Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Mtoto Aliyeitwa Maskini
    Amkeni!—1998 | Juni 8
    • Mtoto Aliyeitwa Maskini

      KATIKA kijiji kimoja kidogo cha Kiafrika, mwanamume mmoja aliyeitwa Okot na mke wake, Matina, walifurahia kuzaliwa kwa mtoto wao wa kwanza, aliyekuwa binti. Jamaa na marafiki walisafiri hadi kijijini ili kupeleka zawadi na kumtakia mtoto huyo maisha marefu na yenye furaha.

      Wenzi hao waliishi maisha magumu na ya umaskini. Walilima shamba dogo, na nyumba yao ambamo alijifungulia Matina, ilikuwa ya matope na paa ya nyasi. Waliazimia kufanya kazi kwa bidii ili mtoto wao wa kwanza asipate magumu kama wao. Ili kujikumbusha mradi huu, walimwita binti yao Acan, linalomaanisha “Mimi Ni Maskini.”

      Kuna wakati ujao wa aina gani kwa Acan? Ikiwa maisha yake yatafuata kigezo cha maisha ya wengi katika nchi yao, huenda asijifunze kamwe kusoma na kuandika. Atakapokuwa mtu mzima, ikiwa atapata kazi, aweza kupata mshahara unaokaribia dola 190 tu kwa mwaka. Katika nchi yao, matarajio ya muda wa kuishi ni miaka 42 pekee.

      Hali mbaya ya Acan si ya kipekee. Kati ya watu wanaokaribia bilioni 6 duniani, wapatao bilioni 1.3 hupata pesa zipunguazo dola 370 kwa mwaka. Wastani katika nchi tajiri ni dola 21,598. Kila siku, watu 67,000 zaidi hujiunga na umati wa maskini, karibu milioni 25 kila mwaka. Wengi huishi katika nchi zinazositawi—katika Afrika, Asia, na Amerika ya Latini. Lakini hata katika mataifa tajiri, kuna sehemu ndogo-ndogo zilizo na umaskini. Na watu 7 kati ya 10 miongoni mwa walio maskini zaidi ulimwenguni ni wa kike.

      Watu wengi hawaepuki ufukara kamwe. Huwanyima mahitaji yao yaliyo ya msingi zaidi—chakula, mavazi, na makao. Unaweza kuwapokonya uhuru, adhama, elimu, na afya njema. Shirika la Afya Ulimwenguni lasema: “Umaskini hutawala kwa njia yenye kuharibu kila hatua ya maisha ya binadamu, kuanzia wakati wa utungaji wa mimba hadi kaburini. Huungana na maradhi hatari zaidi na yenye maumivu zaidi ili kusababisha maisha duni kwa wote wanaoteseka kutokana nao.”

      Lakini je, kiwango cha maisha hakiendelei kuboreka katika mataifa yanayositawi? Katika baadhi ya mataifa hayo, ndiyo. Katika mengine mengi, sivyo. Gazeti la ukuzi wa kibinadamu Choices hufafanua wazo la kwamba “pengo kati ya maskini na matajiri linapungua kwa sababu hali ya maskini inaboreka” kuwa ‘ngano hatari.’ Badala yake linataarifu: “Twaishi katika ulimwengu ambao kwa kweli umegawanyika kiuchumi, miongoni mwa nchi na ndani ya nchi hizo.”

      Je, umaskini utaendelea kutaabisha jamii ya kibinadamu milele? Katika makala mbili zifuatazo, Amkeni! yachunguza habari hii iliyo tata na kuonyesha utatuzi utakuwa nini.

  • Wafungwa wa Umaskini
    Amkeni!—1998 | Juni 8
    • Njaa na Utapiamlo

      Ayembe, anayeishi Zaire, ana washiriki wa familia 15 ambao humtegemea. Nyakati nyingine familia inaweza kufaulu kula mara moja kwa siku—uji wa mahindi uliokolezwa kwa majani ya mhogo, chumvi na sukari. Nyakati nyingine hawana chochote cha kula kwa siku mbili au tatu. “Mimi hungoja mpaka watoto walie kabla ya kupika,” asema Ayembe.

      Hali yao ni ya kawaida. Katika nchi zinazositawi, mtu 1 kati ya 5 hulala njaa kila usiku. Ulimwenguni pote, karibu watu milioni 800—milioni 200 kati yao wakiwa watoto—hawapati chakula cha kutosha daima. Watoto hawa hawakui kwa njia ya kawaida; mara nyingi huwa wagonjwa. Wao hufanya vibaya shuleni. Wakiwa watu wazima, hupatwa na matokeo ya mambo haya. Hivyo, mara nyingi umaskini huongoza kwenye utapiamlo, ambao nao pia huchangia umaskini.

      Umaskini, njaa kali, na utapiamlo umeenea sana hivi kwamba hushinda jitihada za kisiasa, kiuchumi, na kijamii kuuondoa. Kwa kweli, hali haiboreki bali yawa mbaya zaidi.

      Afya Mbaya

      Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, umaskini ndio “maradhi yenye kufisha zaidi ulimwenguni” na “kisababishi kikuu zaidi cha kifo, maradhi na kuteseka.”

      Kitabu An Urbanizing World: Global Report on Human Settlements, 1996 kilisema kwamba angalau watu milioni 600 katika Amerika ya Latini, Asia, na Afrika waliishi katika makao yaliyo mabaya sana—bila maji ya kutosha, usafi wa kutunza afya, na uondolewaji wa maji machafu—hivi kwamba maisha na afya yao yalitishwa daima. Ulimwenguni pote, zaidi ya watu bilioni moja hawana maji safi. Mamia ya mamilioni hawawezi kugharimia mlo kamili. Mambo haya yote hufanya iwe vigumu kwa maskini kuzuia maradhi.

      Mara nyingi maskini pia hushindwa kutibu maradhi. Maskini wanapokuwa wagonjwa, huenda wasiweze kugharimia dawa zinazofaa au matibabu. Maskini hufa wakiwa wachanga; wale wanaoendelea kuishi huenda wakaishi wakiwa na magonjwa ya kudumu.

      Zahida, mchuuzi mmoja wa sokoni katika Maldives asema: “Umaskini humaanisha afya mbaya, ambayo hukuzuia kufanya kazi.” Bila shaka, ukosefu wa kazi, huongezea umaskini unaopita kiasi. Tokeo huwa mzunguko wenye ukatili na wenye kufisha ambapo umaskini na ugonjwa huchocheana.

      Ukosefu wa Kazi ya Kuajiriwa na Malipo ya Chini

      Upande mwingine wa umaskini ni ukosefu wa kazi ya kuajiriwa. Tufeni pote, watu wapatao milioni 120 wawezao kufanya kazi hawawezi kupata kazi za kuajiriwa. Wakati uleule, karibu watu wengine milioni 700 mara nyingi hufanya kazi kwa muda wa saa nyingi kwa malipo ya chini sana yasiyoweza kutosheleza mahitaji yao ya msingi.

      Rudeen ni dereva wa tuk-tuk katika Kambodia. Asema: “Kwa upande wangu umaskini humaanisha kufanya kazi kwa zaidi ya saa 18 kwa siku, lakini bado sichumi pesa za kutosha kujilisha mwenyewe, mke wangu na watoto wangu wawili.”

      Uharibifu wa Mazingira

      Jambo linaloambatana na umaskini ni kuharibiwa kwa mazingira. Alionelea Elsa, mtafiti katika Guyana, Amerika Kusini: “Umaskini ni uharibifu wa asili: msitu, bara, wanyama, mito na maziwa.” Huu ni mzunguko mwingine wenye kuhuzunisha—umaskini huongoza kwenye uharibifu wa mazingira, ambao huendeleza umaskini unaozidi.

      Kulima shamba ambalo lafaa kukuza mazao mpaka linapokosa rutuba au kutumiwa kwa kusudi jingine ni zoea la zamani za kale. Ndivyo na—ukataji wa misitu kwa ajili ya mbao au fueli au kwa ajili ya kupanda mazao. Kwa sababu ya ongezeko la watu duniani, hali imefikia viwango vya hatari.

      Kulingana na Hazina ya Kimataifa ya Maendeleo ya Kilimo, katika miaka 30 iliyopita, karibu asilimia 20 ya udongo ulio juu ya ardhi wa kukuzia mazao haufai tena kutumika, hasa kwa sababu ya ukosefu wa pesa na tekinolojia inayohitajiwa ili kutekeleza hatua za kuhifadhi. Wakati wa kipindi hicho hicho, mamilioni ya ekari yamekuwa ardhi kame kwa sababu ya kujengwa vibaya na kutodumishwa kwa mifumo ya unyunyiziaji wa maji. Na mamilioni ya ekari za misitu inakatwa kila mwaka ili kutokeza ardhi kwa ajili ya mazao au kupata mbao kwa ajili ya magogo au fueli.

      Uharibifu huu huhusiana na umaskini katika njia mbili. Kwanza, mara nyingi maskini hulazimishwa kuharibu mazingira kwa sababu ya mahitaji yao ya chakula na fueli. Mtu awezaje kuzungumza kuhusu ukuzi unaotegemea maliasili au hali-njema ya vizazi vya wakati ujao, kwa wale walio na njaa na maskini na ambao hulazimika kuharibu maliasili ili kujiendeleza kwa sasa? Pili, mara nyingi matajiri hutumia kwa kujifaidi mali za mazingira za maskini. Kwa hiyo kuharibiwa kwa maliasili na matajiri na maskini huongeza umaskini.

      Elimu

      Alicia, mfanyakazi wa jamii wa mjini katika Filipino, alitaarifu: “Upande mwingine wa umaskini ni mwanamke kuwatuma watoto wake barabarani kuomba-omba badala ya kuwapeleka shuleni kwa sababu kama sivyo hakutakuwa na chochote cha kula. Mama huyo ajua anarudia mzunguko uliomnasa, lakini hakuna njia ya kuponyoka umaskini anayoweza kuona.”

      Watoto wapatao milioni 500 hawapati nafasi za shule. Watu wazima bilioni moja hawana elimu ya kutosha. Bila elimu ni vigumu kupata kazi nzuri ya kuajiriwa. Kwa hiyo umaskini hutokeza ukosefu wa elimu, ambao hutokeza umaskini zaidi.

      Makao

      Kuna ukosefu wa makao katika mataifa maskini, na hata katika mengine yaliyo na mali. Ripoti moja husema kwamba karibu robo milioni ya wakazi wa New York City wamepata kuishi katika makao ya wasiokuwa na makao kwa muda fulani katika miaka mitano iliyopita. Ulaya pia ina maskini wake. Katika London karibu 400,000 wamesajiliwa kuwa hawana makao. Katika Ufaransa watu nusu milioni hawana makao.

      Kotekote katika nchi zinazositawi, hali ni mbaya zaidi. Watu humiminika mijini na majijini, wakivutiwa na ndoto za chakula, kazi za kuajiriwa, na maisha bora. Katika majiji fulani, zaidi ya asilimia 60 ya watu huishi katika mitaa ya vibanda. Hivyo umaskini wa mashambani huchochea umaskini wa mjini.

      Idadi ya Watu

      Jambo linalozidisha matatizo haya yote ni ukuzi wa idadi ya watu. Idadi ya watu ulimwenguni imeongezeka zaidi ya maradufu katika miaka 45 iliyopita. Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba tarakimu hiyo itapaa kufikia bilioni 6.2 ufikapo mwaka wa 2000 na kufikia bilioni 9.8 katika mwaka wa 2050. Sehemu zilizo maskini zaidi ulimwenguni ndizo zina viwango vya juu zaidi vya ukuzi wa idadi ya watu. Kati ya karibu watoto milioni 90 waliozaliwa katika mwaka wa 1995, milioni 85 walizaliwa katika nchi ambazo zina uwezo wa chini sana wa kuwaandalia.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki