Kutambua Dalili na Kuchukua Hatua
DALILI za mshiko wa moyo zitokeapo, ni muhimu kutafuta msaada wa kitiba mara moja, kwani hatari ya kufa ni kubwa zaidi katika muda wa saa moja ya kwanza baada ya kupatwa na mshiko wa moyo. Matibabu ya haraka yaweza kuokoa misuli ya moyo isipate madhara yasiyoweza kurekebishwa. Kadiri misuli ya moyo inavyookolewa, ndivyo uwezo wa moyo kupiga kwa mafanikio uwavyo mkubwa baada ya kupatwa na mshiko wa moyo.
Hata hivyo, baadhi ya mishiko ya moyo haitambuliki, kwa kuwa haionyeshi dalili zozote zenye kuonekana. Katika hali kama hizo huenda mtu huyo asijue kwamba ana maradhi ya ateri ya moyo (CAD). Kwa kusikitisha, kwa wengine mshiko mkubwa wa moyo waweza kuwa ishara ya kwanza ya tatizo la moyo. Moyo uachapo kupiga, kikundi cha tiba ya dharura kisipoitwa mara moja na uhuishaji wa moyo na mapafu (CPR) usipofanywa na mtu aliye karibu, si rahisi kupona.
Kati ya wengi ambao wana dalili za CAD, Harvard Health Letter yaripoti, karibu nusu wataahirisha kutafuta msaada wa kitiba. Kwa nini? “Mara nyingi kwa sababu hawatambui dalili hizo ni za nini au hawazichukui kwa uzito.”
John,a ambaye ni mhasiriwa wa mshiko wa moyo na ambaye pia ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova, asihi hivi: “Unapohisi kwamba kuna kasoro, usikawie kupata tiba kwa hofu ya kwamba utaonekana unatilia chumvi ugonjwa wako. Karibu nife kwa sababu sikuchukua hatua haraka iwezekanavyo.”
Kile Kilichotendeka
John aeleza: “Mwaka mmoja na nusu kabla ya kupatwa na mshiko wa moyo, nilionywa na daktari kuhusu kolesteroli nyingi niliyokuwa nayo, ambayo ni kisababishi kikuu cha CAD. Lakini niliepuka suala hilo, kwa kuwa nilihisi kwamba nilikuwa mchanga—chini ya umri wa miaka 40—na mwenye afya nzuri. Nasikitika sana kwamba sikuchukua hatua wakati huo. Nikapata ishara nyinginezo za kuonya—kukosa pumzi nikijikakamua kidogo tu, maumivu ambayo niliyafikiria kuwa tatizo la umeng’enyaji wa chakula na, kwa miezi kadhaa kabla ya kupatwa na mshiko wa moyo nilikuwa mchovu mno. Nilifikiri kwamba nyingi za dalili hizo zilitokezwa na ukosefu wa usingizi na mkazo mwingi sana wa kazi. Siku tatu kabla ya kupatwa na mshiko wa moyo, nilihisi kile nilichokifikiria kuwa mpindano wa misuli katika kifua changu. Huo ulikuwa mshiko mdogo wa moyo ambao ulitangulia mshiko mkubwa ulionipata siku tatu baadaye.”
Maumivu au msongo wa kifua, ambayo huitwa angina, hutokea kwa karibu nusu ya wale ambao hupatwa na mshiko wa moyo. Wengine hupatwa na dalili za kukosa pumzi au uchovu na udhaifu, zikionyesha kwamba moyo haupati oksijeni ya kutosha kwa sababu ya kuzibwa kwa mshipa wa moyo. Ishara hizo za kuonya zapaswa kufanya mtu amwone daktari akachunguzwe moyo. Dakt. Peter Cohn asema: “Baada ya angina kutibiwa, hakuna uhakikisho kwamba mshiko wa moyo utazuiwa, lakini angalau uwezekano wa kupatwa na mshiko wa moyo hupunguka.”
Huo Mshiko
John aendelea kusema: “Siku hiyo tulikuwa tukienda kucheza softiboli. Nilipokuwa nikila hamburger na viazi vilivyokaangwa kwa chakula cha mchana, nilipuuza hali yangu ya kuhisi vibaya, kichefuchefu, na mbano wa sehemu ya juu ya mwili. Lakini tulipofika uwanja wa kucheza na kuanza kucheza, nilihisi kwamba kuna kasoro fulani. Nilizidi kuhisi vibaya alasiri hiyo.
“Mara kadhaa nililala chali kwenye benchi ya wachezaji, na kujaribu kunyoosha misuli ya kifua changu, lakini misuli hiyo iliendelea kunibana zaidi na zaidi. Nilipokuwa nikicheza, nilijiambia, ‘Labda nimeshikwa na mafua,’ kwa kuwa pindi fulani-fulani nilikuwa nahisi vibaya na udhaifu. Nilipokimbia, ilikuwa wazi kwamba nakosa pumzi. Nikalala kwenye benchi tena. Nilipoketi, nikawa sina shaka kwamba nilikuwa na tatizo baya sana. Nikamwambia mwana wangu James kwa sauti kuu: ‘Nahitaji kwenda hospitali SASA!’ Nikahisi kana kwamba kifua changu kilikuwa kimeporomoka. Maumivu yakawa mengi sana hivi kwamba sikuweza kuamka. Nikafikiria, ‘Huu hauwezi kuwa mshiko wa moyo? Nina umri wa miaka 38 tu!’”
Mwana wa John, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 15, aeleza: “Ilichukua dakika kadhaa tu kwa baba yangu kupoteza nguvu, hivi kwamba ikawa lazima abebwe kuingizwa katika gari. Rafiki yangu akaendesha gari huku akimwuliza baba maswali ili asipoteze fahamu. Hatimaye, baba hakujibu. ‘John!’ rafiki yangu akasema kwa sauti kubwa. Lakini bado baba yangu hakujibu. Kisha baba akashtuka katika kiti, akifurukuta na kutapika. Nikasema kwa sauti kwa kurudia-rudia: ‘Baba! Nakupenda! Tafadhali usife!’ Baada ya kufurukuta, mwili wake wote ukapoa kwenye kiti cha gari. Nikadhani amekufa.”
Hospitalini
“Tukakimbia ndani ya hospitali ili kupata msaada. Dakika mbili au tatu zilikuwa zimepita tangu nidhani baba amekufa, lakini nilitumaini angehuishwa. Kwa mshangao wangu, Mashahidi wa Yehova wenzetu wapatao 20 ambao walikuwa katika uwanja wa mchezo walikuwa katika chumba cha kungoja. Walinifanya nihisi nimefarijiwa na kupendwa, jambo lililosaidia sana wakati huo wenye huzuni. Karibu dakika 15 baadaye, daktari akaja na kueleza: ‘Tumefaulu kumhuisha baba yako, lakini amepata mshiko mkubwa wa moyo. Hatuna hakika kama ataishi.’
“Kisha akaniruhusu kumwona baba kifupi. Maneno ya baba yenye upendo kwa familia yetu yakanigusa sana hisia. Kwa maumivu mengi, alisema: ‘Nakupenda mwana wangu. Sikuzote ukumbuke kwamba Yehova ndiye mtu wa maana zaidi katika maisha zetu. Usiache kumtumikia, na umsaidie mama yako na ndugu zako wasiache kumtumikia. Tuna tumaini thabiti la ufufuo, na nikifa, nataka kuwaona nyote ninaporudi.’ Sote tulikuwa tukilia machozi ya upendo, hofu, na tumaini.”
Mke wa John, Mary, akafika muda wa saa moja baadaye. “Nilipoingia katika chumba cha utibabu wa dharura, daktari aliniambia: ‘Mume wako amepatwa na mshiko mkubwa wa moyo.’ Nikashtuka sana. Alieleza kwamba moyo wa John ulikuwa umetulizwa mara nane. Hatua hii ya dharura huhusisha kutumia volteji ya umeme kukomesha mapigo yenye fujo ya moyo ili urudie mapigo yao ya kawaida. Pamoja na kuhuishwa kwa moyo na mapafu, kuingizwa kwa oksijeni, na dawa za kuingizwa kupitia mishipa, tiba ya kutuliza moyo ni njia ya hali ya juu sana ya kuokoa uhai.
“Nilipomwona John, moyo wangu ukaugua. Alikosa rangi sana, na kulikuwa na neli nyingi na nyaya zilizounganisha mwili wake na mashine za kumchunguzia. Kwa ukimya, nilisali kwa Yehova anipe nguvu ya kuvumilia jaribio hili kwa ajili ya wana wetu watatu, nami nilisali nipate mwongozo wa kufanya maamuzi yenye hekima kuhusu yale ambayo yangekuwa mbele. Nilipokaribia kitanda cha John, nikafikiria, ‘Utamwambia nini mpendwa wako wakati kama huu? Je, kweli sisi tumejitayarishia hali kama hii ya kutisha uhai?’
“‘Mpenzi,’ John akasema, ‘wajua huenda nisiishi. Lakini ni muhimu kwamba wewe na wavulana wetu mdumishe uaminifu kwa Yehova kwa sababu karibuni mfumo huu utaisha na hakutakuwapo tena ugonjwa wala kifo. Nataka kuamka katika mfumo huo mpya na kukuona wewe na wavulana wetu huko.’ Machozi yakatutiririka.”
Daktari Aeleza
“Baadaye daktari aliniita kando na kueleza kwamba uchunguzi umeonyesha kwamba mshiko wa moyo wa John ulisababishwa na kuzibwa kabisa kwa ateri ya mbele ya upande wa kushoto inayoelekea chini. Pia ateri nyingine ilikuwa imezibwa. Daktari akaniambia kwamba ni lazima nifanye uamuzi kuhusu tiba ya John. Machaguo mawili yaliyopatikana ni dawa na angioplasty. Yeye alifikiri angioplasty ingekuwa afadhali, hivyo tukaichagua. Lakini madaktari hawakuahidi kama atapona, kwa kuwa wengi hawaponi mshiko wa moyo wa aina hiyo.”
Tiba ya angioplasty ni mbinu ya upasuaji ambayo kwayo katheta iliyowekewa puto huingizwa katika ateri ya moyo na kisha kuingiziwa hewa ili ifungue mzibo. Tiba hiyo hufanikiwa sana katika kurudisha mtiririko wa damu. Wakati mishipa kadhaa imezibwa sana, mara nyingi upasuaji wa kuunganisha mshipa mwingine na mshipa mkuu (bypass surgery) hupendekezwa.
Matazamio Yasiyo Mazuri
Baada ya kufanyiwa angioplasty, uhai wa John ukaendelea kuwa hatarini kwa muda wa saa 72 nyinginezo. Hatimaye, moyo wake ukaanza kupata nguvu baada ya lile pigo. Lakini, moyo wa John ulikuwa ukipiga kwa nusu tu ya uwezo wao wa zamani, na sehemu yao kubwa ilikuwa imekuwa kovu, hivyo ikatarajiwa sana kwamba angelemaa moyo.
Akikumbuka, John ahimiza: “Tuna wajibu kwa Muumba wetu, familia zetu, ndugu na dada zetu wa kiroho, na sisi wenyewe kutii maonyo na kutunza afya zetu—hasa tukiwa hatarini. Kwa kadiri kubwa, twaweza kusababisha furaha au huzuni. Ni juu yetu.”
Kisa cha John kilikuwa kibaya sana nacho kilihitaji hatua ya dharura. Lakini si kwamba wote wenye kuhisi uchungu kama wa kiungulia wakimbilie daktari. Lakini, aliyojionea John ni onyo, na wale wanaohisi kwamba wana dalili hizo wanapaswa kuchunguzwa.
Ni nini kiwezacho kufanywa ili kupunguza hatari ya kupatwa na mshiko wa moyo? Makala ifuatayo itajadili jambo hilo.
[Maelezo ya Chini]
a Majina yamebadilishwa katika makala hizi.
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
Dalili za Mshiko wa Moyo
• Hisi isiyostarehesha ya msongo, kubanwa, au maumivu kifuani ambayo hudumu zaidi ya dakika chache. Hisi hiyo yaweza kudhaniwa kuwa ni kiungulia chenye maumivu makali
• Maumivu ambayo yaweza kuenea kufikia—au kuwapo kwenye—utaya, shingo, mabega, mikono, viwiko, au mkono wa kushoto pekee
• Maumivu ya muda mrefu katika sehemu ya juu ya fumbatio
• Kukosa pumzi, kizunguzungu, kuzimia, kutokwa jasho, au kuhisi vibaya ukiguswa
• Uchovu—waweza kuhisiwa majuma kadhaa kabla ya kupatwa na mshiko wa moyo
• Kichefuchefu au kutapika
• Mashambulizi ya mara kwa mara ya angina ambayo hayasababishwi na kujikakamua
Dalili hutofautiana kutoka zile zilizo hafifu hadi zile zenye nguvu nazo hazitokei zote katika kila mshiko wa moyo. Lakini dalili zozote kadhaa zitokeapo pamoja, tafuta msaada haraka sana. Hata hivyo, katika visa fulani hakuna dalili; hivyo huitwa mishiko ya moyo isiyo na dalili.
[Sanduku katika ukurasa wa 7]
Hatua za Kuchukuliwa ili Kuokoa Uhai
Wewe au mtu mwingine unayemjua ukiwa na dalili za mshiko wa moyo:
• Tambua dalili.
• Acha chochote unachofanya na uketi au ulale chini.
• Dalili zikidumu kwa zaidi ya dakika chache, piga simu ya msaada wa dharura. Mwambie unayeongea naye kwamba unashuku una mshiko wa moyo, na umpe habari zinazohitajika ili waweze kukupata.
• Ikiwa unaweza kumpeleka mgonjwa kwenye chumba cha tiba ya dharura haraka iwezekanavyo, wewe mwenyewe ukiendesha gari, fanya hivyo. Ukifikiri unapata mshiko wa moyo, omba mtu akupeleke huko.
Unapongoja kikundi cha tiba ya dharura:
• Legeza nguo zilizobana, kutia ndani mshipi au tai. Msaidie huyo mgonjwa astarehe, ukimwekea mito ikiwa ni lazima.
• Dumisha utulivu, iwe ni wewe uliye mgonjwa au uwe msaidiaji wake. Wasiwasi waweza kuongeza uwezekano wa kupatwa na badiliko katika pigo la moyo, ambalo laweza kuua. Sala yaweza kuwa msaada wenye kuimarisha katika kudumisha utulivu.
Mgonjwa akionekana kama ameacha kupumua:
• Kwa sauti kubwa uliza, “Waweza kunisikia?” Ikiwa haitikii, ikiwa moyo haupigi, na ikiwa mgonjwa hapumui, anza kumhuisha moyo na mapafu (CPR).
• Kumbuka hatua tatu za msingi za CPR:
1. Inua kidevu cha huyo mgonjwa, ili njia za hewa zifunguliwe.
2. Njia za hewa zikiwa wazi, huku ukiziba pua ya mgonjwa, puliza polepole mara mbili katika mdomo mpaka kifua kiinuke.
3. Sukuma mara 10 hadi 15 katikati ya kifua kati ya chuchu ili kusukuma damu kutoka kwa moyo na kifua. Kila sekunde 15, rudia kupuliza mara mbili na kufuatia na misukumo 15 mpaka mipwito ya moyo irudi na aanze kupumua tena au mpaka kikundi cha tiba ya dharura kifike.
Hiyo CPR inapaswa kufanywa na mtu ambaye amezoezwa. Lakini kama hakuna mtu ambaye amezoezwa, “CPR yoyote ni afadhali kuliko kukosa kuifanya,” asema Dakt. R. Cummins, mkurugenzi wa utunzi wa dharura ya moyo. Mtu asipoanzisha hatua hizo, uwezekano wa kupona ni mdogo sana. Hiyo CPR huendeleza uhai wa mtu mpaka msaada ufike.
[Picha katika ukurasa wa 5]
Matibabu ya haraka baada ya mshiko wa moyo yanaweza kuokoa na kupunguza madhara kwa moyo