-
Watu Hufikiria Nini Hasa Wakati wa Krismasi?Mnara wa Mlinzi—2005 | Desemba 15
-
-
Watu Hufikiria Nini Hasa Wakati wa Krismasi?
KWA mamilioni ya watu, majira ya sikukuu ni wakati wa kuwa pamoja na familia na marafiki, wakati wa kuimarisha upendo kati yao. Wengine wengi huiona pindi hiyo kuwa wakati wa kufikiria kuzaliwa kwa Yesu Kristo na daraka lake la kuwaokoa wanadamu. Huko Urusi, tofauti na nchi nyinginezo, kuna wakati ambapo watu hawakuruhusiwa kusherehekea Krismasi. Ingawa kwa karne nyingi wafuasi wa Kanisa Othodoksi la Urusi walisherehekea Krismasi waziwazi, hawakuruhusiwa kufanya hivyo katika miaka mingi ya karne ya 20. Kwa nini?
Muda mfupi tu baada ya mapinduzi ya Kikomunisti ya Bolshevik, mwaka wa 1917, serikali ya Sovieti ilianzisha sera ya kikatili ya kutoamini kuwapo kwa Mungu. Sikukuu ya Krismasi pamoja na sherehe zake za kidini hazikukubaliwa tena. Serikali ikaanza kueneza propaganda kuhusu sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya. Pia, viwakilishi vya majira hayo ya sikukuu katika eneo hilo kama vile mti wa Krismasi na Baba Krismasi, ambaye huko Urusi aliitwa Ded Moroz au Babu Frost, vilipigwa marufuku.
Mwaka wa 1935, Warusi walibadili kabisa njia yao ya kusherehekea majira ya sikukuu. Wasovieti walianza tena kutumia Babu Frost, mti wa majira, na kusherehekea Mwaka Mpya, lakini kwa njia tofauti kabisa. Ilisemekana kwamba Babu Frost angeleta zawadi wakati wa Siku ya Mwaka Mpya bali si wakati wa Krismasi. Vivyo hivyo, mti wa Krismasi haungetumiwa tena. Badala yake, kungekuwa na mti wa Mwaka Mpya! Hivyo, kukawa na badiliko kubwa katika Muungano wa Sovieti. Sherehe ya Mwaka Mpya ikachukua mahali pa Krismasi.
Majira ya Krismasi yakawa majira ya sikukuu yasiyo ya kidini. Mti wa sherehe ya Mwaka Mpya ulipambwa kwa mapambo yasiyo ya kidini yaliyoonyesha maendeleo ya Muungano wa Sovieti. Jarida moja la Urusi (Vokrug Sveta) linasema: “Inawezekana kujua historia ya kuanzishwa kwa Ukomunisti kwa kutazama mapambo yaliyo kwenye mti wa sherehe ya Mwaka Mpya ambayo yanaonyesha miaka mbalimbali ya utawala wa Sovieti. Zaidi ya kupamba mti huo kwa sungura wachanga, tepe zenye madoido, na mikate ya mviringo, mapambo mengine yalitengenezwa kama vile yale yenye umbo la mundu, nyundo, na matrekta. Baadaye, mapambo hayo yaliacha kutumiwa na badala yake michongo mingine ikaanza kutumiwa, kama vile michongo ya wachimba migodi na wanaanga, michongo ya mashini za kutoa mafuta baharini, roketi, na magari yanayotumiwa kwenye mwezi.”
Namna gani Siku ya Krismasi? Bila shaka, haikutambuliwa. Badala yake, serikali ya Sovieti iliifanya kuwa siku ya kawaida ya kazi. Wale waliotaka kusherehekea Krismasi kwa sababu zake za kidini, walifanya hivyo kisiri wakihatarisha uhusiano wao na Serikali na kuhofia adhabu ambayo wangepata. Naam, katika karne ya 20 huko Urusi, mambo ya dini yaliacha kuzingatiwa katika majira ya sikukuu.
Badiliko la Hivi Karibuni
Mnamo 1991, Muungano wa Sovieti ulivunjika na watu wakapata uhuru zaidi. Ile sera ya kutoamini kuwapo kwa Mungu ikatoweka. Majimbo mapya mbalimbali hayakufuata mambo ya dini. Serikali na mambo ya dini yalitenganishwa. Watu wengi wa kidini walihisi kwamba wangeweza kudumisha imani yao. Walihisi kwamba njia moja ya kufanya hivyo ni kusherehekea sikukuu ya kidini ya Krismasi. Hata hivyo, baada ya muda mfupi, watu hao walikatishwa tamaa sana. Kwa nini?
Kila mwaka, sikukuu hiyo imekuwa ya kibiashara. Naam, kama ilivyo katika nchi za magharibi, siku hizi majira ya Krismasi ni wakati bora kwa watengenezaji wa bidhaa, wauzaji wa bidhaa kwa jumla, na wachuuzi kupata pesa. Mapambo ya Krismasi hutandazwa waziwazi madukani. Sasa muziki na nyimbo za Krismasi za nchi za magharibi ambazo awali hazikujulikana nchini Urusi, huuzwa madukani. Wauzaji wanaobeba mifuko mikubwa yenye zawadi za Krismasi huuza bidhaa zao ndani ya magari ya moshi na magari mengine ya umma. Hivyo ndivyo hali ilivyo leo.
Hata watu ambao hawapingi biashara hiyo yenye pupa huenda wakaudhika wanapoona jambo lingine lenye kuhuzunisha katika majira ya sikukuu, yaani, kutumia kileo kupita kiasi na matokeo ya kufanya hivyo. Daktari fulani anayefanya kazi katika chumba cha dharura cha hospitali moja huko Moscow alisema hivi: “Madaktari hukubali kwamba wakati wa sherehe za Mwaka Mpya watu wengi huwa na majeraha mengi kutia ndani uvimbe, majeraha yanayosababishwa na kudungwa kisu au kupigwa risasi, na mengi husababishwa na jeuri katika familia, ugomvi unaotokana na ulevi, na misiba barabarani.” Mwanasayansi mmoja mwenye uzoefu wa tawi la Taasisi ya Kisayansi ya Urusi alisema hivi: “Idadi ya watu wanaokufa kwa sababu ya ulevi imeongezeka. Hasa iliongezeka zaidi mwaka wa 2000. Pia, idadi ya watu waliojiua na ya wauaji iliongezeka.”
Kuna jambo lingine linalofanya watu wajiendeshe vibaya nchini Urusi katika majira ya sikukuu. Chini ya kichwa “Warusi Washerehekea Krismasi Mara Mbili,” gazeti moja (Izvestiya) liliripoti hivi: “Kwa kila Warusi kumi, mmoja husherehekea Krismasi mara mbili. Kulingana na uchunguzi uliofanywa na Kituo cha Urusi cha Maoni ya Umma na Utafiti wa Ununuzi na Uuzaji wa Bidhaa, asilimia 8 ya waliohojiwa walikubali kwamba wao husherehekea Mkesha wa Krismasi mnamo Desemba 25, kulingana na kalenda ya Krismasi ya Kikatoliki, na mnamo Januari 7 kulingana na Kanisa Othodoksi . . . Wengi hawasherehekei Krismasi kwa sababu ya umuhimu wake wa kidini bali wanaona huo kuwa wakati mzuri wa kufanya karamu.”a
-
-
Watu Hufikiria Nini Hasa Wakati wa Krismasi?Mnara wa Mlinzi—2005 | Desemba 15
-
-
a Kabla ya mapinduzi ya Oktoba 1917, Warusi walikuwa wakitumia kalenda ya kale ya Yulio, lakini nchi nyingi zilikuwa zimeanza kutumia kalenda ya Gregory. Mnamo 1917 kalenda ya Yulio ilikuwa nyuma ya ile ya Gregory kwa siku 13. Baada ya mapinduzi, Wasovieti walianza kutumia kalenda ya Gregory na hivyo Urusi ikaanza kutumia kalenda ileile iliyotumiwa ulimwenguni pote. Hata hivyo, Kanisa Othodoksi liliendelea kutumia kalenda ya Yulio kwa ajili ya sherehe zao, na kuiita kalenda ya “Mtindo wa Kale.” Huenda umesikia kwamba huko Urusi Krismasi husherehekewa Januari 7. Hata hivyo, kumbuka kwamba Januari 7 katika kalenda ya Gregory ni Desemba 25 katika kalenda ya Yulio. Hivyo, Warusi wengi hupanga majira yao ya sikukuu hivi: Desemba 25, Krismasi ya Magharibi; Januari 1, sherehe isiyo ya kidini ya Mwaka Mpya; Januari 7, Krismasi ya Kanisa Othodoksi; Januari 14, sherehe ya Mwaka Mpya inayofuata Mtindo wa Kale.
-