Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kuishi kwa Woga
    Amkeni!—2005 | Agosti 8
    • Kuishi kwa Woga

      ROXANAa anaogopa kumwambia mume wake kwamba anataka kufanya kazi ya muda. Wakati mmoja, alipomwomba mume wake nauli ili akamtembelee mama yake, alimpiga Roxana kwa nguvu sana hivi kwamba alihitaji kutibiwa. Yeye huishi kwa woga daima.

      Rolando alizoea kumruhusu mke wake arudi nyumbani usiku kwa kutumia usafiri wa umma, lakini sasa yeye huenda kumchukua kwa gari lao. Kumekuwa na visa vingi sana vya jeuri mahali wanapoishi hivi kwamba anahofia usalama wa mke wake.

      Haidé hufanya kazi katikati mwa mji mkuu. Wakati mmoja alipokuwa akirudi nyumbani, alijikuta katikati ya waandamanaji walioanzisha jeuri. Sasa kila mara anaposikia waandamanaji wakipita, yeye huwa na wasiwasi. Anasema hivi: “Sijihisi nikiwa salama. Sitaki kufanya kazi hapa tena. Lakini sina la kufanya.”

      Roxana, Rolando, na Haidé wanaathiriwa na woga, na si woga ambao mtu huwa nao wakati tu hali ya dharura inapotokea. Wanaathiriwa na woga huo daima. Watu wanapolazimika kuishi kwa woga, huenda wakahisi hawana nguvu. Woga unaweza kuwanyima furaha kwa kuwazuia wasifanye wanachotaka. Woga unaweza kutawala fikira za watu na kuwazuia kukazia fikira mambo mengine.

      Kuishi kwa woga hufadhaisha sana. Mara nyingi kunasababisha mshuko wa moyo na kunaweza kudhuru afya. Gazeti linalozungumzia masuala ya afya linaeleza kwamba “mfadhaiko huzuia mfumo wa kinga usifanye kazi na hilo huchangia magonjwa mengi. Mwili utaonyesha dalili za madhara ya muda mrefu, hasa katika viungo vilivyoathiriwa. Mtu anaweza kupatwa na tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu, ugonjwa wa moyo, ugonjwa wa figo, magonjwa ya tumbo, vidonda vya tumbo, kuumwa na kichwa, kukosa usingizi, mshuko wa moyo, na wasiwasi. Kufadhaika kwa muda mrefu chini ya hali hizo huchosha.”

      Katika ulimwengu wa leo ni jambo la kawaida kuishi kwa woga. Je, tutawahi kuishi katika ulimwengu ambao watu wataishi bila woga?

      [Maelezo ya Chini]

      a Majina fulani yamebadilishwa.

  • Kwa Nini Watu Wengi Sana Huishi kwa Woga?
    Amkeni!—2005 | Agosti 8
    • Kwa Nini Watu Wengi Sana Huishi kwa Woga?

      WANADAMU wanakumbwa na woga mwingi. Woga ni hisia isiyoweza kuonekana ambayo humpata kila mtu, ingawa mara nyingi haitambuliwi. Hali hiyo imesababishwa na nini? Ni nini huwafanya watu fulani waogope wanapotoka nyumbani? Kwa nini watu wengi hawajihisi wakiwa salama kazini? Kwa nini watu wengi huwa na wasiwasi kuhusu usalama wa watoto wao? Ni hatari gani huwafanya watu wawe na woga wakiwa ndani ya nyumba zao?

      Bila shaka, kuna sababu nyingi ambazo huwafanya watu wawe na woga lakini tutazungumzia hatari nne zinazoweza kuwapata watu daima, yaani, jeuri katika majiji, kusumbuliwa kingono, kulalwa kinguvu, na jeuri nyumbani. Kwanza na tuchunguze jeuri katika majiji. Habari hiyo inafaa sasa kwa sababu karibu nusu ya watu ulimwenguni huishi katika majiji.

      Hatari Katika Majiji

      Huenda ikawa majiji ya kwanza yalijengwa kwa ajili ya ulinzi, lakini watu wengi leo huona majiji kuwa maeneo hatari. Mahali ambapo wakati mmoja palionwa kuwa penye ulinzi sasa panaogopesha. Majiji yenye watu wengi ni mahali panapopendwa na majambazi, na katika majiji fulani, maeneo ya maskini yaliyo na taa chache barabarani na polisi wachache ni hatari.

      Nyakati nyingine, watu huwa na sababu nzuri ya kuogopa kwani watu wengi sana hufa kikatili. Kulingana na ripoti moja ya Shirika la Afya Ulimwenguni, kila mwaka, watu milioni 1.6 huuawa kikatili ulimwenguni pote. Barani Afrika, kati ya kila watu 100,000, wastani wa watu 60.9 huuawa kikatili kila mwaka.

      Watu, maeneo, na mashirika mengi yaliyoonwa kuwa mahali salama sasa yanaonwa kuwa tisho kwa usalama. Kwa mfano, viwanja vingi vya michezo, shule, na maduka sasa yanaonwa kuwa maeneo yenye uhalifu mwingi sana. Katika visa fulani, viongozi wa kidini, wafanyakazi wa jamii, na walimu, ambao wanapaswa kuandaa ulinzi, wamewakatisha watu tamaa. Ripoti kwamba baadhi ya watu hao huwatendea vibaya watoto huwafanya wazazi wasite kuwaacha watoto wao chini ya ulinzi wa wengine. Polisi wanapaswa kuwalinda watu, lakini katika majiji fulani ni jambo la kawaida kwa polisi kuwa wafisadi na kutumia mamlaka vibaya. Kuhusu walinda “usalama,” katika nchi fulani bado watu hukumbuka vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo wapendwa wao walitoweka baada ya kuchukuliwa na wanajeshi. Kwa hiyo, katika sehemu mbalimbali za ulimwengu, badala ya kupunguza woga, polisi na wanajeshi wamefanya watu wawe na woga mwingi hata zaidi.

      Kitabu Citizens of Fear—Urban Violence in Latin America kinasema: “Wakazi wa majiji makuu ya Amerika Kusini huishi kwa woga daima, chini ya hali hatari zaidi duniani. Katika eneo hilo kubwa, watu wapatao 140,000 hufa kikatili kila mwaka, na raia mmoja kati ya watatu ameathiriwa na jeuri moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja.” Pia katika sehemu nyingine za dunia, maandamano ya kisiasa hutukia mara nyingi katika miji mikuu. Maandamano hayo yanapokuwa na jeuri, watu wengi hutumia nafasi hiyo kupora vitu madukani, huku ghasia zikizuka. Wanaofanya biashara jijini wanaweza kujipata katikati ya umati wenye hasira.

      Katika nchi nyingi, kumekuwa na pengo kubwa kati ya hali ya maisha ya matajiri na maskini na hilo limetokeza chuki isiyo ya wazi. Vikundi vikubwa vya watu wenye vurugu ambao huhisi wamenyimwa mahitaji ya msingi wamepora maeneo ambako matajiri huishi. Hilo bado halijatendeka katika majiji fulani, lakini inaonekana kwamba hali hiyo italipuka, ni kwamba tu hakuna ajuaye ni lini.

      Huenda tisho la wezi na mapinduzi likaogopesha watu, lakini kuna mambo mengine yanayosababisha wasiwasi na hivyo kuzidisha hali ya woga.

      Woga Unaosababishwa na Kusumbuliwa Kingono

      Kila siku, mamilioni ya wanawake huogopa sana kupigiwa mbinja, kufanyiwa ishara za matusi, na kutazamwa kwa njia ya kimahaba. Gazeti Asia Week linasema: “Uchunguzi unaonyesha kwamba mwanamke mmoja Mjapani kati ya wanne ametendewa vibaya kingono hadharani, huku asilimia 90 ya visa hivyo vikitokea katika magari ya moshi. . . . Asilimia 2 tu ya waathiriwa ndio huchukua hatua wanapotendewa hivyo. Wengi walisema kuwa hawakuchukua hatua yoyote kwa sababu ya kuwaogopa watu waliowatendea vibaya.”

      Kusumbuliwa kingono kumeongezeka sana nchini India. Mwandishi mmoja wa habari nchini humo anasema kwamba “kila mara mwanamke anapotoka nje ya nyumba yake yeye huogopa. Kila anapopiga hatua yeye huaibishwa na kutukanwa.” Ripoti moja kutoka jiji fulani la India ambako wakaaji hujivunia kuwa na barabara salama kwa kadiri inasema: “[Jiji hili] halina tatizo barabarani bali ofisini. . . . Asilimia 35 ya wanawake waliohojiwa walidai kwamba walisumbuliwa kingono kazini. . . . Asilimia 52 ya wanawake walisema kwamba kwa sababu ya kusumbuliwa kingono kazini wao hupendelea kufanya kazi za mishahara midogo . . . mahali ambapo watashughulika [tu] na wanawake.”

      Woga wa Kulalwa Kinguvu

      Kuna jambo ambalo huwaogopesha wanawake zaidi kuliko kupoteza heshima yao. Nyakati nyingine, kusumbuliwa kingono ni kama kutishwa kulalwa kinguvu. Inaeleweka kwa nini wanawake wengi huogopa kulalwa kinguvu kuliko kuuawa. Huenda mwanamke akajipata akiwa peke yake mahali ambapo anaogopa kuwa anaweza kulalwa kinguvu. Huenda akamwona mwanamume asiyemjua au asiyemwamini. Moyo wake unapiga haraka-haraka huku akiwa na wasiwasi anapojaribu kuchanganua hali hiyo. ‘Atafanya nini? Nitakimbia wapi? Je, nipige mayowe?’ Visa kama hivyo vinapotukia mara nyingi, hudhoofisha afya ya mwanamke pole kwa pole. Watu wengi huamua kutoishi mijini au kutotembea mijini kwa sababu ya kuogopa mambo kama hayo.

      Kitabu The Female Fear kinasema: “Wanawake wengi wanaoishi mijini hukabiliana na woga, wasiwasi, na kuteseka kila siku. Woga wa kulalwa kinguvu huwafanya wanawake wahisi kwamba wanapaswa kujilinda daima wasishambuliwe, kuwa macho na chonjo, jambo ambalo hufanya mwanamke awe na wasiwasi mtu fulani anapotembea nyuma yake, hasa usiku. Hiyo ni . . . hisia ambayo wanawake huwa nayo daima.”

      Wanawake wengi huathiriwa na uhalifu wenye jeuri. Hata hivyo, karibu wanawake wote huathiriwa na woga wa jeuri. Kichapo cha Umoja wa Mataifa, The State of World Population 2000, kinasema: “Ulimwenguni pote, angalau mwanamke mmoja kati ya watatu amewahi kupigwa, kulazimishwa kufanya ngono, au kutendewa vibaya kwa njia nyingine, mara nyingi na mtu anayemjua.” Je, woga huo mwingi umeenea sehemu nyingine? Ni jambo la kawaida kadiri gani kwa watu kuishi kwa woga ndani ya nyumba zao wenyewe?

      Kuogopa Jeuri Nyumbani

      Kupiga wake kisiri ili kuwafanya watii ni ukosefu mkubwa wa haki unaotendeka ulimwenguni pote, na hivi karibuni tu ndipo jambo hilo limeonwa kuwa uvunjaji wa sheria katika sehemu nyingi. Huko India, ripoti moja ilidai kwamba “angalau asilimia 45 ya wanawake Wahindi huzabwa makofi, hupigwa mateke au kuchapwa na waume zao.” Kutendewa vibaya na mwenzi ni jambo linalosababisha tatizo baya sana la afya ulimwenguni. Shirika la Upelelezi la Marekani linaripoti kwamba wanawake walio kati ya umri wa miaka 15 na 44 nchini humo hujeruhiwa kupitia jeuri ya nyumbani kuliko jumla ya majeraha wanayopata kutokana na aksidenti za magari, kuvamiwa na majambazi, na kulalwa kinguvu. Kwa hiyo, jeuri ya nyumbani ni hatari zaidi kuliko ugomvi wa kawaida ambao huishia kwa kuchapana makofi. Wanawake wengi huishi kwa woga wa kujeruhiwa au kuuawa wakiwa nyumbani. Uchunguzi wa kitaifa uliofanywa nchini Kanada ulionyesha kwamba wakati mmoja, thuluthi ya wanawake waliojeruhiwa nyumbani waliogopa kwamba wangeuawa. Nchini Marekani, watafiti wawili walikata kauli hivi: “Nyumbani ndipo mahali hatari zaidi kwa wanawake na mara nyingi wao hutendewa kwa ukatili na kuteswa wakiwa huko.”

      Kwa nini wanawake wengi hushindwa kuvunja mahusiano hayo hatari? Watu wengi hujiuliza: ‘Kwa nini hawatafuti msaada? Kwa nini wasiondoke?’ Mara nyingi woga ndio huwazuia. Imesemekana kwamba woga ndio hasa huendeleza jeuri ya nyumbani. Kwa kawaida, wanaume ambao huwatendea vibaya wake zao hutumia jeuri kuwadhibiti kisha kuwanyamazisha kwa kuwatisha kwamba watawaua. Hata kama mwanamke anayepigwa atakuwa na ujasiri wa kutafuta msaada, huenda asisaidiwe. Hata watu wanaochukia jeuri za aina nyingine huelekea kupunguza uzito, kupuuza, au kutetea jeuri inayosababishwa na waume. Pia, huenda mume ambaye humtendea mke wake vibaya, akaonwa na watu wengine kuwa mtu mwenye kupendeza. Mara nyingi, marafiki hawawezi kuamini kwamba yeye humpiga mke wake. Wanawake wengi ambao hutendewa vibaya huhisi kwamba hawana la kufanya ila kuishi kwa woga daima kwa kuwa watu hawawaamini nao hawana mahali pa kutorokea.

      Nyakati nyingine, wanawake ambao huamua kuondoka hukabili usumbufu mwingine, yaani, kunyemelewa. Uchunguzi wa hivi karibuni uliofanyiwa wanawake zaidi ya elfu moja katika jimbo la Louisiana, huko Amerika Kaskazini ulionyesha kwamba asilimia 15 ya wanawake hao waliripoti kwamba walinyemelewa. Unaweza kuwazia woga waliokuwa nao. Mtu ambaye amekutisha anaendelea kukunyemelea kila mahali unapoenda. Anakupigia simu, anakufuata, anakutazama, na kukungojea. Huenda hata akamuua mnyama wako kipenzi. Ameazimia kukuogopesha!

      Huenda hujapatwa na woga wa aina hiyo. Lakini woga huathiri utendaji wako wa kila siku kwa kadiri gani?

      Je, Woga Huathiri Utendaji Wako?

      Kwa kuwa tunaishi kwa woga, huenda tusitambue jinsi ambavyo woga huathiri maamuzi tunayofanya kila siku. Woga huathiri utendaji wako mara nyingi kadiri gani?

      Je, wewe au washiriki wa familia yako huogopa kurudi nyumbani mkiwa peke yenu usiku kwa sababu ya kuogopa jeuri? Je, wewe huogopa kutumia usafiri wa umma? Je, hatari za kusafiri zimefanya uchague kazi utakayofanya? Au je, kuwaogopa wafanyakazi wenzako au watu wengine ambao lazima ushughulike nao kumeathiri uchaguzi wako wa kazi? Je, woga umeathiri uhusiano wako na wengine au tafrija unazofurahia? Labda woga wa kukutana na walevi na watu wenye fujo umekuzuia kwenda kutazama michezo na maonyesho fulani? Je, woga umeathiri mambo unayofanya shuleni? Kwa sababu ya wazazi wengi kuogopa kwamba watoto wao watakuwa wahalifu, wao huchagua shule watakazowapeleka, na woga huo pia hufanya wazazi wengi kwenda kuwachukua watoto wao shuleni kwa gari ingawa wangeweza kutembea au kutumia usafiri wa umma kurudi nyumbani.

      Kwa kweli wanadamu wanaishi kwa woga mwingi. Lakini wanadamu wameogopa jeuri kwa muda mrefu. Je, kweli tunaweza kutarajia mabadiliko? Je, kuishi bila woga ni ndoto tu? Au je, kuna sababu nzuri ya kutarajia kwamba wakati ujao watu wataishi bila kuogopa chochote?

  • Je, Inawezekana Kuishi Bila Woga?
    Amkeni!—2005 | Agosti 8
    • Je, Inawezekana Kuishi Bila Woga?

      JE, MTU anayeishi katika ulimwengu huu hatari anaweza kuishi bila woga kabisa? Huenda isiwezekane. Hata watu wanaomwamini Mungu hukabili hatari zinazowafanya wawe na wasiwasi. Kwa mfano, katika karne ya kwanza W.K. mtume Paulo aliyesafiri kwa mapana na marefu alitaja kwamba alivunjikiwa na meli, akapata hatari kutokana na mito, hatari kutoka kwa wanyang’anyi wa njia kuu, na hatari ndani ya jiji. (2 Wakorintho 11:25-28) Vivyo hivyo leo, wengi wetu hulazimika kukabiliana na hali hatari.

      Hata hivyo, tunaweza kuchukua hatua za kujilinda na kwa kupunguza hatari, huenda tukapunguza wasiwasi. Biblia inasema: “Mtu mwerevu ni yule ambaye ameona msiba na kujificha, lakini wasio na uzoefu wameendelea mbele nao lazima waumie.” (Methali 22:3) Tunaweza kuchukua hatua zipi zinazofaa?

      Kuchukua Hatua za Kujilinda

      Inapendeza kwamba ingawa Biblia iliandikwa zamani sana, ina kanuni nyingi ambazo bado zinaweza kutumiwa ili kuepuka hatari leo. Kwa mfano, inasema: “Mtu yeyote mwenye hekima, macho yake yamo katika kichwa chake; lakini mjinga anaendelea kutembea katika giza tupu.” (Mhubiri 2:14) Ni jambo la hekima kujua ni nani aliye karibu nawe na kuepuka mahali penye giza iwezekanapo. Huenda ukatumia barabara zilizo na nuru ya kutosha unaporudi nyumbani, hata ikiwa itamaanisha kutembea umbali mrefu kidogo. Pia Biblia inasema: “Wawili ni afadhali kuliko mmoja . . . Mtu akiweza kumshinda nguvu mmoja aliye peke yake, wawili wakiwa pamoja wataweza kusimama dhidi yake.” (Mhubiri 4:9, 12) Ikiwa unaishi eneo hatari, je, unaweza kupanga urudi nyumbani pamoja na mtu mwingine?

      Ukishambuliwa na jambazi, ni jambo la hekima kukumbuka kwamba uhai ni wenye thamani zaidi kuliko mali. (Mathayo 16:26) Pia ni jambo la hekima kukumbuka kwamba umati wenye hasira unapokusanyika, ni hatari na unaweza kufanya jambo lolote.—Kutoka 23:2.

      Ukisumbuliwa na mtu fulani anayejaribu kukutongoza, kukuambia mizaha michafu, au kukugusa kwa njia isiyofaa, ni vizuri kumkataza kwa uthabiti. Huenda ikakubidi kuondoka kama Yosefu alivyofanya wakati mwanamke fulani asiye na maadili alipomshika. ‘Alikimbia na kwenda nje.’ (Mwanzo 39:12) Ikiwa huwezi kuondoka, unaweza kusema: “Acha kufanya hivyo!” au “Usiniguse!” au “Sifurahishwi na maneno hayo.” Ukiweza, epuka maeneo ambako watu husumbuliwa kwa ukawaida.

      Kukabiliana na Woga Nyumbani

      Unaweza kufanya nini ikiwa unamwogopa mume mjeuri? Ni vizuri kufikiria jinsi unavyoweza kutoroka iwapo mwenendo wa mume wako utahatarisha afya au uhai wako au wa watoto wako.a Biblia inasimulia jinsi Yakobo alivyopanga kwa uangalifu namna ambavyo angetoroka ikiwa ndugu yake Esau angekuwa mjeuri. Kama ilivyotukia, hakuhitaji kufanya hivyo, lakini lilikuwa jambo la hekima kufanya mpango huo. (Mwanzo 32:6-8) Njia ya kutorokea inaweza kutia ndani kutafuta mtu unayeweza kukimbilia kwake hali ya dharura inapotokea. Unaweza kuzungumza na mtu huyo mapema kuhusu mahitaji yako. Huenda ikafaa kuweka hati na vitu vingine muhimu mahali unapoweza kuvipata kwa urahisi.

      Pia huenda ukamripoti mume wako anayekutendea vibaya kwa wenye mamlaka na kutafuta ulinzi wao.b Biblia inafundisha kwamba lazima kila mtu akabiliane na matokeo ya matendo yake. (Wagalatia 6:7) Biblia husema hivi kuhusu mamlaka za serikali: “Hiyo ni mhudumu wa Mungu kwako kwa faida yako. Lakini ikiwa unafanya mabaya, ogopa.” (Waroma 13:4) Kupigwa nyumbani ni uhalifu mbaya kama tu kupigwa barabarani. Pia katika nchi nyingi ni kosa kunyemelea watu.

      Kuchukua hatua ambazo tumezungumzia kunaweza kupunguza woga kwa kiasi fulani. Lakini Biblia haitoi tu mashauri yanayofaa. Ni kitabu chenye unabii unaotegemeka ambacho hufunua yale ambayo Mungu anafanya sasa na atakayofanya wakati ujao. Biblia inatoa tumaini gani kwa watu ambao hulazimika kuishi kwa woga?

      Woga Mwingi Uliopo Unaonyesha Nini?

      Mtume Paulo aliandika maneno haya muhimu: “Katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo. Kwa maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, . . . wasio na upendo wa asili, wasiotaka makubaliano yoyote, wachongezi, wasiojizuia, wakali, wasiopenda wema.” (2 Timotheo 3:1-3) Bila shaka maneno hayo yanataja nyakati zenye kuogopesha sana!

      Yesu alipozungumzia “umalizio wa mfumo wa mambo,” alisema hivi: “Taifa litasimama kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; na kutakuwa na matetemeko makubwa ya nchi, na katika mahali pamoja baada ya pengine kutakuwa na tauni na upungufu wa chakula; kutakuwa na mambo yenye kuogopesha na ishara kubwa kutoka mbinguni.” (Mathayo 24:3, 7, 8; Luka 21:10, 11) Kwa hiyo, hatupaswi kushangazwa na “mambo yenye kuogopesha” ambayo tumeona na ambayo yamechangia woga mwingi leo. Lakini yanamaanisha nini?

      Yesu alisema: “Mnapoona mambo hayo yakitukia, jueni kwamba ufalme wa Mungu uko karibu.” (Luka 21:31) Katika siku zetu, tunaweza kutazamia serikali ya Mungu itawale kutoka mbinguni juu ya wanadamu wote. (Danieli 2:44) Maisha yatakuwaje wakati huo?

      Kuishi Bila Woga!

      Biblia inaeleza kuhusu wakati ujao ambapo vita vitakwisha, hakutakuwa na watenda maovu, nayo dunia itajaa watu wanaompenda Mungu. Petro, mtume wa Yesu, aliandika kuhusu “siku ya hukumu na ya kuangamizwa kwa watu wasiomwogopa Mungu” itakayokuja wakati ujao. Hakutakuwa na mtu yeyote mwovu wa kuogopwa kwani “uadilifu utakaa” duniani. (2 Petro 3:7, 9, 13) Hebu wazia kitulizo tutakachopata kuishi miongoni mwa watu wanaotumainiana na kupendana kikweli! Tumaini hilo hutusaidia tuwe na maoni yanayofaa kuhusu nyakati hizi hatari. Hazitaendelea kuwapo milele.—Zaburi 37:9-11.

      Nabii wa Yehova aliambiwa hivi kwa faida ya wale wanaohangaika: “Waambieni wale wanaohangaika moyoni: ‘Iweni na nguvu. Msiogope. Tazameni! Mungu wenu atakuja na kisasi, Mungu akiwa na malipo. Yeye mwenyewe atakuja na kuwaokoa ninyi.’” (Isaya 35:4) Kwa hiyo, watumishi wa Mungu wa kweli wanaweza kutazamia wakati ujao wakiwa na uhakika. (Wafilipi 4:6, 7) Watu ambao wamelazimika kuishi kwa woga, wanafarijika sana kujua kwamba Yehova hajabadili kusudi lake la awali kwamba dunia ijawe na watu wanaomjua na wanaoonyesha sifa zake zenye upendo.—Mwanzo 1:26-28; Isaya 11:9.

      Tunajua kwamba hakuna jambo linaloweza kumzuia Yehova asitimize makusudi yake yenye upendo kwa ajili ya wanadamu. (Isaya 55:10, 11; Waroma 8:35-39) Tunapoelewa hilo, maneno ya Zaburi inayojulikana sana huwa na maana ya pekee. Tunasoma hivi: “Yehova ni Mchungaji wangu. . . . Anaiburudisha nafsi yangu. Ananiongoza katika mapito ya uadilifu kwa ajili ya jina lake. Hata ingawa ninatembea katika bonde lenye kivuli kizito, siogopi chochote kibaya, kwa maana wewe uko pamoja nami.” (Zaburi 23:1-4) Ingawa huenda nyakati zenye kuogopesha zikawa mbaya sana, kwa hakika hivi karibuni kutakuwa na ulimwengu usio na woga.

      [Maelezo ya Chini]

      a Kuhusu hali zinazopatana na kanuni za Biblia ambazo zinaweza kumfanya mtu atengane na mwenzi wake wa ndoa, ona gazeti la Amkeni!, Februari 8, 2002, ukurasa wa 10.

      b Kuhusu watu waliopatwa na jeuri nyumbani, ona gazeti la Amkeni!, Novemba 8, 2001, ukurasa wa 3 hadi 12, na Amkeni!, Februari 8, 1993, ukurasa wa 3 hadi 14.

      [Picha katika ukurasa wa 8-10]

      Hivi karibuni, Mungu ataleta ulimwengu usiokuwa na woga

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki