Maradhi ya Moyo—Tisho kwa Uhai
KILA mwaka mamilioni ya wanaume na wanawake ulimwenguni pote hupatwa na mishiko ya moyo. Wengi hupona wakiwa na athari ndogo. Wengine hawaponi. Kwa wengine zaidi moyo huharibika sana hivi kwamba “kuna shaka kama wanaweza kurudia utendaji muhimu,” mtaalamu wa moyo Peter Cohn asema, akiongezea: “Basi, ni lazima kutibu dalili za mishiko ya moyo haraka iwezekanavyo.”
Moyo ni msuli unaopiga damu iende kotekote mwilini. Katika mshiko wa moyo (myocardial infarction), sehemu ya misuli ya moyo hufa inapokosa damu. Ili udumu ukiwa wenye afya, moyo huhitaji oksijeni na lishe nyinginezo ambazo hubebwa kwa damu. Moyo hupata hizo kupitia ateri za moyo, ambazo zimezingira moyo.
Maradhi yaweza kuathiri sehemu yoyote ya moyo. Hata hivyo, maradhi ya kawaida zaidi ni yale ya kudhuru kichini-chini yapatayo mishipa ya moyo ambayo huitwa atherosclerosis. Maradhi hayo yatokeapo, mkusanyo wa mafuta, hukua katika kuta za ateri. Baada ya kipindi fulani, mkusanyo huo waweza kuongezeka na kuwa mgumu, kujaa ndani ya ateri, na kuziba mtiririko wa damu inayoenda moyoni. Ni maradhi haya ya ateri ya moyo (CAD) ambayo husababisha mishiko mingi sana ya moyo.
Kuziba kwa ateri moja au zaidi huharakisha shambulio moyo unapopungukiwa oksijeni. Hata katika ateri ambazo hazijazibwa sana, mkusanyo wa mafuta waweza kuvunjika vipande-vipande na kufanyiza mgando wa damu (thrombus). Ateri zenye maradhi pia huathiriwa kwa urahisi na mpindano. Mgando wa damu waweza kujifanyiza mahali pa mpindano, ukitokeza kemikali ambayo huzidi kubana ukuta wa ateri, jambo ambalo hutokeza mshiko wa moyo.
Misuli ya moyo inapokosa oksijeni kwa muda fulani, tishu zilizo kandokando zaweza kupatwa na madhara. Tofauti na tishu nyinginezo, misuli ya moyo haijifanyizi upya. Kadiri ya urefu wa mshiko wa moyo, ndivyo moyo uzidivyo kupatwa na madhara na ndivyo uwezekano wa kufa uongezekavyo. Mfumo wa mawasiliano wa moyo ukipatwa na madhara, pigo la kawaida la moyo laweza kuvurugika na moyo waweza kuanza kutetemeka-tetemeka sana. Katika badiliko kama hilo la pigo la moyo, moyo hupoteza uwezo wao wa kupiga damu kwa njia ifaayo. Kwa muda wa dakika kumi ubongo hufa na kifo hutokea.
Hivyo, tiba ya mapema ya wanatiba waliozoezwa ni muhimu. Hiyo yaweza kuokoa moyo usiendelee kupatwa na madhara, yaweza kuzuia au kutibu mabadiliko-badiliko katika pigo la moyo, au hata kuokoa uhai wa mtu.