Kwa Nini Kuna Chuki Sana?
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UJERUMANI
“KWA nini”—maneno mafupi, lakini yenye kudai jibu. Kwa kielelezo, yalipoonekana katika karatasi iliyokuwa miongoni mwa marundo ya maua na vichezeo vya aina ya teddy bear vilivyokuwa vimewekwa nje ya shule moja kule Dunblane, Scotland, Machi 1996. Siku chache tu mapema, mtu fulani aliingia ndani haraka akawapiga risasi watoto 16 pamoja na mwalimu wao na kuwaua. Aliwajeruhi wengine kadhaa kisha akajipiga risasi. Bila shaka, alijawa na chuki—alijichukia, aliwachukia wengine, na alichukia jumuiya kwa ujumla. Wazazi na marafiki wenye huzuni na vilevile mamilioni ya watu ulimwenguni kote waliuliza swali lilo hilo, ‘Kwa nini? Kwa nini watoto wasio na hatia wafa hivi?’
Jambo la kwamba ulimwengu umejaa chuki mbaya ambayo haiwezi kuelezeka yaelekea halijakupita. Kwa hakika, kwa sababu moja au nyingine, huenda ikawa kwamba wewe mwenyewe umepata kuwa mhasiriwa wa chuki. Labda wewe vilevile umepata kuuliza, ‘Kwa nini?’—labda zaidi ya mara moja.
Chuki za Aina Nzuri na za Aina Mbaya
“Chuki” hufafanuliwa kuwa “uhasama mkubwa na karaha.” Bila shaka, inanufaisha kuwa na “uhasama mkubwa na karaha” dhidi ya mambo ambayo yanadhuru au ambayo yanaweza kuharibu mahusiano ya kibinafsi ya mtu. Ikiwa kila mtu angekuwa na chuki ya aina hii, kwa kweli ulimwengu ungekuwa mahali bora zaidi pa kuishi. Lakini, kwa kusikitisha wanadamu wasiokamilika huelekea kuchukia mambo wasiyopaswa kuyachukia wakiwa na sababu zisizo nzuri.
Chuki yenye kuharibu hutegemea ubaguzi, kutokuwa na ujuzi, au kuarifiwa vibaya na mara nyingi husababishwa na “hofu, hasira, au kuhisi kujeruhiwa,” kulingana na ufafanuzi mmoja. Kwa kuwa haina msingi mzuri, chuki hii hutokeza mabaya na kwa kurudia-rudia hulizusha lile swali, ‘Kwa nini?’
Sisi sote twajua watu ambao tabia zao na mazoea yao huenda yakatuudhi nyakati nyingine na ambao tunaona ugumu wa kushirikiana nao. Lakini kuudhiwa ni jambo moja; tamaa ya kuwajeruhi wengine kimwili ni jambo jingine tofauti kabisa. Kwa hiyo, huenda tukapata ugumu wa kufahamu jinsi mtu awezavyo kufungia chuki moyoni kwa vikundi vizima vya watu, mara nyingi watu ambao hata yeye hawafahamu. Huenda ikawa kwamba hawakubaliani na maoni yake ya kisiasa, ni wa dini tofauti, au ni wa kabila jingine, lakini je, hiyo ni sababu ya kuwachukia?
Na bado, chuki ya aina hiyo ipo! Katika Afrika chuki iliyafanya makabila ya Wahutu na Watutsi yachinjane nchini Rwanda mwaka wa 1994, ikifanya ripota mmoja aulize: “Chuki sana kadiri hiyo ilirundamanaje katika nchi ndogo hivyo?” Katika Mashariki ya Kati, chuki imesababisha mashambulizi ya magaidi yanayofanywa na Waarabu na Waisraeli washupavu. Katika Ulaya chuki ilitokeza kusambaratika kwa ile iliyokuwa Yugoslavia. Na kulingana na ripoti moja ya gazeti la habari, nchini Marekani pekee “vikundi vya chuki vipatavyo 250” vinaeneza mawazo ya ubaguzi wa kijamii. Kwa nini kuna chuki sana? Kwa nini?
Chuki ina misingi imara sana hivi kwamba hata wakati ambapo mapambano ambayo imesababisha yametatuliwa, hiyo hudumu. Ama tunaweza kuelezaje ugumu wa kudumisha amani na wa kukomesha mapigano katika nchi zilizovurugwa na vita na zenye mapigo ya magaidi? Tunaweza kuelezaje kile kilichotukia baada ya mkataba wa amani uliotiwa sahihi mwishoni mwa 1995 katika Paris kusema kwamba jiji la Sarajevo liungane tena chini ya Shirikisho la Bosnia na Herzegovina-Kroatia? Wengi wa Waserbia walioishi huko walianza kutoroka jiji hilo na viunga vyake wakiogopa kulipiziwa kisasi. Likiripoti kwamba watu walikuwa wakipora na kuchoma majengo waliyokuwa wakiacha, gazeti Time lilimalizia hivi: “Sarajevo limeungana tena; watu wake hawajaungana.”
Amani miongoni mwa watu wanaochukiana ni amani bandia tu, haina thamani kama noti bandia. Ikiwa haina chochote cha thamani kuitegemeza, hiyo yaweza kuporomoka kwa mkazo mdogo sana. Lakini kuna chuki sana ulimwenguni na hakuna upendo sana. Kwa nini?
[Blabu katika ukurasa wa 4]
Chuki yenye kuharibu hutegemea ubaguzi, kutokuwa na ujuzi, au kuarifiwa vibaya