Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Jamii Mbalimbali—Hutegemeza Uhai
    Amkeni!—2001 | Septemba 22
    • Harakati za Kubadili Maumbile ya Mimea

      Uchunguzi wa chembe za urithi umetokeza taaluma mpya inayoitwa biotekinolojia. Kama jina hilo linavyodokeza, taaluma hiyo huchanganya biolojia na tekinolojia ya kisasa kupitia mbinu kama vile kubadili chembe za urithi za vitu vilivyo hai (genetic engineering). Baadhi ya yale yanayoitwa makampuni mapya ya biotekinolojia, hukazia mno kilimo na yanajitahidi sana kupata idhini maalumu ya kutokeza mbegu zinazozaa sana, zinazokinza magonjwa, ukame, baridi kali, na zinazopunguza matumizi ya kemikali hatari. Ingenufaisha sana kama miradi hiyo ingeweza kutimizwa. Lakini watu fulani wana wasiwasi kuhusu mazao yaliyobadilishwa maumbile.

      Kitabu Genetic Engineering, Food, and Our Environment chasema kwamba “mbinu ya kutokeza mimea ya jamii mbalimbali ina mipaka ya kiasili.” “Ua la waridi laweza kuchavushwa na ua jingine la waridi, lakini ua la waridi haliwezi kamwe kuchavushwa na kiazi. . . . Kwa upande mwingine, kubadili maumbile kwa kawaida huhusisha kuchukua chembe za urithi za jamii moja na kuzitia katika jamii nyingine kwa madhumuni ya kutokeza tabia fulani za pekee. Kwa mfano, huenda hilo likamaanisha kuchukua chembe ya urithi kutoka kwa samaki wa aktiki ambayo inaweza kutokeza kemikali isiyoganda, na kuitia katika kiazi ama stroberi ili ziweze kustahimili baridi kali. Sasa mimea inaweza kutiwa chembe za bakteria, virusi, wadudu, wanyama au hata za wanadamu.”a Hivyo basi, biotekinolojia inawaruhusu wanadamu kuvuka mipaka ya kiasili inayobainisha chembe za urithi za jamii mbalimbali.

      Sawa na harakati za kuboresha uzalishaji, zile zinazoitwa na watu fulani harakati za kubadili maumbile hutokeza chembe za urithi za aina moja tu—watu wengine wanasema hali hiyo ni mbaya hata zaidi kwa sababu wataalamu wa chembe za urithi wanaweza kutokeza kiumbe kwa chembe bila kujamiiana au kupitia ukuzaji wa tishu. Mbinu hizo hutokeza viumbe wanaofanana kabisa au viumbe pacha. Kwa hiyo, wengi wangali wanahangaishwa na kudidimia kwa ukuzaji wa aina mbalimbali za mimea. Hata hivyo, mimea iliyobadilishwa maumbile imezusha masuala mapya, kama vile athari za mimea hiyo kwa wanadamu na mazingira. “Tunaingia hima-hima bila kufikiri katika muhula mpya wa biotekinolojia ya kilimo tukiwa na matumaini makubwa, bila kujizuia sana, na bila kujua matokeo yake,” akasema mwandishi wa sayansi Jeremy Rifkin.b

      Kwa upande mwingine, kuweza kubadilisha maumbile ya chembe za urithi ni hatua inayoweza kunufaisha sana. Hivyo basi, makampuni yanashindana kupata idhini maalumu ya kutokeza mbegu mpya na mimea mingine iliyobadilishwa maumbile.

  • Jamii Mbalimbali—Hutegemeza Uhai
    Amkeni!—2001 | Septemba 22
    • a Bado kuna ubishi mkali kuhusu jinsi vyakula vilivyobadilishwa maumbile vinavyoweza kuathiri mazingira, afya ya wanadamu na ya wanyama. Kuchanganya chembe za urithi za viumbe wa jamii tofauti kabisa kumewafanya wengine watilie shaka uhalali wa jambo hilo.—Ona Amkeni!, Aprili 22, 2000, ukurasa wa 25-27.

      b Gazeti la New Scientist laripoti kwamba viazi-sukari vya Ulaya “vilivyobadilishwa maumbile ili vikinze dawa moja ya kuua magugu, vimekuwa na chembe zisizotarajiwa za kukinza dawa nyingine.” Chembe hizo za ajabu zilitokea wakati viazi-sukari vilipochavushwa bila mpango na aina nyingine ya kiazi-sukari kilichobadilishwa maumbile ili kikinze dawa tofauti ya kuua magugu. Baadhi ya wanasayansi wanahofu kwamba kuenea kwa mimea ambayo inakinza dawa za kuua magugu kwaweza kutokeza magugu sugu ambayo hayawezi kuangamizwa kwa dawa.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki