-
Maradhi ya Moyo—Tisho kwa UhaiAmkeni!—1996 | Desemba 8
-
-
Maradhi ya Moyo—Tisho kwa Uhai
KILA mwaka mamilioni ya wanaume na wanawake ulimwenguni pote hupatwa na mishiko ya moyo. Wengi hupona wakiwa na athari ndogo. Wengine hawaponi. Kwa wengine zaidi moyo huharibika sana hivi kwamba “kuna shaka kama wanaweza kurudia utendaji muhimu,” mtaalamu wa moyo Peter Cohn asema, akiongezea: “Basi, ni lazima kutibu dalili za mishiko ya moyo haraka iwezekanavyo.”
Moyo ni msuli unaopiga damu iende kotekote mwilini. Katika mshiko wa moyo (myocardial infarction), sehemu ya misuli ya moyo hufa inapokosa damu. Ili udumu ukiwa wenye afya, moyo huhitaji oksijeni na lishe nyinginezo ambazo hubebwa kwa damu. Moyo hupata hizo kupitia ateri za moyo, ambazo zimezingira moyo.
Maradhi yaweza kuathiri sehemu yoyote ya moyo. Hata hivyo, maradhi ya kawaida zaidi ni yale ya kudhuru kichini-chini yapatayo mishipa ya moyo ambayo huitwa atherosclerosis. Maradhi hayo yatokeapo, mkusanyo wa mafuta, hukua katika kuta za ateri. Baada ya kipindi fulani, mkusanyo huo waweza kuongezeka na kuwa mgumu, kujaa ndani ya ateri, na kuziba mtiririko wa damu inayoenda moyoni. Ni maradhi haya ya ateri ya moyo (CAD) ambayo husababisha mishiko mingi sana ya moyo.
Kuziba kwa ateri moja au zaidi huharakisha shambulio moyo unapopungukiwa oksijeni. Hata katika ateri ambazo hazijazibwa sana, mkusanyo wa mafuta waweza kuvunjika vipande-vipande na kufanyiza mgando wa damu (thrombus). Ateri zenye maradhi pia huathiriwa kwa urahisi na mpindano. Mgando wa damu waweza kujifanyiza mahali pa mpindano, ukitokeza kemikali ambayo huzidi kubana ukuta wa ateri, jambo ambalo hutokeza mshiko wa moyo.
Misuli ya moyo inapokosa oksijeni kwa muda fulani, tishu zilizo kandokando zaweza kupatwa na madhara. Tofauti na tishu nyinginezo, misuli ya moyo haijifanyizi upya. Kadiri ya urefu wa mshiko wa moyo, ndivyo moyo uzidivyo kupatwa na madhara na ndivyo uwezekano wa kufa uongezekavyo. Mfumo wa mawasiliano wa moyo ukipatwa na madhara, pigo la kawaida la moyo laweza kuvurugika na moyo waweza kuanza kutetemeka-tetemeka sana. Katika badiliko kama hilo la pigo la moyo, moyo hupoteza uwezo wao wa kupiga damu kwa njia ifaayo. Kwa muda wa dakika kumi ubongo hufa na kifo hutokea.
Hivyo, tiba ya mapema ya wanatiba waliozoezwa ni muhimu. Hiyo yaweza kuokoa moyo usiendelee kupatwa na madhara, yaweza kuzuia au kutibu mabadiliko-badiliko katika pigo la moyo, au hata kuokoa uhai wa mtu.
-
-
Kutambua Dalili na Kuchukua HatuaAmkeni!—1996 | Desemba 8
-
-
Kutambua Dalili na Kuchukua Hatua
DALILI za mshiko wa moyo zitokeapo, ni muhimu kutafuta msaada wa kitiba mara moja, kwani hatari ya kufa ni kubwa zaidi katika muda wa saa moja ya kwanza baada ya kupatwa na mshiko wa moyo. Matibabu ya haraka yaweza kuokoa misuli ya moyo isipate madhara yasiyoweza kurekebishwa. Kadiri misuli ya moyo inavyookolewa, ndivyo uwezo wa moyo kupiga kwa mafanikio uwavyo mkubwa baada ya kupatwa na mshiko wa moyo.
Hata hivyo, baadhi ya mishiko ya moyo haitambuliki, kwa kuwa haionyeshi dalili zozote zenye kuonekana. Katika hali kama hizo huenda mtu huyo asijue kwamba ana maradhi ya ateri ya moyo (CAD). Kwa kusikitisha, kwa wengine mshiko mkubwa wa moyo waweza kuwa ishara ya kwanza ya tatizo la moyo. Moyo uachapo kupiga, kikundi cha tiba ya dharura kisipoitwa mara moja na uhuishaji wa moyo na mapafu (CPR) usipofanywa na mtu aliye karibu, si rahisi kupona.
Kati ya wengi ambao wana dalili za CAD, Harvard Health Letter yaripoti, karibu nusu wataahirisha kutafuta msaada wa kitiba. Kwa nini? “Mara nyingi kwa sababu hawatambui dalili hizo ni za nini au hawazichukui kwa uzito.”
John,a ambaye ni mhasiriwa wa mshiko wa moyo na ambaye pia ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova, asihi hivi: “Unapohisi kwamba kuna kasoro, usikawie kupata tiba kwa hofu ya kwamba utaonekana unatilia chumvi ugonjwa wako. Karibu nife kwa sababu sikuchukua hatua haraka iwezekanavyo.”
Kile Kilichotendeka
John aeleza: “Mwaka mmoja na nusu kabla ya kupatwa na mshiko wa moyo, nilionywa na daktari kuhusu kolesteroli nyingi niliyokuwa nayo, ambayo ni kisababishi kikuu cha CAD. Lakini niliepuka suala hilo, kwa kuwa nilihisi kwamba nilikuwa mchanga—chini ya umri wa miaka 40—na mwenye afya nzuri. Nasikitika sana kwamba sikuchukua hatua wakati huo. Nikapata ishara nyinginezo za kuonya—kukosa pumzi nikijikakamua kidogo tu, maumivu ambayo niliyafikiria kuwa tatizo la umeng’enyaji wa chakula na, kwa miezi kadhaa kabla ya kupatwa na mshiko wa moyo nilikuwa mchovu mno. Nilifikiri kwamba nyingi za dalili hizo zilitokezwa na ukosefu wa usingizi na mkazo mwingi sana wa kazi. Siku tatu kabla ya kupatwa na mshiko wa moyo, nilihisi kile nilichokifikiria kuwa mpindano wa misuli katika kifua changu. Huo ulikuwa mshiko mdogo wa moyo ambao ulitangulia mshiko mkubwa ulionipata siku tatu baadaye.”
Maumivu au msongo wa kifua, ambayo huitwa angina, hutokea kwa karibu nusu ya wale ambao hupatwa na mshiko wa moyo. Wengine hupatwa na dalili za kukosa pumzi au uchovu na udhaifu, zikionyesha kwamba moyo haupati oksijeni ya kutosha kwa sababu ya kuzibwa kwa mshipa wa moyo. Ishara hizo za kuonya zapaswa kufanya mtu amwone daktari akachunguzwe moyo. Dakt. Peter Cohn asema: “Baada ya angina kutibiwa, hakuna uhakikisho kwamba mshiko wa moyo utazuiwa, lakini angalau uwezekano wa kupatwa na mshiko wa moyo hupunguka.”
Huo Mshiko
John aendelea kusema: “Siku hiyo tulikuwa tukienda kucheza softiboli. Nilipokuwa nikila hamburger na viazi vilivyokaangwa kwa chakula cha mchana, nilipuuza hali yangu ya kuhisi vibaya, kichefuchefu, na mbano wa sehemu ya juu ya mwili. Lakini tulipofika uwanja wa kucheza na kuanza kucheza, nilihisi kwamba kuna kasoro fulani. Nilizidi kuhisi vibaya alasiri hiyo.
“Mara kadhaa nililala chali kwenye benchi ya wachezaji, na kujaribu kunyoosha misuli ya kifua changu, lakini misuli hiyo iliendelea kunibana zaidi na zaidi. Nilipokuwa nikicheza, nilijiambia, ‘Labda nimeshikwa na mafua,’ kwa kuwa pindi fulani-fulani nilikuwa nahisi vibaya na udhaifu. Nilipokimbia, ilikuwa wazi kwamba nakosa pumzi. Nikalala kwenye benchi tena. Nilipoketi, nikawa sina shaka kwamba nilikuwa na tatizo baya sana. Nikamwambia mwana wangu James kwa sauti kuu: ‘Nahitaji kwenda hospitali SASA!’ Nikahisi kana kwamba kifua changu kilikuwa kimeporomoka. Maumivu yakawa mengi sana hivi kwamba sikuweza kuamka. Nikafikiria, ‘Huu hauwezi kuwa mshiko wa moyo? Nina umri wa miaka 38 tu!’”
Mwana wa John, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 15, aeleza: “Ilichukua dakika kadhaa tu kwa baba yangu kupoteza nguvu, hivi kwamba ikawa lazima abebwe kuingizwa katika gari. Rafiki yangu akaendesha gari huku akimwuliza baba maswali ili asipoteze fahamu. Hatimaye, baba hakujibu. ‘John!’ rafiki yangu akasema kwa sauti kubwa. Lakini bado baba yangu hakujibu. Kisha baba akashtuka katika kiti, akifurukuta na kutapika. Nikasema kwa sauti kwa kurudia-rudia: ‘Baba! Nakupenda! Tafadhali usife!’ Baada ya kufurukuta, mwili wake wote ukapoa kwenye kiti cha gari. Nikadhani amekufa.”
Hospitalini
“Tukakimbia ndani ya hospitali ili kupata msaada. Dakika mbili au tatu zilikuwa zimepita tangu nidhani baba amekufa, lakini nilitumaini angehuishwa. Kwa mshangao wangu, Mashahidi wa Yehova wenzetu wapatao 20 ambao walikuwa katika uwanja wa mchezo walikuwa katika chumba cha kungoja. Walinifanya nihisi nimefarijiwa na kupendwa, jambo lililosaidia sana wakati huo wenye huzuni. Karibu dakika 15 baadaye, daktari akaja na kueleza: ‘Tumefaulu kumhuisha baba yako, lakini amepata mshiko mkubwa wa moyo. Hatuna hakika kama ataishi.’
“Kisha akaniruhusu kumwona baba kifupi. Maneno ya baba yenye upendo kwa familia yetu yakanigusa sana hisia. Kwa maumivu mengi, alisema: ‘Nakupenda mwana wangu. Sikuzote ukumbuke kwamba Yehova ndiye mtu wa maana zaidi katika maisha zetu. Usiache kumtumikia, na umsaidie mama yako na ndugu zako wasiache kumtumikia. Tuna tumaini thabiti la ufufuo, na nikifa, nataka kuwaona nyote ninaporudi.’ Sote tulikuwa tukilia machozi ya upendo, hofu, na tumaini.”
Mke wa John, Mary, akafika muda wa saa moja baadaye. “Nilipoingia katika chumba cha utibabu wa dharura, daktari aliniambia: ‘Mume wako amepatwa na mshiko mkubwa wa moyo.’ Nikashtuka sana. Alieleza kwamba moyo wa John ulikuwa umetulizwa mara nane. Hatua hii ya dharura huhusisha kutumia volteji ya umeme kukomesha mapigo yenye fujo ya moyo ili urudie mapigo yao ya kawaida. Pamoja na kuhuishwa kwa moyo na mapafu, kuingizwa kwa oksijeni, na dawa za kuingizwa kupitia mishipa, tiba ya kutuliza moyo ni njia ya hali ya juu sana ya kuokoa uhai.
“Nilipomwona John, moyo wangu ukaugua. Alikosa rangi sana, na kulikuwa na neli nyingi na nyaya zilizounganisha mwili wake na mashine za kumchunguzia. Kwa ukimya, nilisali kwa Yehova anipe nguvu ya kuvumilia jaribio hili kwa ajili ya wana wetu watatu, nami nilisali nipate mwongozo wa kufanya maamuzi yenye hekima kuhusu yale ambayo yangekuwa mbele. Nilipokaribia kitanda cha John, nikafikiria, ‘Utamwambia nini mpendwa wako wakati kama huu? Je, kweli sisi tumejitayarishia hali kama hii ya kutisha uhai?’
“‘Mpenzi,’ John akasema, ‘wajua huenda nisiishi. Lakini ni muhimu kwamba wewe na wavulana wetu mdumishe uaminifu kwa Yehova kwa sababu karibuni mfumo huu utaisha na hakutakuwapo tena ugonjwa wala kifo. Nataka kuamka katika mfumo huo mpya na kukuona wewe na wavulana wetu huko.’ Machozi yakatutiririka.”
Daktari Aeleza
“Baadaye daktari aliniita kando na kueleza kwamba uchunguzi umeonyesha kwamba mshiko wa moyo wa John ulisababishwa na kuzibwa kabisa kwa ateri ya mbele ya upande wa kushoto inayoelekea chini. Pia ateri nyingine ilikuwa imezibwa. Daktari akaniambia kwamba ni lazima nifanye uamuzi kuhusu tiba ya John. Machaguo mawili yaliyopatikana ni dawa na angioplasty. Yeye alifikiri angioplasty ingekuwa afadhali, hivyo tukaichagua. Lakini madaktari hawakuahidi kama atapona, kwa kuwa wengi hawaponi mshiko wa moyo wa aina hiyo.”
Tiba ya angioplasty ni mbinu ya upasuaji ambayo kwayo katheta iliyowekewa puto huingizwa katika ateri ya moyo na kisha kuingiziwa hewa ili ifungue mzibo. Tiba hiyo hufanikiwa sana katika kurudisha mtiririko wa damu. Wakati mishipa kadhaa imezibwa sana, mara nyingi upasuaji wa kuunganisha mshipa mwingine na mshipa mkuu (bypass surgery) hupendekezwa.
Matazamio Yasiyo Mazuri
Baada ya kufanyiwa angioplasty, uhai wa John ukaendelea kuwa hatarini kwa muda wa saa 72 nyinginezo. Hatimaye, moyo wake ukaanza kupata nguvu baada ya lile pigo. Lakini, moyo wa John ulikuwa ukipiga kwa nusu tu ya uwezo wao wa zamani, na sehemu yao kubwa ilikuwa imekuwa kovu, hivyo ikatarajiwa sana kwamba angelemaa moyo.
Akikumbuka, John ahimiza: “Tuna wajibu kwa Muumba wetu, familia zetu, ndugu na dada zetu wa kiroho, na sisi wenyewe kutii maonyo na kutunza afya zetu—hasa tukiwa hatarini. Kwa kadiri kubwa, twaweza kusababisha furaha au huzuni. Ni juu yetu.”
Kisa cha John kilikuwa kibaya sana nacho kilihitaji hatua ya dharura. Lakini si kwamba wote wenye kuhisi uchungu kama wa kiungulia wakimbilie daktari. Lakini, aliyojionea John ni onyo, na wale wanaohisi kwamba wana dalili hizo wanapaswa kuchunguzwa.
Ni nini kiwezacho kufanywa ili kupunguza hatari ya kupatwa na mshiko wa moyo? Makala ifuatayo itajadili jambo hilo.
[Maelezo ya Chini]
a Majina yamebadilishwa katika makala hizi.
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
Dalili za Mshiko wa Moyo
• Hisi isiyostarehesha ya msongo, kubanwa, au maumivu kifuani ambayo hudumu zaidi ya dakika chache. Hisi hiyo yaweza kudhaniwa kuwa ni kiungulia chenye maumivu makali
• Maumivu ambayo yaweza kuenea kufikia—au kuwapo kwenye—utaya, shingo, mabega, mikono, viwiko, au mkono wa kushoto pekee
• Maumivu ya muda mrefu katika sehemu ya juu ya fumbatio
• Kukosa pumzi, kizunguzungu, kuzimia, kutokwa jasho, au kuhisi vibaya ukiguswa
• Uchovu—waweza kuhisiwa majuma kadhaa kabla ya kupatwa na mshiko wa moyo
• Kichefuchefu au kutapika
• Mashambulizi ya mara kwa mara ya angina ambayo hayasababishwi na kujikakamua
Dalili hutofautiana kutoka zile zilizo hafifu hadi zile zenye nguvu nazo hazitokei zote katika kila mshiko wa moyo. Lakini dalili zozote kadhaa zitokeapo pamoja, tafuta msaada haraka sana. Hata hivyo, katika visa fulani hakuna dalili; hivyo huitwa mishiko ya moyo isiyo na dalili.
[Sanduku katika ukurasa wa 7]
Hatua za Kuchukuliwa ili Kuokoa Uhai
Wewe au mtu mwingine unayemjua ukiwa na dalili za mshiko wa moyo:
• Tambua dalili.
• Acha chochote unachofanya na uketi au ulale chini.
• Dalili zikidumu kwa zaidi ya dakika chache, piga simu ya msaada wa dharura. Mwambie unayeongea naye kwamba unashuku una mshiko wa moyo, na umpe habari zinazohitajika ili waweze kukupata.
• Ikiwa unaweza kumpeleka mgonjwa kwenye chumba cha tiba ya dharura haraka iwezekanavyo, wewe mwenyewe ukiendesha gari, fanya hivyo. Ukifikiri unapata mshiko wa moyo, omba mtu akupeleke huko.
Unapongoja kikundi cha tiba ya dharura:
• Legeza nguo zilizobana, kutia ndani mshipi au tai. Msaidie huyo mgonjwa astarehe, ukimwekea mito ikiwa ni lazima.
• Dumisha utulivu, iwe ni wewe uliye mgonjwa au uwe msaidiaji wake. Wasiwasi waweza kuongeza uwezekano wa kupatwa na badiliko katika pigo la moyo, ambalo laweza kuua. Sala yaweza kuwa msaada wenye kuimarisha katika kudumisha utulivu.
Mgonjwa akionekana kama ameacha kupumua:
• Kwa sauti kubwa uliza, “Waweza kunisikia?” Ikiwa haitikii, ikiwa moyo haupigi, na ikiwa mgonjwa hapumui, anza kumhuisha moyo na mapafu (CPR).
• Kumbuka hatua tatu za msingi za CPR:
1. Inua kidevu cha huyo mgonjwa, ili njia za hewa zifunguliwe.
2. Njia za hewa zikiwa wazi, huku ukiziba pua ya mgonjwa, puliza polepole mara mbili katika mdomo mpaka kifua kiinuke.
3. Sukuma mara 10 hadi 15 katikati ya kifua kati ya chuchu ili kusukuma damu kutoka kwa moyo na kifua. Kila sekunde 15, rudia kupuliza mara mbili na kufuatia na misukumo 15 mpaka mipwito ya moyo irudi na aanze kupumua tena au mpaka kikundi cha tiba ya dharura kifike.
Hiyo CPR inapaswa kufanywa na mtu ambaye amezoezwa. Lakini kama hakuna mtu ambaye amezoezwa, “CPR yoyote ni afadhali kuliko kukosa kuifanya,” asema Dakt. R. Cummins, mkurugenzi wa utunzi wa dharura ya moyo. Mtu asipoanzisha hatua hizo, uwezekano wa kupona ni mdogo sana. Hiyo CPR huendeleza uhai wa mtu mpaka msaada ufike.
-
-
Hatari Hiyo Inaweza Kupunguzwaje?Amkeni!—1996 | Desemba 8
-
-
Hatari Hiyo Inaweza Kupunguzwaje?
MARADHI ya ateri ya moyo (CAD) yameshirikishwa na mambo kadhaa ya urithi, mazingira, na mtindo-maisha. Maradhi ya ateri ya moyo na mshiko wa moyo waweza kusababishwa na hatari zinazohusiana na moja au zaidi ya mambo hayo, hatari hizo zikichukua miaka, au hata miongo kujikuza.
Umri, Jinsia, na Urithi
Kadiri umri uzidivyo kuongezeka ndivyo hatari ya kupatwa na mshiko wa moyo izidivyo kuongezeka. Karibu asilimia 55 ya mishiko ya moyo hutukia miongoni mwa watu wenye umri unaozidi miaka 65. Asilimia ipatayo 80 ya wale ambao hufa kutokana na mishiko ya moyo ni wenye umri wa miaka 65 au zaidi.
Wanaume wenye umri ulio chini ya miaka 50 wamo hatarini kuliko wanawake wa rika hilo. Baada ya hedhi kukoma, hatari ya mwanamke kupatwa na mshiko wa moyo huongezeka kwa sababu ya upungufu mkubwa wa homoni ya estrojeni yenye kuwakinga. Kulingana na makadirio fulani, tiba ya kurudisha estrojeni yaweza kupunguza hatari za maradhi ya moyo katika wanawake kwa asilimia 40 au zaidi, ingawa inaweza kuongeza hatari ya kupatwa na kansa fulani.
Urithi waweza kuchangia sana. Wale ambao wazazi wao walipatwa na mshiko wa moyo wakiwa hawajafikia umri wa miaka 50 wamo hatarini zaidi ya kupatwa na mshiko wa moyo. Hata kama wazazi walipatwa na mshiko wa moyo baada ya umri wa miaka 50, bado kuna hatari zaidi. Ikiwa kuna historia ya matatizo ya moyo katika familia, yaelekea watoto watasitawisha matatizo kama hayo.
Suala la Kolesteroli
Kolesteroli, ambayo ni aina ya shahamu, ni muhimu kwa uhai. Hiyo hutengenezwa katika ini, nayo damu huibeba na kuipeleka katika chembe, ikiwa katika molekuli ziitwazo lipoprotini. Aina mbili za lipoprotini ni zile zenye msongamano wa chini (kolesteroli ya LDL) na zile zenye msongamano wa juu (kolesteroli ya HDL). Kolesteroli yaweza kuwa kisababishi hatari cha CAD wakati ambapo kuna kolesteroli nyingi mno ya LDL katika damu.
Lipoprotini ya msongamano wa juu hufikiriwa kuwa ina fungu la kulinda kwa kuondoa kolesteroli kutoka kwenye tishu na kuirudisha kwenye ini ambako hiyo hubadilishwa na kuondolewa katika mwili. Ikiwa LDL ni nyingi na HDL ni chache, kuna uwezekano mkubwa wa kupatwa na maradhi ya moyo. Kupunguza kiwango cha LDL kwaweza kupunguza sana hatari. Kuchunga aina ya mlo unaokula ni njia kubwa katika matibabu haya, na mazoezi yaweza kusaidia. Dawa mbalimbali zaweza kusaidia, lakini baadhi yazo zina athari mbaya.a
Mlo usio na kolesteroli nyingi wala mafuta mengi ndio hupendekezwa. Kubadili vyakula vyenye mafuta mengi, kama vile siagi, kwa vyakula visivyo na mafuta mengi, kama mafuta ya canola au mafuta ya zeituni, kwaweza kupunguza LDL na kuhifadhi HDL. Kwa upande mwingine, jarida American Journal of Public Health lasema kwamba mafuta ya mboga, yaliyotiliwa hidrojeni au kutiliwa hidrojeni chache, ambayo hupatikana katika siagi nyingi na bidhaa nyingi za mafuta ya mboga yaweza kuongeza LDL na kupunguza HDL. Kupunguza kula nyama zenye mafuta mengi na kula nyama za kuku au bata mzinga zisizo na mafuta mengi hupendekezwa pia.
Uchunguzi mbalimbali umeonyesha kwamba vitamini E, beta-karotene, na vitamini C zaweza kupunguza mafuta mengi ndani ya ateri za wanyama. Uchunguzi mmoja ulikata kauli kwamba hizo zaweza pia kupunguza visa vya mshiko wa moyo katika wanadamu. Kila siku kula mboga na matunda yenye kiasi kingi cha beta-karotene na karotenoidi nyinginezo pamoja na vitamini C, kama vile nyanya, mboga yenye majani makubwa ya kijani-cheusi, pilipili, karoti, viazi vitamu, matikiti, zaweza kulinda kwa kadiri fulani dhidi ya CAD.
Pia vitamini B6 na magnesi zasemwa kuwa zafaa. Nafaka kama vile shayiri na oti na vilevile maharagwe, dengu, na mbegu fulani zaweza kusaidia. Kwa kuongezea, inafikiriwa kwamba kula samaki kama yule nyama-nyekundu, makareli, heringi, au tuna angalau mara mbili kwa juma kwaweza kupunguza hatari ya kupatwa na CAD, kwa kuwa hizi zina kiasi kingi cha omega-3 na asidi nyingi zisizo na mafuta mengi.
Mtindo-Maisha wa Kukaakaa
Watu ambao hukaakaa wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupatwa na mshiko wa moyo. Wao hutumia sehemu kubwa ya siku zao bila kuwa watendaji nao hawafanyi mazoezi kwa ukawaida. Mishiko ya moyo mara nyingi hutukia katika watu hawa baada ya kufanya utendaji wa kujikakamua kama vile kulima kwa bidii, kukimbia-kimbia, kuinua vyuma vizito, au kuondoa theluji kwa koleo. Lakini hatari ya kupatwa na mshiko wa moyo hupunguka kati ya watu ambao hufanya mazoezi kwa ukawaida.
Kutembea kwa kasi kwa muda wa dakika 20 hadi 30 mara tatu au mara nne kwa juma kwaweza kupunguza hatari ya kupatwa na mshiko wa moyo. Mazoezi ya kawaida huboresha uwezo wa moyo kupiga, husaidia kupoteza uzito, na yaweza kupunguza viwango vya kolesteroli na kupunguza msongo wa damu.
Msongo wa Juu wa Damu, Uzito wa Kupita Kiasi, na Ugonjwa wa Kisukari
Msongo wa juu wa damu waweza kudhuru kuta za ateri na kuwezesha kolesteroli ya LDL kuingia ndani ya kuta za ateri na kufanyiza mkusanyo wa mafuta. Mkusanyo huo uongezekapo, kunakuwa na ukinzani kwa mtiririko wa damu na hivyo msongo wa damu huongezeka.
Msongo wa damu wapaswa kuchunguzwa kwa ukawaida, kwa kuwa huenda dalili yoyote ya tatizo hilo isiweze kuonekana. Kwa kila upungufu wa msongo wakati moyo umetulia, hatari ya mshiko wa moyo yaweza kupunguzwa kwa asilimia 2 hadi 3. Tiba ya kupunguza msongo wa damu yaweza kusaidia. Kuchunga mlo, na katika hali fulani kupunguza ulaji wa chumvi, pamoja na kufanya mazoezi kwa ukawaida ya kupunguza uzito kwaweza kusaidia kudhibiti msongo wa juu wa damu.
Uzito kupita kiasi huendeleza msongo wa juu wa damu na kutokeza kasoro za mafuta. Kuepuka unene kupita kiasi au kuutibu ni njia ya msingi ya kuzuia kisukari. Kisukari huzidisha CAD na kuongeza hatari za kupatwa na mshiko wa moyo.
Kuvuta Sigareti
Kuvuta sigareti ni kisababishi kikuu cha usitawi wa CAD. Katika Marekani, huko husababisha kwa njia ya moja kwa moja karibu asilimia 20 ya vifo vitokezwavyo na maradhi yote ya moyo na karibu asilimia 50 ya mishiko ya moyo katika wanawake walio chini ya umri wa miaka 55. Kuvuta sigareti huongeza msongo wa damu na kuingiza kemikali zenye sumu, kama vile nikotini na kaboni monoksidi, katika mkondo wa damu. Kemikali hizo nazo hudhuru ateri.
Wavutaji wa sigareti pia huhatarisha wale ambao huvuta moshi wao. Uchunguzi waonyesha kwamba watu wasiovuta sigareti wanaoishi na wavutaji wa sigareti wana hatari zaidi ya kupatwa na mshiko wa moyo. Hivyo, kwa kuacha kuvuta sigareti, mtu aweza kupunguza hatari kwake mwenyewe na hata anaweza kuokoa uhai wa wapendwa wake wasiovuta sigareti.
Mkazo
Wale wenye CAD wakiwa chini ya mkazo mkali wa kihisia moyo au wa kiakili, wao hukabili hatari kubwa zaidi ya kupatwa na mshiko wa moyo na kifo cha ghafula kuliko watu ambao wana ateri zenye afya. Kulingana na uchunguzi mmoja, mkazo waweza kufanya ateri zenye kujaa mafuta zifinyae, na hilo hupunguza mtiririko wa damu kufikia asilimia 27. Mifinyo mikubwa ilionekana hata katika ateri zenye maradhi madogo. Uchunguzi mwingine ulidokeza kwamba mkazo mkali waweza kutokeza hali zinazoweza kufanya mafuta katika kuta za mishipa kupasuka, na kutokeza mshiko wa moyo.
Gazeti Consumer Reports on Health lasema: “Baadhi ya watu huonekana kupitia maisha wakiwa na mtazamo mbaya. Wao ni wenye madharau, ni wenye hasira, nao hukasirika kwa urahisi. Ingawa wengi wa watu huachilia uchokozi kidogo, watu wakali huitikia kupita kiasi.” Hasira ya daima na uhasama huinua msongo wa damu, huongeza mipigo ya moyo, na kuchochea ini kuacha kolesteroli katika mkondo wa damu. Hilo huharibu ateri za moyo na kuchangia kusababisha CAD. Hasira hufikiriwa kuongeza maradufu hatari ya kupatwa na mshiko wa moyo, na hiyo hudumu kwa angalau muda wa saa mbili. Ni nini kinachoweza kusaidia?
Kulingana na The New York Times, Dakt. Murray Mittleman alisema kwamba watu ambao walijaribu kudumisha utulivu katika hali za kuamsha hisia moyo waweza kupunguza hatari ya kupatwa na mshiko wa moyo. Maneno hayo yafanana sana na maneno yaliyorekodiwa katika Biblia karne nyingi zilizopita: “Moyo mtulivu ni uhai wa mwili.”—Mithali 14:30, NW.
Mtume Paulo alijua kile kilichomaanishwa na kuwa chini ya mkazo. Yeye alisema juu ya mahangaiko ambayo yalimkumba kila siku. (2 Wakorintho 11:24-28) Lakini alipata msaada wa Mungu akaandika: “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”—Wafilipi 4:6, 7.
Ingawa kuna mambo mengine yahusikayo na matatizo ya moyo, yale yaliyozungumzwa hapa yaweza kusaidia kutambua hatari ili mtu aweze kuchukua hatua ifaayo. Hata hivyo, wengine wamejiuliza jinsi hali ilivyo kwa wale ambao ni lazima waishi na matokeo ya mshiko wa moyo. Mtu anaweza kupona kwa kadiri gani?
-
-
Kupata NafuuAmkeni!—1996 | Desemba 8
-
-
Kupata Nafuu
BAADA ya kupatwa na mshiko wa moyo, ni kawaida kwa mtu kuwa mwoga na mwenye hangaiko. Je, nitapatwa na mshiko mwingine wa moyo? Je, nitalemazwa au nitashindwa kufanya mengi kwa sababu ya maumivu na kupoteza nguvu na nishati?
John, aliyetajwa katika makala yetu ya pili, alitumaini kwamba kadiri wakati ulivyopita, hali yake ya kusikia vibaya kila siku na maumivu ya kifua yangepungua. Lakini baada ya miezi michache, yeye alisema: “Bado hayajapungua. Hilo, pamoja na kuchoka kwa urahisi na kucheza-cheza kwa moyo wangu, hunifanya nijiulize daima, ‘Nitapatwa na mshiko mwingine wa moyo?’”
Jane, kutoka Marekani, aliyekuwa mjane mchanga wakati alipopatwa na mshiko wa moyo, alikiri: “Nilifikiri kwamba singeishi au kwamba ningepata mshiko mwingine wa moyo na kufa. Nikawa na hofu kwa kuwa nilikuwa na watoto watatu wa kulea.”
Hiroshi, wa Japani, alisimulia: “Nilishtuka kuambiwa kwamba moyo wangu hauwezi kutenda kama ulivyofanya awali; uwezo wao wa kupiga ulipunguka kwa asilimia 50. Nilikuwa na hakika kwamba ningelazimika kupunguza baadhi ya utendaji wangu nikiwa mhudumu wa Mashahidi wa Yehova, kwa kuwa niliweza kufanya chini ya nusu ya yale niliyokuwa nikifanya.”
Mtu akosapo nguvu, vipindi vya kushuka moyo na hisia za kutofaa zaweza kumwingilia. Marie, mwenye umri wa miaka 83 ambaye ni Mwaustralia aliyejitoa kwa kazi ya kuhubiri kwa wakati wote ya Mashahidi wa Yehova, aliomboleza hivi: “Kushindwa kwangu kuwa mwenye utendaji kama hapo awali kulinihuzunisha. Badala ya kusaidia wengine, sasa nilihitaji msaada.” Katika Afrika Kusini, Harold alisema: “Nilishindwa kufanya kazi kwa miezi mitatu. Kile nilichoweza kufanya wakati huo kilikuwa tu kutembea-tembea katika bustani. Jambo hilo lilinifadhaisha sana!”
Upasuaji wa kutumia mishipa mingine ya kupitisha damu ulihitajika baada ya Thomas, wa Australia, kupatwa na mshiko wa pili wa moyo. Yeye alisema: “Siwezi kuvumilia maumivu sana, na kufanyiwa upasuaji mkuu kulinishinda hata kuwazia.” Jorge, wa Brazili, alisema hivi baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo: “Kwa sababu ya hali yangu mbaya ya kifedha, niliogopa kwamba ningemwacha mke wangu peke yake bila msaada. Nilihisi kwamba nisingeishi muda mrefu zaidi.”
Kupata Nafuu
Ni nini ambacho kimesaidia wengi wapate nafuu na kurudia hisia-moyo zao thabiti? Jane aonelea: “Nilipohisi hofu ya ghafula, sikuzote nilimwendea Yehova katika sala na kumtwika mzigo wangu na kumwachia.” (Zaburi 55:22) Sala husaidia mtu kupata nguvu na amani ya akili ambazo ni muhimu anapokuwa na mahangaiko.—Wafilipi 4:6, 7.
John na Hiroshi walishiriki katika programu za kuwafanya wapate nafuu. Mlo mzuri na mazoezi yaliimarisha mioyo yao, hivi kwamba wote wawili walirudia kazi. Nao walisema walipona kiakili na kihisia-moyo kwa sababu ya uwezo wa kutegemeza wa roho ya Mungu.
Kupitia utegemezo wa ndugu zake wa Kikristo, Thomas alipata moyo mkuu wa kukabili upasuaji. Yeye alisema: “Kabla ya upasuaji, mwangalizi mmoja alinitembelea akasali nami. Kwa njia ya kugusa moyo kabisa, aliomba Yehova aniimarishe. Usiku huo nilikazia akili sala yake na kuhisi nimebarikiwa sana kuwa na wazee kama yeye ambao hisia-mwenzi zao wakati wa vipindi hivyo vyenye kufadhaisha ndizo baadhi ya mambo yanayofanya mtu apate nafuu.”
Anna, kutoka Italia, alikabiliana na mshuko-moyo kwa njia hii: “Ninapokuwa nimeshuka moyo, mimi hufikiria baraka zote ambazo tayari nimepokea nikiwa mmoja wa watumishi wa Mungu na baraka ambazo zitakuja chini ya Ufalme wa Mungu. Jambo hilo hunisaidia kupata utulivu.”
Marie anashukuru sana kwa msaada wa Yehova. Familia yake imekuwa ikimtegemeza, naye asema: “Ndugu zangu na dada zangu wa kiroho, kila mmoja akiwa na kifurushi chake cha kubeba, waliweka kando wakati ili kunizuru, kunipigia simu, au kunitumia kadi. Ningeweza kuhuzunikaje huku nikionyeshwa upendo mwingi hivi?”
Hakuna Wapweke
Imesemwa kwamba moyo unaopona haupaswi kuwa mpweke. Utegemezo wa familia na marafiki hutimiza fungu kubwa zuri katika kupona kwa wale ambao mioyo yao ni lazima ipone kihalisi na kitamathali.
Michael, wa Afrika Kusini, alieleza hivi: “Ni vigumu kueleza wengine jinsi kukata tamaa kulivyo. Lakini niingiapo katika Jumba la Ufalme, hangaiko ambalo akina ndugu huonyesha hunichangamsha sana na kuniondolea huzuni.” Henry, wa Australia, pia aliimarishwa kwa upendo wa kina na uelewevu ambao kutaniko lilionyesha. Yeye alisema: “Nilihitaji sana maneno hayo mororo yenye kutia moyo.”
Jorge alithamini kina cha hangaiko ambalo wengine walionyesha kwa kusaidia familia yake kifedha mpaka alipoweza kurudia kazi yake. Olga, wa Sweden, vilevile alithamini msaada halisi ambao ndugu na dada wengi wa kiroho waliwapa yeye na familia yake. Wengine walimfanyia ununuzi, huku wengine wakisafisha nyumba yake.
Mara nyingi, wagonjwa wa moyo ni lazima wapunguze kushiriki katika utendaji waupendao sana. Sven, wa Sweden, asimulia: “Nyakati nyingine ni lazima niepuke kushiriki katika huduma wakati halihewa ni yenye upepo mno au ni baridi mno, kwa kuwa hiyo hutokeza mpindano wa moyo. Nathamini uelewevu ambao wengi wa Mashahidi wenzangu wameonyesha katika jambo hili.” Na anapolazimika kuwa kitandani bila kuondoka, Sven aweza kusikiliza mikutano kwa sababu akina ndugu kwa upendo humrekodia katika ukanda. “Wao hunijulisha kile kinachoendelea katika kutaniko, na hiyo hufanya nihisi kuwa mshiriki.”
Marie, ambaye hulala kitandani sikuzote, ahisi kwamba amebarikiwa kutembelewa na wale ambao anajifunza Biblia nao. Kwa njia hiyo yeye aweza kuendelea kuzungumzia wakati ujao mzuri ajabu ambao anatazamia. Thomas ni mwenye shukrani kwa hangaiko analoonyeshwa: “Wazee wamekuwa wenye fadhili sana nao wamepunguza migawo wanayonipa.”
Familia Zahitaji Utegemezo
Hali yaweza kuwa ngumu kwa washiriki wa familia kama ilivyo kwa mhasiriwa. Wao hupatwa na mkazo mwingi na hofu. Kuhusu hangaiko la mke wake, Alfred, wa Afrika Kusini, alionelea: “Niliporudi nyumbani kutoka hospitali, mke wangu alikuwa akiniamsha mara nyingi usiku kuona ikiwa ningali nilikuwa mzima, naye alikuwa akisisitiza nimwone daktari kila baada ya miezi mitatu nikapimwe.”
Mithali 12:25 yasema kwamba “uzito katika moyo wa mtu huuinamisha.” Carlo, wa Italia, asema kwamba tangu apatwe na mshiko wa moyo, mke wake mwenye upendo na utegemezo “ameshuka moyo.” Lawrence, kutoka Australia, alisema: “Mojawapo mambo ya kuangalia ni kwamba mwenzako anatunzwa. Mkazo waweza kuwa mkubwa zaidi kwa mwenzi wako.” Hivyo, twapaswa kukumbuka sikuzote mahitaji ya familia nzima, kutia ndani watoto. Hali hiyo yaweza kuwalemaza kihisia moyo na kimwili.
James, aliyetajwa katika makala ya pili, alikuja kuwa mnyamavu baada ya mshiko wa moyo wa babake. Yeye alisema: “Nilihisi kwamba singeweza kufurahia michezo tena kwa sababu nilifikiri kwamba mara nitakapofanya hivyo, jambo baya lingetokea.” Kumwambia babake hofu yake na kufanyia kazi kukuza uhusiano mzuri pamoja na wengine kulisaidia kuondosha wasiwasi wake. Katika pindi hiyo James alifanya kitu kingine ambacho kilikuja kuwa na uvutano mkubwa sana katika maisha yake. Yeye alisema: “Niliongeza funzo langu la kibinafsi la Biblia na utayarishaji wangu wa mikutano ya Kikristo.” Miezi mitatu baadaye aliweka wakfu maisha yake kwa Yehova naye akaonyesha wakfu wake kwa ubatizo wa maji. “Tangu wakati huo,” yeye asema, “nimesitawisha uhusiano wa karibu sana na Yehova. Kwa kweli nina mengi sana ya kumshukuru.”
Baada ya kupatwa na mshiko wa moyo, mtu hupata nafasi achunguze upya maisha yake. Kwa kielelezo, mtazamo wa John ulibadilika. Yeye alisema: “Unaona ubatili wa kufuatia mambo ya kilimwengu na kutambua jinsi upendo wa familia na marafiki ulivyo muhimu na jinsi tulivyo wenye maana sana kwa Yehova. Uhusiano wangu pamoja na Yehova, familia yangu, na ndugu na dada wa kiroho ni wa kutangulizwa hata zaidi sasa.” Akikumbuka masaibu yake, yeye aliongezea: “Siwezi kuwazia kukabiliana na hilo bila tumaini letu la wakati ambapo mambo haya yatakuja kurekebishwa. Ninaposhuka moyo, mimi hufikiria wakati ujao, na kile kinachotendeka sasa chawa kidogo tu.”
Wapatwapo na mishuko ya moyo wakati wanapopata nafuu, waokokaji hao wa mishiko ya moyo wana tumaini imara kwa Ufalme ambao Yesu Kristo alitufundisha kusali kuuhusu. (Mathayo 6:9, 10) Ufalme wa Mungu utaletea wanadamu uhai udumuo milele katika ukamilifu kwenye dunia iliyo paradiso. Kisha maradhi ya moyo na ulemazo mwingine wote utaondolewa milele. Huo ulimwengu mpya upo mbele tu. Kwa kweli, maisha bora zaidi yangali yanakuja!—Ayubu 33:25; Isaya 35:5, 6; Ufunuo 21:3-5.
-