Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 5/8 uku. 31
  • Jinsi ya Kuepuka Msiba wa Tufeni Pote

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Jinsi ya Kuepuka Msiba wa Tufeni Pote
  • Amkeni!—1999
  • Habari Zinazolingana
  • Umoja wa Mataifa—Njia Bora Zaidi?
    Amkeni!—1992
  • Jitihada Inayoendelea ya Kutafuta Suluhisho
    Amkeni!—2000
  • Kufanya Mimba Yako Iwe Salama Zaidi
    Amkeni!—2003
  • Watoto—Ni Faida au Ni Hasara?
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 5/8 uku. 31

Jinsi ya Kuepuka Msiba wa Tufeni Pote

UMOJA WA MATAIFA LINAUITA KWA KUFAA “MSIBA WA TUFENI POTE.” MWANAMKE HUFA KILA DAKIKA ULIMWENGUNI POTE KWA SABABU YA UJAUZITO NA KUJIFUNGUA.

Idadi kubwa ya vifo hivi hutukia katika nchi zinazositawi. Huku akiwa ni mwanamke 1 tu kati ya 10,000 anayekufa huko Ulaya kwa sababu zinazohusiana na ujauzito na 1 kati ya 12,500 Marekani, uwiano huo huongezeka hadi kufikia 1 kati ya 73 katika Amerika ya Latini, na 1 kati ya 54 katika Asia, na kiwango chenye kutisha cha 1 kati ya 21 katika Afrika!

Kwa kuwa idadi kubwa ya vifo hivi 600,000 vinavyotokea kila mwaka kwa sababu ya ujauzito vingeweza kuzuiwa kwa msaada wa wakunga wenye ustadi, shirika la Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa (UNICEF) na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) sasa yanakazia kuzoeza wanawake (na wanaume) wawe wakunga stadi.

Katika nchi zenye uhaba wa madaktari, wakunga waliozoezwa wanaweza kuokoa uhai. Dakt. France Donnay wa shirika la UNICEF na Anne Thompson mshauri wa shirika la WHO hivi majuzi walipokuwa wakihojiwa na shirika la Redio la Umoja wa Mataifa, walisema kwamba kuwapa wakunga waliozoezwa mamlaka zaidi tayari kumekuwa na matokeo. Kwa mfano, walisema kwamba katika nchi kadhaa za Kiafrika, vifo vya akina mama vilipungua sana wakati wakunga waliporuhusiwa kuondoa kondo za nyuma zilizobaki baada ya kujifungua. Maendeleo kama hayo yanafanywa Indonesia, ambako kuna mradi wa kuwazoeza wakunga wawili kwa kila kijiji. Kufikia sasa, wakunga wapatao 55,000 wamezoezwa.

“Katika nchi zilizositawi, ukunga pia unakaziwa,” kikasema kipindi cha Perspective kwenye shirika la Redio la Umoja wa Mataifa. Nchi kama vile Ufaransa, Uholanzi, Sweden, na Uingereza hazikuacha kamwe zoea la ukunga, na katika Marekani, ukunga unarejeshwa. Nchi hizi zinathamini wakunga, kwa sababu wanaandaa utunzaji wa kibinafsi na wa kuendelea, akasema Anne Thompson, ambaye pia ni mkunga aliyezoezwa. “Kwa vyovyote vile, uchungu wa uzazi waweza kuendelea kwa muda usio dhahiri hadi kufikia muda wa saa 24 na matabibu hawana wakati wa kusubiri tu kwa muda wa saa 24.” Lakini bado aliongezea kwamba, mojawapo ya sababu zinazochangia kujifungua kuliko salama ni “kuwapo kwa mtu mwenye kusikitika, mwenye uelewevu, na ufahamu na anayeweza kumtia moyo mwanamke anayejifungua.”

Kipindi cha Perspective kilionyesha pia kwamba “kila mwaka kunakuwa na visa milioni 60 vya kujifungua ambapo mwanamke hutunzwa na mshiriki wa familia, mkunga wa kienyeji asiyezoezwa—au bila mtu awaye yote.” Umoja wa Mataifa unajitahidi kubadilisha zoea hili. Ili kuanza, shirika la WHO lilichagua kichwa “Uzazi Salama” kwa ajili ya Siku ya Afya Ulimwenguni mwaka wa 1998. “Tunajua kwamba uzazi salama hautafikiwa katika miaka 2 au 3 ijayo,” akasema Dakt. Donnay. Ingawa hivyo, mradi wao ni kuwa na “mkunga mwenye ustadi kwa ajili ya kila mwanamke anayejifungua.”

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]

UN/J. Isaac

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki