Hatari Hiyo Inaweza Kupunguzwaje?
MARADHI ya ateri ya moyo (CAD) yameshirikishwa na mambo kadhaa ya urithi, mazingira, na mtindo-maisha. Maradhi ya ateri ya moyo na mshiko wa moyo waweza kusababishwa na hatari zinazohusiana na moja au zaidi ya mambo hayo, hatari hizo zikichukua miaka, au hata miongo kujikuza.
Umri, Jinsia, na Urithi
Kadiri umri uzidivyo kuongezeka ndivyo hatari ya kupatwa na mshiko wa moyo izidivyo kuongezeka. Karibu asilimia 55 ya mishiko ya moyo hutukia miongoni mwa watu wenye umri unaozidi miaka 65. Asilimia ipatayo 80 ya wale ambao hufa kutokana na mishiko ya moyo ni wenye umri wa miaka 65 au zaidi.
Wanaume wenye umri ulio chini ya miaka 50 wamo hatarini kuliko wanawake wa rika hilo. Baada ya hedhi kukoma, hatari ya mwanamke kupatwa na mshiko wa moyo huongezeka kwa sababu ya upungufu mkubwa wa homoni ya estrojeni yenye kuwakinga. Kulingana na makadirio fulani, tiba ya kurudisha estrojeni yaweza kupunguza hatari za maradhi ya moyo katika wanawake kwa asilimia 40 au zaidi, ingawa inaweza kuongeza hatari ya kupatwa na kansa fulani.
Urithi waweza kuchangia sana. Wale ambao wazazi wao walipatwa na mshiko wa moyo wakiwa hawajafikia umri wa miaka 50 wamo hatarini zaidi ya kupatwa na mshiko wa moyo. Hata kama wazazi walipatwa na mshiko wa moyo baada ya umri wa miaka 50, bado kuna hatari zaidi. Ikiwa kuna historia ya matatizo ya moyo katika familia, yaelekea watoto watasitawisha matatizo kama hayo.
Suala la Kolesteroli
Kolesteroli, ambayo ni aina ya shahamu, ni muhimu kwa uhai. Hiyo hutengenezwa katika ini, nayo damu huibeba na kuipeleka katika chembe, ikiwa katika molekuli ziitwazo lipoprotini. Aina mbili za lipoprotini ni zile zenye msongamano wa chini (kolesteroli ya LDL) na zile zenye msongamano wa juu (kolesteroli ya HDL). Kolesteroli yaweza kuwa kisababishi hatari cha CAD wakati ambapo kuna kolesteroli nyingi mno ya LDL katika damu.
Lipoprotini ya msongamano wa juu hufikiriwa kuwa ina fungu la kulinda kwa kuondoa kolesteroli kutoka kwenye tishu na kuirudisha kwenye ini ambako hiyo hubadilishwa na kuondolewa katika mwili. Ikiwa LDL ni nyingi na HDL ni chache, kuna uwezekano mkubwa wa kupatwa na maradhi ya moyo. Kupunguza kiwango cha LDL kwaweza kupunguza sana hatari. Kuchunga aina ya mlo unaokula ni njia kubwa katika matibabu haya, na mazoezi yaweza kusaidia. Dawa mbalimbali zaweza kusaidia, lakini baadhi yazo zina athari mbaya.a
Mlo usio na kolesteroli nyingi wala mafuta mengi ndio hupendekezwa. Kubadili vyakula vyenye mafuta mengi, kama vile siagi, kwa vyakula visivyo na mafuta mengi, kama mafuta ya canola au mafuta ya zeituni, kwaweza kupunguza LDL na kuhifadhi HDL. Kwa upande mwingine, jarida American Journal of Public Health lasema kwamba mafuta ya mboga, yaliyotiliwa hidrojeni au kutiliwa hidrojeni chache, ambayo hupatikana katika siagi nyingi na bidhaa nyingi za mafuta ya mboga yaweza kuongeza LDL na kupunguza HDL. Kupunguza kula nyama zenye mafuta mengi na kula nyama za kuku au bata mzinga zisizo na mafuta mengi hupendekezwa pia.
Uchunguzi mbalimbali umeonyesha kwamba vitamini E, beta-karotene, na vitamini C zaweza kupunguza mafuta mengi ndani ya ateri za wanyama. Uchunguzi mmoja ulikata kauli kwamba hizo zaweza pia kupunguza visa vya mshiko wa moyo katika wanadamu. Kila siku kula mboga na matunda yenye kiasi kingi cha beta-karotene na karotenoidi nyinginezo pamoja na vitamini C, kama vile nyanya, mboga yenye majani makubwa ya kijani-cheusi, pilipili, karoti, viazi vitamu, matikiti, zaweza kulinda kwa kadiri fulani dhidi ya CAD.
Pia vitamini B6 na magnesi zasemwa kuwa zafaa. Nafaka kama vile shayiri na oti na vilevile maharagwe, dengu, na mbegu fulani zaweza kusaidia. Kwa kuongezea, inafikiriwa kwamba kula samaki kama yule nyama-nyekundu, makareli, heringi, au tuna angalau mara mbili kwa juma kwaweza kupunguza hatari ya kupatwa na CAD, kwa kuwa hizi zina kiasi kingi cha omega-3 na asidi nyingi zisizo na mafuta mengi.
Mtindo-Maisha wa Kukaakaa
Watu ambao hukaakaa wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupatwa na mshiko wa moyo. Wao hutumia sehemu kubwa ya siku zao bila kuwa watendaji nao hawafanyi mazoezi kwa ukawaida. Mishiko ya moyo mara nyingi hutukia katika watu hawa baada ya kufanya utendaji wa kujikakamua kama vile kulima kwa bidii, kukimbia-kimbia, kuinua vyuma vizito, au kuondoa theluji kwa koleo. Lakini hatari ya kupatwa na mshiko wa moyo hupunguka kati ya watu ambao hufanya mazoezi kwa ukawaida.
Kutembea kwa kasi kwa muda wa dakika 20 hadi 30 mara tatu au mara nne kwa juma kwaweza kupunguza hatari ya kupatwa na mshiko wa moyo. Mazoezi ya kawaida huboresha uwezo wa moyo kupiga, husaidia kupoteza uzito, na yaweza kupunguza viwango vya kolesteroli na kupunguza msongo wa damu.
Msongo wa Juu wa Damu, Uzito wa Kupita Kiasi, na Ugonjwa wa Kisukari
Msongo wa juu wa damu waweza kudhuru kuta za ateri na kuwezesha kolesteroli ya LDL kuingia ndani ya kuta za ateri na kufanyiza mkusanyo wa mafuta. Mkusanyo huo uongezekapo, kunakuwa na ukinzani kwa mtiririko wa damu na hivyo msongo wa damu huongezeka.
Msongo wa damu wapaswa kuchunguzwa kwa ukawaida, kwa kuwa huenda dalili yoyote ya tatizo hilo isiweze kuonekana. Kwa kila upungufu wa msongo wakati moyo umetulia, hatari ya mshiko wa moyo yaweza kupunguzwa kwa asilimia 2 hadi 3. Tiba ya kupunguza msongo wa damu yaweza kusaidia. Kuchunga mlo, na katika hali fulani kupunguza ulaji wa chumvi, pamoja na kufanya mazoezi kwa ukawaida ya kupunguza uzito kwaweza kusaidia kudhibiti msongo wa juu wa damu.
Uzito kupita kiasi huendeleza msongo wa juu wa damu na kutokeza kasoro za mafuta. Kuepuka unene kupita kiasi au kuutibu ni njia ya msingi ya kuzuia kisukari. Kisukari huzidisha CAD na kuongeza hatari za kupatwa na mshiko wa moyo.
Kuvuta Sigareti
Kuvuta sigareti ni kisababishi kikuu cha usitawi wa CAD. Katika Marekani, huko husababisha kwa njia ya moja kwa moja karibu asilimia 20 ya vifo vitokezwavyo na maradhi yote ya moyo na karibu asilimia 50 ya mishiko ya moyo katika wanawake walio chini ya umri wa miaka 55. Kuvuta sigareti huongeza msongo wa damu na kuingiza kemikali zenye sumu, kama vile nikotini na kaboni monoksidi, katika mkondo wa damu. Kemikali hizo nazo hudhuru ateri.
Wavutaji wa sigareti pia huhatarisha wale ambao huvuta moshi wao. Uchunguzi waonyesha kwamba watu wasiovuta sigareti wanaoishi na wavutaji wa sigareti wana hatari zaidi ya kupatwa na mshiko wa moyo. Hivyo, kwa kuacha kuvuta sigareti, mtu aweza kupunguza hatari kwake mwenyewe na hata anaweza kuokoa uhai wa wapendwa wake wasiovuta sigareti.
Mkazo
Wale wenye CAD wakiwa chini ya mkazo mkali wa kihisia moyo au wa kiakili, wao hukabili hatari kubwa zaidi ya kupatwa na mshiko wa moyo na kifo cha ghafula kuliko watu ambao wana ateri zenye afya. Kulingana na uchunguzi mmoja, mkazo waweza kufanya ateri zenye kujaa mafuta zifinyae, na hilo hupunguza mtiririko wa damu kufikia asilimia 27. Mifinyo mikubwa ilionekana hata katika ateri zenye maradhi madogo. Uchunguzi mwingine ulidokeza kwamba mkazo mkali waweza kutokeza hali zinazoweza kufanya mafuta katika kuta za mishipa kupasuka, na kutokeza mshiko wa moyo.
Gazeti Consumer Reports on Health lasema: “Baadhi ya watu huonekana kupitia maisha wakiwa na mtazamo mbaya. Wao ni wenye madharau, ni wenye hasira, nao hukasirika kwa urahisi. Ingawa wengi wa watu huachilia uchokozi kidogo, watu wakali huitikia kupita kiasi.” Hasira ya daima na uhasama huinua msongo wa damu, huongeza mipigo ya moyo, na kuchochea ini kuacha kolesteroli katika mkondo wa damu. Hilo huharibu ateri za moyo na kuchangia kusababisha CAD. Hasira hufikiriwa kuongeza maradufu hatari ya kupatwa na mshiko wa moyo, na hiyo hudumu kwa angalau muda wa saa mbili. Ni nini kinachoweza kusaidia?
Kulingana na The New York Times, Dakt. Murray Mittleman alisema kwamba watu ambao walijaribu kudumisha utulivu katika hali za kuamsha hisia moyo waweza kupunguza hatari ya kupatwa na mshiko wa moyo. Maneno hayo yafanana sana na maneno yaliyorekodiwa katika Biblia karne nyingi zilizopita: “Moyo mtulivu ni uhai wa mwili.”—Mithali 14:30, NW.
Mtume Paulo alijua kile kilichomaanishwa na kuwa chini ya mkazo. Yeye alisema juu ya mahangaiko ambayo yalimkumba kila siku. (2 Wakorintho 11:24-28) Lakini alipata msaada wa Mungu akaandika: “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”—Wafilipi 4:6, 7.
Ingawa kuna mambo mengine yahusikayo na matatizo ya moyo, yale yaliyozungumzwa hapa yaweza kusaidia kutambua hatari ili mtu aweze kuchukua hatua ifaayo. Hata hivyo, wengine wamejiuliza jinsi hali ilivyo kwa wale ambao ni lazima waishi na matokeo ya mshiko wa moyo. Mtu anaweza kupona kwa kadiri gani?
[Maelezo ya Chini]
a Amkeni! halipendekezi matibabu ya kitiba, ya mazoezi, au ya ulaji lakini linatoa habari zilizofanyiwa utafiti vizuri. Ni lazima kila mtu aamue mwenyewe kile atakachofanya.
[Picha katika ukurasa wa 9]
Kuvuta sigareti, kukasirika upesi, kula vyakula vyenye mafuta, na kuishi maisha ya kukaakaa huongeza hatari ya kupatwa na mshiko wa moyo