Surströmming—Mlo Mtamu Wenye Uvundo
Na Mleta-habari Wa Amkeni! Katika Sweden
Katika karne ya 16, vita baina ya Sweden na jiji la Lübeck, Ujerumani, ilikuwa imepamba moto. Kwa kuwa Lübeck lilimiliki bahari, bidhaa za kutoka nje hazikupatikana kwa urahisi na chumvi ikawa haba. Kulikuwa na kiasi kidogo sana cha chumvi ya kuhifadhia samaki aina ya heringi, ambao walikuwa chakula kikuu kaskazini mwa Sweden. Ili kupunguza matumizi ya chumvi, mtu fulani aliweka chumvi kidogo sana katika pipa lenye heringi. Chumvi hiyo haikutosha samaki hao kwa hiyo wakaanza kunuka. “Wameoza” ndivyo wengi walivyosema.
KATIKA hali za kawaida samaki hao wangetupwa, lakini wengi hawakuwa na jambo la kufanya kwa sababu ya njaa kuu iliyowakumba, kwa hiyo wakala samaki hao. Kila mtu alishangaa kwamba ladha ya mlo huo haikuwa ya samaki waliooza; hata wengine waliiona ladha yake chungu kidogo kuwa ya kupendeza. Samaki hao hawakuwa wameoza bali walikuwa wamechachuka. Uvumi ulienea juu ya mlo huu wa pekee, na kwa kuwa chumvi ilikuwa ghali hata wakati kulipokuwa na amani, kuchachusha kukawa njia ya kawaida ya kuhifadhi heringi miongoni mwa watu maskini kaskazini mwa Sweden, ambako haikuwa rahisi kupata vyakula vya karibuni.
Kulingana na hekaya, hivyo ndivyo mlo wenye kupendwa na wengi ulivyobuniwa. Tangu wakati huo watu wa Sweden wameupenda sana mlo huu wa pekee ambao wamerithi. Si kila mtu anayeamini hekaya hii. Wasomi fulani hudai kwamba kuchachusha kulitumiwa kuhifadhi samaki katika Sweden na katika sehemu nyinginezo katika Kizio cha Kaskazini kabla ya karne ya 16.
Wajulikana kwa Harufu Yake
Bila kujali asili yake, surströmming hujulikana sana kwa sababu ya uvundo wake. Mwishoni mwa karne ya 19, mtungaji mmoja wa kitabu cha mapishi aliandika hivi kwa kukejeli: “Kwa watu hawa [wapenzi wa chakula hicho], mlo huo ni mtamu usio na kifani; lakini hauandaliwi kamwe kwenye karamu isipokuwa mkaribishaji awe anataka kula peke yake au labda awe anakaribisha wageni wasio na uwezo wa kunusa.” Leo imethibitishwa kuwa alikosea. Licha ya harufu yake, surströmming huandaliwa katika karamu nao huonwa kuwa mlo mtamu sana. Watu hawali tena mlo huu kwa ukawaida wakati wa jioni au wa mchana. Marafiki hualikwa kwenye mlo wa surströmming katika vikusanyiko. Unapendwa sana kila mahali Sweden, hata ingawa sehemu iliyo maarufu sana kwa mlo huu bado ni sehemu ya pwani ya kaskazini-mashariki inayoitwa High Coast.
Mlo huu ungali wa pekee sana kwa Wasweden. Ni watu wachache sana nje ya Sweden ambao wanajua au wameonja surströmming. Wageni wanaoalikwa wasiokuwa na habari juu ya “mlo huu mtamu” kwa kawaida hupigwa na bumbuazi angalau kwa sababu mbili. Kwanza wao hushtuka wakati kopo linapofunuliwa na uvundo kuanza kuenea. Basi wao hufikia mkataa wa kwamba mlo huo umeoza na kwamba bila shaka mwenyeji wao atautupa na kuwaandalia mlo tofauti. Ndipo wapigwapo na bumbuazi hata zaidi—wakati mwenyeji pamoja na wageni wale wengine wanapoanza kihalisi kula samaki hao wenye uvundo, huku wakionekana kufurahia mno! Wageni fulani wenye ujasiri wamejifunza kufurahia surströmming; wengine bado. Aliyekuwa mpishi maarufu Keith Floyd alisema hivi alipoona surströmming kwa mara ya kwanza na labda ndiyo mara ya mwisho: “Kitu chenye kuchukiza sana isivyoelezeka.” Floyd amewahi kula viwavi katika Afrika, mbilimbibahari huko China, na fira huko Vietnam, pamoja na vitu vinginevyo. Lakini hangeweza kustahimili surströmming. Yeye alisema hivi: “Mara nyingi watu huniuliza kitu chenye kuchukiza zaidi ambacho nimewahi kula. Sasa ninajua jibu.” Jaribio la kupelekea Wamarekani mlo huo katika miaka ya 1930 halikufua dafu wakati maofisa wa forodha huko New York walipofunua kopo na kudhani kwamba walikuwa wameshambuliwa kwa gesi ya sumu. Wakatangaza kwamba chakula hicho “hakifai kuliwa.”
Hata Wasweden wana maoni mbalimbali juu ya mlo huo. Mlo huo haumwachi mtu yeyote bila uchaguzi. Ama unaupenda, au unauchukia kabisa. Tabibu mmoja katika makao ya Malkia Christina katikati ya karne ya 17, Anders Sparman, aliandika kwamba surströmming ulinuka kama kinyesi kilichobwagwa karibuni. Kwa upande mwingine, mwanabotania mashuhuri wa Sweden wa karne ya 18 Carolus Linnaeus, alisifu sana mlo huo hata akaandika maelezo muhimu sana ya upishi katika vitabu vyake. Mara nyingi Wasweden walio katika nchi za kigeni husema kwamba surströmming ni mojawapo ya vitu wanavyotamani sana.
Kitabu Längs Höga Kusten husema kwamba majaribio yenye kufanikiwa ya kuondoa harufu yake yamefanywa bila faida yoyote kiuchumi. Wataalamu wa ladha za vyakula hukazia sana kwamba surströmming haupendezi bila harufu yake.
Unatayarishwaje?
Kuna njia nyingi za kula surströmming. Wale wanaoupenda sana hula tu bila kuongezea kitu kingine, moja kwa moja kutoka kwenye kopo. Watu fulani hata wameonekana wakila mlo huo pamoja na lingonberries na maziwa! Lakini kwa kawaida huliwa kwenye mkate wenye siagi, vitunguu vilivyokatwakatwa vizuri, nyanya, na viazi, na kisha wengi hupenda kunywa pia bia baridi. Maandalizi haya yamewafanya watu wengi waliochukia surströmming wawe wapenzi wake.
Samaki wa heringi huvuliwa mnamo Aprili kabla ya kutaga mayai. Kichwa na utumbo wake huondolewa, lakini mayai huachwa ili yaongeze ladha. Kidole tumbo huachwa pia, kwa kuwa kina vimengenya muhimu kwa uchachushaji. Kwa siku chache, heringi hutiwa kwenye mapipa yenye maji yaliyokolea chumvi, ambayo huondoa damu na mafuta. Kisha samaki hawa hutiwa katika mapipa yaliyo na maji yenye chumvi ya wastani ili wakomae na kuchacha kwa muda wa karibu miezi miwili. Mnamo Julai samaki hawa hutiwa kwenye makopo na kugandishwa. Ubora wa samaki hawa hutegemea kukolea kwa maji ya chumvi na joto ambamo mapipa huwekwa. Kila mtayarishaji ana siri yake ambayo huificha sana.
Uchachushaji huendelea hata baada ya samaki kutiwa kwenye kopo. Kwa hiyo, kujaribu kufunua kopo bila tahadhari yaelekea kutatokeza kituko kisichopendeza. Huenda ule msongo mkubwa ukarusha mchuzi kila mahali. Ili kuepuka jambo hili, kopo lapasa kufunuliwa nje ya nyumba au majini!
Kwa muda mrefu, kulikuwa na agizo la mfalme lililotaarifu kwamba makopo ya kwanza ya mwaka ya surströmming hayangeuzwa madukani kabla ya Alhamisi ya tatu ya mwezi wa Agosti kila mwaka. Hata hivyo, katika majira ya kupukutika ya mwaka wa 1998, agizo hili liliondolewa, na sasa surströmming waweza kuuzwa wakati wowote mwakani. Lakini yaonekana kwamba kufuatia madai ya wengi, Alhamisi ya tatu ya Agosti itaendelea kuwa mojawapo ya siku zinazopendwa sana katika mwaka na wakazi wa High Coast na wapenzi wengine wa surströmming.
[Picha katika ukurasa wa 26]
Mlo wa “surströmming” huandaliwa kwa mkate wa Sweden, viazi, vitunguu, na jibini, nao waweza kushawishi hata mtu anayeuchukia sana ajaribu kuuonja
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]
Samaki kwenye ukurasa wa 25-26: Animals/Jim Harter/Dover Publications, Inc.