Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 9/8 kur. 5-8
  • Ulimwengu Ufundishwao Kuchukia

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ulimwengu Ufundishwao Kuchukia
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kuanza na Wachanga
  • Dini Hufundisha Nini?
  • Hofu, Hasira, au Hisia ya Kupatwa na Madhara
  • Je, Chuki Itakoma Wakati Wowote?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1995
  • Njia Pekee ya Kukomesha Chuki
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2000
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2005
  • Kwa Nini Kuna Chuki Sana?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Toleo la Watu wote)—2022
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 9/8 kur. 5-8

Ulimwengu Ufundishwao Kuchukia

WATU ni wenye ubinafsi kiasili. Na ubinafsi, usipodhibitiwa, unaweza kugeuka ukawa chuki. Na wanadamu si wenye ubinafsi tu kiasili, lakini zaidi ya hiyo jamii ya wanadamu hasa huzoeza watu kuwa wenye ubinafsi!

Bila shaka, kujumlisha maneno hakufai sikuzote, lakini mielekeo fulani imeenea sana hivi kwamba haiwezi kupuuzwa tu kuwa mambo ya ujumla. Je, si kweli kwamba mara nyingi wanasiasa hupendezwa zaidi na kushinda uchaguzi kuliko kuwasaidia watu ambao wanawakilisha bungeni? Je, si kweli kwamba mara nyingi wafanya-biashara hupendezwa zaidi na kuchuma pesa, kwa njia mbaya ikiwa lazima, kuliko kuzuia bidhaa zenye madhara zisifikie soko? Je, si kweli kwamba mara nyingi makasisi hupendezwa zaidi na kuwa mashuhuri au kuchuma pesa kuliko kuongoza makundi yao katika njia za adili na za upendo?

Kuanza na Wachanga

Watoto wanapolelewa katika mazingira ya uendekevu, kwa hakika wao wanazoezwa kuwa wenye ubinafsi, kwa kuwa ufikirio na hali ya kutokuwa na ubinafsi hupuuzwa ili kuandalia tamaa zao za kitoto. Shuleni na chuoni, wanafunzi wanafundishwa kujitahidi kuwa namba moja, si tu kimasomo bali pia kimichezo. Shime ni, “Ukiwa wa pili, hiyo ni sawa tu na kuwa wa mwisho!”

Michezo ya vidio yenye kuonyesha ujeuri hufundisha vijana kusuluhisha matatizo kwa njia ya ubinafsi—angamiza tu adui! Mwelekeo ambao haukuzi upendo kamwe! Zaidi ya mwongo mmoja uliopita, ofisa mkuu wa afya wa Marekani alitoa onyo kwamba michezo ya vidio ni tisho kwa vijana. Alisema: “Kila kitu ni angamiza adui. Hakuna kitu chenye kujenga katika hii michezo.” Barua iliyoandikiwa The New York Times ilisema kwamba michezo mingi ya vidio “huridhisha silika zilizopotoka zaidi za wanadamu” kisha ikaongezea: “Hiyo inasitawisha kizazi cha wabalehe kisichojali na chenye hasira-hasira.” Shabiki mmoja wa michezo ya vidio kutoka Ujerumani alikuwa mnyoofu sana hivi kwamba akakiri ukweli wa taarifa hiyo ya mwisho aliposema: “Nilipokuwa nikiicheza [michezo ya vidio] nilihamishwa hadi ulimwengu wa ndoto ambamo shime ya kale ilitumika: ‘Ua au uuawe.’”

Chuki inapochanganyana na ubaguzi wa kijamii, hiyo huwa mbaya hata zaidi. Kwa hiyo Wajerumani kwa wazi wanahangaika juu ya kuwapo kwa vidio zenye kushikilia mambo ya kidesturi ambazo huonyesha ujeuri dhidi ya wageni, hasa dhidi ya Waturuki. Na wana sababu nzuri ya kuhangaika, kwa kuwa tangu Januari 1, 1994, Waturuki walifanyiza asilimia 27.9 ya wakazi wageni wapatao 6,878,100 walio nchini Ujerumani.

Hisia za ubaguzi husitawisha yale ambayo utukuzo wa taifa hufundisha watoto tangu utoto sana, yaani, si kosa kuchukia maadui wa taifa lenu. Insha moja iliyoandikwa na George M. Taber, ambaye huchangia makala za Time, ilisema: “Kati ya hali zote za kisiasa katika historia, labda yenye nguvu zaidi ni utukuzo wa taifa.” Aliendelea kueleza: “Damu nyingi zaidi imemwagwa katika jina lake kuliko iliyomwagwa na jambo jingine lolote ila dini. Kwa karne nyingi viongozi wamechochea umati wenye ushupavu kwa kulaumu kabila fulani la jirani kuwa chanzo cha matatizo yao yote.”

Chuki ya kudumu dhidi ya makabila, jamii, na watu wa mataifa mengine ndiyo kisababishi cha matatizo mengi katika ulimwengu wa leo. Na kuhofu wageni kunaongezeka. Hata hivyo, kwa kupendeza, kikundi fulani cha wataalamu wa elimu ya jamii walio Wajerumani kiligundua kwamba kuwahofu wageni hudhihirika zaidi katika mahali wanapoishi wageni wachache. Hiyo yaonekana kuthibitisha kwamba kuhofu wageni mara nyingi husababishwa na ubaguzi kuliko kutokana na mambo ambayo mtu mwenyewe amejionea. “Ubaguzi wa vijana mara nyingi hukuzwa na marafiki na familia zao,” wataalamu hao wa elimu ya jamii waligundua. Kwa hakika, asilimia 77 kati ya wale waliohojiwa, hata ingawa walikubali ubaguzi, hawakuwa na uwasiliano wa moja kwa moja na wageni au kama ulikuwepo, basi ulikuwa kidogo sana.

Si vigumu kufundisha somo la kuwa mwenye ubinafsi, kwa kuwa sisi sote tumerithi kiasi fulani cha ubinafsi kutoka kwa wazazi wasiokamilika. Lakini, dini ina fungu gani katika pambano baina ya upendo na chuki?

Dini Hufundisha Nini?

Kwa ujumla, watu hufikiri kwamba dini husitawisha upendo. Lakini, kama ni hivyo, kwa nini tofauti za kidini ndizo kisababishi kikuu cha uvutano ulio katika Ireland ya Kaskazini, Mashariki ya Kati, na India, tukitaja vielelezo vitatu tu? Bila shaka, watu wengine hubisha kwamba tofauti za kisiasa, wala si za kidini, ndizo zinazotokeza mvurugo. Hilo ni jambo la kubishaniwa. Kwa vyovyote vile, ni wazi kwamba dini mashuhuri imeshindwa kukazia watu upendo wenye nguvu uwezao kushinda ubaguzi wa kisiasa na kikabila. Na basi waumini wengi Wakatoliki na Waothodoksi, na wale wa imani nyingine, huruhusu ubaguzi, ambao hutokeza ujeuri.

Hakuna jambo baya kwa kujaribu kukanusha mafundisho na mazoea ya kikundi fulani cha kidini ambayo mtu huenda akahisi ni yenye makosa. Lakini, je, hiyo yampa haki ya kutumia ujeuri katika kupigana nacho au washiriki wake? Kitabu The Encyclopedia of Religion chakiri hivi kwa unyoofu: “Viongozi wa kidini wameitisha mashambulio yenye jeuri dhidi ya vikundi vingine vya kidini kwa kurudia-rudia katika historia ya Mashariki ya Karibu na ya Ulaya.”

Ensaiklopedia hiyo hufunua kwamba ujeuri ni sehemu ya asili ya dini, kwa kusema: “Wafuasi wa Darwin hawako peke yao katika kukubali kwamba ni lazima kuwe na mapambano ili kuwe na ukuzi wa kijamii na wa kiakili. Dini imekuwa chanzo cha mapambano yasiyokoma, cha ujeuri, na hivyo, cha ukuzi.”

Ujeuri hauwezi kutetewa kuwa unahitajika ndipo kuwe na ukuzi, kwa kuwa huo ni kinyume cha kanuni ijulikanayo sana iliyowekwa na Yesu Kristo wakati mtume Petro alipojaribu kumlinda. Petro ‘alinyoosha mkono wake na kufuta upanga wake na kumpiga mtumwa wa kuhani wa cheo cha juu na kuondoa sikio lake. Kisha Yesu akamwambia: “Rudisha upanga wako mahali pao, kwa maana wale wote wauchukuao upanga wataangamia kwa upanga.”’—Mathayo 26:51, 52; Yohana 18:10, 11.

Ujeuri unaoelekezwa dhidi ya watu mmoja-mmoja—wawe watu wazuri au wabaya—si njia ya upendo. Hivyo, watu ambao hugeukia ujeuri hutenda kinyume cha dai lao la kumwiga Mungu mwenye upendo. Majuzi, mtungaji Amos Oz alisema: “Ni kawaida kwa washupavu wa kidini . . . kwamba ‘maagizo’ wanayopokea kutoka kwa Mungu sikuzote ni, hasa moja: Ua. Yule mungu wa washupavu wote aelekea zaidi kuwa ibilisi.”

Biblia husema jambo ambalo linafanana na hilo: “Watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi ni dhahiri kwa jambo hili: Kila mtu ambaye haendelezi uadilifu hatokani na Mungu, wala yeye ambaye hapendi ndugu yake. Kila mtu ambaye huchukia ndugu yake ni muua-binadamu-kikatili, nanyi mwajua kwamba hakuna muua-binadamu-kikatili aliye na uhai udumuo milele ukikaa katika yeye. Ikiwa yeyote atoa taarifa: ‘Mimi nampenda Mungu,’ na bado anachukia ndugu yake, yeye ni mwongo. Kwa maana yeye ambaye hapendi ndugu yake, ambaye ameona, hawezi kuwa anapenda Mungu, ambaye hajaona. Na amri hii tunayo kutoka kwake, kwamba yeye ambaye hupenda Mungu apaswa kuwa anapenda ndugu yake pia.”—1 Yohana 3:10, 15; 4:20, 21.

Dini ya kweli ni lazima ifuate kiolezo cha upendo, ambacho hutia ndani kuwaonyesha hata maadui upendo. Twasoma hivi kuhusu Yehova: “Yeye hufanya jua lake lichomoze juu ya watu waovu na wema na kufanya mvua inyeshe juu ya watu waadilifu na wasio waadilifu.” (Mathayo 5:44, 45; ona pia 1 Yohana 4:7-10.) Ni tofauti kama nini na Shetani, mungu wa chuki! Yeye huwavutia na kuwashawishi watu wakaishi maisha za ufasiki, uhalifu, na ubinafsi, na hivyo wakijaza maisha zao uchungu na huzuni. Yeye huendelea kufanya hivyo akijua vema kwamba mtindo-maisha huo uliopotoka hatimaye utatokeza uharibifu wao. Je, ndiye aina ya mungu astahiliye kutumikiwa, yule ambaye hawezi—na kwa wazi hata hataki—kuwalinda walio wake?

Hofu, Hasira, au Hisia ya Kupatwa na Madhara

Jambo la kwamba mambo haya hutokeza chuki huthibitishwa kwa urahisi. Ripoti moja ya Time yasema: “Tangu miaka yenye matatizo ya 1930 vikundi vingi vyenye kushikilia sana desturi Ulaya havijapata kutumia fursa nyingi mno . . . Wakihofia kazi zao, watu huelekeza hasira zao dhidi ya kushindwa kwa serikali zenye siasa za kadiri na kuwalaumu wageni walio miongoni mwao.” Jörg Schindler, katika Rheinischer Merkur/Christ und Welt, alivuta uangalifu kwenye makumi ya maelfu ya wakimbizi wa kisiasa ambao wamemiminikia Ujerumani kwa zaidi ya miongo miwili ambayo imepita. Gazeti The German Tribune laonya: “Ubaguzi wa kijamii umeongezeka kotekote Ulaya.” Mmiminiko wa wahamiaji wengi sana hutokeza hisia za chuki. Watu husikika wakilalamika: ‘Wanatugharimu fedha, wanachukua kazi zetu, wao ni hatari kwa binti zetu.’ Theodore Zeldin, mshiriki wa Chuo cha St. Antony, katika Oxford, alisema watu “ni wenye jeuri kwa sababu wao huhisi wametishwa au kutwezwa. Ni kisababishi cha hasira zao ndicho kinachohitaji kuchunguzwa.”

Mtangazaji wa televisheni wa Uingereza Joan Bakewell atumia maneno yafaayo kufafanua ulimwengu wetu, ulimwengu ufundishao raia zake kuchukia. Yeye aandika: “Mimi si Mkristo mwenye imani ya kidesturi, lakini natambua katika mafundisho ya Yesu kweli kubwa sana: uovu ni kutokuwapo kwenye msiba kwa upendo. . . . Najua twaishi katika jamii ambayo haisifu sana fundisho la upendo. Kwa hakika, jamii iliyo mbovu hivi kwamba inakataa fundisho kama hilo kuwa la kipuuzi, la kihisia-moyo, lisilowezekana, ambalo hudhihaki mawazo ya kutanguliza hali ya kujali na kutokuwa mwenye ubinafsi mbele ya faida na upendezi wa kibinafsi. ‘Tuone mambo kihalisi’ jamii husema inaposhikilia mambo ya kibiashara ya karibuni zaidi, inapodanganya juu ya wajibu wake na kupuuza uthibitisho unaoionyesha kwamba imekosea. Ulimwengu kama huo hutokeza watu wasiofaulu, wapweke, watu ambao wamepoteza mambo yaonwayo na jamii kuwa ya kutangulizwa ya ufanisi, kujistahi na familia zenye furaha.”

Kwa wazi, mungu wa ulimwengu huu, Shetani, anafundisha wanadamu kuchukia. Lakini tukiwa mmoja-mmoja, twaweza kujifunza kupenda. Makala ifuatayo itaonyesha jinsi jambo hilo linavyowezekana.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Je, yawezekana kwamba michezo ya vidio inafundisha watoto wako kuchukia?

[Picha katika ukurasa wa 8]

Ujeuri wa vita ni ishara ya kutokuwa na ujuzi na kuwa na chuki

[Hisani]

Pascal Beaudenon/Sipa Press

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki