Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Maswali Kutoka Kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi—2012 | Desemba 15
    • Maswali Kutoka Kwa Wasomaji

      Kabla ya kupata ujuzi wa ile kweli, mimi na mke wangu tulitamani sana kupata mtoto, hivyo tulitumia mbinu ya kutunga mimba nje ya tumbo la uzazi, yaani, “in vitro fertilization.” Baadhi ya mayai yetu yaliyotungishwa (viini-tete) hayakutumiwa; yaligandishwa na kuhifadhiwa kwenye barafu. Je, ni lazima yaendelee kuhifadhiwa au yanaweza kuharibiwa?

      Jambo hili ni mojawapo ya mambo mazito ya kimaadili ambayo wenzi wa ndoa wanakabili wanapochagua kutungisha mimba nje ya tumbo la uzazi. Kila wenzi wa ndoa wanawajibika mbele za Yehova kuhusu uamuzi watakaofanya. Hata hivyo, inaweza kuwa rahisi kufanya uamuzi wakifahamu mambo fulani kuhusu mbinu hiyo isiyo ya asili ya kutungisha mimba.

      Mwaka wa 1978, mwanamke mmoja huko Uingereza alikuwa wa kwanza kubeba mimba iliyotungiwa kwenye maabara. Hangepata mimba kwa sababu mirija yake ya uzazi ilikuwa imeziba, hivyo shahawa hazingeweza kufikia mayai yake ya uzazi. Wataalamu wa kitiba walimfanyia upasuaji na kuchukua mayai yake yaliyokomaa, wakayatia katika bakuli la kioo, kisha wakayaunganisha na shahawa za mume wake. Kiini-tete kilichotokezwa kilitiwa ndani ya virutubishi ili kikue, kisha kikapandikizwa kwenye tumbo lake la uzazi. Baadaye, mwanamke huyo alijifungua mtoto msichana. Mbinu hiyo, na mbinu nyingine za aina hiyo zinaitwa katika Kiingereza in vitro fertilization (IVF), yaani, kutunga mimba nje ya tumbo la uzazi katika bakuli la kioo (vitro).

      Ingawa mbinu hiyo huwa tofauti katika nchi mbalimbali, kwa ujumla inahusisha mambo yafuatayo: Kwa majuma kadhaa, mke hupewa vidonge vya kuchochea vifuko vyake vya mayai (ovari) vitokeze mayai mengi. Huenda mume akaambiwa apige punyeto ili shahawa zitoke. Mayai na shahawa zilizosafishwa huunganishwa katika maabara. Mayai mengi yanaweza kutungishwa mimba na kuanza kugawanyika, kisha yanakuwa viini-tete vya kibinadamu. Baada ya siku moja hivi, viini-tete hivyo hukaguliwa kwa makini ili kutenganisha vile ambavyo vina kasoro na vile ambavyo vinaonekana havina kasoro na ambavyo vinaweza kujipandikiza katika tumbo la uzazi na kukua. Baada ya siku tatu hivi, kwa kawaida viini-tete viwili au vitatu vilivyo bora kabisa huingizwa ndani ya tumbo la uzazi la mke ili kuwe na uwezekano mkubwa zaidi wa kubeba mimba. Ikiwa kiini-tete kimoja au viwili vitajipandikiza katika tumbo la uzazi, basi, yeye ni mjamzito, na inatarajiwa kwamba atajifungua wakati ukifika.

      Lakini namna gani viini-tete vinavyobaki, kutia ndani vile vilivyoonekana kuwa vina kasoro au dhaifu? Viini-tete hivyo vya ziada vikiachwa, havitaendelea kuwa hai. Kwa hiyo, kabla havijafa, viini-tete hivyo vya ziada vinaweza kugandishwa katika umajimaji wa nitrojeni. Kwa nini? Endapo jaribio la kwanza la IVF halitafaulu, baadhi ya viini-tete hivyo vilivyohifadhiwa vinaweza kutumiwa katika jaribio lingine la IVF kwa bei nafuu. Hata hivyo, jambo hilo linatokeza masuala ya kimaadili. Kama wale wenzi wa ndoa waliouliza swali lililo mwanzoni, wengi hushindwa kuamua watafanyaje na viini-tete vyao vilivyogandishwa. Huenda hawahitaji watoto zaidi. Labda umri wa wazazi hao umesonga sana au hawawezi kugharimia jaribio lingine kama hilo la kupata mtoto. Huenda wanaogopa hatari zinazohusiana na kupata mimba za mapacha.a Au huenda mwenzi mmoja au wote wawili wakafa ama kuoa au kuolewa na mtu mwingine na hivyo kufanya hali iwe ngumu. Naam, kuna mambo mengi ya kuhangaikia, na hivyo wenzi fulani wa ndoa huendelea kugharimia hifadhi ya viini-tete kwa miaka mingi.

      Katika mwaka wa 2008, mtaalamu mmoja mkuu wa masuala ya viini-tete alisema katika gazeti la The New York Times kwamba wazazi wengi hawajui wafanye nini na viini-tete vilivyobaki. Makala hiyo ilisema hivi: “Angalau viini-tete 400,000 vinahifadhiwa katika kliniki nchini kote, na idadi hiyo inazidi kuongezeka kila siku . . . Viini-tete vinaweza kubaki hai kwa miaka kumi au zaidi ikiwa vitagandishwa vizuri lakini si vyote huendelea kuwa hai vinapoondolewa kwenye barafu.” (Italiki ni zetu.) Jambo hilo linafanya Wakristo watue kidogo na kufikiria. Kwa nini?

      Wenzi wa ndoa Wakristo wanaokabili masuala yanayohusu mbinu za IVF wanaweza kufikiria athari za hali nyingine ya kitiba. Huenda Mkristo akalazimika kuamua hatua ya kuchukua kuhusu mpendwa wake aliye mahututi na anayeishi kwa msaada wa mashine ya kutegemeza uhai, kama ile ya kumsaidia mgonjwa kupumua. Wakristo wa kweli hawaungi mkono wazo la kumwacha mgonjwa afe bila kutibiwa; wanathamini sana uhai kulingana na Kutoka 20:13 na Zaburi 36:9. Gazeti la Amkeni! la Kiingereza la Mei 8, 1974, lilisema hivi: “Kwa kuwa wanaheshimu maoni ya Mungu kuhusu utakatifu wa uhai, na kwa sababu ya dhamiri zao na kwa kuwa wanatii sheria za serikali, wale wanaotaka kuishi kupatana na kanuni za Biblia hawawezi kamwe kuruhusu madaktari waharakishe kifo cha mgonjwa asiyepona,” yaani, wakomeshe kimakusudi uhai wake. Hata hivyo, katika hali fulani uhai wa mgonjwa unategemezwa tu na mashine. Ni lazima watu wa familia waamue kama mgonjwa huyo atabaki katika mashine hiyo au la.

      Ni kweli kwamba hali hiyo haifanani na hali inayowakabili wenzi wa ndoa waliotumia mbinu ya IVF na ambao sasa wamehifadhi viini-tete. Lakini huenda wakapendekezewa waondoe viini-tete vilivyohifadhiwa katika nitrojeni, na kuviacha vife. Bila kugandishwa, viini-tete vinaweza kudhoofika na kufa. Wenzi hao wa ndoa watalazimika kuamua kama wataruhusu jambo hilo.—Gal. 6:7.

      Kwa kuwa wenzi wa ndoa waliamua wenyewe kutumia mbinu ya IVF kupata mimba ili hatimaye wapate mtoto, huenda wakaamua kuendelea kulipia gharama ya kuhifadhi viini-tete vilivyogandishwa au kuvitumia baadaye kujaribu tena kupata mtoto. Hata hivyo, wenzi wengine wa ndoa huenda wakaamua kwamba wataacha kuvitunza viini-tete vilivyogandishwa, wakiona kuwa viko hai tu kwa sababu vimehifadhiwa kwa njia isiyo ya asili. Wakristo wanaokabili uamuzi huo wanawajibika mbele za Mungu kutumia dhamiri yao iliyozoezwa na Biblia. Wangependa kuwa na dhamiri safi, bila kupuuza dhamiri za wengine.—1 Tim. 1:19.

      Wakristo wanaokabili uamuzi huo wanawajibika mbele za Mungu kutumia dhamiri yao iliyozoezwa na Biblia

      Mtaalamu mmoja wa tezi za homoni za uzazi aligundua kwamba wenzi wengi wa ndoa “walichanganyikiwa na pia kuathiriwa sana na daraka la kuamua jinsi watakavyoshughulikia viini-tete vyao [vilivyogandishwa].” Alifikia mkataa huu: “Kwa wenzi wengi wa ndoa, inaonekana kwamba hakuna uamuzi mzuri.”

      Ni wazi kwamba Wakristo wa kweli wanaofikiria kutumia mbinu ya IVF wanapaswa kuchanganua mambo yote mazito yanayohusiana na mbinu hiyo. Biblia inashauri hivi: “Mtu mwerevu huona hatari na kujificha, lakini wajinga wanaendelea mbele na kuumia.”—Met. 22:3, NET Bible.

  • Maswali Kutoka Kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi—2012 | Desemba 15
    • a Namna gani ikiwa kijusi kinachokua tumboni kinaonekana kuwa na kasoro au viini-tete kadhaa vimepandikizwa tumboni? Kuua vijusi hivyo kimakusudi ni kutoa mimba. Ni jambo la kawaida kupata mimba za mapacha (wawili, watatu, au zaidi) unapotumia mbinu ya IVF, na hilo huongeza hatari kama vile mama kujifungua kabla ya wakati na kuvuja damu nyingi. Mwanamke aliyebeba vijusi vingi tumboni anaweza kuambiwa “achague vijusi vinavyofaa,” ili kijusi kimoja au kadhaa viuawe. Huo utakuwa utoaji mimba wa kukusudia, ambao ni sawa na kuua.—Kut. 21:22, 23; Zab. 139:16.

  • Maswali Kutoka Kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi—2012 | Desemba 15
Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki