Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w95 6/15 kur. 3-4
  • Je, Chuki Itakoma Wakati Wowote?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je, Chuki Itakoma Wakati Wowote?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kupanda Mbegu za Chuki
  • Matokeo ya Chuki
  • Kwa Nini Kuna Chuki Sana?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Toleo la Watu wote)—2022
  • Tunaweza Kushinda Chuki!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Toleo la Watu wote)—2022
  • Kwa Nini Kuna Chuki Sana?
    Amkeni!—1997
  • Wakati Ambapo Chuki Haitakuwapo Tena!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Toleo la Watu wote)—2022
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1995
w95 6/15 kur. 3-4

Je, Chuki Itakoma Wakati Wowote?

IKIWA umetazama hata habari chache katika televisheni, unatambua chuki. Chuki ndiyo msingi wa mgawanyiko unaoleta machinjo makubwa ya karibu kila siku yanayoacha alama ya damu. Kutoka Belfast hadi Bosnia, kutoka Jerusalem hadi Johannesburg, watu wasiohusika na wasio na kinga huchinjwa.

Kwa kawaida washambuliwa huwa hawajulikani kwa washambuliaji. “Uhalifu” wao wa pekee ni kwamba pengine wao ni wa “upande mwingine.” Katika kisasi chenye ukatili, vifo kama hivyo huenda vikawa kulipiza kisasi kwa sababu ya ukatili fulani wa awali au aina fulani ya “utakaso wa kabila.” Kila jeuri inayotokea huchochea chuki kati ya vikundi vyenye uhasama.

Mfululizo huo wa chuki waonekana kuwa unaongezeka. Uadui baina ya watu wa ukoo mmoja unatokea kati ya makabila, jamii mbalimbali, vikundi vya kikabila au vya kidini. Je, kweli chuki inaweza kuondolewa? Ili kujibu hilo, tunahitaji kuelewa visababishi vya chuki, kwa kuwa hatukuzaliwa na mwelekeo wa chuki.

Kupanda Mbegu za Chuki

Zlata Filipovic, msichana mchanga Mbosnia kutoka Sarajevo, bado hajajifunza kuchukia. Katika kitabu chake cha kuweka kumbukumbu yeye huandika mambo ya kusisimua kuhusu jeuri ya kati ya makabila: “Sikuzote mimi huuliza, Kwa sababu gani? Ya nini? Ni nani anayesababisha? Mimi huuliza lakini sipati jibu. . . . Miongoni mwa wasichana rafiki zangu, miongoni mwa rafiki zetu, katika familia yetu, mna Waserbia na Wakroati na Waislamu. . . . Sisi huchangamana na walio wazuri, si walio wabaya. Na miongoni mwa walio wazuri mna Waserbia na Wakroati na Waislamu, sawa na ilivyo miongoni mwa walio wabaya.”

Kwa upande mwingine, watu wazima wengi, hufikiri kinyume. Wao hufikiri kwamba wana sababu ya kutosha ya kuchukiana. Kwa nini?

Ukosefu wa haki. Huenda shina la chuki ni ukosefu wa haki na uonevu. Kama Biblia isemavyo, “uonevu tu waweza kufanya mwenye hekima kutenda kwa ukichaa.” (Mhubiri 7:7, New World Translation) Watu waonewapo au kutendwa kinyama, ni rahisi kwao kusitawisha chuki kwa wanaowaonea. Na ijapokuwa huenda likawa jambo lisilo la kufikiri kuzuri, au “ukichaa,” chuki hiyo mara nyingi huelekezwa dhidi ya kabila lote.

Wakati ukosefu wa haki, wa kweli au wa kuwaziwa, huenda ukawa shina hasa la chuki, si huo pekee. Jambo jingine ni ubaguzi.

Ubaguzi. Ubaguzi mara nyingi huletwa na kutofahamu mambo kuhusu kundi la kikabila au taifa. Kwa sababu ya mambo ya kusikiwa, uadui wa kidesturi, au kutokubaliana na mtu mmoja au wawili, watu fulani huenda wakalipa kabila au taifa zima sifa mbaya. Mara ubaguzi upandwapo, unaweza kupofusha watu kutoka kwa ukweli. “Sisi huchukia watu fulani kwa sababu hatuwajui; na hatutawajua kwa sababu tunawachukia,” asema mwandikaji Mwingereza Charles Caleb Colton.

Kwa upande mwingine, wanasiasa na wanahistoria, wanaweza kuendeleza ubaguzi kimakusudi kwa ajili ya faida za kisiasa au za kitaifa. Hitler alikuwa kielelezo kikubwa. Georg, aliyekuwa mshiriki wa kikundi cha Vijana wa Hitler, asema hivi: “Propaganda za Nazi kwanza zilitufundisha kuchukia Wayahudi, halafu Warusi, kisha ‘maadui wote wa utawala wa Nazi.’ Nikiwa tineja, niliamini yale niliyoambiwa. Baadaye, niligundua kwamba nilikuwa nimedanganywa.” Kama ilivyokuwa katika Ujerumani ya Nazi na penginepo, ubaguzi wa rangi au wa vikundi vya kikabila umetetewa na utukuzo wa taifa, chanzo kingine cha chuki.

Utukuzo wa taifa, ukabila, na ubaguzi wa rangi. Katika kitabu chake The Cultivation of Hatred, mwanahistoria Peter Gay husimulia yaliyotokea wakati vita ya ulimwengu ya kwanza ilipotokea: “Katika jitihada za uaminifu, utukuzo wa taifa ulitokeza sana juu ya mambo yale mengine yote. Upendo wa mtu kwa nchi yake na chuki kwa maadui wayo ulikuwa kisababishi kikubwa sana cha chuki iliyotokezwa na karne ndefu ya kumi na tisa.” Maneno ya Kijerumani ya utukuzo wa taifa yalieneza wimbo wa kivita uitwao “Wimbo wa Chuki.” Gay aeleza, wachochezi wa chuki katika Uingereza na Ufaransa walitunga hadithi kuhusu wanajeshi wa Ujerumani wakinajisi wanawake na kuua watoto. Mwanajeshi Mwingereza, Siegfried Sassoon, asimulia kiini cha propaganda ya vita ya Uingereza: “Inaonekana, mtu alikuwa ameumbwa aue Wajerumani.”

Kama vile utukuzo wa taifa, kutukuza kupita kiasi kikundi fulani cha kikabila au watu wa rangi fulani kwaweza kuleta chuki ya vikundi tofauti vya kikabila au watu wa rangi tofauti. Ukabila unaendelea kutokeza jeuri katika nchi nyingi za Afrika wakati uleule ubaguzi wa rangi bado unaathiri Ulaya Magharibi na Amerika Kaskazini. Kitu kingine chenye kutenganisha ambacho huenda kikapatana na utukuzo wa taifa ni dini.

Dini. Mapigano mabaya zaidi ulimwenguni yanahusika sana na dini. Katika Ireland Kaskazini, Mashariki ya Kati, na kwingineko, watu huchukiwa kwa sababu ya dini wanayodai kufuata. Zaidi ya karne mbili zilizopita, mwandikaji Mwingereza Jonathan Swift alisema: “Tuna dini ya kutosha kutufanya tuchukiane, lakini isiyotosha kutufanya tupendane.”

Katika 1933, Hitler alimwambia kasisi wa Osnabrück hivi: ‘Kuhusu Wayahudi, mimi nitaendelea tu na maoni yaleyale ambayo Kanisa Katoliki limekuwa nayo kwa miaka 1,500.’ Machinjo yake yenye chuki kwa watu wasio na hatia hayakuwahi kamwe kushutumiwa na viongozi wengi wa kidini Wajerumani. Paul Johnson, katika kitabu chake A History of Christianity, asema kwamba “Kanisa liliwatenga Wakatoliki walioandika katika wasia kuwa wakifa wangependa kuchomwa, . . . lakini halikuwazuia kufanya kazi katika kambi za mateso au za kifo.”

Viongozi fulani wa kidini hata wamepita kiasi katika kukubali chuki—wameitakasa. Katika 1936, Vita ya Hispania ya Wenyewe kwa Wenyewe ilipotokea, Papa Pius 11 alishutumu ‘chuki ya kikweli ya kishetani dhidi ya Mungu’ ya wafuasi wa Republicans—ijapokuwa kulikuwa na makasisi Wakatoliki upande wa Republican. Sawa na hayo, Kardinali Gomá, aliyekuwa mkuu wa kidini wa Hispania wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, alidai kwamba ‘mapatano ya amani hayawezekani bila vita.’

Chuki ya kidini haionyeshi dalili yoyote ya kupungua. Katika 1992 gazeti Human Rights Without Frontiers lilishutumu jinsi wakuu wa Kanisa Othodoksi la Kigiriki walivyokuwa wakichochea chuki dhidi ya Mashahidi wa Yehova. Lilitaja, miongoni mwa vielelezo vingi, kisa cha kasisi wa Othodoksi ya Kigiriki aliyechukua hatua za kisheria dhidi ya Mashahidi wawili wenye umri wa miaka 14. Shtaka lilikuwa nini? Aliwashtaki kwa ‘kujaribu kumfanya abadili dini yake.’

Matokeo ya Chuki

Ulimwenguni pote, mbegu za chuki zinapandwa na kutiliwa maji kupitia ukosefu wa haki, ubaguzi, utukuzo wa taifa, na dini. Tokeo lisilozuilika ni hasira, uchokozi, vita, na uharibifu. Usemi wa Biblia kwenye 1 Yohana 3:15 watusaidia tuone uzito wa jambo hili: “Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji.” Kwa hakika, mahali chuki inasitawi, amani—ikiwapo—inahatarishwa.

Elie Wiesel, mshindi wa Tuzo ya Nobel na mwokokaji wa Maangamizi Makubwa, aandika hivi: “Kazi ya mwokokaji ni kutoa ushahidi wa yale yaliyotokea . . . Ni lazima uonye watu kwamba mambo haya yaweza kutokea, kwamba uovu waweza kutokea. Chuki ya jamii, jeuri, ibada ya sanamu—bado zinasitawi.” Historia ya karne ya 20 hutoa uthibitisho kwamba chuki si moto utakaopoa wenyewe.

Je, kweli chuki itapata kung’olewa kutoka mioyo ya watu? Je, sikuzote chuki ni yenye kuharibu, au kuna upande unaofaa? Acha tuone.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki