Je, Wewe Huhukumu kwa Kutazama Sura?
JE, WEWE huhukumu kitabu kwa kutegemea jalada lake? Ungeweza kupumbazwa. Ili kuepuka hilo, kwanza unatazama yaliyomo ndani ya kitabu hicho. Jambo hili latolewa kielezi na kisa cha mhusika mashuhuri kutoka sanaa-jadiiya ya Kituruki, Nasreddin Hoja (Neno la Kituruki hoja lamaanisha “mwalimu.”) Yeye “ni mjanja na mshamba, mwenye hekima na mpumbavu . . . . Ni mchaji, lakini ana mapungukiwa ya kibinadamu.” Yeye “hashindwi na hali zisizo za kawaida na zisizofaa maishani.”—Tales of the Hoja, cha John Noonan, Aramco World, Septemba-Oktoba 1997.
Hadithi moja husimuliwa kuhusu safari aliyofunga kuzuru ofisa Mturuki na kula mlo wa mchana pamoja naye. “Akiwa na wasiwasi, [Nasreddin] alishuka kutoka kwa punda na kubisha mlango wa mbele wenye kuvutia. Ulipofunguliwa, aliona kwamba tayari karamu ilikuwa inaendelea. Lakini kabla ya kujitambulisha, mkaribishaji wake, akitazama nguo zake za safari zilizochafuka, alimkatiza bila adabu kwa kumwambia kwamba waombaji hawakukaribishwa.”
Nasreddin aliondoka, akaenda kwenye mfuko wa matandiko yake, na “akabadili kwa kujivika vazi lake lililo bora zaidi: kanzu ya hariri yenye fahari iliyorembwa kwa manyoya, na kilemba kikubwa cha hariri. Akiwa amepambwa hivyo, alirudi kwenye mlango wa mbele na kubisha tena.
“Wakati huu, mkaribishaji wake alimkaribisha kwa uchangamfu . . . Watumishi wakamwandalia chakula kitamu. Nasreddin Hoja akamwaga bakuli ya mchuzi ndani ya mmoja wa mifuko ya kanzu lake. Kwa mshangao wa wageni-waalikwa wengine, alitia vipande vya nyama iliyochomwa ndani ya mikunjo ya kilemba chake. Kisha, akiwa mbele ya mkaribishaji wake aliyeshtuka, alisukuma upande wa vazi lake uliokuwa na manyoya ndani ya sahani ya pilau, akinong’ona ‘Kula, manyoya, kula!’
“‘Jambo hili lamaanisha nini?’ akadai mkaribishaji.
“‘Bwana wangu mpendwa,’ akajibu huyo Hoja, ‘nayalisha mavazi yangu. Kulingana na jinsi ulivyonitendea nusu saa iliyopita, ni wazi kwamba mavazi yangu, na sio mimi, ndiyo madhumuni yako ya ukaribishaji-wageni!’”
Ni mara nyingi kadiri gani sisi huhukumu kwa njia inayofaa au isiyofaa kwa kutazama sura peke yake! Wakati nabii Samweli alipofikiri kuwa ndugu ya Daudi, Eliabu, lazima awe ndiye chaguo la Yehova la mfalme atakayefuata wa Israeli, Yehova alimwambia: “Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo.” (1 Samweli 16:7) Ndiyo, Yehova huhukumu kwa kutegemea hali ya moyo, si kwa kutazama sura. Wewe hufanyaje?
[Picha katika ukurasa wa 31]
Yehova alimwonya Samweli asipumbazwe na sura