazo kama hayo? Je, kusababu kwa njia hiyo hakuhitaji ‘kubadilishwa’ kwingi kwa mambo ya hakika?
Lakini, kuna wanasayansi wenye maarifa na wenye kustahiwa ambao hawaoni uhitaji wa kubadili mambo ya hakika ili yalingane na falsafa zinazoenea kuhusu chanzo cha uhai. Badala ya hivyo, wao huruhusu mambo ya hakika yaonyeshe mkataa ufaao. Mambo yapi ya hakika na mkataa upi?
Habari na Akili
Akihojiwa katika sinema ya masimulizi, Profesa Maciej Giertych, ambaye ni mtaalamu wa mambo ya chembe za urithi katika Taasisi ya Masomo ya Miti ya Shule ya Sayansi ya Poland, alijibu hivi:
“Tumejua sasa habari nyingi sana zilizo katika chembe za urithi. Sayansi haiwezi kueleza jinsi habari hizo ziwezavyo kujitokeza zenyewe. Akili fulani inahitajika ili kuzitokeza; habari hizo haziwezi kutukia kwa nasibu. Kuchanganya tu herufi hakutokezi maneno.” Yeye aliongezea: “Kwa mfano, zile chembe zenye kutatanisha sana za DNA, RNA, na ule mfumo wa kufanyiza protini ni lazima zilikuwa kamili tangu mwanzoni kabisa. Kama sivyo, uhai haungekuwako. Ufafanuzi wa pekee ufaao ni kwamba habari nyingi sana zilitokana na mtu fulani mwenye akili.”
Kadiri ujifunzavyo kuhusu maajabu ya uhai, ndivyo inavyoonekana kuwa jambo la akili kukubali mkataa huu: Mtu fulani mwenye akili anahitajika ili kuanzisha uhai. Ni mtu yupi huyo?
Kama ambavyo imesemwa tayari, mamilioni ya watu wenye elimu wakata kauli ya kwamba uhai duniani ni lazima uwe ulitokezwa na mtu mwenye akili ya juu, mbuni fulani. Ndiyo, baada ya kuchunguza jambo hilo kwa haki, wao wamekubali kwamba hata katika enzi hii ya kisayansi, ni jambo lenye kufaa kukubaliana na mshairi mmoja wa Biblia ambaye alisema hivi zamani sana kuhusu Mungu: “Wewe ndiwe asili ya uhai.”—Zaburi 36:9, Biblia Habari Njema.
Uwe umefikia uamuzi thabiti kuhusu jambo hilo au la, ebu tuelekeze akili zetu kwenye baadhi ya maajabu ambayo yanakuhusu wewe binafsi. Kufanya hivyo kwaridhisha sana na kwaweza kutusaidia sana kuelewa jambo hili ambalo linahusu uhai wetu.
[Sanduku katika ukurasa wa 30]
Kuna Uwezekano Gani wa Uhai Kuanza kwa Nasibu?
“Ni nasibu, na nasibu pekee ndiyo iliyoanzisha uhai, tokea umajimaji hadi mwanadamu,” asema mshindi wa tuzo la Nobeli Christian de Duve, akisema juu ya chanzo cha uhai. Lakini, je, ni sawa kusema kwamba ni nasibu iliyoanzisha uhai?
Nasibu ni nini? Wengine hufikiria kwamba uhai ulianza kwa njia ya uwezekano wa nasibu, kama ile inayotukia unaporusha sarafu juu. Lakini, wanasayansi wengi hawalioni neno “nasibu” kwa njia hiyo kuhusu chanzo cha uhai. Neno hilo lisilo dhahiri “nasibu” linatumiwa mahali pa neno dhahiri kabisa “kisababishi,” hasa wakati ambapo kisababishi hicho hakijulikani.
“Kuiona ‘nasibu’ kuwa kama mtu kana kwamba tunaongea juu ya msababishi,” asema mtaalamu wa biolojia na fizikia Donald M. MacKay, “ni kama kuacha mawazo ya kisayansi na kukubali mawazo fulani ya kihekaya ya kidini.” Vivyo hivyo, Robert C. Sproul asema hivi: “Kwa kukiita kile kisababishi kisichojulikana ‘nasibu’ kwa muda mrefu hivyo, watu wanaanza kusahau kwamba maneno hayo yalibadilishwa. . . . Kule kudhani kwamba ‘nasibu ni sawa na kisababishi kisichojulikana’ kunaeleweka kwa wengi kuwa ‘nasibu ndiyo kisababishi.’”
Kwa mfano, mshindi wa tuzo la Nobeli Jacques L. Monod, alitumia wazo hilo la kwamba nasibu ni sawa na kisababishi. “Nasibu pekee, ikiwa peke yake kabisa na bila kujua, [ndiyo] iliyoanzisha mfumo huu wa kustaajabisha sana wa mageuzi,” yeye aliandika. “Hatimaye mwanadamu anajua kwamba yuko peke yake katika ulimwengu usio na kitu, na ambako yeye alitokea tu kwa nasibu.” Ona kwamba yeye asema: ‘KWA nasibu.’ Monod afanya kile ambacho wengine wengi hufanya—yeye aisifu nasibu kuwa kisababishi cha uhai. Nasibu inasemwa kwamba ndiyo iliyoanzisha uhai duniani.
Hata kamusi zinaonyesha kwamba “nasibu” ndiyo “kisababishi kisicho na utu na kisicho na kusudi ambacho ndicho kilianzisha matukio yasiyoelezeka.” Kwa hiyo, ikiwa mtu asema juu ya uhai kutokana na nasibu, yeye amaanisha kwamba uhai ulisababishwa na kitu kisichojulikana. Je, yawezekana kwamba watu fulani hata huendeleza “Nasibu” kwa herufi kubwa—wakimaanisha kwamba ndiyo Muumba?
[Sanduku katika ukurasa wa 35]
“[Bakteria ndogo sana] inafanana sana na watu kuliko ule mchanganyiko wa kemikali uliofanyizwa na Stanley Miller, kwa sababu tayari hiyo bakteria ina uhai. Kwa hiyo kupiga hatua ya kutoka kwa bakteria hadi watu ni afadhali kuliko kupiga hatua kutoka mchanganyiko wa asidi-amino hadi bakteria.” —Profesa wa Biolojia Lynn Margulis
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 36, 37]
Ni Mazuri Lakini Yatilika Shaka
Majaribio ya Stanley Miller mnamo 1953 mara nyingi hutajwa kuwa uthibitisho wa kwamba uhai ungaliweza kujitokeza wenyewe katika wakati uliopita. Lakini, maelezo yake yanategemea dhana ya kwamba anga la awali la dunia lilikuwa “likipunguka.” Hiyo ikimaanisha kwamba anga lilikuwa na kiwango kidogo tu cha oksijeni safi. Kwa nini anga lilikuwa hivyo?
Kitabu The Mystery of Life’s Origin: Reassessing Current Theories chasema kwamba ikiwa oksijeni nyingi sana ilikuwapo, ‘hakuna asidi-amino hata moja ambayo ingalifanyizwa, na ikiwa zingefanyizwa kwa nasibu, hizo zingeharibika haraka.’a Je, dhana ya Miller kuhusu lile liitwalo eti anga la kale ina msingi thabiti kwa kadiri gani?
Katika hati bora iliyochapishwa miaka miwili baada ya majaribio yake, Miller aliandika: “Bila shaka, mawazo hayo ni makisio, kwa kuwa hatujui kama Dunia ilikuwa na anga lenye kupunguka ilipofanyizwa. . . . Hakuna uthibitisho wa moja kwa moja ambao umepatikana.”—Journal of the American Chemical Society, Mei 12, 1955.
Je, uthibitisho uliwahi kupatikana? Miaka 25 baadaye, mwandikaji wa sayansi Robert C. Cowen aliripoti: “Wanasayansi wanalazimika kufikiria tena dhana zao. . . . Hakuna uthibitisho ambao umetokea wa kuunga mkono wazo la anga lenye kujaa hidrojeni na linalopunguka kwa kasi, lakini uthibitisho mwingine wapinga jambo hilo.”—Technology Review, Aprili 1981.
Na tangu wakati huo? Mnamo 1991, John Horgan aliandika katika Scientific American: “Katika mwongo mmoja uliopita, dhana za Urey na Miller kuhusu anga zimetokeza shaka. Majaribio yaliyofanywa katika maabara na kule kufanyizwa tena kwa anga katika kompyuta . . . yanadokeza kwamba mnururisho wa miale ya urujuani-mno kutoka kwenye jua, ambao leo umekingwa na hewa ya ozoni ya anga, ungaliharibu molekuli za hidrojeni katika anga. . . . Anga kama hilo la [kaboni dioksidi na nitrojeni] halingetokeza hali nzuri ya kufanyizwa kwa asidi-amino na vitu vingine vilivyokuwapo kabla ya uhai kutokea.”
Basi, ni kwa nini watu wengi wangali wanasisitiza kwamba anga la awali la dunia lilikuwa likipunguka, likiwa na oksijeni kidogo? Katika kitabu Molecular Evolution and the Origin of Life, Sidney W. Fox na Klaus Dose wajibu: Ni lazima anga lilikosa oksijeni kwa sababu, kwanza, “majaribio katika maabara yaonyesha kwamba mageuzi ya kemikali . . . yangezuiwa kabisa na oksijeni” na kwa sababu vitu kama asidi-amino “si thabiti wakati wa kufanyizwa kwa miamba ikiwa kuna oksijeni.”
Je, huko si kusababu kwa kutegemea matokeo tu? Inasemekana kwamba anga la awali lilikuwa linapunguka kwa sababu kama sivyo uhai haungejitokeza wenyewe. Lakini, hakuna uthibitisho wa kwamba lilikuwa likipunguka.
Kuna jambo jingine dogo muhimu: Katika yale majaribio ya Miller, ikiwa ule mchanganyiko wa hewa unawakilisha anga, cheche za umeme zikiwakilisha radi, na maji yenye kuchemka kuwakilisha bahari, ni nini au nani anayewakilishwa na mwanasayansi anayepanga na kufanya majaribio hayo?
[Maelezo ya Chini]
a Oksijeni ni hewa yenye utendaji sana. Kwa mfano, hiyo hujichanganya na chuma na kufanyiza kutu au kujichanganya na hidrojeni na kufanyiza maji. Ikiwa kungalikuwa na oksijeni nyingi zaidi katika anga wakati asidi-amino zilipokuwa zikifanyizwa, ingejichanganya haraka na asidi-amino na kuharibu molekuli wakati zingekuwa zikiendelea kufanyizwa.
[Sanduku katika ukurasa wa 38]
Mkono wa Kulia, Mkono wa Kushoto
Tunajua kwamba kuna glavu za mkono wa kulia na za mkono wa kushoto. Ndivyo ilivyo pia na molekuli za asidi-amino. Kati ya asidi-amino 100 zijulikanazo, ni 20 tu hutumiwa katika protini, na hizo zote ni zenye mkono wa kushoto. Wanasayansi wafanyizapo asidi-amino katika maabara, kwa kuiga kile wanachofikiria kuwa huenda kilitukia katika umajimaji uliotangulia uhai, wao hupata idadi sawa za molekuli za mkono wa kulia na za mkono wa kushoto. “Aina hii ya mgawanyo wa nusu-nusu,” laripoti The New York Times, si “ndivyo uhai ulivyo, kwani uhai hutegemea asidi-amino za mkono wa kushoto pekee.” Jambo linalofanya viumbe vilivyo hai vifanyizwe kwa asidi-amino za mkono wa kushoto pekee ni “fumbo kubwa sana.” Hata asidi-amino zinazopatikana katika miamba ya angani, “nyingi sana zilikuwa zenye mkono wa kushoto.” Dakt. Jeffery L. Bada, ambaye huchunguza masuala yanayohusu chanzo cha uhai, asema kwamba “uvutano fulani nje ya dunia huenda ulitimiza fungu fulani ili kuamua juu ya mkono wa kushoto au wa kulia wa asidi-amino za kibiolojia.”
[Sanduku katika ukurasa wa 40]
“Ili kujaribu kuthibitisha mawazo ambayo amefuatia sana, [mwanadamu] amefanya majaribio . . . yanayodai kuwa kile ambacho kwa kweli kimefanyizwa na kubuniwa na mtu aliye hai eti kimetokana na chanzo kisicho na uhai.” —Origin and Development of Living Systems.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 41]
“Tendo Lililopangwa na Mtu Mwenye Akili”
Mtaalamu Mwingereza wa nyota Sir Fred Hoyle ambaye amechunguza ulimwengu na uhai uliomo ndani yake kwa miongo mingi, hata anakubali kwamba uhai duniani ulitoka kwenye anga la nje. Akitoa hotuba katika Taasisi ya Tekinolojia ya California, yeye alizungumzia utaratibu wa asidi-amino katika protini.
“Tatizo kubwa katika biolojia,” Hoyle alisema, “si hasa uhakika wa kwamba protini imefanyizwa kwa mnyororo wa asidi-amino ambazo zimeunganishwa kwa njia fulani, lakini kwamba mpango dhahiri wa asidi-amino huupa mnyororo huo sifa za kustaajabisha . . . Ikiwa asidi-amino zingaliunganishwa kiholela, kungalikuwa na mipango mingi sana ambayo haingetimiza chochote katika makusudi ya chembe hai. Ukikumbuka kwamba kimeng’enya cha kawaida kina mnyororo wa angalau miunganisho 200 na kwamba kuna uwezekano wa kuwako kwa mipango 20 kwa kila muunganisho, ni rahisi kuona kwamba kuna uwezekano mkubwa sana wa kutokea kwa mipango mingi isiyofaa, zaidi ya hesabu ya atomu zote zilizo katika makundi yote ya nyota yawezayo kuonekana kwa kutumia darubini kubwa zaidi. Hiyo inahusu kimeng’enya kimoja tu, na kuna zaidi ya vimeng’enya 2000, hasa vikitumikia makusudi tofauti-tofauti. Basi, hizo asidi-amino zilipataje kuunganishwa kihususa hivyo?”
Hoyle aliongezea: “Badala ya kukubali uwezekano mdogo kabisa wa kwamba uhai ulitokana na nguvu za asili zisizoongozwa, inaonekana kuwa afadhali kufikiri kwamba uhai ulianzishwa kwa tendo lililopangwa na mtu mwenye akili.”
[Sanduku katika ukurasa wa 44]
Profesa Michael J. Behe alisema: “Kwa mtu ambaye yuko tayari kutafuta maelezo zaidi kuliko tu kisababishi cha uhai kisicho na akili, uamuzi wa wazi ni kwamba mifumo mingi ya uhai imefanyizwa. Hiyo haikubuniwa kwa sheria za asili, wala kwa nasibu na sharti; badala ya hivyo, ilipangwa. . . . Jinsi uhai ulivyo hasa na jinsi ambavyo umefanyizwa, huo umetokana na mtu mwenye akili.”
[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 42]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Hata kutazama tu ulimwengu wenye kutatanisha na utendaji wenye kutatanisha katika kila chembe ya mwili hutokeza swali, Mambo haya yote yalitokeaje?
•Utando wa chembe
Hudhibiti kinachoingia na kutoka kwenye chembe
•Kiini
Makao makuu ya utendaji wa chembe
•Kromosomu
Zina DNA, chembe za kupanga mambo ya urithi
•Ribosomu
Mahali ambapo protini hufanyizwa
•Kijiini
Mahali ambapo ribosomu hufanyizwa
•Mitokondria
Mahali ambapo molekuli ambazo huandaa nishati kwa ajili ya chembe hutengenezewa
[Picha katika ukurasa wa 33]
Wanasayansi wengi sasa hukiri kwamba molekuli zenye kutatanisha ambazo ndizo msingi wa uhai hazingeweza kujitokeza zenyewe tu katika umajimaji fulani uliotangulia uhai