-
Desturi za Krismasi-Je, Ni za Kikristo?Mnara wa Mlinzi—2000 | Desemba 15
-
-
Ebu fikiria kwa muda mfupi baadhi ya desturi za nchi ya Mexico. Huenda kufanya hivyo kukakusaidia ubadili maoni yako kuhusu msimu wa sikukuu hii.
Posada, “Wanaume Watatu Wenye Hekima,” na Nacimiento
Sherehe huanza Desemba 16 kwa posada. Kitabu Mexico’s Feasts of Life chasema hivi: “Ni wakati wa posada, siku tisa zenye kupendeza sana kabla ya Mkesha wa Krismasi, ambazo huashiria safari yenye upweke ya Yosefu na Maria ya kuzungukazunguka katika jiji la Bethlehemu na wakati ambapo hatimaye walionyeshwa fadhili na kupewa makao. Familia na marafiki hukusanyika pamoja kila usiku ili kuigiza siku zilizotangulia kuzaliwa kwa Kristo.”
Kimapokeo, kikundi cha watu hubeba sanamu ya Maria na Yosefu kwenye nyumba na kuomba makao au posada kwa kuimba. Wale waliomo nyumbani huimba kwa kuitikia hadi mwishowe wageni wanaruhusiwa kuingia ndani. Kisha karamu huanza ambapo watu fulani—wakiwa wamefungwa macho kwa kitambaa na wakiwa na bakora mkononi—hupokezana zamu wakijaribu kuvunja piñata, nyungu kubwa iliyopambwa ambayo inaning’inia kwenye kamba. Baada ya kuvunjwa, vitu vilivyomo ndani (peremende, matunda, na kadhalika) hukusanywa na watu wanaosherehekea. Baada ya hapo kunakuwa na chakula, vinywaji, muziki, na dansi. Karamu nane za posada hufanywa kuanzia Desemba 16 hadi Desemba 23. Tarehe 24, Nochebuena (mkesha wa Krismasi) husherehekewa, na familia hujitahidi kukutana pamoja ili kula mlo wa pekee.
Baada ya muda mfupi kuna Sikukuu ya Mwaka Mpya, ambayo husherehekewa kwa karamu zenye makelele mengi sana. Jioni ya Januari 5, Tres Reyes Magos (“wanaume watatu wenye hekima”) wanatazamiwa kuletea watoto vichezeo. Kilele huashiriwa na karamu inayofanywa Januari 6, ambapo rosca de Reyes (keki yenye umbo la duara) huandaliwa. Keki hiyo inapoliwa, mtu fulani hupata katika kipande chake mwanasesere mdogo anayefananisha mtoto Yesu. Anayepata mwanasesere huyo huwajibika kupanga na kuandaa karamu ya mwisho Februari 2. (Katika sehemu fulani kuna wanasesere wadogo watatu, wanaofananisha “wanaume watatu wenye hekima.”) Kama uonavyo, karamu zinazohusiana na Krismasi huendelea kwa muda mrefu.
Katika pindi hii, nacimiento (Mandhari ya kuzaliwa kwa Kristo) huwa yenye kutokeza sana. Ni nini kinachohusika katika pindi hii? Katika sehemu za umma na vilevile makanisani na nyumbani, mandhari hujengwa yakiwa na sanamu (kubwa au ndogo) zilizotengenezwa kwa kauri, mbao, au udongo. Sanamu hizo hufananisha Yosefu na Maria wakipiga magoti mbele za hori yenye kitoto kilichotoka tu kuzaliwa. Mara nyingi kunakuwa na wachungaji na Los Reyes Magos (“wanaume wenye hekima”). Mandhari hiyo huonyesha hori, na huenda kukawa na wanyama kadhaa ili kuikamilisha. Hata hivyo, sanamu iliyo muhimu zaidi ni mtoto mchanga aliyezaliwa, ambaye anaitwa kwa Kihispania el Niño Dios (Mtoto-Mungu). Sanamu ya mtoto huyo mchanga yaweza kuwekwa hapo kwenye Mkesha wa Krismasi.
Kuchunguza Desturi za Kuzaliwa kwa Kristo
Kuhusu sherehe za Krismasi kama zijulikanavyo ulimwenguni pote, kichapo The Encyclopedia Americana chasema: “Desturi nyingi zinazohusianishwa na Krismasi leo hazikuwa desturi za Krismasi hapo awali, badala yake zilikuwa desturi za kabla ya Ukristo na zisizo za Kikristo ambazo zilikubaliwa na kanisa la Kikristo. Desturi nyingi za Krismasi zenye shangwe, hufuata kigezo cha Saturnalia, ambayo ni sherehe ya Kiroma iliyosherehekewa katikati ya Desemba. Kwa mfano, kutokana na sherehe hii, kulitokea karamu zenye madoido mengi, kupeana zawadi, na kuwasha mishumaa.”
Katika Amerika ya Kusini, desturi hizo za msingi za Kuzaliwa kwa Kristo, pamoja na desturi nyinginezo hufuatwa. Huenda ukajiuliza ‘zilitoka wapi?’ Kwa kweli, wengi wanaotaka kutii Biblia wanatambua kwamba desturi fulani ni sherehe za ibada ya Waazteki. Gazeti El Universal la Mexico City, lilisema hivi: “Watawa kutoka mashirika mbalimbali ya watawa walitumia sherehe za Waazteki kutegemeza kazi yao ya kueneza-evanjeli na ya umishonari kwa sababu sherehe hizo, kulingana na kalenda ya kidini ya Waazteki, zilisadifiana na kalenda ya Katoliki ya liturujia. Mahali pa sherehe za miungu ya kabla ya enzi ya Kihispania pakachukuliwa na sherehe za miungu ya Kikristo, wakaanzisha sherehe za Ulaya na kutumia pia sherehe za Kihindi, ambazo zilitokeza mchanganyiko wa tamaduni ambazo ni chimbuko la maneno ya Kimexico cha asili.”
Kichapo The Encyclopedia Americana chaeleza hivi: “Michezo ya kuigiza ya Kuzaliwa kwa Kristo ikawa sehemu ya sherehe ya Krismasi hapo awali . . . Inasemekana michezo hiyo ya kuigiza hori kanisani ilianzishwa na Mtakatifu Francis.” Michezo hii ya kuigiza inayokazia kuzaliwa kwa Kristo ilifanywa katika makanisa wakati Mexico ilipofanywa kuwa koloni. Ilipangwa na watawa wa kiume wa “Mtakatifu Francis” ili kufundisha Wahindi kuhusu Kuzaliwa kwa Kristo. Baadaye posada zikawa mashuhuri zaidi. Bila kujali kusudi lake la awali, namna posada zinavyofanywa leo yafunua asili yao ya kweli. Ukiwa Mexico wakati wa msimu huu, unaweza kuona au kuhisi kitu fulani ambacho mwandishi wa El Universal alikazia katika maelezo yake: “Posada ambazo zilikuwa njia ya kutukumbusha safari ya wazazi wa Yesu wakitafuta makao ambapo Mtoto-Mungu angeweza kuzaliwa, leo ni siku za ulevi, matendo mabaya kupindukia, ulafi, mambo ya ubatili, na uhalifu mwingi zaidi.”
Wazo la nacimiento liliibuka nyakati za Ukoloni kutokana na michezo iliyoigizwa na watu katika makanisa. Ingawa watu fulani huvutiwa na wazo hilo, je, linaonyesha kwa usahihi kile ambacho Biblia husema? Hilo ni swali linalofaa. Wakati wanaoitwa wanaume watatu wenye hekima—ambao kwa kweli walikuwa wanajimu—walipozuru Yesu na familia yao hawakuwa wakiishi tena katika hori. Muda ulikuwa umepita, na familia hiyo ilikuwa inaishi katika nyumba. Utafurahia kusoma habari kamili ya simulizi hili lililopuliziwa linalopatikana katika Mathayo 2:1, 11. Unaweza kuona pia kwamba Biblia haisemi kulikuwa na wanajimu wangapi.a
Katika Amerika ya Kusini, wale wanaume watatu wenye hekima wanachukua mahali pa Baba Krismasi. Bado, kama ifanywavyo katika nchi nyingine, wazazi wengi huficha vichezeo katika nyumba. Kisha asubuhi ya Januari 6, watoto huvitafuta, kana kwamba vililetwa na wale wanaume watatu wenye hekima. Wakati huo wauza-vichezeo hupata pesa nyingi, na wengine wametajirika kutokana na jambo ambalo watu wengi wanyofu huliona kuwa fantasia tu. Watu wengi kutia ndani watoto wadogo, wanazidi kukosa imani katika ngano ya wanaume watatu wenye hekima. Ingawa wengine hawafurahii kupungua kwa watu wanaoamini ngano hiyo, mtu aweza kutarajia iweje kwa fantasia inayofuatwa tu kwa sababu ya desturi na kujinufaisha kifedha?
-
-
Desturi za Krismasi-Je, Ni za Kikristo?Mnara wa Mlinzi—2000 | Desemba 15
-
-
a Kuna habari nyingine ambazo hazipasi kupuuzwa: Katika nacimiento ya Mexico, mtoto anaitwa “Mtoto-Mungu” kukiwa na wazo la kwamba Mungu mwenyewe ndiye aliyekuja duniani kama mtoto. Hata hivyo, Biblia huonyesha Yesu kuwa Mwana wa Mungu aliyezaliwa duniani; hakuwa sawa wala hakutoshana na Yehova, Mungu mweza yote. Ona ukweli wa jambo hilo, unaopatikana katika Luka 1:35; Yohana 3:16; 5:37; 14:1, 6, 9, 28; 17:1, 3; 20:17.
-