Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 5/8 kur. 4-8
  • Jitihada za Kuwaokoa Watoto

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Jitihada za Kuwaokoa Watoto
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Uhai wa Vijana Zaidi ya Milioni 50 Uko Hatarini
  • Maji Safi Mahali pa Mwendo Mfupi
  • Mepesi na Magumu ya Elimu
  • Watoto Walio Wafanyakazi wa Afya
  • Umaskini, Vita, na UKIMWI
  • Jitihada Inayoendelea ya Kutafuta Suluhisho
    Amkeni!—2000
  • Afya Imeboreka Tufeni Pote Lakini—Si kwa Kila Mtu
    Amkeni!—1999
  • Kinachoamua Afya Yako—Lile Uwezalo Kufanya
    Amkeni!—1995
  • Watoto Wanastahili Kupendwa na Kuthaminiwa
    Amkeni!—2000
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 5/8 kur. 4-8

Jitihada za Kuwaokoa Watoto

“Tumekusanyika kwenye Mkutano wa Viongozi wa Ulimwengu Kuhusu Watoto ili tujitie katika wajibu wa pamoja na kufanya himizo la ulimwengu wote—kumpa kila mtoto wakati ujao ulio bora.”—Kongamano la Umoja wa Mataifa, 1990.

MARAIS na mawaziri wakuu kutoka nchi zaidi ya 70 walikusanyika katika Jiji la New York Septemba 29 na 30, 1990, kuzungumza hali mbaya ya watoto wa ulimwengu.

Hilo kongamano lilikaza fikira za mataifa juu ya mateso ya watoto yaliyo ya kusikitisha sana, msiba wa duniani pote ambao umefichwa uvunguni. Peter Teeley mjumbe wa United States alionyesha wazi hivi: “Kama bundi-madoadoa 40,000 wangekuwa wakifa kila siku, watu wangeteta sana. Lakini watoto 40,000 wanakufa, na jambo hilo hata halionekani sana.”

Vichwa vyote vya serikali waliokusanyika walikubaliana kwamba ni lazima hatua ichukuliwe—haraka. Walijitia katika “wajibu mzito kutanguliza sana haki za watoto, kuwaokoa na kuwalinda na kuwakuza.” Walifanya madokezo gani thabiti?

Uhai wa Vijana Zaidi ya Milioni 50 Uko Hatarini

Lengo kuu lilikuwa kuokoa watoto zaidi ya milioni 50 ambao wangeelekea kufa katika miaka ya 1990. Uhai wa wengi wa vijana hao ungeweza kuokolewa kwa kutekeleza hatua zifuatazo za afya.

• Kama mama wote katika nchi zinazositawi wangesihiwa wanyonyeshe watoto wao wachanga kwa angalau miezi minne hadi sita, watoto milioni moja wangeokolewa kwa mwaka.

• Kutumia sana utibabu wa kurudisha maji mwilini kupitia mdomoni (ORT) kungeweza kupunguza nusu ya kadiri ya wanaokufa kwa ugonjwa wa kuhara, ambao huua watoto milioni nne kila mwaka.a

• Kueneza chanjo mahali pengi na kutumia dawa zisizo ghali za kuua vijasumu kungeweza kuzuia mamilioni ya vifo vingine visababishwavyo na magonjwa kama surua, pepopunda, na mchochota wa mapafu.

Je! namna hiyo ya programu ya afya yawezekana? Labda gharama ingefika dola bilioni 2.5 kwa mwaka kufikia mwisho wa mwongo huu. Hiyo ingekuwa gharama ndogo kwa sababu ingehusisha dunia nzima. Kampuni za kutengeneza tumbaku za Amerika hutumia kiasi hicho kila mwaka—kwa matangazo ya sigareti tu. Kila siku mataifa ya ulimwengu humimina kiasi hichohicho juu ya matumizi ya kijeshi. Je! fedha hizo zingeweza kutumiwa juu ya afya ya watoto walio katika hatari ya kufa? Azimio la Umoja wa Mataifa Kuhusu Haki za Mtoto husema wazi kwamba “wanadamu wana deni la kumpa mtoto kilicho bora kabisa.”

Bila shaka, kumpa “kila mtoto wakati ujao ulio bora” kwahusisha mengi zaidi ya kuwaokoa wasife mapema. Sandra Huffman, msimamizi wa Kitovu cha Kuzuia Utapiamlo wa Watoto, aeleza katika gazeti Time kwamba “utibabu wa kurudisha maji mwilini kupitia mdomoni hauzuii ugonjwa wa kuhara, huokoa watoto wasife tu kutokana nao. . . . Jambo ambalo twahitaji kufanya sasa,” yeye aongeza, “ni kukaza fikira juu ya jinsi tuwezavyo kuzuia ugonjwa wenyewe, si kifo chenyewe tu.”

Ili kuuendeleza—zaidi ya kuuokoa tu—uhai wa mamilioni ya watoto, programu kadhaa zenye malengo makubwa zimeanzishwa. (Ona sanduku katika ukurasa 6.) Hakuna yoyote yazo itakayokuwa rahisi kutimizwa.

Maji Safi Mahali pa Mwendo Mfupi

Felicia Onu alikuwa akitumia saa tano kila siku kwenda kutekea maji familia yake. Mara nyingi maji aliyopeleka nyumbani yalikuwa machafu. (Maji ya jinsi hiyo huleta ambukizo la kila mwaka kutokana na buu ambalo huingia mwilini na huchangia kuzusha vipindi vya kuhara kwa watu wengi.) Lakini katika 1984, kisima kilichimbwa na bomba la kupiga maji kwa mkono likawekwa katika kijiji chao cha Ugwulangwu mashariki mwa Naijeria.

Sasa yeye hutembea meta mia chache tu kupata maji safi. Watoto wake wana afya zaidi, na maisha yake yamekuwa rahisi zaidi. Watu zaidi ya bilioni moja walio kama Felicia walipata maji safi katika miaka ya 1980. Lakini mamilioni ya wanawake na watoto bado hutumia saa nyingi kila siku wakibeba mitungi yenye maji kidogo kuliko kiasi kile kipigwacho hivihivi tu katika bomba la choo cha mkaaji wa wastani wa nchi za Magharibi.

Mepesi na Magumu ya Elimu

Maximino ni mvulana mwenye akili wa miaka 11 aishiye eneo la sehemu za ndani za Kolombia. Ijapokuwa yeye hutumia saa kadha kwa siku akisaidia baba yake kupalilia mimea yao, anaendelea vizuri shuleni. Yeye huenda Escuela Nueva, au Shule Mpya, iliyo na programu yenye kubadilisha-badilisha mipango ili kusaidia watoto wafikie kiwango cha masomo yao ikiwa wamelazimika kukosa kuhudhuria shule siku chache—tukio la kawaida, hasa wakati wa mavuno. Walimu ni haba sana katika shule ya Maximino. Vitabu vya masomo ni vichache. Watoto hutiwa moyo kusaidiana mambo wasiyoelewa, na wao wenyewe ndio hufanya sehemu kubwa ya kazi ya kuiendesha shule. Mfumo huo wa kutafuta mbinu mpya za kuanzisha mambo—uliofanyizwa kwa njia maalumu kutimiza mahitaji ya jumuiya maskini za mashambani—unajaribiwa katika nchi nyingine nyingi.

Maelfu ya kilometa kutoka Kolombia, katika jiji kubwa moja la Asia, huishi mvulana mwingine mwenye akili wa miaka 11, jina lake Melinda. Hivi majuzi ameacha shule ili atumie saa 12 kwa siku achokorechokore moja la marundo makubwa ya takataka za jiji kutafuta vikorokoro vya vyuma na plastiki. “Mimi nataka kusaidia baba yangu ili tupate mlo kila siku,” asema Melinda. “Kama nisingemsaidia, huenda ikawa tusingeweza kujiambulia chakula.” Hata siku iwapo na matokeo mazuri, yeye huleta nyumbani theluthi moja tu ya dola moja.

Watoto Walio Wafanyakazi wa Afya

Katika viunga vya jiji la India la Bombay kuna mji wa vijengo na vijumba hafifu uitwao Malvani, ambako ugonjwa umekuwako tangu jadi. Hatimaye mambo yanakuwa nafuu, kwa msaada wa wafanyakazi wa afya wenye bidii kama Neetu na Aziz. Wao huzuru familia mbalimbali kuchunguza kama watoto wadogo wamechanjwa, au kama wana ugonjwa wa kuhara, upele, au upungufu wa damu. Neetu na Aziz wana miaka 11 tu. Walijitolea kufanya kazi katika programu ambamo watoto hugawiwa kuangalia afya ya watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano. Kwa sababu ya jitihada za Neetu na Aziz—na jitihada za watoto wengine wengi kama wao—karibu watoto wote wa Malvani wamechanjwa, wazazi walio wengi wajua jinsi ya kutumia utibabu wa kurudisha maji mwilini kupitia mdomoni, na kanuni za afya za ujumla zimepata maendeleo.

Ulimwenguni pote, hatua kubwa sana zinapigwa ili kuwachanja watoto wadogo dhidi ya magonjwa yaliyo ya kawaida sana. (Ona chati katika ukurasa 8.) Sasa Bangladesh imechanja zaidi ya asilimia 70 ya vitoto vyayo vichanga, na China imechanja zaidi sana ya asilimia 95. Kama kila nchi inayositawi ingeweza kufikia asilimia 90, wastadi wa afya waamini kwamba kungekuwa na kinga ya kijumuiya. Walio wengi sana wakiisha kuchanjwa, huwa ni vigumu zaidi ugonjwa huo kupitishwa kwa wengine.

Umaskini, Vita, na UKIMWI

Hata hivyo, jambo la kuhuzunisha ni kwamba ingawa hatua kubwa inapigwa katika utunzaji wa afya na elimu, matatizo mengine yabaki yakiwa yameimarika sana. Matatu kati ya yale yanayotatiza sana kung’olewa ni umaskini, vita, na UKIMWI.

Katika miaka ya majuzi maskini wa ulimwengu wamekuwa wakizidi kuwa maskini. Mapato katika maeneo fukara ya Afrika na Amerika ya Kilatini yamepungua kwa asilimia 10 au zaidi katika mwongo uliopita. Wazazi katika mabara hayo—ambako asilimia 75 ya mapato ya familia hutumiwa kwa chakula—hawawezi kamwe kuwapa watoto wao chakula chenye usawaziko.

‘Wape watoto mboga na ndizi,’ akaambiwa Grace kwenye kliniki yao ya afya. Lakini Grace, ambaye ni mama mwenye watoto kumi, aishiye Afrika Mashariki, hana fedha za kutumia kwa chakula, na hakuna maji ya kutosha ili akuze mimea hiyo katika kisehemu cha kumi tu cha hektari moja cha kiwanja cha familia. Hawana la kufanya ila kuishi na shida ya kula mahindi na maharagwe na kukaa njaa nyakati fulani. Ikiwa mielekeo ya wakati uliopo itaendelea, haielekei matazamio yatapata nafuu kwa familia ya Grace wala kwa mamilioni ya nyinginezo zilizo kama yake.

Ijapokuwa watoto wa Grace ni maskini hivyo, bado wao ni afadhali kuliko Kim Seng wa Kusini-Mashariki mwa Asia, ambaye baba yake aliuawa katika vita ya wenyeji kwa wenyeji kisha mama yake akafa njaa. Kim Seng, ambaye pia karibu afe kwa sababu ya utapiamlo, hatimaye alipata hifadhi katika kambi ya wakimbizi. Wengi wa wale watoto milioni tano ambao hukaa wakinyong’onyea katika kambi za wakimbizi ulimwenguni pote wameteswa na magumu kama hayo.

Mwanzoni mwa karne hii, ni asilimia 5 tu ya majeruhi wa vita waliokuwa raia. Sasa tarakimu hiyo imevuvumka kuwa asilimia 80, na walio wengi wa majeruhi hao wa vita ni wanawake au watoto. Wale ambao huenda wakaponyoka maumizo ya kimwili bado huteseka kihisia-moyo. “Siwezi kusahau jinsi mama yangu alivyouawa,” asema mtoto mkimbizi mmoja kutoka nchi moja kusini-kati mwa Afrika. “Walimshika mama yangu kwa nguvu wakamtenda mabaya. Baadaye walimfungafunga na kumchoma kwa kisu. . . . Nyakati fulani mimi huota juu ya jambo hilo.”

Mapigano yenye jeuri yafulizapo kufokafoka katika nchi moja baada ya nyingine, yaonekana haiepukiki kwamba watoto wasio na hatia wataendelea kuteswa na madhara ya vita. Zaidi ya hilo, msukosuko wa kimataifa hudhuru pia watoto wasiohusika moja kwa moja katika hayo mapigano. Majeshi humeza mapesa ambayo yangeweza kutumiwa kuandaa elimu, kanuni za kuondoa takataka, na utunzaji wa afya ulio bora zaidi. Matumizi ya kijeshi yafanywayo na nchi zenye viwanda ulimwenguni ni zaidi ya jumla ya mapato ya kila mwaka ya nusu ya wanadamu walio maskini zaidi. Hata katika nchi 46 za ulimwengu zilizo maskini zaidi ulimwenguni, kiasi cha fedha ambacho wao hutumia kwa mashine za kijeshi kinalingana na kiasi watumiacho kwa afya na elimu zikiwa pamoja.

Mbali na umaskini na vita, muuaji mwingine huwanyemelea watoto wa ulimwengu. Katika miaka ya 1980, ambapo maendeleo makubwa yalikuwa yakifanywa katika pambano dhidi ya surua, pepopunda, na ugonjwa wa kuhara, tatanisho jipya la afya liliibuka: UKIMWI. Shirika la Afya Ulimwenguni lakadiria kwamba kufikia mwaka 2000, watoto milioni kumi watakuwa wameambukizwa. Walio wengi kati yao hawatatimiza kamwe umri wa miaka miwili, na itakuwa vigumu wowote kati yao kuishi zaidi ya miaka mitano. “Hatua isipochukuliwa karibuni, UKIMWI watisha kufutilia mbali maendeleo yote ambayo tumefanya katika kuokoa watoto muda wa miaka 10 iliyopita,” aomboleza Dakt. Reginald Boulos, daktari wa watoto wa Haiti.

Kutokana na pitio fupi hilo, ni wazi kwamba ijapokuwa mambo fulani ya kusifika yamefanywa, ile shabaha ya ‘kumpa kila mtoto wakati ujao ulio bora’ yabaki kuwa kibarua kigumu mno. Je! kuna tumaini lolote kwamba siku moja hiyo ndoto itatimizwa?

[Maelezo ya Chini]

a Utibabu wa kurudisha maji mwilini kupitia mdomoni huandalia watoto umajimaji, chumvi, na glukosi ambavyo vyahitajiwa kuzuia athari za ugonjwa wa kuhara za kukausha maji mwilini na kuleta kifo. Shirika la Afya Ulimwenguni liliripoti katika 1990 kwamba uhai wa watu zaidi ya milioni moja kwa mwaka unaokolewa na mbinu hiyo. Kwa maelezo zaidi, ona toleo la Februari 8, 1987 la Amkeni!, kurasa 21-23.

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

Miradi kwa Miaka ya 1990: —Takwa Gumu la Kuwaokoa Watoto

Yale mataifa yenye kuhudhuria Mkutano wa Viongozi wa Ulimwengu Kuhusu Watoto yalijitia katika wajibu wa mambo kadhaa magumu. Haya ndiyo watumainiyo kuyatimiza kufikia mwaka 2000.

Chanjo. Programu za chanjo wakati uliopo huokoa watoto milioni tatu kila mwaka. Lakini wengine milioni mbili wangali wanakufa. Kwa kuchanja asilimia 90 au zaidi kati ya watoto wa ulimwengu dhidi ya magonjwa yaliyo ya kawaida sana, vingi vya vifo hivyo vingeweza kuepukwa.

Elimu. Katika miaka ya 1980, kwa kweli idadi ya wenye kujiandikisha kwenda shule ilipungua katika nyingi za nchi zilizo maskini zaidi za ulimwengu. Mradi ni kugeuza mwelekeo huo na kuhakikisha kwamba kufikia mwisho wa mwongo huu, kila mtoto atakuwa na nafasi ya kwenda shuleni.

Utapiamlo. Maofisa wa Shirika la Hazina ya Watoto la Umoja wa Mataifa huamini kwamba “kukiwa na miongozo ifaayo, . . . sasa ulimwengu waweza kulisha watoto wote wa ulimwengu na kuweza kuondoa namna zilizo mbaya zaidi za utapiamlo.” Madokezo yalitolewa kupunguza nusu ya idadi ya watoto wenye utapiamlo wakati wa mwongo uliopo. Kutimiza jambo hilo kungeokoa watoto milioni 100 na maumivu makali ya njaa.

Maji safi na kanuni za kuondoa takataka. Katika 1987, Ripoti ya Brundtland ilieleza hivi: “Katika ulimwengu unaositawi, kionyeshi kizuri zaidi cha kiwango cha afya katika jumuiya ni wingi wa mabomba ya kuchotea maji wala si wingi wa vitanda hospitalini.” Kwa sasa watu zaidi ya bilioni moja hawawezi kupata maji safi, na idadi iliyo mara mbili ya hao hawana njia safi ya kuondolea mbali takataka. Shabaha ni kuandalia watu ulimwenguni pote njia ya kuweza kupata maji ya kunywa na njia safi ya kuondolea mbali takataka za kibinadamu.

Ulinzi. Katika mwongo uliopita, vita vimesababisha majeruhi ya watoto zaidi ya milioni tano. Watoto wengine milioni tano wamekoseshwa makao. Wakimbizi hao, na pia yale mamilioni ya watoto wa barabarani na watoto walio wafanyakazi, wahitaji ulinzi haraka. Mapatano Kuhusu Haki za Mtoto—sasa yakiwa yameidhinishwa na zaidi ya nchi mia moja—hujaribu kulinda watoto wote hao kutokana na jeuri na utumizi mbaya.

[Chati katika ukurasa wa 7]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

VISABABISHI VIKUU VYA VIFO VYA WATOTO

(Watoto wa Chini ya Miaka Mitano)

MAMILIONI YA VIFO KILA MWAKA (Makadirio ya 1990):

MILIONI 0.51 Kifaduro

MILIONI 0.79 Pepopunda ya wakati wa Kuzaliwa

MILIONI 1.0 Malaria

MILIONI 1.52 Surua (Ukambi)

MILIONI 2.2 Maambukizo Mengine ya Kupumua

MILIONI 4.0 Ugonjwa wa Namna ya Kuhara

MILIONI 4.2 Visababishi Vingine

Chanzo: WHO na UNICEF

[Chati katika ukurasa wa 8]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

MAENDELEO YA KUWACHANJA WATOTO KATIKA ULIMWENGU UNAOSITAWI 1980-1988

1980-1988

Asilimia ya watoto walio chini ya miezi 12 ambao wamechanjwa

MIAKA

1980 1988

DPT3* 24% 66%

UGONJWA

WA KUPOOZA 20% 66%

KIFUA KIKUU 29% 72%

UKAMBI 15% 59%

* DPT3: Chanjo ya muungano wa kinga ya DIPTERIA, KIFADURO, na PEPOPUNDA.

CHANZO: SHIRIKA LA AFYA ULIMWENGUNI na UNICEF (tarakimu za 1980 hazitii ndani China)

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 4]

Picha: Godo-Foto

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki