Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Unaweza Kuboresha Afya Yako
    Amkeni!—2011 | Machi
    • Unaweza Kuboresha Afya Yako

      RUSTAM, anayeishi Urusi ana maisha yenye shughuli nyingi sana. Zamani alikuwa na mazoea yasiyofaa, lakini akagundua kwamba yanaathiri afya yake. Aliacha kuvuta sigara na kunywa kileo kupita kiasi. Lakini bado alijihisi akiwa mchovu sana baada ya kufanya kazi siku nzima mbele ya kompyuta yake.

      Ingawa Rustam alianza kazi saa mbili asubuhi, alijihisi ni kana kwamba bado hajaamka hadi saa nne asubuhi, na alikuwa mgonjwa mara kwa mara. Kwa sababu hiyo, alifanya mabadiliko katika ratiba yake. Matokeo yakawa nini? Anasema hivi: “Katika muda wa miaka saba iliyopita, sijakosa kazi kwa zaidi ya siku mbili kwa mwaka kwa sababu ya ugonjwa. Ninajihisi nikiwa mzima kabisa—nikiwa macho na makini—na ninafurahia maisha!”

      Ram, mke wake, na watoto wao wawili wanaishi Nepal. Eneo wanaloishi si safi na limejaa mbu na nzi. Zamani, Ram na familia yake waliugua mara kwa mara kutokana na magonjwa ya mfumo wa kupumua na maambukizo ya macho. Wao pia walifanya mabadiliko ambayo yaliboresha sana afya yao.

      Chukua Hatua za Kuboresha Afya Yako!

      Iwe mtu ni tajiri au maskini, watu wengi hawaoni jinsi mazoea yao yanavyoathiri afya yao. Wao huona kwamba wanaweza kuwa na afya nzuri bila jitihada zozote. Maoni hayo yasiyofaa huwafanya watu wengi wasijitahidi kuboresha afya yao na kuishi maisha yenye kuridhisha.

      Kwa kweli, uwe tajiri au maskini, kuna mambo ya msingi unayoweza kufanya ili kulinda na kuboresha afya yako na ya familia yako. Je, kuna faida zozote za kujitahidi kufanya hivyo? Bila shaka! Unaweza kuboresha maisha yako na kuepuka kuyafupisha.

      Kwa maneno na matendo, wazazi wanaweza kuwafundisha watoto wao kuwa na mazoea mazuri, na hilo litawasaidia kuwa na afya nzuri. Hata ikiwa watatumia wakati na pesa kufanya hivyo, faida ni kwamba watapunguza kuteseka, watapunguza wakati unaopotea kutibu ugonjwa, na hawatatumia pesa nyingi kulipia gharama za matibabu. Kuna msemo unaosema, Heri kuzuia kuliko kuponya.

      Katika habari zinazofuata, tutazungumzia njia tano za msingi ambazo zimewasaidia Rustam, Ram, na wengine wengi. Njia hizo zinaweza kukusaidia wewe pia!

      [Picha katika ukurasa wa 3]

      Rustam

      [Picha katika ukurasa wa 3]

      Ram na familia yake wakiteka maji safi ya kunywa

  • Njia ya 1—Kula Vizuri
    Amkeni!—2011 | Machi
    • Njia ya 1—Kula Vizuri

      “Kula chakula. Usile kingi. Kula hasa mboga.” Kwa maneno hayo machache, mwandishi Michael Pollan anaeleza kwa ufupi mazoea ya kula yanayofaa ambayo yametumiwa kwa muda mrefu. Anamaanisha nini?

      ◯ Kula vyakula ambavyo havijatengenezwa viwandani. Kula vyakula “halisi”—vyakula vinavyotolewa moja kwa moja kutoka shambani ambavyo watu wamekuwa wakila kwa miaka mingi—badala ya vyakula vya kisasa vilivyotengenezwa viwandani. Kwa kawaida, vyakula vilivyotengenezwa viwandani na vyakula vyepesi vya mikahawa vina sukari, chumvi, na mafuta mengi, na inadhaniwa kwamba vitu hivyo husababisha magonjwa ya moyo, kiharusi, kansa, na magonjwa mengine hatari. Unapopika, jaribu kuchemsha, kuoka, na kuchoma badala ya kukaanga chakula. Jaribu kutumia vikolezo na viungo ili usitumie chumvi nyingi. Hakikisha kwamba nyama imeiva vizuri, na usile kamwe chakula kilichoharibika.

      ◯ Usile chakula kingi. Shirika la Afya Ulimwenguni linaripoti ongezeko la watu wanene kupita kiasi, tatizo ambalo mara nyingi husababishwa na kula kupita kiasi. Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba katika sehemu fulani za Afrika, “idadi ya watoto walionenepa kupita kiasi ni kubwa kuliko ya wale walio na utapiamlo.” Watoto walionenepa kupita kiasi wamo katika hatari ya kupatwa na matatizo ya afya sasa na wakati ujao, kutia ndani kisukari. Wazazi, wawekeeni watoto wenu mfano mzuri kwa kula kwa kiasi.

      ◯ Kula hasa mboga. Chakula chenye lishe kinatia ndani matunda mbalimbali, mboga, na nafaka isiyokobolewa maganda badala ya nyama na vyakula vyenye wanga. Mara moja au mbili kwa juma, jaribu kula samaki badala ya nyama. Punguza vyakula vilivyotolewa virutubisho kama vile tambi, mkate mweupe, na mchele mweupe. Lakini epuka mazoea hatari ya kula yanayofuatwa na watu ili kupunguza uzito. Wazazi, lindeni afya ya watoto wenu kwa kuwasaidia wawe na mazoea ya kula vyakula vyenye lishe. Kwa mfano, wapeni kokwa na matunda na mboga zilizosafishwa vizuri badala ya viazi vilivyokaangwa au peremende.

      ◯ Kunywa vinywaji vingi. Watu wazima na watoto wanapaswa kunywa maji mengi na vinywaji vingine visivyo na sukari kila siku. Kunywa vinywaji vingi hasa wakati kuna joto jingi na unapofanya kazi ngumu na mazoezi. Vinywaji hivyo husaidia kumeng’enya chakula, kuondoa sumu mwilini, kufanya ngozi iwe laini, na kupunguza uzito. Vinakusaidia kuhisi na kuonekana mwenye afya. Epuka kunywa kileo kupita kiasi na vinywaji vingi vyenye sukari. Soda moja kwa siku inaweza kumfanya mtu aongeze kilo 6.8 kwa mwaka.

      Katika nchi fulani, jitihada kubwa sana inahitajika ili kupata maji safi na ni bei ghali sana. Hata hivyo, ni muhimu kunywa maji. Yanahitaji kuchemshwa au kutiwa dawa. Inasemekana kwamba watu wengi zaidi hufa kwa kunywa maji yaliyo na viini kuliko wale wanaokufa kutokana na vita au matetemeko ya nchi; inaripotiwa kwamba kila siku, watoto 4,000 hufa kutokana na maji machafu. Shirika la Afya Ulimwenguni linapendekeza kwamba watoto wachanga wanyonye maziwa ya mama peke yake kwa miezi sita ya kwanza, kisha wanyonye maziwa ya mama pamoja na vyakula vingine hadi watakapofikia umri wa miaka miwili hivi.

  • Njia ya 2—Tunza Mwili Wako
    Amkeni!—2011 | Machi
    • Njia ya 2—Tunza Mwili Wako

      “Hakuna mtu anayeuchukia mwili wake kwa vyovyote; bali huulisha na kuutunza.” (Waefeso 5:29) Kuchukua hatua rahisi kutunza mwili wako kunaweza kuleta mabadiliko makubwa katika afya yako.

      ◯ Pumzika vya kutosha. “Konzi moja ya pumziko ni afadhali kuliko konzi mbili za kazi ngumu na kufuatilia upepo.” (Mhubiri 4:6) Vikengeusha-fikira na hekaheka za maisha ya sasa zimefanya watu wasiwe na wakati wa kulala. Lakini usingizi ni muhimu ili mtu awe na afya nzuri. Utafiti umeonyesha kwamba tunapolala, mwili na ubongo wetu hujirekebisha, na hivyo kuboresha kumbukumbu na hisia zetu.

      Usingizi huimarisha mfumo wa kinga na kupunguza hatari ya kupatwa na maambukizo, kisukari, ugonjwa wa moyo, kansa, kunenepa kupita kiasi, kushuka moyo, na pengine hata ugonjwa wa Alzheimer. Badala ya kuzuia usingizi kwa kula peremende, kafeini, au vitu vingine, tunapohisi usingizi tunapaswa kulala. Watu wazima wanahitaji kulala kwa kati ya saa saba au nane kila usiku ili wahisi na kuonekana wakiwa na afya na kufanya kazi vizuri. Vijana wanahitaji kulala kwa saa nyingi zaidi. Vijana ambao hawalali vyakutosha wanaweza kupatwa na matatizo ya kiakili na kusinzia wanapoendesha gari.

      Usingizi ni muhimu hasa tunapokuwa wagonjwa. Miili yetu inaweza kushinda magonjwa fulani kama vile mafua tukilala kwa muda mrefu zaidi na kunywa vinywaji vingi.

      ◯ Tunza meno yako. Kupiga mswaki na kutumia uzi mwembamba kuondoa uchafu katikati ya meno kila baada ya kula, na hasa kabla ya kulala, kutazuia meno yasioze, magonjwa ya fizi, na kung’olewa jino. Bila meno hatuwezi kunufaika kabisa na vyakula tunavyokula. Inaripotiwa kwamba tembo hawafi kwa sababu ya uzee bali wao hufa polepole kwa sababu ya njaa kwa kuwa meno yao yanapodhoofika, wao hushindwa kutafuna chakula vizuri. Watoto ambao wamefundishwa kupiga mswaki na kuondoa uchafu katikati ya meno kwa kutumia uzi mwembamba baada ya kula watafurahia afya bora ujanani na maishani.

      ◯ Mwone daktari. Magonjwa fulani huhitaji uchunguzi wa daktari. Kwa kawaida, ugonjwa ukigunduliwa mapema, unaweza kutibiwa kwa urahisi na mtu atatumia pesa kidogo. Kwa hiyo, usipojihisi vizuri, badala ya kujaribu kutibu dalili tu, mwone daktari ili achunguze kisababishi ni nini.

      Kufanyiwa uchunguzi kwa ukawaida na daktari anayeaminika kunaweza kuzuia matatizo mengine hatari, kama vile tu kumwona daktari wakati wa uja-uzito kunaweza kuzuia matatizo baadaye.a Hata hivyo, kumbuka kwamba madaktari hawawezi kufanya miujiza. Ponyo kamili la magonjwa yetu yote litatukia tu wakati Mungu atakapofanya “vitu vyote kuwa vipya.”—Ufunuo 21:4, 5.

      [Maelezo ya Chini]

      a Ona habari “Mama Wenye Afya, Watoto Wenye Afya,” katika toleo la Amkeni! la Novemba (Mwezi wa 11) 2009.

  • Njia ya 3—Fanya Mazoezi
    Amkeni!—2011 | Machi
    • Njia ya 3—Fanya Mazoezi

      “Ikiwa mazoezi yangekuwa dawa, hiyo ingekuwa ndiyo dawa ambayo watu wengi wangependekezewa na madaktari ulimwenguni pote.” (Chuo Kikuu cha Kitiba cha Emory) Kati ya mambo yote tunayoweza kufanya ili kuboresha afya yetu, hakuna lolote lenye manufaa zaidi kuliko mazoezi.

      ◯ Jitahidi. Mazoezi ya mwili yanaweza kufanya uwe na furaha zaidi, uwe na akili makini, uwe na nguvu zaidi, utimize mengi, na upunguze uzito, iwapo pia utakula chakula chenye lishe. Mazoezi hayahitaji kufanywa kupita kiasi au hadi uumie ili unufaike. Kufanya mazoezi kwa kiasi mara kadhaa kwa juma kunaweza kunufaisha sana.

      Mazoezi kama vile, kutembea haraka, kukimbia polepole, kuendesha baiskeli, na michezo mingine inayohitaji utumie nguvu, ambayo itafanya moyo wako upige haraka zaidi na utokwe na jasho, yatafanya uwe mstahimilivu zaidi na kuzuia usipatwe na mshtuko wa moyo na kiharusi. Kufanya mazoezi hayo ya viungo pamoja na mazoezi ya kuinua vyuma hufanya mifupa, misuli ya ndani, na viungo viwe na nguvu. Mazoezi hayo pia hufanya chakula kiyeyuke haraka, na hilo husaidia mtu asinenepe kupita kiasi.

      ◯ Tumia miguu yako. Mazoezi huwanufaisha watu wa umri wote, na hawahitaji kwenda kwenye ukumbi wa kufanyia mazoezi ili wanufaike. Unahitaji tu kutembea badala ya kutumia gari, basi, au lifti. Badala ya kungojea gari mbona usitembee? Huenda hata ukafika mahali unapokwenda haraka zaidi. Wazazi, watieni moyo watoto wenu wacheze michezo inayohusisha mazoezi ya mwili, ikiwezekana nje ya nyumba. Tofauti na michezo inayofanya watoto wakae kitako tu, kama vile michezo ya video, michezo inayohusisha mazoezi ya mwili hufanya miili yao iwe na nguvu na husaidia viungo vyao vifanye kazi kwa upatano.

      Hata uanze kufanya mazoezi ukiwa na umri gani, mazoezi ya kiasi yanaweza kukunufaisha. Ikiwa una umri mkubwa au una matatizo ya afya na hufanyi mazoezi, ni jambo la hekima kutafuta ushauri wa daktari kabla ya kuanza kufanya mazoezi. Lakini aanza haraka iwezekanavyo! Mazoezi yanayofanywa hatua kwa hatua bila kupita kiasi yanaweza kuwasaidia hata wazee kuwa na misuli yenye nguvu na mifupa mizito. Yanaweza pia kuwasaidia wazee wasiwe wakianguka.

      Mazoezi yalimsaidia Rustam, aliyetajwa katika habari ya kwanza ya mfululizo huu. Miaka saba iliyopita, yeye na mke wake walianza kukimbia polepole kila asubuhi, siku tano kwa juma. Anasema hivi: “Mwanzoni, tulitafuta visababu ili tusiende. Lakini kuwa na mwenzi wa kufanya mazoezi kumetusaidia sana. Sasa limekuwa zoea ambalo tunafurahia.”

      [Picha katika ukurasa wa 6]

      Kufanya mazoezi kunaweza kufurahisha

  • Njia ya 4—Linda Afya Yako
    Amkeni!—2011 | Machi
    • Njia ya 4—Linda Afya Yako

      “Mtu mwerevu ni yule ambaye ameona msiba na kujificha.” (Methali 22:3) Kuchukua hatua rahisi za kujilinda kunaweza kukusaidia uepuke magonjwa na kuteseka kwingi, na pia kupoteza wakati na pesa.

      ◯ Dumisha usafi. “Kunawa mikono ndilo jambo moja muhimu unaloweza kufanya ili kuzuia kuenea kwa maambukizo na kuwa na afya na hali njema,” inasema ripoti ya Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa ya Kuambukiza vya Marekani. Asilimia 80 hivi ya maambukizo huenezwa kupitia mikono michafu. Kwa hiyo, nawa mikono mara nyingi iwezekanavyo kila siku. Fanya hivyo hasa kabla ya kutayarisha chakula, au kugusa au kusafisha kidonda, na pia baada ya kumgusa mnyama, kwenda msalani, au kumbadili mtoto nepi.

      Kunawa kwa kutumia sabuni ni bora kuliko kutumia kemikali za kuua viini zilizo na alkoholi. Watoto watakuwa na afya bora ikiwa wazazi watawazoeza kunawa mikono na kutogusa midomo na macho yao kwa mikono. Kuoga kila siku na kuwa na nguo na matandiko safi pia kutachangia kuwa na afya bora.

      ◯ Epuka magonjwa ya kuambukizwa. Epuka kuwa karibu au kutumia vyombo vya kulia vya mtu mwenye mafua au homa. Mate yao na umajimaji unaotoka puani unaweza kukuambukiza magonjwa hayo. Magonjwa yanayoambukizwa kupitia damu kama vile mchochota wa ini aina ya B na C na UKIMWI hupitishwa kupitia ngono, kutumia sindano kujidunga dawa za kulevya, na kutiwa damu mishipani. Chanjo zinaweza kuzuia maambukizo fulani, lakini bado mtu mwenye hekima atachukua hatua zinazofaa za kujilinda anapokuwa karibu na mtu mwenye ugonjwa wa kuambukizwa. Epuka kuumwa na wadudu. Usiketi au kulala nje bila kinga wakati kuna mbu wengi au wadudu wengine wanaoeneza magonjwa. Tumia chandarua cha kuzuia wadudu, hasa kwa ajili ya watoto, na ujipake dawa ya kuzuia wadudu.a

      ◯ Hakikisha nyumba yako ni safi. Jitahidi sana kudumisha nyumba yako ikiwa nadhifu na safi, ndani na nje. Hakikisha kwamba maji hayajikusanyi mahali popote na hivyo kufanya mbu wazaane. Takataka, uchafu, na vyakula ambavyo havijafunikwa huvutia wadudu na wanyama wenye viini ambavyo husababisha magonjwa. Ikiwa hakuna choo, jenga choo cha shimo badala ya kwenda choo shambani. Funika shimo la choo ili kuzuia nzi ambao hupitisha maambukizo ya macho na magonjwa mengine.

      ◯ Epuka kujijeruhi. Fuata sheria za usalama unapofanya kazi, unapoendesha baiskeli, pikipiki, au gari. Hakikisha kwamba gari lako ni salama. Vaa nguo za kujikinga na vifaa vinavyofaa vya kujikinga kama vile miwani, kofia, viatu, na pia mikanda ya usalama na vifaa vya kulinda masikio. Epuka kukaa kwenye jua kwa muda mrefu kwa kuwa hilo husababisha kansa na pia kufanya ngozi ipate makunyazi mapema. Ikiwa wewe huvuta sigara, acha. Kuacha sasa kutapunguza sana hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo, kansa ya mapafu, na kiharusi.b

      [Maelezo ya Chini]

      a Ona makala zenye kichwa, “Magonjwa Yanayoenezwa na Wadudu,” katika toleo la Amkeni! la Mei 22, 2003 (22/5/2003).

      b Ona makala zenye kichwa, “Jinsi ya Kuacha Kuvuta Sigara,” katika toleo la Amkeni! la Mei 2010.

  • Njia ya 5—Jitie Moyo na Uwachochee Watu wa Familia
    Amkeni!—2011 | Machi
    • Njia ya 5—Jitie Moyo na Uwachochee Watu wa Familia

      “Mtu aliye mwerevu atatenda kwa ujuzi.” (Methali 13:16) Kupata habari za msingi kuhusu afya kunaweza kukuchochea ufanye mabadiliko yanayohitajiwa ili wewe na familia yako muwe na afya bora.

      ◯ Endelea kujifunza. Katika nchi nyingi, shule za umma na za kibinafsi huwa na programu na vitabu vinavyozungumzia habari mbalimbali kuhusu afya. Tumia maandalizi hayo, na ujifunze jinsi ya kuboresha afya yako na kuepuka kuihatarisha. Uwe na akili iliyofunguka, na uwe tayari kufanya marekebisho machache.

      Mazoea mazuri unayojifunza na kufuata yatawanufaisha watoto wako na watoto wao pia. Wazazi wanapoweka mfano mzuri kuhusu kula vyakula vyenye lishe, usafi, mazoea mazuri ya kulala, kufanya mazoezi, na kuzuia magonjwa, watoto wao watanufaika.—Methali 22:6.

      ◯ Ni nini zaidi linalohitajiwa? Kutaka tu kuwa na afya nzuri hakutoshi. Inaweza kuwa vigumu kuacha mazoea mabaya ya muda mrefu, na mara nyingi unahitaji kujitahidi sana kufanya hata mabadiliko madogo. Hata wanapokabili hatari ya kupatwa na ugonjwa mbaya au kifo, huenda watu fulani wasifanye mambo ambayo wanajua yatawafaidi. Ni nini kinachoweza kuwachochea kuchukua hatua? Sisi sote tunahitaji kuzingatia kusudi kuu la maisha.

      Wenzi wa ndoa wanahitaji kuwa na afya nzuri na wenye nguvu ili waendelee kusaidiana. Wazazi wanataka kuendelea kuwategemeza na kuwazoeza watoto wao. Watoto wenye umri mkubwa wanahitaji kuwatunza watu wa ukoo waliozeeka. Na kuongezea hayo, tunataka kuinufaisha jamii badala ya kuwa mzigo. Mambo hayo yote yanahusisha kuwapenda na kuwajali wengine.

      Kichochezi kikubwa ni kuthamini na kujitoa kwa Muumba wetu. Wale wanaomwamini Mungu wanataka kulinda zawadi yake ya uhai ambayo ni yenye thamani sana. (Zaburi 36:9) Tunapokuwa na afya, tunaweza kumtumikia Mungu kwa nguvu. Hiyo ndiyo sababu kubwa zaidi inayotuchochea tutunze afya yetu.

      [Blabu katika ukurasa wa 8]

      Furahia faida za kuwa na afya nzuri

  • Chukua Hatua za Kuboresha Afya Yako
    Amkeni!—2011 | Machi
    • Chukua Hatua za Kuboresha Afya Yako

      UNAMKUMBUKA Ram, aliyetajwa katika habari ya kwanza ya mfululizo huu? Kama watu wengine wengi ulimwenguni pote, Ram hakujua umuhimu wa kula vizuri na mazoea mengine ya kila siku ambayo huchangia afya nzuri. Anasema: “Habari yenye kichwa, ‘Vyakula Bora Unavyoweza Kupata’ katika gazeti la Amkeni! (Mei 8, 2002) ilinisaidia kuona kwa nini ni muhimu kula chakula chenye lishe.”

      Ram anaeleza: “Tukiwa familia, tulijaribu kufuata yale ambayo tulijifunza katika gazeti hilo. Baada ya muda, tuligundua kwamba mfumo wetu wa kinga ulipata nguvu. Mwanzoni, kwa kuwa hatukuwa tukila vyakula vyenye lishe, tulipatwa na mafua mara kwa mara, lakini sasa hatuugui mafua sana. Pia, katika gazeti la Amkeni! lililokuwa na habari yenye kichwa ‘Njia Sita za Kutunza Afya,’ tulijifunza njia rahisi na zisizogharimu sana za kupata maji safi ya kunywa.”—Septemba 22, 2003 (22/9/2003).

      “Habari nyingine inayopatikana katika gazeti la Amkeni! ilinisaidia kuboresha afya yangu na ya familia yangu. Ilikuwa na kichwa ‘Sabuni ni “Chanjo”’ katika toleo la Novemba 22, 2003. Tulijaribu kufuata mapendekezo yaliyotajwa haraka iwezekanavyo. Sasa hatupatwi tena na maambukizo ya macho kama hapo awali.

      “Eneo tunamoishi, watu hawajali sana kwamba kuna nzi na mbu wengi. Lakini tulipotazama video The Bible—Its Power in Your Life,a familia yetu ilijifunza kwamba tunapaswa kuepuka wadudu hao. Hilo linatusaidia kudumisha afya nzuri.”

      Usikate tamaa! Ikiwa unahitaji kufanya mabadiliko yoyote, utafanikiwa ikiwa utaanza hatua kwa hatua na usijiwekee miradi usiyoweza kufikia. Kwa mfano, jaribu kupunguza kiasi cha vyakula visivyo na lishe unavyokula badala ya kuacha mara moja. Jaribu kulala mapema kidogo na kufanya mazoezi kidogo. Afadhali kufanya jambo kwa kiasi kidogo kuliko kutolifanya kabisa. Kwa kawaida, kusitawisha mazoea yanayofaa huchukua muda, labda majuma au hata miezi kadhaa. Kwa hiyo, usipoona mara moja matokeo ya jitihada zako, usikate tamaa. Ukijikakamua, licha ya mambo yenye kuvunja moyo, afya yako itakuwa bora.

      Haiwezekani kuwa na afya kamilifu katika ulimwengu huu usio mkamilifu. Tunapokuwa wagonjwa huenda ikawa si kwa sababu ya uzembe wetu, bali kwa sababu ya udhaifu wa kibinadamu tuliorithi. Kwa hiyo, usiache mahangaiko kuhusu afya, au mambo mengine, yakufadhaishe au yakutie wasiwasi. Yesu aliuliza: “Ni nani kati yenu ambaye kwa kuhangaika, anaweza kuongeza kipimo cha mkono mmoja kwenye uhai wake?” (Luka 12:25) Badala yake, jaribu kuepuka mambo ambayo yatafupisha maisha yako au kukuzuia kutimiza mengi. Kufanya hivyo kutakuwezesha kufurahia afya bora kadiri iwezekanavyo hadi wakati ambapo katika ulimwengu mpya wa Mungu “hakuna mkaaji atakayesema: ‘Mimi ni mgonjwa.’”—Isaya 33:24.

      [Maelezo ya Chini]

      a Imetolewa na Mashahidi wa Yehova.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki