Sisi Ni Wenye Afya Kiasi Gani?
DOLA ELFU moja kwa siku! Kiasi hicho ndicho hutumiwa na watu katika United States kutunza afya. Wakaaji wa Jamhuri ya Muungano ya Ujeremani hutumia zaidi ya sehemu moja kwa tano ya mapato yao ya ujumla taifani, au dachi-maki zaidi ya milioni elfu 340 kwa mwaka, ili kutimiza mahitaji yao ya afya. Hali ni kama hiyo katika hesabu kubwa zaidi ya mataifa yaliyoendelea kiviwanda au yaliyositawi.
Hakuna shaka kwamba raia wa wastani katika nchi hizi anazidi kuhangaikia afya. Vitabu na vidio zenye kuhusu ulaji na mazoezi zaendelea kuwekwa kwanza katika orodha za bidhaa zenye kuuzwa kwa wingi zaidi. Vyakula vya afya, vitamini na mavazi ya kufanyia mazoezi vimekuwa vitu vyenye kutokeza biashara ya mamilioni mengi ya dola. Na siku hizi mtu mwenye mafanikio haonwi tena kuwa ni yule bwanyenye mtafuna sigara bali ni jamaa mwenye sura safi, mwenye kuhangaika awe na hali nzuri ya afya.
Kwa kuwa afya na hali nzuri ya mwili yapewa uangalifu na upendezi mwingi jinsi hii, je! kweli sisi ni wenye afya sana kuliko watu wa vizazi vilivyotangulia? Je! mapesa mengi ambayo yametumiwa kuhusu gharama za kitiba na utunzaji wa afya yametokeza halinjema ya kimwili kwa sisi sote? Kwa kweli, sisi ni wenye afya kiasi gani?
Hali Ilivyo Leo
Tofauti na vile tungeweza kutarajia, ripoti za kutoka nchi zilizo tajiri na maskini kuzunguka ulimwengu zaonyesha kwamba leo hali ya watu si yenye afya. Ikinena kuhusu hali zenye kutofautiana za afya ulimwenguni pote, ripoti moja iliyotayarishwa na Taasisi ya Worldwatch yasema hivi: “Ingawa mahitaji yao ya afya hutofautiana sana, matajiri na maskini wana jambo moja kwa ujumla: wote hufa isivyo lazima. Matajiri hufa kwa ugonjwa wa moyo na kansa, maskini hufa kwa kuhara, mchochota wa mapafu, na surua.”
Kujapokuwa na maendeleo ya utafiti wa tiba, magonjwa ya moyo na kansa yaendelea kuwa pigo kubwa la nchi zenye utajiri mwingi. Kwa uhakika, ripoti moja katika The New England Journal of Medicine yasema hivi: “Sisi hatuoni sababu ya kutazamia mema kuhusu maendeleo ya ujumla katika miaka ya majuzi. Hakuna sababu ya kufikiri kwamba, kwa ujumla, kansa yazidi kupungua.” Kwa habari ya hangaiko lenye kuongezeka sana la kuwa na hali nzuri ya afya, hali hiyo yatajwa kwa muhtasari na Dakt. Michael McGinnis wa Idara ya Afya na Huduma za United States: “Walio wengi sana wajua umaana wa kuwa na hali nzuri ya afya. Lakini wao wenyewe hawajaichukua hatua. Waamerika hawana hali nzuri ya afya kama vile wafikirivyo.”
Kwa upande mwingine, “robo moja ya watu wa ulimwengu hawana maji ya kunywa na njia safi ya kuondoa takataka za kibinadamu,” yasema ripoti hiyo ya Worldwatch. “Tokeo ni kwamba, magonjwa ya kuhara ni ya kawaida katika sehemu zote za Ulimwengu wa Tatu na ndicho kisababishi kikubwa zaidi ulimwenguni cha vifo vya watoto wachanga.” Kuhara, mchochota wa mapafu, surua (ukambi), diftheria, kifua kikuu, na magonjwa mengine, kila mwaka huua watoto milioni 15 walio chini ya umri wa miaka mitano na kuzuia ukuzi wa kawaida wa mamilioni zaidi. Hata hivyo, hali ya kinyumenyume halisi cha yote haya ni kwamba wastadi wahisi kwamba kadiri kubwa ya hali hii yaweza kuzuiwa kwa urahisi.
Ingawa watoto katika mataifa yaliyositawi huenda wakaepushwa na tanzia hizo, kuna ishara zenye kugutusha kwamba afya ya ujumla ya vijana leo inazorota badala ya kupata nafuu. Kwa kielelezo, The Guardian la London, chini ya kichwa kikuu “Watoto ‘Ni Wenye Afya Kuliko Miaka 35 Iliyopita,’” yaripoti kwamba uchunguzi wa Baraza la Utafiti wa Kitiba umepata “maongezeko makubwa ya kulazwa hospitali kwa watoto wa kufikia miaka minne, kuongezeka mara tatu kwa visa vya pumu, na ongezeko mara sita la ugonjwa wa ngozi miongoni mwa kizazi kipya.” Yalipatikana pia maongezeko makubwa ya kisukari cha watoto, unene wa kupita kiasi, mkazo, na magonjwa ya mihemko.
Uchunguzi wa taifani pote katika United States umefunua pia kwamba hali ya kimwili ya watoto wa shule leo haiko kama ipasavyo kuwa. “Hiyo ndiyo siri yenye kutunzwa zaidi leo katika Amerika—ule ukosefu wa vijana wa kuwa na hali nzuri ya afya,” asema George Allen, mwenyekiti wa Baraza la Rais Kuhusu Hali Nzuri ya Mwili na Michezo. Tarakimu zilizotolewa karibuni zaidi na baraza hilo zaonyesha kwamba asilimia 40 ya wavulana na asilimia 70 ya wasichana wa miaka 6 hadi 17 hawawezi kuinua kidevu mara moja tu katika mazoezi ya mwili. Uchunguzi mwingine ulipata kwamba matineja leo wana mkazo mwingi wa damu, viwango vya kupita kiasi vya kolesteroli katika damu na vya shahamu mwilini, bila kutaja matatizo mazito ya mihemko, na pia matatizo ya kutumia vibaya dawa za kulevya na alkoholi.
Kutazama Mbele
Walio wengi kati yetu twang’amua kwamba, kwa kadiri fulani, hali yetu ya afya maishani mwote huamuliwa na hali ya afya wakati wa utoto wetu. Kwa hiyo, haishangazi kwamba George Allen alionelea hivi: “Jambo lenye kunihangaisha ni kwamba msipofanya vijana wajifunze kuwa na hali nzuri ya afya sasa, hawatajifunza kamwe wakiwa watu wazima.” Ndivyo ilivyo kuhusu mataifa yanayoendelea kusitawi, isipokuwa jambo la kwamba watoto wengi huko hawapewi fursa ya kusitawi wakawe watu wazima wenye afya.
Ingawa ni yenye kusononesha, matatizo hayo si yasiyotatulika. Hata kama waishi wapi, kuna jambo ambalo wewe ukiwa mtu mmoja waweza kufanya kuhusu afya yako na ile ya jamaa yako. Hata hivyo, mengi hutegemea oni lako juu ya afya yako na juu yako mwenyewe. Kwa kweli, maswali haya huenda yakaulizwa: yangeweza kuulizwa: Afya ni nini? Waweza kufanya nini udumishe afya njema? Maswali haya yatafikiriwa katika makala zinazofuata.