-
Mungu ni Kimbilio Langu na Nguvu ZanguMnara wa Mlinzi—1997 | Mei 1
-
-
Badala ya kuachiliwa huru baada ya kumaliza kifungo changu, nilikamatwa na Gestapo. Nilipaswa kutia sahihi julisho rasmi kwamba singeweza tena kuwa mtendaji nikiwa Shahidi wa Yehova. Nilikataa kwa uthabiti, ndipo afisa akaghadhibika, akasimama ghafula, na kutoa hati ya kuamuru nitiwe kizuizini. Hiyo hati imeonyeshwa pichani. Bila kuruhusiwa kuona wazazi wangu, nilipelekwa mara moja katika kambi ndogo ya mateso ya wanawake katika Lichtenburg kwenye mto Elbe. Muda mfupi baada ya hapo nilikutana na Käthe. Alikuwa amekuwa katika kambi ya mateso katika Moringen tangu Desemba 1936, lakini kambi hiyo ya mateso ilipofungwa, yeye, pamoja na dada wengine wengi, wakaja Lichtenburg. Baba yangu alikuwa kizuizini pia, na sikumwona tena hadi 1945.
Katika Lichtenburg
Sikuruhusiwa kujiunga na wale Mashahidi wengine wa kike mara moja, kwa kuwa walikuwa wakiadhibiwa kwa sababu fulani. Katika mojawapo ya kumbi, niliona vikundi viwili vya wafungwa—wanawake walioketi kwa kawaida kwenye meza na Mashahidi waliopaswa kuketi siku nzima juu ya vibago na ambao hawakupewa chochote cha kula.b
Nilikubali kwa utayari mgawo wowote wa kazi, nikitumaini kukutana na Käthe kwa njia fulani. Na hivyo ndivyo ilivyotokea. Alikuwa akienda kazini pamoja na wafungwa wengine wawili tulipokutana. Nikiwa mwenye shangwe mno, nilimkumbatia. Lakini mlinzi wa kike alituripoti mara moja. Tulihojiwa, na kutoka wakati huo na kuendelea, tukatenganishwa kwa kusudi. Hilo lilikuwa jambo gumu sana.
Matukio mengine mawili katika Lichtenburg hayawezi kusahaulika. Katika pindi moja wafungwa wote walipaswa kukusanyika uani kusikiliza mojawapo ya hotuba za kisiasa za Hitler redioni. Sisi Mashahidi wa Yehova tulikataa, kwa kuwa sherehe za kizalendo zilihusika. Hivyo walinzi walitugeuzia mabomba, wakitupuliza na maji yenye kutoka kwa nguvu na kutufukuza sisi wanawake tusio na kinga kutoka orofa ya nne hadi uani. Hapo ilitubidi kusimama tukiwa tumelowa kabisa.
Katika pindi nyingine mimi, pamoja na Gertrud Oehme na Gertel Bürlen, tuliamuriwa kurembesha makao makuu ya mkuu wa gereza kwa taa za umeme, kwa kuwa siku ya kuzaliwa ya Hitler ilikuwa ikikaribia. Tulikataa, huku tukitambua mbinu za Shetani za kujaribu kutuongoza kuvunja uaminifu-maadili wetu kupitia maridhiano mbalimbali kwa mambo madogo-madogo. Ikiwa adhabu, kila mmoja wetu dada vijana alipaswa kukaa majuma matatu yaliyofuata akiwa peke yake katika seli ndogo, yenye giza. Lakini Yehova alikuwa karibu nasi na, hata katika mahali penye kuogofya kama hapo, alijithibitisha mwenyewe kuwa kimbilio.
-
-
Mungu ni Kimbilio Langu na Nguvu ZanguMnara wa Mlinzi—1997 | Mei 1
-
-
b Gazeti Trost, (Consolation) lililochapishwa na Watch Tower Society katika Bern, Uswisi, mwezi wa Mei 1, 1940, ukurasa 10, liliripoti kwamba katika pindi moja Mashahidi wa Yehova wa kike katika Lichtenburg hawakupewa mlo wa mchana kwa siku 14 kwa sababu walikataa kuonyesha ishara ya heshima nyimbo za Nazi zilipochezwa. Kulikuwa na Mashahidi wa Yehova 300 huko.
-