-
Kutambua Daraka la Yesu Akiwa Daudi Mkuu Zaidi na Sulemani Mkuu ZaidiMnara wa Mlinzi—2009 | Aprili 15
-
-
Daudi Alimfananisha Kristo
4, 5. (a) Yesu na Daudi wanalingana katika njia gani mbalimbali? (b) Kwa nini Yesu anaweza kuitwa Daudi Mkuu Zaidi?
4 Yesu alizaliwa Bethlehemu kama Daudi, miaka 1,100 hivi baada ya Daudi kuzaliwa. Yesu pia hakuonwa na wengi kuwa mfalme. Yaani, watu wengi katika Israeli hawakutarajia mfalme wa aina hiyo. Hata hivyo, Yehova alikuwa amemchagua Yesu kama alivyomchagua Daudi. Na kama Daudi, Yesu alipendwa na Yehova.a (Luka 3:22) ‘Roho ya Yehova ilianza kutenda kazi juu’ ya Yesu kama ilivyotenda juu ya Daudi.
5 Daudi na Yesu wanalingana katika mambo mengine mengi. Kwa mfano, Daudi alisalitiwa na mshauri wake Ahithofeli, naye Yesu alisalitiwa na mtume wake Yuda Iskariote. (Zab. 41:9; Yoh. 13:18) Daudi na Yesu walikuwa na bidii nyingi sana kwa ajili ya mahali pa ibada ya Yehova. (Zab. 27:4; 69:9; Yoh. 2:17) Yesu alikuwa pia mrithi wa Daudi. Kabla ya Yesu kuzaliwa, malaika alimwambia mama yake hivi: “Yehova Mungu atampa kiti cha ufalme cha Daudi baba yake.” (Luka 1:32; Mt. 1:1) Hata hivyo, Yesu ni mkuu zaidi kuliko Daudi kwa sababu ahadi zote kumhusu Masihi zingetimizwa na Yesu. Yeye ndiye Daudi Mkuu Zaidi, yule Mfalme wa Kimasihi aliyetazamiwa kwa muda mrefu.—Yoh. 7:42.
Mfuate Yule Mfalme-Mchungaji
6. Daudi alikuwa mchungaji mzuri katika njia gani?
6 Yesu ni mchungaji pia. Mchungaji mwema ana sifa gani? Analitunza, analilisha, na kulilinda kundi lake kwa uaminifu na kwa ujasiri. (Zab. 23:2-4) Daudi alipokuwa kijana alikuwa mchungaji, naye aliwatunza vizuri sana kondoo wa baba yake. Alitenda kwa ujasiri wakati kondoo hao walipokabili hatari na alihatarisha uhai wake ili kuwalinda kutokana na simba na dubu.—1 Sam. 17:34, 35.
7. (a) Ni nini kilichomtayarisha Daudi kutimiza madaraka yake akiwa mfalme? (b) Yesu alionyesha jinsi gani kwa matendo kwamba yeye ndiye Mchungaji Mwema?
7 Miaka ambayo Daudi alikaa mashambani na milimani akiwatunza kondoo ilimtayarisha kutimiza wajibu na madaraka mazito zaidi ya kulichunga taifa la Israeli.b (Zab. 78:70, 71) Yesu pia ameonyesha kwa matendo kwamba yeye ni mchungaji bora kabisa. Yehova anamwongoza na kumpa nguvu za kulichunga ‘kundi lake dogo’ na pia “kondoo wengine.” (Luka 12:32; Yoh. 10:16) Hivyo, Yesu ndiye yule Mchungaji Mwema. Anajua kundi lake vizuri sana hivi kwamba anamwita kila kondoo kwa jina. Anawapenda sana kondoo wake hivi kwamba alipokuwa duniani alijitoa kwa kupenda kwa ajili yao. (Yoh. 10:3, 11, 14, 15) Akiwa Mchungaji Mwema, Yesu anatimiza mambo ambayo Daudi hangeweza kamwe kutimiza. Fidia au dhabihu yake ya ukombozi iliwapa wanadamu nafasi ya kuokolewa kutoka katika kifo. Hakuna kitu kinachoweza kumzuia asilichunge ‘kundi lake dogo’ ili lipate uhai usioweza kufa mbinguni na kuwaongoza ‘kondoo wake wengine’ kupata uzima wa milele katika ulimwengu mpya wenye uadilifu usio na watu hatari ambao ni kama mbwa-mwitu.—Soma Yohana 10:27-29.
Mfuate Yule Mfalme Anayeshinda
8. Daudi alithibitika jinsi gani kuwa mfalme anayeshinda?
8 Akiwa mfalme, Daudi alikuwa shujaa mwenye ujasiri ambaye aliilinda nchi ya watu wa Mungu, na “Yehova akaendelea kumwokoa Daudi popote alipoenda.” Chini ya uongozi wa Daudi, mipaka ya taifa hilo ilipanuka kutoka mto wa Misri mpaka mto Efrati. (2 Sam. 8:1-14) Kwa uwezo wa Yehova, Daudi alikuja kuwa mtawala mwenye nguvu zaidi. Biblia inasema: “Sifa ya Daudi ikaanza kuenea katika nchi zote, na Yehova akatia hofu yake juu ya mataifa yote.”—1 Nya. 14:17.
9. Eleza jinsi Yesu alivyoshinda akiwa Mfalme Aliyechaguliwa.
9 Kama Mfalme Daudi, Yesu pia hakuwa mwoga alipokuwa mwanadamu. Akiwa Mfalme Aliyechaguliwa, alionyesha mamlaka yake juu ya roho waovu, na kuwaokoa watu kutoka kwa uvutano wao. (Marko 5:2, 6-13; Luka 4:36) Hata adui wake mkuu, Shetani Ibilisi, hana uwezo juu yake. Kwa uwezo wa Yehova, Yesu aliushinda ulimwengu, ambao unakaa katika nguvu za Shetani.—Yoh. 14:30; 16:33; 1 Yoh. 5:19.
10, 11. Yesu ana daraka gani akiwa Mfalme-Shujaa wa Vita huko mbinguni?
10 Miaka 60 hivi baada ya Yesu kufa na kufufuliwa kwenye uhai mbinguni, mtume Yohana alipata maono ya kinabii kuhusu Yesu akitimiza daraka Lake akiwa Mfalme-Shujaa wa Vita huko mbinguni. Yohana anaandika hivi: “Tazama! farasi mweupe; na yule anayeketi juu yake alikuwa na upinde; naye akapewa taji, naye akaenda akishinda na kukamilisha ushindi wake.” (Ufu. 6:2) Yesu ndiye anayepanda farasi huyo mweupe. ‘Alipewa taji’ mwaka wa 1914 wakati alipowekwa kuwa Mfalme katika Ufalme wa mbinguni. Baada ya hapo, “akaenda akishinda.” Ndiyo, kama Daudi, Yesu ni mfalme anayeshinda. Muda mfupi baada ya kuwekwa kuwa Mfalme wa Ufalme wa Mungu, alimshinda Shetani katika vita na kumtupa duniani pamoja na roho wake waovu. (Ufu. 12:7-9) Ataendelea kupanda farasi na kushinda mpaka ‘atakapokamilisha ushindi wake,’ na kuuharibu kabisa mfumo mwovu wa Shetani.—Soma Ufunuo 19:11, 19-21.
11 Hata hivyo, kama Daudi, Yesu ni mfalme mwenye huruma, naye ataulinda “umati mkubwa” ili uokoke Har-Magedoni. (Ufu. 7:9, 14) Zaidi ya hayo, chini ya utawala wa Yesu na wale warithi wenzake 144,000 waliofufuliwa, kutakuwa na “ufufuo wa waadilifu na wasio waadilifu pia.” (Mdo. 24:15) Wale watakaofufuliwa duniani watakuwa na tumaini la kuishi milele. Watakuwa na maisha mazuri ajabu wakati ujao! Sote na tuazimie kuendelea ‘kufanya yaliyo mema,’ ili tuishi wakati ambapo dunia itajaa raia waadilifu na wenye furaha wa yule Daudi Mkuu Zaidi.—Zab. 37:27-29.
-
-
Kutambua Daraka la Yesu Akiwa Daudi Mkuu Zaidi na Sulemani Mkuu ZaidiMnara wa Mlinzi—2009 | Aprili 15
-
-
a Huenda jina Daudi linamaanisha “Mpendwa.” Wakati Yesu alipobatizwa na wakati alipogeuka umbo, Yehova alizungumza kutoka mbinguni akimwita “mwanangu, mpendwa.”—Mt. 3:17; 17:5.
b Daudi alikuwa pia kama mwana-kondoo anayemtumaini mchungaji wake. Alimtegemea yule Mchungaji Mkuu Zaidi, Yehova, ili amlinde na kumwongoza. Alisema hivi akiwa na uhakika kabisa: “Yehova ni Mchungaji wangu. Sitakosa chochote.” (Zab. 23:1) Yohana Mbatizaji alimtambulisha Yesu kuwa “Mwana-Kondoo wa Mungu.”—Yoh. 1:29.
-