Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Maktaba Funguo za Kupata Ujuzi
    Amkeni!—2005 | Mei 22
    • ‘Ensaiklopedia ya Kale ya Ujuzi wa Mwanadamu’

      Wazia kwamba uko katika nchi ya Mashariki ya Kati ambayo leo ni Iraq. Ni mwaka wa 650 K.W.K. Uko katika jiji la Ninawi lenye kuta ndefu (karibu na Mosul ya leo). Mbele yako kuna jengo kubwa la kifalme la Mfalme Ashurbanipali, mtawala wa Ashuru, Misri, na Babiloni.a Ukiwa umesimama karibu na mlango wa jumba hilo unawaona wanaume wakikokota magudulia ya udongo ndani ya jumba hilo. Wanaume hao wamerudi tu kutoka sehemu za mbali za ufalme wa Ashuru kwani wanajitahidi kukusanya kitabu chochote kinachozungumzia masuala ya kijamii, kitamaduni, na desturi mbalimbali za kidini za watu wanaoishi chini ya Mfalme Ashurbanipali. Unapofungua moja ya magudulia hayo unaona yamejaa mabamba ya udongo yenye umbo la mstatili na ambayo yana upana wa sentimeta 8 na urefu wa sentimeta 10 hivi.

      Unamfuata mwanamume mmoja ndani ya jumba hilo na kuwaona waandishi wenye kalamu za mfupa wakichora maumbo kama ya kabari katika mabamba madogo ya udongo wenye unyevu. Wanatafsiri hati za lugha ya kigeni katika Kiashuri. Baadaye, mabamba hayo yataokwa katika joko, na hivyo kuyahifadhi kabisa maandishi hayo. Maandishi hayo yanawekwa katika vyumba vyenye rafu nyingi ambazo zina mamia ya magudulia. Kwenye miimo ya milango ya vyumba hivyo, kuna mabamba yenye habari kuhusu maandishi yaliyohifadhiwa katika kila chumba. Mabamba ya udongo zaidi ya 20,000 katika maktaba hiyo yana habari kuhusu masuala ya biashara, desturi za kidini, sheria, historia, tiba, na fiziolojia ya binadamu na wanyama, nayo hufanyiza kile ambacho msomi mmoja alieleza kuwa “ensaiklopedia ya ujuzi wa mwanadamu.”

      Maktaba Nyingine Kabla na Baada ya Ile ya Ninawi

      Kulikuwa na maktaba nyingine kubwa kabla ya ile ya Ashurbanipali huko Ninawi. Mfalme Hammurabi alijenga maktaba katika jiji la Borsippa, la Babiloni miaka elfu moja kabla ya Ashurbanipali. Ramesesi wa Pili alianzisha maktaba maarufu katika jiji la Thebesi, Misri, zaidi ya miaka 700 kabla ya Ashurbanipali. Lakini maktaba ya Ashurbanipali ndiyo maktaba “kubwa zaidi katika ulimwengu wa kale” kwa sababu ilikuwa na habari za aina nyingi na rekodi nyingi sana. Miaka 350 ilipita kabla maktaba nyingine kubwa zaidi kujengwa.

  • Maktaba Funguo za Kupata Ujuzi
    Amkeni!—2005 | Mei 22
    • [Picha katika ukurasa wa 18]

      Mfalme Ashurbanipali wa Ashuru, ambaye maktaba yake ilikuwa na mabamba ya kikabari ya udongo, mwaka wa 650 K.W.K.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki