Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Haki ya Kweli Lini na Jinsi Gani?
    Mnara wa Mlinzi—1998 | Juni 15
    • Haki ya Kweli Lini na Jinsi Gani?

      WASIO na hatia hapaswi kuwa na sababu yoyote ya kuhofu haki ya kweli. Kwa kweli, karibu kila mahali raia wana sababu ya kushukuru ikiwa nchi yao ina mfumo wa sheria ambao hujaribu kuhakikisha kwamba kuna haki. Mfumo wa namna hiyo huhusisha muundo fulani wa sheria, jeshi la polisi ili kuzitekeleza, na mahakama za kutekeleza haki. Wakristo wa kweli hustahi mfumo wa kihukumu wa sehemu ambamo huishi, kwa kupatana na onyo la upole la Biblia la “[kuwa] katika ujitiisho kwa mamlaka zilizo kubwa.”—Waroma 13:1-7.

      Hata hivyo, mifumo ya kihukumu katika nchi mbalimbali imefanya makosa yenye kudhuru na yenye kuaibisha.a Badala ya kuwaadhibu wenye hatia na kuwalinda wasio na hatia, nyakati nyingine watu wasio na hatia wameadhibiwa kwa ajili ya uhalifu ambao hawakuufanya. Watu wengine wamekaa gerezani kwa muda wa miaka mingi, wakiachiliwa tu kabla ya kukamilisha kifungo chao kukiwa na shaka kubwa kama walikuwa na hatia na kama kupatikana kwao na hatia kulikuwa halali. Kwa sababu hiyo, wengi wanauliza, Je, kutakuwako na haki ya kweli kwa ajili ya kila mtu? Ikiwa ndivyo, ni lini na jinsi gani? Ni nani tuwezaye kutumaini awalinde wasio na hatia? Na kuna tumaini gani kwa ajili ya wahasiriwa wa ukosefu wa haki?

      Haki Yenye Kasoro

      Katika miaka ya 1980, Ujerumani ilishuhudia “mojawapo ya taratibu za kisheria zenye kushtusha zaidi za kipindi cha baada ya vita,” wakati ambapo mama fulani alihukumiwa kifungo cha maisha kwa kuua kimakusudi binti zake wawili. Hata hivyo, miaka kadhaa baadaye, ushahidi uliotolewa dhidi yake ulichunguzwa tena, naye akaachiliwa akisubiri kufanyiwa kesi upya. Gazeti la habari la Die Zeit liliripoti katika mwaka wa 1995 kwamba, hukumu ya kwanza “ingeweza kuthibitika kuwa kosa la kihukumu.” Hata kufikia wakati wa kuandika makala hii, mwanamke huyo alikuwa amekaa gerezani muda wa miaka tisa akiwa hana uhakika kama yeye ana hatia au hana hatia.

      Jioni moja katika Novemba 1974, sehemu ya kati ya jiji la Birmingham, Uingereza, ilisukwasukwa na mlipuko wa mabomu mawili yaliyowaua watu 21. Lilikuwa tukio ambalo “hakuna mtu yeyote katika Birmingham atalisahau kamwe,” akaandika Chris Mullen, ambaye ni Mbunge. Baadaye, “wanaume sita ambao hawakuhusika na mlipuko huo walipatikana na hatia ya uuaji kimakusudi ulio mkubwa zaidi katika historia ya Uingereza.” Baadaye kupatikana kwao na hatia kulifutiliwa mbali—lakini baada tu ya wanaume hao kukaa gerezani kwa muda wa miaka 16!

      Mshauri wa mambo ya sheria, Ken Crispin aliripoti kuhusu kesi ambayo “katika historia ya sheria ya Australia, ilivutia akili za umma katika njia ya pekee.” Familia fulani ilikuwa imepiga kambi karibu na mwamba uitwao Ayers Rock, wakati mtoto wao mchanga alipotoweka, asionekane tena kamwe. Mama yake alishtakiwa kuua kimakusudi, akapatikana na hatia, na kuhukumiwa kifungo cha maisha. Katika mwaka wa 1987, baada ya kufungwa jela kwa muda wa miaka zaidi ya mitatu, uchunguzi rasmi uligundua kwamba ushahidi uliotolewa dhidi yake haungetosha kumtia hatiani. Aliachiliwa na kusamehewa.

      Mwanamke mwenye umri wa miaka 18 aliyekuwa akiishi kusini mwa Marekani, aliuawa mwaka wa 1986. Mwanamume wa makamo alishtakiwa, akapatikana na hatia, na kuhukumiwa kifo. Alikaa katika chumba cha wanaohukumiwa kifo kwa muda wa miaka sita kabla ya kuthibitishwa kwamba, hakuwa amehusika na huo uhalifu.

      Je, hivi ni vielelezo nadra vya makosa ya kihukumu? David Rudovsky wa Chuo Kikuu cha Shule ya Sheria ya Pennsylvania asema hivi: “Nimekuwa katika mfumo wa sheria kwa miaka ipatayo 25 na nimeona kesi nyingi sana. Ningesema kwamba wale wenye kupatikana na hatia na ambao kwa kweli hawana hatia . . . ningewakadiria kuwa kati ya asilimia tano na asilimia 10.” Crispin auliza swali hili lenye kusumbua: “Je, kunao watu wengine wasio na hatia ambao wanaketi kwa kuvunjika moyo katika seli za magereza?” Je, makosa kama hayo yenye kuhuzunisha yanawezaje kutokea?

  • Haki ya Kweli Lini na Jinsi Gani?
    Mnara wa Mlinzi—1998 | Juni 15
    • Faraja kutoka katika Maandiko Matakatifu

      Katika Novemba 1952, Derek Bentley na Christopher Craig walivunja na kuingia katika ghala la bidhaa za biashara huko Croydon, karibu na London, Uingereza. Bentley alikuwa na umri wa miaka 19 naye Craig alikuwa na umri wa miaka 16. Polisi waliitwa, na Craig akampiga risasi na kumwua mmoja wa polisi hao. Craig alikaa gerezani kwa muda wa miaka tisa, ilhali Bentley alinyongwa katika Januari 1953 kwa kuua kimakusudi.

      Iris, dada ya Bentley, amefanya kampeni kwa miaka 40 ili kuliondolea jina la Derek hatia ya uuaji kimakusudi ambao hakuufanya. Katika mwaka wa 1993, Mamlaka ya Kifalme ilitoa msamaha kuhusiana na hiyo hukumu, ikikiri kwamba Derek Bentley hangalipaswa kamwe kunyongwa. Iris Bentley aliandika juu ya hiyo kesi katika kitabu Let Him Have Justice:

      Mwaka mmoja hivi kabla ya huo ufyatuaji wa risasi, Derek alikutana na Shahidi wa Yehova barabarani . . . Dada Lane aliishi katika Fairview Road, mahali palipokuwa karibu na kwetu, naye alimwalika Derek nyumbani kwake kusikiliza hadithi za Biblia. . . . Jambo lililosaidia lilikuwa kwamba Dada Lane alikuwa amerekodi hizo hadithi za Biblia, ambazo alimwazima [kwa kuwa Derek hakujua kusoma vizuri]. . . . Alikuwa akirudi kuniambia mambo ambayo huyo dada alikuwa amemwambia, mambo kama vile sisi sote tutafufuliwa baada ya kufa.”

      Iris Bentley alimzuru ndugu yake katika chumba cha wanaohukumiwa kifo kabla hajafishwa. Alihisije? “Mambo hayo ambayo Dada Lane alimwambia yalimsaidia kukabiliana na siku hizo chache za mwisho.”—Italiki ni zetu.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki