Kinachoamua Afya Yako—Lile Uwezalo Kufanya
KINYUME na mchele au unga, afya haiwezi kugawanywa na wafanyakazi wa kutoa misaada ya chakula. Haiji ikiwa mfukoni kwa sababu si bidhaa bali ni hali. “Afya,” lafafanua WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni), “ni hali-njema kamili ya kimwili, kiakili na kijamii.” Basi, ni nini huamua kiasi cha hiyo hali-njema?
Nyumba ya kadiri huenda ijengwe kwa kutumia bao, misumari, na mabati, lakini sehemu mbalimbali mara nyingi hutegemezwa na nguzo nne za pembeni. Vivyo hivyo, afya yetu huamuliwa na athari kadhaa, bali zote zahusiana na “pembe” nne ziathirizo. Hizo ni (1) tabia, (2) mazingira, (3) utunzi wa kitiba, na (4) mfanyizo wa kibiolojia. Kama vile uwezavyo kuimarisha nyumba yako kwa kuboresha hali ya nguzo hizo, ndivyo unavyoweza kufanya afya yako iwe bora kwa kuboresha hali ya visababishi hivi vyenye kuathiri. Swali ni, Hilo laweza kufanywaje na rasilimali chache?
Tabia Yako na Afya Yako
Kati ya hivyo visababishi vinne, tabia yako ndiyo iliyo na uwezo mkubwa zaidi wa kuidhibiti. Kuibadili kwa uzuri kwaweza kusaidia. Ni kweli, umaskini huwekea mipaka mabadiliko uwezayo kufanya katika mlo na mazoea yako, lakini kwa kutumia machaguo yanayopatikana waweza kufanyiza tofauti iliyo kubwa. Ona kielelezo kifuatacho.
Kwa kawaida mama ana uchaguzi kati ya kumnyonyesha mtoto wake matiti na kumnyonyesha chupa. Kunyonyesha matiti, lasema Shirika la Hazina ya Watoto la Umoja wa Mataifa, ni “chaguo kubwa, kimwili na kiuchumi.” Maziwa ya mama, wasema wastadi, ni “chakula cha msingi chenye afya,” cha kukipa kitoto “mkolezo ufaao wa protini kihususa, shahamu, usukari, vitamini, madini na elementi titi huhitajiwa kwa ajili ya ukuzi wenye upatani.” Maziwa ya matiti pia husafirisha protini zenye kupiga maradhi, au mazindiko, kutoka kwa mama hadi kwa kitoto, yakikipa kitoto uanzilishi wa kukumbana na maradhi.
Hasa katika mabara ya kitropiki yaliyo na hali mbaya za usafi wa afya, kunyonyesha matiti ni bora zaidi. Kinyume na maziwa ya chupa, maziwa ya matiti hayawezi kutiwa maji kupita kiasi ili kuokoa fedha, makosa hayawezi kufanywa wakati yanapotayarishwa, na sikuzote hupakuliwa kutoka kwa chombo safi. Kinyume, “kitoto kinacholishwa kwa chupa katika jamii maskini,” yaandika Synergy, gazeti fulani kutoka Shirika la Kanada la Afya ya Kimataifa, “kwa kukadiria kina uelekeo wa kufa mara 15 zaidi kutokana na maradhi ya kuharisha na mara nne zaidi kutokana na homa ya mapafu kuliko kitoto kinacholishwa kwa matiti tu.”
Kisha kuna faida ya kiuchumi. Katika ulimwengu unaositawi, maziwa ya unga-unga ni ghali. Kwa kielelezo, katika Brazili, kulisha mtoto kwa chupa huenda kutumie moja kwa tano ya mapato ya mwezi ya familia maskini. Fedha zinazohifadhiwa kwa kunyonyesha matiti zaweza kuandaa milo yenye afya kwa familia nzima—kutia na mama.
Kukiwa na faida zote hizi, ungetazamia kunawiri kwa kunyonyesha. Hata hivyo, wafanyakazi wa afya katika Filipino waripoti kwamba kunyonyesha huko “kwatishwa na kutoweka kabisa,” na uchunguzi mmoja katika Brazili ulionyesha kwamba mojapo ya visababishi vikubwa vinavyoshirikishwa na ufaji wa vitoto kutokana na maambukizo ya upumuaji ni “kukosa kuvinyonyesha matiti.” Hata hivyo, kitoto chako huenda kiokoke janga hilo. Wewe una chaguo.
Ingawaje, jitihada za mama za kulinda afya ya kitoto mara nyingi hudhoofishwa na tabia zisizofaa za washiriki wengine wa familia. Fikiria kielelezo cha mama mmoja katika Nepal. Yeye hushiriki chumba kimoja chenye uvuguvugu pamoja na mume wake na bintiye mwenye umri wa miaka mitatu. Chumba hicho kidogo, laandika gazeti la Panoscope, kimejaa moshi wa jikoni na wa tumbaku. Mtoto huyo anaugua ambukizo la upumuaji. “Siwezi kumzuia mume wangu kuvuta sigareti,” huyo mama aguna. “Sasa mimi nanunua sigareti kwa ajili ya mume wangu na dawa kwa ajili ya mtoto wangu.”
Kwa kusikitisha, tatizo la mwanamke huyo laendelea kuwa la kawaida kadiri watu zaidi katika nchi zinazositawi watumiavyo vibaya mapato yahitajiwayo sana kwa kuanza kuvuta sigareti. Kwa kweli, kwa kila mvutaji anayeacha kuvuta sigareti katika Ulaya au Marekani, watu wawili waanza kuvuta sigareti katika Amerika ya Kilatini au Afrika. Matangazo ya biashara yenye kupotosha, chaandika kitabu cha Kiholanzi Roken Welbeschouwd, yastahili kulaumiwa sana. Shime kama “Varsity: kwa ajili ya akili shwari” na “Gold Leaf: sigareti muhimu sana kwa watu wa maana sana” husadikisha maskini kwamba uvutaji wa sigareti unaungamanishwa na maendeleo na mafanikio. Lakini kinyume ndilo kweli. Huchoma pesa zako na huharibu afya yako.
Fikiria hili. Kila wakati mtu avutapo sigareti, yeye hufupisha matazamio yake ya kuishi kwa dakika kumi na huongeza hatari ya kupatwa na maradhi ya ghafula ya moyo na pigo la moyo, pamoja na kansa ya mapafu, koo, na mdomo na maradhi mengine. Gazeti UN Chronicle lasema hivi: “Utumiaji wa tumbaku ni kisababishi kikubwa kuliko vyote kitokezacho kifo cha mapema na ulemavu ulimwenguni kiwezacho kizuiwa.” Tafadhali ona kwamba lasema “kiwezacho kuzuiwa.” Unaweza kuizima sigara yako ya mwisho.
Bila shaka, kuna machaguo mengi zaidi ya kitabia yaathiriyo afya yako. Sanduku katika makala haya kwenye ukurasa 11 laorodhesha habari fulani ambayo unaweza kusoma katika maktaba ya Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova. Hakika, kujielewesha huhitaji jitihada. Hata hivyo, ofisa fulani wa WHO asema hivi: “Hamwezi kuwa na jamii yenye afya bila uhusika wa watu waelewevu walioeleweshwa na kuelimishwa kuhusu hali yao ya afya.” Basi chukua hatua hii isiyo ya malipo na uboreshe afya: Jielimishe.
Afya na Mazingira ya Nyumbani
Mazingira yanayoathiri afya yako zaidi, chaarifu kitabu The Poor Die Young, ni nyumbani na ujirani wako. Mazingira yako yaweza kuwa hatari kwa afya kwa sababu ya maji. Maambukizo, magonjwa ya ngozi, kuhara, kipindupindu, kuhara damu, homa ya matumbo, na mauguo mengine yasababishwayo na maji yasiyotosha na yasiyodhuru.
Ikiwa unanawa mikono yako huhitaji zaidi ya kufungua mfereji, huenda iwe vigumu kwako kung’amua kadiri ya wakati watu wanaokosa maji nyumbani hutumia kupata maji kila siku. Mara nyingi zaidi ya watu 500 hutumia mfereji mmoja. Hilo huhitaji kungojea. Lakini watu wa mapato madogo hufanya kazi kwa saa nyingi, na kungojea, chaandika kitabu Environmental Problems in Third World Cities, “hutwaa wakati ambao ungeweza kutumiwa katika kuchuma mapato fulani.” Si ajabu kwamba ili kuokoa wakati familia ya watu sita mara nyingi huchukua ndoo za maji zipunguazo 30 zinazohitajiwa kila siku kwa ajili ya familia ya kiasi hicho. Lakini kisha kunakuwa na maji kidogo sana ya kusafisha chakula, vyombo, na nguo na siha ya kibinafsi. Hili laongoza kwa hali ambayo, kwa kufuatiza, yavutia chawa na nzi, ambazo huhatarisha afya ya familia.
Ebu fikiria hali hii. Ikiwa wewe hutegemea baiskeli ili kufika kwenye kazi iliyo mbali, je, ungeiona kuwa ni hasara kutumia wakati fulani kila juma ili kuweka mafuta kwenye mnyororo, kuchunguza breki, au kubadilisha spoki? La, kwani wang’amua kwamba hata ukipata saa chache sasa kwa kupuuza udumishaji wa baiskeli, huenda utapoteza siku nzima ya kazi baadaye wakati baiskeli yako inapoharibika. Vivyo hivyo, huenda ukapata saa fulani na pesa kidogo kila juma unapokosa kuchota maji ya kutosha ili kudumisha afya yako, lakini baadaye huenda upoteze siku nyingi na pesa wakati ambapo, kwa sababu ya udumishaji afya mbaya, afya yako inapoharibika.
Kuteka maji ya kutosha kwaweza kufanywa kuwa mradi wa familia. Hata ingawa utamaduni wa mahali huenda ushurutishe kwamba mama na watoto watumike wakiwa watwaa maji, baba mwenye kujali hatazuilia misuli yake ili asichote maji mwenyewe.
Hata hivyo, baada ya maji kufika nyumbani, tatizo la pili huzuka—jinsi ya kuyatunza yakiwa safi. Wastadi wa afya watoa ushauri hivi: Usiweke maji ya kunywa na yale yanayotumiwa kwa makusudi mengine mahali pamoja. Sikuzote funika ndoo ya kuhifadhia maji ikiwa na kifuniko kilichofunga ndi. Ruhusu maji yatulie kwa muda fulani ili kwamba uchafu utuame. Usiyaguse maji na vidole vyako unapoyachota, bali tumia kijiko safi kilicho na kishikio kirefu. Safisha ndoo ya maji kwa ukawaida ukitumia mmumunyo upararishao, na baada ya hilo uisuze na maji safi. Na maji ya mvua? Kwa hakika ni mapatano fulani (mradi imenyesha!), na yanaweza kuwa safi ikiwa hakuna uchafu ulioingia humo kwenye tangi la kuhifadhi pamoja na maji ya mvua na ikiwa tangi lenyewe limelindwa kutokana na wadudu na wanyama wadogo na wanyama wengine.
Unapokuwa na mashaka kuhusu kama maji hayo ni safi, WHO ladokeza kwamba uongeze dutu yenye kutoa klorini ndani yayo, kama vile sodium hypochlorite au calcium hypochlorite. Ni yenye kufanya kazi, nayo si ghali. Mathalani, katika Peru, mbinu hii hugharimu familia ya mapato ya wastani si zaidi ya dola mbili kwa mwaka.
Afya na Utunzaji wa Afya
Mara nyingi maskini wafahamu aina mbili tu za utunzaji wa afya: (1) unaopatikana bali ulio ghali na (2) usio ghali bali usiopatikana. Donna Maria, mmoja wa wakaaji wa mitaa michafu ya São Paulo wapatao 650,000, aeleza kuwa aina ya utunzaji upatikanao ni ule wa kwanza: “Kwetu sisi, utunzaji mzuri wa afya ni kama bidhaa zinazoonyeshwa kwenye dirisha la jumba la ununuzi wa anasa. Twaweza kuziangalia, bali hatuwezi kuzifikilia.” (Gazeti Vandaar) Kwa kweli, Donna Maria aishi katika jiji lililo na hospitali zitoazo oparesheni za kurekebisha mipito ya damu moyoni, uatika moyo, kichungulia cha CAT, na utibabu mwingine wa hali ya juu. Kwa huyo mwanamke, vitu hivi havifikiliki.
Ikiwa utunzaji wa afya usiowezekana ni kama bidhaa ya kianasa katika jumba la mauzo, basi utunzaji wa afya ugharimikao wafanana na bidhaa ya gharama ndogo ambayo kwa hiyo wateja wa mapato ya chini waifikia kwa wakati uleule. Majuzi ikaandika ripoti ya habari katika nchi fulani ya Amerika Kusini: ‘Wagonjwa wasimama kwenye mstari kwa siku mbili ili kumwona tabibu. Hakuna nafasi hospitalini. Hospitali za umma zakosa pesa, madawa, na chakula. Mfumo wa utunzaji wa afya ni mgonjwa.’
Ili kuboresha huo utunzaji wa afya unaozidi kufifia kwa ajili ya halaiki, WHO polepole limebadili kazi layo kutoka kwa udhibiti wa maradhi hadi uendelezaji wa afya kwa kuelimisha watu katika kuzuia na kudhibiti maradhi. Programu ziendelezazo utunzaji wa afya wa msingi, kama vile ulishaji unaofaa, maji safi, na usafi uletao afya na kuepuka magonjwa, laandika UN Chronicle, zimetokeza katika “afya ya tufeni iliyoboreka kwa njia yenye kutokeza.” Je, programu hizi hukunufaisha wewe? Moja yazo huenda imekunufaisha. Ipi hiyo? EPI (Programu Iliyopanuliwa juu ya Uchanjaji).
“Mchanjaji amemweka mwakilishi kuwa mgeni anayefahamika sana nyumbani na vijijini,” ikaandika ripoti juu ya EPI. Wakati wa mwongo uliopita, sindano za chanjo zilihisiwa kutoka Amazon hadi kwenye Himalayas, na kufikia 1990, WHO liliripoti, asilimia 80 ya vitoto ulimwenguni vilikuwa vimechanjwa dhidi ya maradhi sita yenye kuua.a Kila mwaka, EPI inaokoa uhai wa watoto zaidi ya milioni tatu. Wengine 450,000 ambao wangekuwa walemavu wanaweza kutembea, kukimbia na kucheza. Basi, kwa kukinga maradhi, wazazi wengi hufanya maamuzi ya kibinafsi ili watoto wao wachanjwe.
Nyakati nyingine huwezi kuzuia ugonjwa, lakini bado waweza kuudhibiti. “Imekadiriwa kwamba kwa kufikiriwa zaidi ya nusu ya utunzaji wote wa afya,” lasema gazeti World Health, “ni utunzaji wa kibinafsi au utunzaji unaoandaliwa na familia.” Mojapo ya utunzaji wa aina hiyo ya kibinafsi ni sahili, mchanganyo usio ghali wa chumvi, sukari, na maji safi uitwao oral rehydration solution (ORS).
Wataalamu wengi wa afya huona tiba hiyo ya kurudisha maji kupitia kinywa, kutia na kutumia ORS, kuwa matibabu yenye matokeo zaidi kwa ajili ya kuhara kuondoako maji mwilini. Kikitumiwa ulimwenguni pote ili kudhibiti visa vya kuhara bilioni 1.5 vinavyotukia kila mwaka katika nchi zinazositawi, kifuko kidogo cha uchumvi wa ORS kinachogharimu senti kumi tu kingeweza kuokoa uhai mwingi wa watoto milioni 3.2 wanaokufa kutokana na maradhi ya kuhara kila mwaka.
Ingeweza, lakini utumizi wa madawa ya kuzuia kuhara katika nchi fulani, laarifu Essential Drugs Monitor, gazeti moja la WHO, ungali “watumiwa kwa ukawaida zaidi kuliko utumizi wa ORS.” Mathalani, katika nchi fulani zinazositawi, madawa yatumiwa mara tatu zaidi ili kutibu kuhara kuliko ORS. “Utumizi huu wa madawa usio wa lazima wagharimu mno,” laandika gazeti hilo. Familia zilizo maskini huenda hata ziuze chakula kwa ajili ya kusudi hili. Zaidi ya hilo, yaonya, madawa ya kuzuia kuhara hayana thamani inayofaa iliyothibitika, na mengine ni hatari. “Madaktari hawapaswi kupendekeza madawa kama hayo, . . . na familia hazipasi kuyanunua.”
Badala ya kudokeza madawa, WHO latoa yafuatayo kwa ajili ya kutibu kuhara (1) Kinga kukosa kwa maji mwilini kwa kumpa mtoto vinywaji vingi, kama vile supu ya wali ama chai. (2) Ikiwa mtoto bado anakuwa amekosa maji mwilini, mwone mfanyakazi wa afya kwa ajili ya uchunguzi, nawe umtibu mtoto kwa ORS. (3) Lisha mtoto kama kawaida wakati na baada ya kuhara. (4) Ikiwa mtoto amekosa maji mwilini kweli kweli, apaswa kurudishiwa maji kupitia mishipa.b
Ikiwa huwezi kupata ORS iliyotayarishwa mapema, fuata mchanganyo huu sahili kwa makini: Changanya kijiko kimoja cha chai cha chumvi, vijiko vinane vilivyojaa vya sukari, na lita moja ya maji safi. Mpe kikombe kimoja baada ya kila kuhara, na nusu ya hicho kwa watoto wadogo sana. Ona kisanduku kwenye ukurasa 10 kwa habari zaidi juu ya habari hii.
Na kuhusu kisababishi namba nne, mfanyizo wetu wa kibiolojia, iweje? Waweza kuathiriwaje? Makala ifuatayo itazungumzia swali hilo.
[Maelezo ya Chini]
a Wauaji hao sita ni ugonjwa wa ngozi, ukambi, polio, pepo punda, kifua kikuu, na kifaduro. WHO lapendekeza kwamba mchochota ini B, ambao huua watu wengi zaidi kuliko UKIMWI uuavyo sasa, pia umetiwa katika programu ya uchanjaji.
b Finya ngozi ya fumbatio la mtoto. Ikiwa ngozi yachukua muda mrefu kupita sekunde mbili ili kurudia hali yayo ya kawaida, huenda mtoto amekosa maji mwilini kweli kweli.
[Sanduku katika ukurasa wa 8, 9]
UTUNZAJI WA AFYA WA MSINGI—UNATENDAJE KAZI?
Ili kupata jibu la swali hili, Amkeni! lilizungumza na Dakt. Michael O’Carroll, mwakilishi wa WHO katika Amerika Kusini. Madondoo fulani yafuatilia hivi.
‘TULIRITHI mfumo wa utunzaji wa afya unaotegemezwa juu ya mtazamo fulani wa kitiba. Ikiwa wewe ni mgonjwa, mwone daktari fulani. Hakuna kufikiria kwamba ulikunywa chupa mbili za wiski. Hufikirii kwamba hujafanya mazoezi kamwe. Unamwona daktari na kusema: “Daktari, niponye.” Kisha daktari anaweka kitu ndani ya mdomo wako, akudunga kitu mkononi, akata kitu kwako, au akuweka kitu fulani. Sasa, nasema kwa dhihaka hapa, kama uelewavyo, ili kukufanya uelewe, lakini aina hii ya kitiba imefanikiwa sana. Sisi tumefikiria matatizo ya kijamii kuwa matatizo ya kitiba. Kujiua, utapiamlo, na utumizi mbaya wa madawa umekuwa tatizo la kitiba. Bali si hivyo. Hata si matatizo ya afya. Ni matatizo ya kijamii yakiwa na matokeo ya kiafya na kitiba.
‘Kisha, wakati wa miaka 20 iliyopita, watu walisema, “Ala, fikiria kwanza. Twafanya mambo kwa njia isivyo. Twahitaji kuchunguza upya mtazamo wetu kuhusu afya.” Kanuni fulani zifanyizazo mwono wa utunzaji wa afya wa msingi zikatokea, kama vile:
‘Ni jambo la kibinadamu zaidi na ugharimikaji wenye matokeo baadaye kuzuia maradhi kuliko kuyatibu. Kwa kielelezo, ni kinyume cha kanuni hii kujenga kliniki ya upasuaji-moyo ikiwa hamfanyi lolote kuhusu visababishi. Hilo halimaanishi kwamba usitibu maradhi yatukiapo. Bila shaka utatibu. Ikiwa kuna shimo katika mtaa linalosababisha aksidenti kila siku ya juma, utamtibu anayeanguka na kuvunjika mguu, lakini jambo lililo la kibinadamu na kugharimika kwenye matokeo ni: Kulijaza shimo hilo.
‘Kanuni nyingine ni kutumia rasilimali zako za afya kwa matokeo zaidi. Ni kinyume cha kanuni hii kumpeleka mtu fulani kwenye kliniki kwa ajili ya tatizo liwezalo kushughulikiwa nyumbani. Au kumpeleka mtu fulani kwa hospitali tata ili kutibiwa tatizo ambalo lingeweza kushughulikiwa katika kliniki. Ama kumpeleka daktari, aliyezoezwa kwa miaka kumi kwenye chuo kikuu, ili kuchanja ilhali mtu fulani aliyezoezwa kwa miezi sita aweza kufanya kazi hiyohiyo. Kunapokuwa na uhitaji wa daktari ili kufanya kazi aliyozoezwa kwayo, apaswa kuwako. Hivi ndivyo utunzaji wa afya wa msingi utuarifuvyo: Elimisheni watu, zuieni maradhi, na mtumie rasilimali zenu za afya kwa hekima.’
[Sanduku katika ukurasa wa 10]
ORS NYINGINE KWA AJILI YA KIPINDUPINDU
WHO sasa lapendekeza ORS itokayo kwa wali, badala ya ORS wastani itokayo kwa glukosi, itumiwe kutibu wagonjwa wa kipindupindu. Machunguzo yaonyesha kwamba wagonjwa wa kipindupindu wanaotibiwa na ORS itokayo kwa wali walikuwa na uharaji uliopungua kwa asilimia 33 na visa vifupi vya kuhara kuliko wagonjwa waliopewa ORS ya wastani. Lita moja ya ORS itokayo kwa wali hutengenezwa kwa kubadilisha gramu 20 za sukari na gramu 50-80 za wali wa uunga-unga.—Essential Drug Monitor.
[Sanduku katika ukurasa wa 11]
USOMAJI WA ZIADA . . .
Tabia: “Afya Nzuri—Waweza Kufanya Nini Kuihusu?” (Amkeni!, Desemba 8, 1989) “Tumbaku na Afya Yako—Kweli Kuna Uhusiano?” (Amkeni!, Julai 8, 1989) “Kuwasaidia Watoto Kubaki Hai!” (Amkeni!, Septemba 22, 1988) “Kile Alkoholi Ifanyacho kwa Mwili Wako”—Amkeni!, Machi 8, 1980, (Zote katika Kiingereza.)
Mazingira: “Kukabiliana na Tatizo la Usafi” (Amkeni!, Septemba 22, 1988) “Uwe Msafi, Uwe na Afya!”—Amkeni!, Septemba 22, 1977, (Zote katika Kiingereza.)
Utunzaji afya: “Hatua Nyingine za Kuokoa Uhai” (Amkeni!, Septemba 22, 1988) “Kinywaji Fulani Chenye Chumvi Kiokoacho Uhai!”—Amkeni!, Septemba 22, 1985, (Zote katika Kiingereza.)
[Picha katika ukurasa wa 7]
Kuchota maji huchukua muda na ni kazi pia
[Hisani]
Mark Peters/Sipa Press
[Picha katika ukurasa wa 9]
Maji salama ya kutosha—ni lazima kwa ajili ya afya nzuri
[Hisani]
Mark Peters/Sipa Press