Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 6/22 kur. 7-10
  • Ulaji Wako—Je, Waweza Kukuua?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ulaji Wako—Je, Waweza Kukuua?
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ulaji Wako na Maradhi ya Moyo
  • Fungu la Kolesteroli
  • Kolesteroli Iliyo Katika Damu na Ulaji
  • Mafuta na Kolesteroli
  • Sababu Inayofanya Upaswe Kupunguza Mafuta na Kolesteroli
  • Kansa na Ulaji
  • Hatari Hiyo Inaweza Kupunguzwaje?
    Amkeni!—1996
  • Afya Njema—Waweza Kuifanyia Nini?
    Amkeni!—1990
  • Kuchagua Mlo Wenye Afya
    Amkeni!—1997
  • Je, Kahawa Inaongeza Kiasi cha Kolesteroli Mwilini Mwako?
    Amkeni!—2000
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 6/22 kur. 7-10

Ulaji Wako—Je, Waweza Kukuua?

“Ateri zako za moyo zimezibika vibaya sana, zimezibika kwa asilimia 95 hivi . . . Wakati huu yaelekea kwamba utapatwa na mshiko wa moyo muda fulani usio mbali sana.”

JOE mwenye umri wa miaka 32 hakuamini maneno hayo ya mtaalamu wa moyo ambaye alimchunguza ili kujua ni nini kilichokuwa kisababishi cha maumivu yake ya kifua. Karibu nusu ya wale watakaokufa kwa maradhi ya moyo hata hawajui kama wanayo.

Lakini ni nini kilichosababisha hali ya Joe? ‘Kwa miaka 32 nilikula chakula cha kawaida cha Wamarekani “ulaji uliojaa nyama na bidhaa za maziwa,”’ aomboleza Joe. ‘Kwa namna fulani sikuchukua kwa uzito uhakika wa kwamba ulaji wa Wamarekani ni wenye hatari kwa afya yangu.’

Ulaji Wako na Maradhi ya Moyo

Kulikuwa na kasoro gani na ulaji wa Joe? Kimsingi, ulikuwa na kolesteroli na mafuta mengi mno, hasa mafuta kifu. Tangu ujana wake, Joe alikuwa akijiweka katika hatari ya kupatwa na maradhi ya ateri za moyo kwa karibu kila kijiko cha chakula. Kwa hakika, ulaji wenye mafuta mengi, unahusianishwa na visababishi vitano kati ya visababishi kumi vya kifo katika Marekani. Kisababishi cha kwanza ni maradhi ya ateri za moyo.

Uhusiano kati ya ulaji na maradhi ya moyo waonekana katika uchunguzi uliofanywa katika nchi saba kwa wanaume 12,000 wenye umri wa miaka 40 hadi 49. Tofauti hizo kubwa zatokeza ufahamu wa ndani hasa. Uchunguzi huo ulionyesha kwamba wanaume wa Finland—wanaokula asilimia 20 ya kalori zao zikiwa mafuta kifu—walikuwa na viwango vya juu vya kolesteroli iliyo katika damu, ilhali wanaume Wajapani—wanaokula asilimia 5 ya kalori zao zikiwa mafuta kifu—walikuwa na viwango vya chini vya kolesteroli iliyo katika damu. Na wanaume wa Finland walikuwa hatarini mwa kupatwa na mshiko wa moyo mara sita kuliko wanaume Wajapani!

Hata hivyo, maradhi ya ateri za moyo si nadra tena katika Japani. Katika miaka kadhaa ambayo imepita, vyakula vya kutayarishwa haraka vya mtindo wa nchi za Magharibi vimekuja kupendwa na wengi huko, utumizi wa mafuta ya wanyama umeongezeka kwa asilimia 800. Sasa, wavulana Wajapani wana viwango vya juu vya kolesteroli iliyo katika damu kuliko wavulana Wamarekani wa umri huohuo! Kwa wazi, mafuta na kolesteroli iliyo katika mlo zaonwa kuwa visababishi vya hali yenye kutisha uhai, hasa maradhi ya moyo.

Fungu la Kolesteroli

Kolesteroli ni kitu cheupe kilicho kama nta ambacho ni muhimu kwa uhai. Hicho hupatikana katika chembe za wanadamu na wanyama wote. Ini letu hutokeza kolesteroli, nayo pia hupatikana kwa viwango tofauti-tofauti katika vyakula tulavyo. Damu hupeleka kolesteroli hadi kwenye chembe ikiwa katika molekuli ziitwazo lipoprotini, ambazo huwa na kolesteroli, mafuta, na protini. Aina mbili za lipoprotini ambazo hubeba kiasi kikubwa cha kolesteroli iliyo katika damu ni lipoprotini zisizo na protini nyingi (LDL) na lipoprotini zilizo na protini nyingi (HDL).

Aina za LDL zina kolesteroli nyingi. Zinapozunguka katika mkondo wa damu, hizo huingia katika chembe kupitia vipokezi vya LDL kwenye kuta za chembe na humeng’enyushwa ili zitumiwe na chembe. Chembe nyingi mwilini zina vipokezi kama hivyo, nazo huchukua baadhi ya LDL. Lakini ini limebuniwa kwa njia ya kwamba asilimia 70 ya kuondoshwa kwa LDL kutoka kwenye mkondo wa damu na vipokezi vya LDL hutukia hapo.

Kwa upande ule mwingine, HDL ni molekuli zinazohitaji sana kolesteroli. Zinapopita katika mkondo wa damu, hizo hufyonza kolesteroli ya ziada na kuisafirisha hadi kwenye ini. Ini humeng’enyusha kolesteroli hiyo na kuiondosha kutoka mwilini. Hivyo mwili umebuniwa kwa njia ya ajabu utumie kolesteroli unayohitaji na kuondosha iliyobaki.

Tatizo hutokea wakati kuna LDL nyingi mno katika damu. Hizo huongeza uwezekano wa ujengekaji wa utando kwenye kuta za ateri. Ujengekaji wa utando utokeapo, ateri huwa nyembamba na kiwango cha damu ibebayo oksijeni iwezayo kupita katika ateri hizo hupungua. Hali hii huitwa atherosclerosis. Utaratibu huo huendelea polepole na bila kuonyesha dalili zozote, ukichukuwa miongo ili kudhihirisha dalili ziwezazo kutambuliwa. Dalili moja ni maumivu ya kifuani, kama yale yaliyompata Joe.

Ateri ya moyo izibikapo kabisa, mara nyingi kwa mgando wa damu, sehemu ya moyo inayopokea damu kutoka kwa ateri hiyo hufa. Tokeo ni kufa kwa ghafula kwa tishu ya tabaka ya katikati ya ukuta wa moyo—hali ijulikanayo vema kuwa mshiko wa moyo. Hata kuzibika nusu kwa ateri ya moyo kwaweza kuongoza kwenye kifo cha tishu ya moyo, hali ambayo huenda isitokeze dalili kama vile kutohisi vizuri kimwili. Kuzibika kwa ateri katika sehemu nyinginezo za mwili kwaweza kusababisha mishtuko ya akili, uozo wa miguu kutokana na ukosefu wa damu, na hata kukosa kwa figo kufanya kazi.

Si ajabu kwamba LDL huitwa kolesteroli mbaya, na HDL kolesteroli nzuri. Ikiwa upimaji unaonyesha kwamba kuna kiwango cha juu cha LDL katika damu, au kiwango cha chini cha HDL, hatari ya kupatwa na maradhi ya moyo ni kuu.a Mara nyingi upimaji sahili wa damu utaonyesha hatari iliyopo muda mrefu kabla ya mtu kupatwa na dalili za wazi kama vile, maumivu kifuani. Basi, ni jambo la maana kudhibiti kiwango chako cha kolesteroli iliyo katika damu. Ebu sasa tuone jinsi ulaji wako uwezavyo kuathiri kiwango hicho.

Kolesteroli Iliyo Katika Damu na Ulaji

Kolesteroli ni sehemu ya kiasili ya chakula kitokanacho na wanyama. Nyama, mayai, samaki, kuku, na bidhaa za maziwa zote huwa na kolesteroli. Kwa upande ule mwingine, vyakula vitokanavyo na mimea, havina kolesteroli.

Mwili hutokeza kolesteroli yote inayohitajiwa, kwa hiyo kolesteroli iliwayo kutoka kwa chakula ni ya ziada. Nyingi ya kolesteroli yetu iliyo katika chakula hufikia mwisho kwenye ini. Kwa kawaida, kolesteroli iliyo katika chakula iingiapo katika ini, ini huichakata na kupunguza utokezaji walo lenyewe wa kolesteroli. Utaratibu huo husawazisha kiwango cha kolesteroli katika damu.

Hata hivyo, ni nini hutukia ikiwa mlo umejaa sana kolesteroli hivi kwamba haiwezi kuchakatwa haraka na ini? Uwezekano wa kolesteroli kuingia moja kwa moja katika chembe za ukuta wa ateri huongezeka. Hilo likitokea, utaratibu wa atherosclerosis hutukia. Hali huwa hatari hasa ikiwa mwili waendelea kufanyiza kiwango hichohicho cha kolesteroli licha ya kiwango kinacholiwa cha kolesteroli iliyo katika chakula. Katika Marekani, mtu 1 kati ya watu 5 ana hilo tatizo.

Basi, ni mwendo wa hekima kupunguza kula kolesteroli iliyo katika chakula. Lakini kisehemu kingine cha chakula chetu kina athari kubwa hata zaidi kwenye kiwango cha kolesteroli iliyo katika damu—mafuta kifu.

Mafuta na Kolesteroli

Mafuta huwa ya vikundi viwili: mafuta kifu na yasiyo kifu. Mafuta yasiyo kifu yanaweza kuwa ama monounsaturated au polyunsaturated. Mafuta yasiyo kifu yanakufaa kuliko yaliyo kifu, kwa kuwa kula mafuta kifu huongeza kiwango cha kolesteroli katika damu. Mafuta kifu hufanya hivyo kwa njia mbili: Hayo husaidia kufanyiza kolesteroli zaidi katika ini, nayo hukandamiza vipokezi vya LDL kwenye chembe za ini, yakipunguza uharaka wa kuondolewa kwa LDL kutoka kwenye damu.

Mafuta kifu hupatikana hasa katika vyakula vitokanavyo na wanyama, kama vile siagi, kiini cha yai, mafuta ya nguruwe, maziwa, aiskrimu, nyama, na kuku. Hayo pia yamejaa katika chokoleti, nazi na mafuta yazo, mafuta ya mboga, na mawese. Mafuta kifu huganda katika halijoto ya chumba.

Kwa upande ule mwingine, mafuta yasiyo kifu, huwa ya kiowevu katika halijoto ya chumba. Vyakula vilivyo na mafuta aina ya monounsaturated na polyunsaturated yaweza kusaidia kupunguza kiwango cha kolesteroli yako katika damu ikiwa utavitumia badala ya vyakula vyenye mafuta kifu.b Ingawa mafuta aina ya polyunsaturated, yaliyo ya kawaida sana katika mafuta ya nafaka na mafuta ya alizeti, hupunguza kolesteroli nzuri na mbaya, mafuta aina ya monounsaturated, yaliyo mengi katika mafuta ya mzeituni na mafuta ya canola, hupunguza kolesteroli mbaya tu bila kuathiri kolesteroli nzuri.

Bila shaka mafuta ni sehemu muhimu ya ulaji wetu. Kwa mfano, bila mafuta, hakuwezi kuwapo ufyonzaji wa vitamini A, D, E, na K. Hata hivyo mahitaji ya mafuta ya mwili ni machache sana. Mahitaji hayo hutimizwa kwa kula mboga, maharagwe, nafaka, na matunda. Kwa hiyo kupunguza ulaji wa mafuta kifu hakunyimi mwili virutubisho vihitajiwavyo.

Sababu Inayofanya Upaswe Kupunguza Mafuta na Kolesteroli

Je, ulaji uliojaa mafuta na kolesteroli sikuzote utaongeza kolesteroli iliyo katika damu? Si lazima iwe hivyo. Thomas, aliyetajwa katika makala ya kwanza, aliamua kupimwa damu baada ya kuhojiwa na Amkeni! Matokeo yalifunua kwamba viwango vyake vya kolesteroli vilikuwa mnamo mipaka inayofaa. Ini lake bila shaka liliweza kusawazisha kiwango cha kolesteroli.

Hata hivyo, hilo halimaanishi kwamba Thomas hayuko hatarini. Chunguzi za hivi majuzi zaonyesha kwamba kolesteroli itokanayo na chakula yaweza kuathiri hatari ya maradhi ya ateri za moyo bila hata kuathiri kolesteroli iliyo katika damu. “Vyakula vyenye kolesteroli nyingi hutokeza maradhi ya moyo hata katika watu walio na kiwango cha kolesteroli ya chini iliyo katika damu,” asema Dakt. Jeremiah Stamler, wa Chuo Kikuu cha Northwestern. “Na hiyo ndiyo sababu kula kolesteroli chache kwapasa kuwa jambo la kuhangaikiwa na watu wote, haidhuru kiwango chao cha kolesteroli iliyo katika damu ni kipi.”

Pia kuna jambo la mafuta katika ulaji. Mafuta mengi sana katika damu, yawe ni mafuta kifu au yasiyo kifu katika chakula, husababisha chembe nyekundu za damu kugandamana pamoja. Damu iliyokuwa nzito jinsi hiyo haipiti katika mishipa midogo ya damu, ikisababisha tishu kutopata virutubisho vinavyohitajika. Chembe zilizogandamana pamoja zikisonga katika ateri pia hukatiza msambazo wa oksijeni kwa kuta za ateri, ikisababisha nyuso za ateri ziharibike, ambapo utando waweza kwa urahisi kuanza kujifanyiza. Lakini kuna hatari nyingine ya kula viwango vyenye kupita kiasi vya mafuta.

Kansa na Ulaji

“Mafuta yote—kifu na yasiyo kifu—yanahusika katika ukuzi wa namna fulani za chembe za kansa,” asema Dakt. John A. McDougall. Uchunguzi mmoja wa matukio ya kimataifa ya kansa ya koloni na puru na kansa ya matiti ulionyesha tofauti zenye kutia hofu kati ya mataifa ya Magharibi, ambapo milo imejaa mafuta, na mataifa yanayoendelea. Kwa kielelezo, katika Marekani, kansa ya koloni na puru ndiyo kansa ya pili ya kawaida kwa wote wanaume na wanawake, huku kansa ya matiti ikiwa ya kawaida zaidi kwa wanawake.

Kulingana na Shirika la Kansa la Marekani, vikundi vya watu wanaohamia nchi iliyo na matukio mengi ya kansa hatimaye hupatwa na kansa ya nchi hiyo, kutegemea urefu wa wakati wanaochukua kujibadili kwa mtindo-maisha na ulaji mpya. “Wajapani wanaohamia Hawaii,” chaonelea kitabu cha mapishi cha shirika hilo la kansa, “wanapatwa na namna ya kansa ya Magharibi: wanapatwa sana na kansa ya koloni na matiti, hawapatwi sana na kansa ya tumbo—jambo ambalo liko kinyume cha namna ya kansa ya Japani.” Kwa wazi, kansa inahusiana na ulaji.

Ikiwa mlo wako umejaa mafuta kamili, mafuta kifu, kolesteroli, na kalori, wahitaji kufanya mabadiliko. Ulaji mzuri waweza kuongoza kwenye afya njema na waweza hata kuepusha athari mbaya za ulaji mbaya. Mtu afikiriapo machaguo kama vile upasuaji wa moyo wenye maumivu, ambao mara nyingi hugharimu dola 40,000 au zaidi, kwa hakika kuchagua ulaji mzuri ni jambo lifaalo.

Kwa kuchagua kwa busara unachokula, waweza kupunguza uzito, kuboresha jinsi unavyohisi, na kujisaidia kuepuka au kutangua maradhi fulani. Madokezo kuhusu hilo yamezungumziwa katika makala ifuatayo.

[Maelezo ya Chini]

a Kolesteroli hupimwa katika miligramu kwa desilita. Kiwango kifaacho cha kolesteroli ya jumla—jumla ya LDL, HDL, na kolesteroli katika lipoprotini nyinginezo na katika damu—ni chini ya miligramu 200 kwa desilita. Kiwango cha HDL cha miligramu 45 kwa desilita au juu huonwa kuwa kizuri.

b Miongozo ya Mlo ya 1995 kwa Ajili ya Wamarekani hupendekeza ulaji wa jumla wa mafuta usiozidi asilimia 30 ya kalori za kila siku na hupendekeza kupunguza mafuta kifu kufikia chini ya asilimia 10 za kalori. Upungufu wa asilimia 1 wa ulaji wa kalori wa mafuta kifu kwa kawaida husababisha kushuka kwa kiwango cha kolesteroli iliyo katika damu kwa miligramu 3 kwa desilita.

[Picha katika ukurasa wa 8]

Sehemu-mtambuko ya ateri za moyo: (1) zikiwa wazi kabisa, (2) zikiwa zimezibika nusu, (3) zikiwa zimezibika karibu kabisa

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki