Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Ukweli Kuhusu Sherehe Zinazopendwa
    Amkeni!—2001 | Oktoba 8
    • Neno la Kiingereza “Halloween” ni ufupisho wa usemi, “All Hallows’ Eve” unaomaanisha, mkesha wa Siku ya Watakatifu Wote. Lakini, jina hilo linalodhaniwa kuwa la Kikristo huficha vyanzo vya sherehe hiyo ambavyo si vitakatifu. Kwa kweli, wasomi wanasema kwamba sherehe ya Halloween ilianza mapema kabla ya Ukristo—wakati Waselti wa kale walipoishi Uingereza na Ireland. Kwa kutumia kalenda inayotegemea mzunguko wa mwezi, Waselti waligawanya mwaka katika majira mawili—miezi yenye giza ya baridi kali na miezi yenye nuru ya kiangazi. Wakati wa mwezi mpevu, karibu Novemba 1, Waselti walisherehekea sikukuu ya Samhain, iliyoashiria “Mwisho wa Kiangazi.”a

      Sherehe hiyo, iliyoashiria mwanzo wa mwaka mpya wa Waselti, ilifanywa mwishoni mwa kiangazi, baada ya mavuno kukusanywa na mifugo kuingizwa vizimbani kutoka malishoni. Waselti waliamini kwamba kadiri siku zilivyozidi kuwa fupi, ndivyo ilivyokuwa muhimu kulitia jua nishati mpya kupitia desturi za kichawi na dhabihu mbalimbali. Mioto yote ilizimwa wakati mwaka ulipokuwa ukimalizika, na mwaka mpya ulifunguliwa kwa kuwasha mioto mikubwa mitakatifu ambayo ilitumiwa kuwasha mioto midogo katika kila nyumba. Mioto hiyo mikubwa ni kama ile inayowashwa leo wakati wa sherehe ya Usiku wa Guy Fawkes nchini Uingereza na Brazili mnamo mwezi wa Juni. Ilidhaniwa kwamba mioto hiyo ingefukuza roho waovu.

      Iliaminika kwamba mipaka inayotenga wanadamu na viumbe wa roho iliondolewa wakati wa sherehe ya Samhain, na hivyo roho wazuri na waovu, walitangatanga ulimwenguni. Ilidhaniwa kwamba nafsi za wafu zilirejea nyumbani, na familia ziliandaa chakula na kinywaji kwa ajili ya wageni hao wa roho zikitumaini kwamba vitu hivyo vingeweza kuwatuliza na hivyo kuwaepusha na misiba. Kwa hiyo, watoto wanapovalia kama mazimwi au wachawi na kwenda nyumba kwa nyumba wakiomba zawadi ya Halloween au wakiwatisha watu, wanaiga desturi za kale za Samhain pasipo kujua. Jean Markale anasema hivi katika kitabu chake Halloween, histoire et traditions (Historia na Desturi za Halloween): “Watoto wanapopokea zawadi, wanaonyesha kwa njia ya mfano na pasipo kujua, ushirikiano wa kidugu uliopo kati ya wanadamu na viumbe wa roho. Ndiyo sababu Halloween . . . huonwa kuwa sherehe takatifu.”

      Kwa kuwa watu waliamini kwamba mipaka kati ya ulimwengu halisi na makao ya viumbe wa roho iliondolewa, walifikiri kwamba wanadamu wangeweza kuvuka kwa urahisi kwenye makao ya viumbe wa roho. Kwa hiyo sherehe ya Samhain ilikuwa pindi nzuri ya kujua siri za wakati ujao. Mitofaa au miti ya kokwa za hazel ilionwa kuwa mitakatifu, na matunda yake yalitumiwa kubashiri habari za ndoa, ugonjwa, na kifo. Kwa mfano, matofaa yenye alama za pekee yalitiwa katika beseni la maji. Mwanamume au mwanamke angeweza kuchagua mwenzi wake wa ndoa wa wakati ujao kwa kutwaa tofaa kwa kinywa chake tu. Zoea hilo la kubashiri lingali linaendelea leo katika mchezo wa kutwaa matofaa kwa kinywa wakati wa Halloween.

      Sherehe ya Samhain ilikuwa pia na karamu za ulevi zenye vifijo na nderemo na watu walifanya walivyopenda. “Maadili ya kawaida yalivunjwa au kupotoshwa,” asema Markale. “Mambo yaliyokatazwa yalikubaliwa, na mambo yaliyokubaliwa yalikatazwa.” Mtazamo huo ungali unadhihirishwa leo katika sherehe ya Halloween. Ndiyo sababu inapendwa sana na wengi. Kikizungumzia jambo hilo, kichapo The Encyclopedia of Religion chasema kwamba leo Halloween ni ‘wakati ambapo watu wazima wanaweza pia kuvuka mipaka ya kitamaduni na kupuuza hadhi yao kwa kufanya mambo mapotovu kupindukia. Hivyo basi, maoni ya msingi ya Waselti ya kwamba sherehe hiyo ya kila mwaka ni jioni ya kukiuka mambo ya kawaida ya maisha na kupuuza kanuni zilizopo yamedumu hadi karne ya 20.’

  • Ukweli Kuhusu Sherehe Zinazopendwa
    Amkeni!—2001 | Oktoba 8
    • a Yaelekea Samhain si jina la mungu wa kifo wa Waselti kama inavyosemekana mara nyingi, bali ni jina la sherehe hiyo. Kulingana na Jean Markale, mtaalamu Mfaransa wa historia ya Waselti, huenda mungu wa nuru, aitwaye Lug, ndiye aliyeheshimiwa wakati wa sherehe ya Samhain.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki