Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g90 5/8 kur. 7-12
  • Afya Njema—Waweza Kuifanyia Nini?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Afya Njema—Waweza Kuifanyia Nini?
  • Amkeni!—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Miongozo kwa Maisha Yenye Afya
  • Hisiamoyo na Mtazamio Maishani
  • Mazoea na Uzoelevu
  • Wakati Magonjwa Yote Yataisha
  • Jinsi ya Kulinda Afya Yako
    Amkeni!—1999
  • Ulaji Wako—Je, Waweza Kukuua?
    Amkeni!—1997
  • Je, Unafanya Mazoezi ya Kutosha?
    Amkeni!—2005
  • Sisi Ni Wenye Afya Kiasi Gani?
    Amkeni!—1990
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1990
g90 5/8 kur. 7-12

Afya Njema—Waweza Kuifanyia Nini?

“KWA sehemu likiwa ni tokeo la mafanikio ya kutazamisha ya tiba ya ki-siku-hizi, mtazamo fulani umeenea kwenye sehemu nyingi za ulimwengu kwamba afya ni kitu ambacho madaktari huandalia watu, badala ya kuwa kitu ambacho jumuiya na watu mmoja mmoja hujipatia wenyewe.” Ndivyo alivyoandika Dakt. Halfdan Mahler katika World Health, lile jarida rasmi la Tengenezo la Afya Ulimwenguni.

Bila shaka, madaktari na hospitali huchangia sana afya na halinjema yetu. Hata hivyo, wao hutimiza sehemu ya maponyo. Sisi hutafuta utumishi wao iwapo kuna kasoro, lakini ni mara chache ambapo sisi huwafikiria iwapo twahisi vema. Basi, twaweza kufanya nini tujipatie afya njema?

Miongozo kwa Maisha Yenye Afya

Kwa ujumla, wastadi waafikiana kwamba afya njema hutegemea mambo matatu makubwa: ulaji uliosawazika, mazoezi ya ukawaida, na maisha ya kimadaraka. Kwa hakika habari za kuarifu mambo hayo ni nyingi, na nyingi zazo zinatumika na ni zenye manufaa. Mawazo fulani yafaayo na ya kisasa juu ya jinsi ulaji na mazoezi yahusiana na afya yetu yametolewa katika masanduku “Ulaji Wako na Afya Yako” na “Mazoezi, Hali Nzuri, na Afya.”

Ingawa habari nyingi zenye msaada zapatikana, kwa kusikitisha, mambo ya uhakika yaonyesha kwamba watu walio wengi hawaoni afya njema kuwa ya maana sana katika orodha yao ya mambo ya kutangulizwa. Miongoni mwa mambo mengineyo, “kila mtu ajua kinachotakwa ili kupunguza uzani,” akaeleza Dakt. Marion Nestle wa Ofisi ya Uzuiaji Magonjwa na Uendelezaji Afya katika Washington, “na bado kuwa na uzani mwingi mno hakuelekei kubadilika sana.” Kulingana na ofisi yake, karibu mtu 1 kati ya watu 4 katika United States amepita uzani wa kawaida kwa asilimia 20.

Vivyo hivyo, uchunguzi wa Kitovu cha Kitaifa cha Takwimu za Afya United States wafunua hivi: “Kwa ujumla, kati ya 1977 na 1983 yaonekana kumekuwa na ongezeko la mazoea yasiyofaa afya.” Ni nini haya “mazoea yasiyofaa afya”? Si matatizo ambayo mtu mwenyewe hawezi kuyadhibiti, kama vile ukosefu wa chakula cha kujenga, magonjwa ya kipuku, au uchafuzi. Bali, ni mambo ambayo hasa ni daraka la mtu mwenyewe—mazoea kama kuvuta sigareti, kula kupita kiasi, kunywa kupita kiasi, na utumizi mbaya wa dawa za kulevya.

Kwa wazi, ili kupata afya njema mengi zaidi yahitajiwa kuliko habari za kitiba au za kisayansi. Kichocheo kikubwa zaidi cha kuishi kwa kutimiza daraka letu mmoja mmoja chahitajiwa. Ni lazima tuhamasishwe kufanya si mambo yale tu ambayo yatachangia afya njema bali pia tuepuke mambo ambayo yataibomoa. Twaweza kupata wapi kichocheo na hamasisho hiyo ya kutusaidia tuishi maisha zenye afya?

Ingawa huenda watu walio wengi wasimaizi hivyo, S.I. McMillen, aliye daktari-mtungaji, alieleza hivi katika dibaji ya kitabu chake None of These Diseases: “Mimi nina uhakika kwamba msomaji atavutiwa sana kugundua kwamba mielekezo ya Biblia yaweza kumwokoa na magonjwa fulani yenye kuambukiza, na kansa nyingi zenye kuua, na mtataniko wa magonjwa mengi yahusianayo na utendeano wa mwili na akili ambayo yanaongezeka zijapokuwako jitihada zote za dawa za ki-siku-hizi. . . . Amani haiji kwa vibonge.”

Twaweza kuona kutokana na maelezo haya kwamba ingawa Biblia si kitabu cha masomo ya tiba wala si juzuu la afya, inaandaa kanuni na miongozo iwezayo kutokeza mazoea yenye mafaa na afya njema. Ni nini baadhi ya kanuni hizi?

Hisiamoyo na Mtazamio Maishani

Kwa kielelezo, “sayansi ya kitiba yatambua kwamba hisiamoyo kama vile hofu, majonzi, husuda, uchungu wa moyo na chuki huleta mengi ya magonjwa yetu,” akasema Dakt. McMillen aliyetangulia kunukuliwa. “Makadirio yatofautiana kutoka asilimia 60 hadi karibu asilimia 100.”

Jambo gani laweza kufanywa kurekebisha jambo hilo? Kwa kupendeza, yapata miaka 3,000 iliyopita, Biblia ilionyesha wazi hivi: “Moyo mtulivu ndio muundo wa kimnofu, lakini wivu ni ubovu kwa mifupa.” (Mithali 14:30, NW) Lakini mtu hupataje “moyo mtulivu”? Shauri la Biblia ni kwamba: “Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya.” (Waefeso 4:31) Maana yake, ili kuona shangwe ya afya njema ya kimwili, ni lazima tujifunze kudhibiti hisiamoyo zetu.

Bila shaka, hii ni tofauti na ushauri wa madaktariakili na wasaikolojia fulani wa ki-siku-hizi. Mara nyingi wao hupendekeza kwamba tuonyeshe hisia zetu kimatendo kuliko kujaribu kuzidhibiti. Kufoka na kufungulia kasirani iliyojazana ndani ya mtu huenda kukaleta kitulizo cha muda kwa mtu mwenye kuhisi akiwa mwenye kubanwa na kusumbuka. Lakini hiyo yafanya nini kwa uhusiano wake na wale walio karibu yake, na huenda hiyo ikafyatusha tendo-mwitikio gani kwa upande wao? Si vigumu kuwazia mkaziko wa mawazo na fahamu zenye kutatanika vibaya, licha ya uwezekano wa majeraha ya kimwili, ambayo yangetokea ikiwa kila mmoja angeonyesha hisia zake kimatendo kuliko kujaribu kuzidhibiti. Hiyo hufanyiza tu mrudiano wa mabaya usio na mwisho.

Bila shaka, si rahisi kuziweza hisiamoyo hizi zenye madhara, hasa ikiwa mtu ana elekeo la kujiacha aongozwe na kasirani na hasira kali. Ndiyo sababu Biblia yaendelea kusema hivi: “Iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane.” (Waefeso 4:32) Yaani, yasema kwamba mahali pa hisia hasi zenye madhara twapaswa kuweka zilizo chanya.

Hisia chanya hizo kuelekea wengine zatufanyia nini sisi? “Kujali kwafaa uhai,” aandika Dakt. James Lynch katika kitabu chake The Broken Heart. “Amrisho la ‘kupenda jirani yako kama ujipendavyo mwenyewe’ si amrisho la kiadili tu—ni lenye kuhusu mwili.” Kuhusu manufaa ambazo mahusiano chanya hayo huleta, Robert Taylor, daktariakili, aliongezea hivi: “Kujua kwamba una watu ambao waweza kugeukia nyakati za uhitaji kwaweza kuandaa hisia za maana sana za usalama, matazamio mema na tumaini—yote hayo yakiwa ni mambo yawezayo kuwa dawa nzuri sana kwa mkazo.” Hivyo, ingawa tiba ya ki-siku-hizi huenda ikajaribu kutokeza maponyo ya baadhi ya magonjwa yaitwayo yenye kuhusiana na utendeano wa akili na mwili, mielekezo sahili ya Biblia yaweza kusaidia kuyazuia yasitukie pale mwanzoni. Mtu yeyote aliye na nia ya kutumia miongozo ya Biblia atanufaika kihisiamoyo na kimwili.

Mazoea na Uzoelevu

Kitu kingine ambacho huathiri halinjema yetu ya kihisiamoyo na kimwili ni jinsi tutendeavyo mwili wetu. Kwa jitihada ya kiasi kwa sehemu yetu—kula ifaavyo, kupata mazoezi na pumziko lihitajiwalo, kukaa safi, na kadhalika—mwili wetu utajitunza wenyewe. Hata hivyo, tukizoea kuutenda vibaya, muda si muda utavunjika, na sisi ndio tutateseka.

Ushauri wa Biblia ni kwamba: “Na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho.” (2 Wakorintho 7:1) Twaweza kutumiaje ushauri huo, na manufaa ni nini? Fikiria ripoti inayofuata ya Taasisi ya Worldwatch iliyoko Washington: “Kuvuta sigareti ni ugonjwa wa kipuku kinachokua kwa asilimia 2.1 kwa mwaka, haraka kuliko idadi ya ulimwengu. . . . Ukuzi wa kutumia tumbako ulienda polepole katika miaka ya mapema ya themanini, hasa kwa sababu za kiuchumi, lakini unarudia ongezeko lao la haraka. Sasa watu zaidi ya bilioni moja huvuta sigareti, wakitumia sigareti karibu trilioni 5 kwa mwaka, wastani wa zaidi ya nusu pakiti kwa siku.”

‘Ugonjwa kipuku huu unaokua’ umekuwa na athari gani? Sanduku linalofuata latoa mambo ya kufikiriwa kimakini. Orodha haionyeshi mambo yote, lakini ujumbe ni wazi: Uzoelevu wa tumbako una nguvu na gharama kubwa. Ni zoea lenye kudhuru afya ya wazoelevu na ya wale walio karibu yao.

Namna gani jitihada za kukomesha zoea hilo? Zijapokuwako kampeni zote za kupinga uvutaji sigareti, fanikio limekuwa dogo ulimwenguni pote. Hii ni kwa sababu kushinda zoea la tumbako ni jitihada ya kujikakamia sana. Utafiti waonyesha kwamba ni 1 tu kati ya 4 wenye kuvuta sigareti ambao hupata kufanikiwa kuvunja zoea hilo. Ni wazi kuwa maonyo yote ya kwamba kuvuta sigareti ni hatari kwa afya si kichocheo cha kutosha.

Hata hivyo, shauri la Biblia lililonukuliwa juu, pamoja na agizo lalo kwa Wakristo kupenda jirani zao kama wao wenyewe, limehamasisha maelfu ambao sasa ni Mashahidi wa Yehova waache kuvuta sigareti. Iwe ni kwenye Majumba ya Ufalme yao, ambako wao hukutana kwa saa kadhaa kila juma, au kwenye mikusanyiko yao, ambako maelfu yao hukutana kwa siku nyingi, hutaona yeyote wao akiwa na sigareti. Nia yao kupokea na kutumia mielekezo ya Biblia imewapa mwanio wa kutimiza mambo ambayo wengine hushindwa kutimiza.

Mazoea mengine yenye madhara yatia ndani kunywa alkoholi kupindukia, utumizi mbaya wa dawa za kulevya, ngono za ovyoovyo na magonjwa ya kuua ambayo yawezekana kutokana nazo, na chungu zima ya matatizo mengine ya kiafya na kijamii yenye kusumbua. Ingawa wenye mamlaka ya afya wamesongwa sana kushughulikia matatizo haya, utaona kwamba Biblia huandaa ushauri wenye kiasi na wenye kutumika.a—Mithali 20:1; Matendo 15:20, 29; 1 Wakorintho 6:13, 18.

Wakati Magonjwa Yote Yataisha

Hata tujaribu kadiri gani kudumisha afya njema, uhakika halisi wabakia kwamba, kwa sasa, sisi twawa wagonjwa na kufa. Na bado, Muumba wa binadamu, Yehova Mungu, licha ya kutuambia kwa nini binadamu huwa mgonjwa na kufa atuambia pia juu ya wakati unaokuja karibuni ambapo magonjwa yote na hata kifo chenyewe yatashindwa. —Warumi 5:12.

Unabii wa Biblia kwenye Isaya 33:24 huahidi hivi: “Hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.” Ufunuo 21:4 waahidi hivi pia: “Naye [Mungu] atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena.” Ndiyo, ahadi ya Muumba ni ulimwengu mpya hapa hapa duniani, ambapo ainabinadamu itainuliwa kwenye ukamilifu wa kibinadamu, na afya ya usitawi mwingi na uhai wa milele ikiwa ndiyo kura ya jamaa ya kibinadamu!—Isaya 65:17-25.

[Maelezo ya Chini]

a Kwa habari za ziada, tafadhali ona sura ya 10 ya kitabu Happiness—How to Find It, kilichotangazwa na Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi Biblia na Trakti ya New York.

[Sanduku katika ukurasa wa 8, 9]

Ulaji Wako na Afya Yako

“Ikiwa wewe . . . huvuti sigareti au hunywi kupindukia, chaguo lako la ulaji laweza kuathiri matazamio yako ya muda mrefu ya afya kuliko kitendo chochote kingine ambacho ungeweza kuchukua.”—Dakt. C. Everett Koop, mpasuaji mkuu wa United States wa hapo zamani.

Katika miaka ya majuzi, wastadi wa afya wamenena wazi juu ya athari zenye madhara ambazo mambo fulani ya ulaji wa mataifa yaliyositawi kiviwanda huwa nazo juu ya afya ya watu. Zaidi ya kuitisha uangalifu kwenye vitu kama tumbako, alkoholi, chumvi, na sukari, mkazo wa pekee umetiwa kwenye uhakika wa kwamba ulaji wa watu wengi una shahamu (mafuta) na kolesteroli nyingi mno na utembo kidogo mno.

“Hangaikio kubwa kabisa,” aendelea Dakt. Koop, “ni ulaji wetu kupindukia wa shahamu na unavyohusiana na hatari ya magonjwa ya daima kama ugonjwa wa moyo, namna fulani za kansa, kisukari, msongo mwingi wa damu, kamata na kunenepa kupita kiasi.” Vivyo hivyo, mpasuaji Mwingereza Dakt. Denis Burkitt na wengine wamekuwa wakiitisha uangalifu kwenye ukatamano kati ya ulaji wenye kupungukiwa utembo na ugonjwa wa moyo, kansa za matumbo, michafuko ya mfuko wa tumbo, kisukari, na magonjwa mengine.

Si mambo yote yanayoeleweka juu ya jinsi ulaji wetu huathiri afya yetu, wala hakuna uafikiano wa ujumla miongoni mwa wastadi wa afya. Hata hivyo, kuna mambo fulani ya kitiba yenye uhakika ambayo yastahiki sana ufikirio wetu.

Punguza Shahamu

Kiwango cha juu cha kolesteroli, alkoholi yenye shahamu, katika damu yahusiana moja kwa moja na uelekeo mkubwa wa ugonjwa wa moyo. Wale walio na ugonjwa wa moyo au historia ya kijamaa ya kuwa nao, na wale ambao wataka kupunguza uelekeo wa kuwa nao, wangefanya vyema kuiweka kolesteroli ya damu iwe kwenye kiwango salama. Jambo gani laweza kufanywa?

Njia ya kwanza ya kinga ambayo hupendekezwa kwa kawaida ni kufuata ulaji wenye kiasi kidogo cha kolesteroli, ambayo hupatikana katika vyakula vyote vya wanyama, kama nyama, mayai, na vinavyofanyizwa kwa maziwa, lakini isiyopatikana katika vyakula-mimea. Hata hivyo, uchunguzi wa hivi majuzi umepata kwamba kula vyakula vyenye kolesteroli nyingi kuna athari ya kiasi tu juu ya kiwango cha kolesteroli ya damu ya mtu. Lakini ikiwa ulaji ni wenye shahamu nyingi pia dabwadabwa (kama shahamu za wanyama, mafuta-mboga ya kukaangia, mawese na mafuta ya nazi), mwinuko wa kolesteroli ya damu ni mwingi katika watu walio wengi. Hivyo, mkazo siku hizi ni kwamba ‘punguza shahamu.’ Ule nyama ya kiasi na isiyonona, ukate shahamu yenye kuonekana, uwachune kuku ngozi, na uweke mipaka ya kula viini-yai, maziwa yenye siagi, jibini ngumu-ngumu, na vyakula vilivyofanyizwa kwa mashine ambavyo vina mawese au mafuta ya nazi.

Ingawa shahamu dabwadabwa zina elekeo la kuinua kiwango cha kolesteroli katika damu, mafuta majimaji yasiyo dabwadabwa (mafuta ya zeituni, ya maharagwe-soi, saflawa, mahindi, na ya mboga nyinginezo), samaki wenye shahamu, na samakiganda hufanya kwa kinyume. Baadhi ya hayo huenda hata yakasaidia kuinua kiasi kifaacho cha kolesteroli iitwayo nzuri, ile protinishahamu ya kiasi kingi, katika damu au kushusha kiwango cha aina ya kolesteroli yenye madhara, ile protinishahamu ya kiasi kidogo.

Kula Utembo Zaidi

Kupunguza shahamu ni sehemu moja tu ya kisa. Vyakula vilivyosafishwa sana na kutengenezwa sana kwa mashine—vyenye unga mweupe mwingi, sukari, viongezeo vya kikemikali, na kadhalika—havina utembo kabisa. Tokeo ni yale yaitwayo magonjwa ya mwerevuko: kufunga choo, kikundu, hernia, kufanyika kwa vifuko wazi katika utumbo, kansa ya utumbompana na mkundu, kisukari, ugonjwa wa moyo, na mengine. “Wanaume wenye kula kiasi kidogo cha utembo walikuwa na hatari kubwa mara tatu zaidi ya kufa kutokana na visababishi vyote kuliko wanaume wenye kula kiasi kingi,” yasema ripoti moja katika Lancet.

Utembo katika ulaji hushiriki fungu lao kwa njia mbili. Hufyonza maji yapitapo katika mfumo wetu wa kuyeyusha chakula, na hupita haraka katika kipito chetu cha uyeyushaji chakula. Wastadi wa afya wahisi kwamba huondoka pamoja na vingi vya vitu vyenye madhara na kuharakisha kuondoka kwavyo mwilini. Tembo fulani zenye kuoama huonwa kuwa hupunguza viwango vya sukari na kolesteroli ya protinishahamu ya kiasi kidogo—msaada mkubwa kwa wenye ugonjwa wa sukari na wa moyo.

Wewe waweza kunufaikaje na maarifa haya juu ya utembo? Ikiwezekana, katika ulaji wako ongeza kiasi cha matunda, mboga, na vyakula vya nafaka isiyochekechwa. Acha kula mkate mweupe na kuanza kula mkate wa unga usiochekechwa na kuongeza nafaka zisizochekechwa kwenye kiamsha-kinywa. Maharagwe pia ni chanzo bora kabisa cha utembo. Na wanga—viazi na mchele—huenda vikawa na vitu vya kuzuia kansa.

Bila shaka, kuna mambo mengine mengi ya ulaji wako ambayo huathiri afya yako. Hata hivyo, kupunguza shahamu na kuongeza utembo ndiyo mambo mawili yanayohitaji kuangaliwa hima katika ulaji wa watu walio wengi.

[Sanduku katika ukurasa wa 10, 11]

Mazoezi, Hali Nzuri, na Afya

Uchunguzi wa miaka 40 wa wanaume kama 17,000 ulipata kwamba wale waliofanya mazoezi kidogo kufikia saa moja au mbili kwa juma (wakitumia kalori 500 hivi) walikuwa na kadiri za kufa zilizo chini kwa asilimia 15 hadi 20 kuliko wale wasiofanya mazoezi. Wale waliofanya mazoezi kwa kujikaza sana (wakichoma kalori 2,000 kwa juma) walikuwa na kadiri ya kufa iliyo chini zaidi kwa theluthi moja. Uchunguzi mwingine umefikia mkataa ule ule: Mazoezi ya ukawaida hupunguza hatari ya msongo mwingi wa damu, ugonjwa wa moyo, na labda hata kansa. Pia mazoezi ya ukawaida husaidia kupigana dhidi ya uzani wa kupita kiasi, kujistahi kwa hali ya chini, mkazo, wasiwasi, na kushuka moyo.

Sababu ambayo mazoezi ya ukawaida yaelekea kufanya yote hayo ni kwamba hayo huinua uwezo na uvumilivu wa mwili wa mtu. Yaani, mazoezi ya ukawaida hufanya mtu awe mwenye hali nzuri. Ingawa hali nzuri haitoi uthibitisho kamili wa afya njema, mwili wenye hali nzuri hauelekei sana kulemewa na maradhi. Pia hupona haraka uwapo mgonjwa. Hali nzuri ya kimwili huenda ikachangia hali njema ya mtu ya kiakili na kihisiamoyo na pia kupunguza athari za uzee.

Gani na Kiasi Gani?

Maswali yaliyo ya kawaida juu ya mazoezi ni, Mazoezi ya aina gani, na kiasi gani? Kwa kweli hiyo hutegemea mtu ataka kutimiza nini. Ni lazima mwanariadha wa Olimpiki ajizoeze kwa muda mrefu na kwa jitihada ili abaki mwenye hali nzuri. Kwa watu walio wengi, huenda mradi ukawa ni kupoteza uzani, kuwa na umbo zuri, kuona shangwe ya afya bora, au kuhisi vema tu. Kwa hao, wastadi wengi wa afya waafikiana kwamba dakika 20 hadi 30 za mazoezi mara tatu kwa juma zahitajiwa ili kuendeleza hali nzuri. Lakini mazoezi ya aina gani?

Hali nzuri yahusisha uwezo wa mwili wa mtu, umri, na uvumilivu, kwa hiyo mazoezi yawe na shabaha ya kuinua kadiri ya mpigomoyo na mpumuo wa mtu wakati wa kujizoeza. Kwa kawaida hayo ndiyo huitwa mazoezi ya kuzidisha upumuaji. Kupiga mbio, kutembea haraka, dansi ya kuzidisha upumuaji, kuruka kamba, kuogelea, na kuendesha baiskeli ni namna za kawaida za mazoezi ya kuzidisha upumuaji, kila moja likiwa na vileta-manufaa na viondoa-manufaa katika ufaaji wa hali, gharama ya mahali na vifaa, elekeo la kujeruhiwa, na kadhalika.

Namna nyingine za mazoezi huimarisha misuli na kuumba mwili. Haya ni kutia na kujizoeza kwa mashine na mizani. Mazoezi hayo huongeza uimara na uvumilivu wa mwili wa mtu na yaweza kuleta maendeleo ya msimamo wa mwili na sura ya mtu pia—yote hayo yakiongezea ufuatiaji wa mwili wenye hali nzuri.

Namna gani mazoezi ya viungo vya mwili ambayo wengi wetu twayakumbuka vizuri sana kutokana na siku zetu za shule? Yalitufaa sana, tuwe au tusiwe tuliyathamini wakati huo. Kujinyoosha, kugeuka, na kujipindapinda hufanya mwili unyumbuke kwa urahisi. Kuruka na kurusha mateke huongeza kasi ya mpigo wa moyo. Mazoezi ya kuchuchumaa kisha kusimama, kulala kifudifudi kisha kujiinua kwa mikono na kuinua kidevu huimarisha misuli. Faida kubwa ya mazoezi hayo ya kujinyoosha kadiri mtu azeekavyo ni kwamba huenda akabaki mnyumbufu na aweze kuendelea akiwa mtendaji kwa muda mrefu zaidi.

Mwisho, kuna michezo ya tafrija—tenisi, mpiraraketi, mpiramwororo, na utendaji mwingine mwingi. Faida ya utendaji huo ni kwamba hufurahisha kuliko namna za mazoezi yasiyo na upendezi na kwa hiyo huenda ukawa ndio wahitajiwa kufanya mtu ajizoeze kwa ukawaida. Ikitegemea mtu huyafuatia kwa ustadi na sulubu ya kadiri gani, utendaji huo huenda ukaandaa au usiandae kiwango cha kutosha cha mkakamko kama namna nyingine za mazoezi. Hata hivyo, husaidia hali ya mwili, huletea maendeleo utendaji ulioratibika wa viungo vya mwili, na huongezea unyumbufu na wepesi wa miendo.

Kukiwa na namna nyingi sana za mazoezi ya kuchagua, siri ya mafanikio ni kuchagua namna moja ambayo ungeonea shangwe, au mchanganyiko wazo. Hiyo itakusaidia ushikamane na madhumuni yako, kwa kuwa uchunguzi huonyesha kwamba kuanzia asilimia 60 hadi 70 ya watu wazima ambao huanza kujizoeza huacha katika muda wa mwezi mmoja hivi. Kumbuka, ukawaida, wala si kiasi tu cha mazoezi, ndilo jambo la maana. Kwa kujitia katika aina tofauti za mazoezi kwenye nyakati tofauti, utaupa mwili wako ukuzi wa sehemu zote, uwe na siha kwa njia ya usawaziko.

Chaguo lako la utendaji lapasa pia kuongozwa na umri wako na hali yako ya ujumla ya afya pale mwanzoni. Bila shaka, wale wenye matatizo ya afya wapaswa kutafuta ushauri wa daktari wao kabla ya kuanza programu ya mazoezi. Vyovyote vile, anza polepole, na uongezee kadiri ufanyavyo maendeleo. Jifunze juu ya namna za mazoezi ambayo wachagua—vitabu na maagizo ni tele kuhusu habari hiyo—nawe utaona shangwe na kunufaika pia kutokana na jitihada zako.

[Sanduku katika ukurasa wa 12]

Gharama ya Kuvuta Sigareti

◻ Tumbako husababisha mateso mengi na kifo kingi zaidi miongoni mwa watu wazima kuliko kisumu kingine chochote katika mazingira.

◻ Gharama ya uhai ulimwenguni pote sasa yakaribia milioni 2.5 kwa mwaka, karibu asilimia 5 ya vifo vyote.

◻ Matumizi ya afya kuongeza hasara za kiuchumi katika [United States] ni kuanzia dola milioni 38 hadi dola milioni elfu 95, au kuanzia dola 1.25 hadi dola 3.15 kwa pakiti. Jumla hizi hazitii ndani gharama ya tumbako yenyewe—karibu dola milioni elfu 30 kwa mwaka.

◻ Labda wavutaji wa moshi utokao kwa wengine wana elekeo mara tatu la kufa kutokana na kansa ya mapafu kuliko vile ingekuwa kama hawangekuwa mahali penye moshi.

◻ Uvutaji wa akina mama hupunguza uwezo wa kimwili na kiakili wa watoto wao, na katika nchi nyingi zaidi ya sehemu moja kwa tano ya watoto wanapumua moshi kwa njia hii.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki