-
Kuwasaidia Vijana Wakabiliane na Hali NgumuAmkeni!—2007 | Machi
-
-
Je, Kuna Madhara ya Kuwasiliana Kwenye Intaneti?
Wazazi na walimu wengi wanahangaishwa na muda ambao vijana wanatumia kwenye vituo vya Intaneti vya kuwasiliana. Vituo hivyo vya Intaneti humwezesha mtu kuanzisha kituo chake na kukiboresha kwa kuweka picha, video, na habari za kibinafsi.
Jambo linalowavutia watu kutumia vituo hivyo ni kwamba vinawawezesha kuwasiliana na marafiki. Vilevile kuanzisha kituo kama hicho humpa kijana nafasi ya kueleza maoni yake. Inaeleweka ni kwa nini vituo hivyo vinavutia sana vijana kwani kipindi cha kubalehe ni wakati ambapo kijana hujaribu kujielewa na kueleza hisia zake katika njia ambayo itawafikia na kuwagusa watu wengine.
Hata hivyo, tatizo moja linalozuka ni kwamba watu fulani hujifafanua kwa kutumia utu wanaotaka kuwa nao badala ya utu wao halisi. “Kuna kijana katika darasa langu ambaye anasema ana umri wa miaka 21 na anaishi Las Vegas,” anasema mvulana mmoja mwenye umri wa miaka 15. Vijana hao wawili wanaishi kilomita 1,600 hivi kutoka Las Vegas.
Ni jambo la kawaida kwa watu kutoa habari za uwongo kama hizo. “Unaweza kufanya jambo lolote kwenye Intaneti,” anasema msichana Mwaustralia mwenye umri wa miaka 18. “Unaweza kujifanya kuwa mtu tofauti kabisa kwani hakuna mtu anayekujua. Unajihisi ukiwa na ujasiri. Unaweza kubuni mambo ili uonekane kuwa mtu mwenye kupendeza zaidi. Unaweza kuingiza picha zako ukiwa umevalia mavazi ambayo kwa kawaida hungevalia au ukifanya mambo ambayo kwa kawaida hungefanya. Unaweza kuandika mambo ambayo wewe mwenyewe huwezi kusema. Unahisi kwamba huwezi kulaumiwa kwa sababu huwezi kupatikana. Hakuna mtu anayekujua vizuri.”
Kama tu njia nyingine za mawasiliano, vituo vya Intaneti vya kuwasiliana vinaweza kuwa na manufaa au madhara. Je, wewe ukiwa mzazi unajua watoto wako wanafanya nini kwenye Intaneti? Je, unahakikisha kwamba wanatumia wakati wao vizuri?a (Waefeso 5:15, 16) Isitoshe, kutumia Intaneti vibaya kunaweza kumhatarisha kijana kwa njia mbalimbali. Baadhi ya njia hizo ni zipi?
-
-
Kuwasaidia Vijana Wakabiliane na Hali NgumuAmkeni!—2007 | Machi
-
-
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]
Vituo vya Kuwasiliana—Simulizi la Msichana Mmoja
“Nilianza kutumia kituo cha Intaneti cha shule yetu kuwasiliana na wanafunzi wenzangu na walimu. Nilianza kutumia saa moja kila juma kwenye kituo hicho. Baada ya muda nikaanza kukitumia kila siku. Nilikuwa nimenaswa sana hivi kwamba wakati ambapo sikuwa nikitumia Intaneti nilikuwa nikifikiria kuihusu. Sikuweza kukazia fikira kitu kingine chochote. Sikuweza kumaliza kazi yangu ya shuleni wala kukaza fikira nilipokuwa kwenye mikutano ya Kikristo, na hata niliwapuuza marafiki wangu. Mwishowe, wazazi wangu walitambua kilichokuwa kikiendelea nao wakaniwekea vizuizi. Ilikuwa vigumu kwangu kukubali vizuizi hivyo. Nilikasirika sana. Lakini sasa ninafurahi kwamba wazazi wangu walifanya hivyo nami nimefanya mabadiliko yanayofaa. Nisingependa kuhisi nimenaswa tena!”—Bianca.
-