-
Kwa Nini Kanisa Linapoteza Uvutano?Amkeni!—1996 | Aprili 8
-
-
Kwa Nini Kanisa Linapoteza Uvutano?
“Kila Mstoiki alikuwa Mstoiki; lakini yu wapi Mkristo katika Jumuiya ya Wakristo?”
RALPH WALDO EMERSON, MWANDIKAJI INSHA NA MSHAIRI MMAREKANI WA KARNE YA 19.
“MIMI ni Mkatoliki—lakini asiye mtendaji,” aeleza mama mmoja mchanga. “Sijishughulishi na dini,” aongeza tineja mmoja. Maelezo yao ni ya kawaida sana miongoni mwa kizazi kichanga cha watu wa Ulaya. Ingawa wazazi wao—au yaelekea zaidi wazazi-wakuu wao—bado ni waenda-kanisani, imani ya kidini haijaziba pengo la kizazi.
Kwa nini mazoea ya kidini yaliyoheshimiwa sana na vizazi vya watu wa Ulaya yameachwa?
Hofu Si Kichocheo Tena
Kwa karne nyingi hofu ya moto wa helo au purgatori ilikuwa na uvutano wenye nguvu kwa watu wa Ulaya. Mahubiri yenye hisia mno na michoro ya kanisa inayoonyesha wazi helo iwakayo isiyoweza kuzimika iliwasadikisha watu wa kawaida kwamba ni uhudhuriaji kanisa wenye staha tu utakaowaokoa kutokana na hukumu. Catechism of the Catholic Church huendelea kutaarifu kwamba “Kanisa huwajibisha waumini ‘kushiriki katika Ushirika Mtakatifu Jumapili na sherehe za kidini.’”a Katika maeneo ya mashambani msongo wa kijamii pia ulikuwa wa kadiri kubwa—kila mtu alitarajiwa kuhudhuria kanisa kila Jumapili.
Lakini nyakati zimebadilika. Watu sasa wajihisi huru kufanya watakalo. Hofu si kichocheo tena. Kanisa limeacha kimya-kimya kukazia fundisho la helo, kwa kuwa Wakatoliki wengi wa Ulaya hata hawaliamini.
Kwa uhakika, ile “dhambi” ya kukosa kuhudhuria Misa ya Jumapili haionwi tena kuwa nzito. Tirso Vaquero, kasisi Mkatoliki katika Madrid, Hispania, akiri: “Mkristo [Mkatoliki] akikosa kuja kwenye Misa Jumapili, tunasikitika kwa unyoofu kwa sababu amepoteza muda huu wa mawasiliano pamoja na Mungu na ndugu zake, si kwa sababu ametenda dhambi. Hilo si jambo la maana sana.”
Kwa hiyo hofu haichochei ujitoaji tena. Namna gani mamlaka ya maadili ya kanisa na viongozi walo—je, wanaweza kudai uaminifu-mshikamanifu wa makundi yao?
Tatizo la Mamlaka
Kukoma kwa hofu ya kidini kumepatana na mzoroto wenye kutokeza katika hali ya maadili ya kanisa. “Kwa karne nyingi tumekuwa na . . . walimu wengi sana wa maadili na walimu wachache sana wenye adili,” alalamika mwanahistoria Mwitalia Giordano Bruno Guerri. Ukosefu huu wa uongozi wa maadili ulionyeshwa wazi na vile vita viwili vya ulimwengu vilivyoharibu Jumuiya ya Wakristo. Makanisa ya Ulaya hayakuwa na uwezo wa kuzuia waumini kujiingiza katika pindi hiyo yenye umwagikaji damu. Vibaya hata zaidi, makanisa yalijihusisha sana katika jitihada za vita—pande zote mbili.
“Vita ya Ulimwengu ya Kwanza, iliyokuwa vita ya wenyewe kwa wenyewe miongoni mwa mafarakano ya Kikristo, ilifungua kipindi cha msiba na aibu kwa Ukristo,” aonelea mwanahistoria Paul Johnson. “Vita ya Ulimwengu ya Pili ilitokeza mashambulizi yenye kuhuzunisha hata zaidi kwa hali ya maadili ya imani ya Kikristo kuliko ile ya Kwanza. Ilifunua ukosefu wa uvutano wa makanisa katika Ujerumani, chanzo cha yale Marekebisho Makubwa ya Kidini, na woga na ubinafsi wa Makao Matakatifu ya papa.”
Mikataba ya Vatikani pamoja na utawala wa Nazi wa Hitler na serikali za Ufashisti za Mussolini katika Italia na Franco katika Hispania pia ziliharibu mamlaka ya maadili ya kanisa. Hatimaye, gharama ya kidini kwa manufaa hiyo ya kisiasa ilikuwa upotezo wa sifa ya ustahili.
Kanisa na Serikali —Kukifungua Hicho Kifungo
Katika karne ya 20, nchi nyingi za Ulaya mwishowe zimefungua kile kifungo kinachounganisha Kanisa na Serikali. Kwa hakika, hakuna nchi yoyote kubwa ya Ulaya inayotambua sasa Ukatoliki wa Kiroma kuwa dini yayo rasmi.
Ingawa huenda bado makanisa makuu yakasaidiwa kifedha na serikali, yamepoteza uvutano wa kisiasa yaliyokuwa nao. Si makasisi wote wamekubali uhalisi huu mpya. Myesuiti mashuhuri Mhispania José María Díez-Alegría aamini kwamba “viongozi wa kanisa [Katoliki] hufikiri—wengi wao kwa unyoofu wote—kwamba hawawezi kutimiza wajibu wao wa kidini bila utegemezo wa serikali.”
Lakini huu utegemezo wa serikali umeporomoka. Hispania, ambayo ilikuwa na serikali ya “kitaifa ya Kikatoliki” tangu 1975 hutolea kielelezo hali hii. Katika miaka ya majuzi mamlaka ya kanisa ya Hispania imekuwa na pigano lenye kuendelea na serikali ya Kisoshalisti kuhusu kutegemeza kanisa kifedha. Askofu wa Teruel, Hispania, hivi majuzi alilalamika kwa wanaparishi wake kwamba ahisi “kunyanyaswa akiwa Mkatoliki” kwa sababu serikali ya Hispania haitolei kanisa utegemezo wa kutosha wa kifedha.
Katika 1990 maaskofu wa Hispania walitangaza kwamba jamii ya Kihispania ilikuwa ikiathiriwa na “tatizo zito sana la dhamiri na adili.” Walimlaumu nani kwa hilo ‘tatizo la maadili’? Hao maaskofu walidai kwamba mojawapo visababishi vikuu kilikuwa “mtazamo wa kiakili wenye shaka unaochochewa mara nyingi na mamlaka ya umma [serikali ya Hispania].” Kwa wazi, maaskofu hao wanatarajia serikali iunge mkono fundisho la Kikatoliki na vilevile kuandaa misaada ya kifedha.
Je, Makasisi Hutenda Yale Wanayohubiri?
Utajiri mkubwa sana wa Kanisa Katoliki sikuzote umekuwa aibu kwa makasisi wanaofanya kazi katika parishi maskini. Iliaibisha hata zaidi wakati Banki ya Vatikani ilipopasishwa hatia katika kile gazeti Time liliita “kashifa mbaya kuliko zote katika Italia ya baada ya vita.” Katika 1987, amri zilitolewa na mahakimu wa Italia za kukamatwa kwa askofu mkuu na maofisa wengine wawili wa banki ya Vatikani. Hata hivyo, kwa sababu ya hadhi ya kipekee ya enzi ya Vatikani, makasisi walioshtakiwa waliepuka kukamatwa. Banki ya Vatikani ilisisitiza kwamba hakuna kosa lililotendwa lakini ilishindwa kufuta wazo la kwamba kanisa halikuwa likitenda yale lifundishayo.—Linganisha Mathayo 23:3.
Mwenendo mbaya wa kingono wenye kutangazwa sana umetokeza madhara hata zaidi. Katika Mei 1992 askofu mmoja wa Ireland, ajulikanaye sana kwa kuunga mkono useja, aliomba dayosisi yake “imsamehe” na “kumwombea.” Alilazimishwa kujiuzulu baada ya kufunuliwa kwamba alikuwa baba ya mvulana mwenye umri wa miaka 17 na alikuwa ametumia fedha za kanisa kumlipia elimu. Mwezi mmoja mapema kasisi Mkatoliki alitokea kwenye televisheni ya Ujerumani pamoja na “mwandamani” wake na watoto wao wawili. Yeye alisema alitamani “kufungua mazungumzo” juu ya suala la hayo mahusiano ya kisiri ambayo makasisi wengi sana huendeleza.
Kashifa hizo hazina budi kuacha alama yazo yenye kudumu. Mwanahistoria Guerri, katika kitabu chake Gli italiani sotto la Chiesa (Waitalia Walio Chini ya Kanisa), adai kwamba “kwa karne nyingi Kanisa limechukiza Waitalia.” Tokeo moja, yeye asema, ni “kusitawi kwa upingaji ulioenea wa uvutano wa makasisi kwa mambo ya kilimwengu, hata miongoni mwa waumini wenye msimamo mzuri.” Huenda Wakatoliki wenye kuchukizwa wakahisi kuuliza makasisi wao swali lilelile ambalo mtume Paulo aliwauliza Warumi: “Kwa kielelezo, wewe wahubiri dhidi ya wizi, lakini je, una uhakika juu ya ufuatiaji wa haki wako mwenyewe? Unashutumu zoea la uzinzi, lakini je, una uhakika juu ya usafi wako mwenyewe?”—Warumi 2:21, 22, Phillips.
Pengo Kati ya Makasisi na Watu wa Kawaida
Tatizo lisilo wazi sana lakini liwezalo kudhoofisha sana ni lile pengo kati ya makasisi na watu wa kawaida. Barua za miongozo ya kiroho kutoka kwa maaskofu yaonekana huudhi wanaparishi badala ya kuwafundisha. Katika uchunguzi mmoja wa Hispania, ni asilimia 28 tu ya wale waliohojiwa “walikubaliana na taarifa za maaskofu.” Idadi sawa na hiyo “haikujali hata kidogo,” na asilimia 18 ilisema kwamba “haikuelewa kile [maaskofu] walichokuwa wakizungumzia.” Askofu mkuu Ubeda wa Majorca, Hispania, alikiri: “Ni lazima sisi maaskofu tukubali lawama yetu ya kuhusika katika taratibu ya kugeuza watu kutokuwa Wakristo—jambo ambalo ni hakika.”
Ukosefu wa ujumbe ulio wazi wa Kimaandiko hutenga hata zaidi watu wa kawaida. Kulingana na Catholic Herald, “makasisi wengi [katika Ufaransa] wameamua kujiingiza katika mambo ya kisiasa ili ‘wafae,’” hata ingawa wengi wa wanaparishi wao wangewapendelea wakazie fikira mambo ya kiroho. Kasisi mmoja aliye pia mtaalamu wa elimu ya jamii Mwitalia Silvano Burgalassi akiri: “Labda [vijana] wamejitenga na Mungu kwa sababu ya kielelezo chetu kibaya. Tumewapatia mchanganyo wa kuridhiana, dini na biashara, ubinafsi na ughoshi.” Haishangazi kwamba makasisi wanapoteza hadhi yao ya kijamii. “Mimi ni Mkatoliki, lakini siamini katika makasisi” ni msemo unaosikiwa mara nyingi kutoka kwa Wahispania Wakatoliki.
Wakatoliki fulani huona ikiwa vigumu kueleza makasisi yaliyo mioyoni mwao, na wengine wana shaka nzito kuhusu mafundisho ya kanisa—hasa yale wanayoona kuwa yasiyo na kiasi au yasiyofanya kazi.
Mafundisho Yasiyoweza Kufahamika
Kielelezo kibaya kilicho wazi ni fundisho rasmi la Katoliki juu ya habari ya helo. Catechism of the Catholic Church hutaarifu: “Fundisho la Kanisa lathibitisha kuwapo kwa helo na umilele wayo.” Hata hivyo, uchunguzi wa hivi majuzi unaonyesha kwamba ni robo tu ya Wakatoliki Wafaransa na thuluthi ya wenzao Wahispania wanaoamini kwamba helo ipo.
Vivyohivyo, inapohusu masuala ya maadili, watu wa Ulaya huelekea kuwa “Wakristo wa fanya-mambo-yako-mwenyewe.” Mimmi, tineja Mlutheri kutoka Sweden, aamini kwamba maswali ya maadili, kama vile kuwa na watoto nje ya kifungo cha ndoa, ni “jambo la mtu kujiamulia.” Wakatoliki Wafaransa walio wengi watakubaliana naye. Wanapokabiliwa na maamuzi ya maana katika maisha, asilimia 80 ilisema kwamba ingefuata mwongozo wa dhamiri yayo badala ya ule wa kanisa.
Wakati uliopita mamlaka ya kanisa ilikuwa na nguvu ya kukomesha sauti yoyote ya kupinga. Kumekuwa na mabadiliko machache sana kulingana na maoni ya Vatikani. Catechism hutaarifu kwa uthabiti kwamba “yote ambayo yamesemwa kuhusu namna ya kufafanua Maandiko ni jambo la uamuzi wa Kanisa.” Hata hivyo, njia hiyo ya kimamlaka ya kushughulikia mambo haiungwi mkono hata kidogo. “Bishano la mamlaka huendelea bila kuzuiwa,” alalamika Antonio Elorza, profesa Mhispania wa mafunzo ya kisiasa. “Kanisa huchagua kujenga mnara uliozungushiwa ukuta, likiimarisha uhalali wa desturi zalo mbele ya historia kuwa usioweza kudhuriwa.” Nje ya huo “mnara uliozungushiwa ukuta,” uvutano wa kanisa na mamlaka yalo huendelea kufifia.
Kando na uchakavu wa kiroho, visababishi vya kijamii ni jambo jingine la maana linalochangia hali ya kutojali dini. Jamii yenye kuzingatia ununuaji wa vitu huandaa vitumbuizo vingi mno na fursa za tafrija—na watu wengi wa Ulaya wana tamaa na njia ya kuvifurahia. Kwa kulinganisha, kwenda kanisani huonekana kuwa njia yenye kuchosha ya kutumia asubuhi ya Jumapili. Isitoshe, ni mara chache sana ibada za kanisa huonekana kushughulikia mahitaji ya kiroho ya watu.
Haielekei kwamba dini ya kidesturi itapata mshiko wayo tena kwa kundi la Ulaya. Je, dini ni kani ya wakati uliopita—ikielekea kutoweka?
-
-
Je, Mwisho wa Dini Uko Karibu?Amkeni!—1996 | Aprili 8
-
-
Je, Mwisho wa Dini Uko Karibu?
“Dunia itajawa na kumjua BWANA, kama vile maji yanavyoifunika bahari.”
ISAYA, NABII MWISRAELI WA KARNE YA 8 K.W.K.
HIVYO nabii Mwebrania Isaya akatabiri kwamba siku moja kila mtu duniani ataunganishwa katika ibada ya Mungu Mweza Yote. Hata hivyo, leo taraja kama hilo huenda likaonwa kuwa mbali sana kuliko wakati mwingineo wote.
Kwa kielelezo, mapema katika karne hii, wanamapinduzi wa Kikomunisti katika Urusi waliamini kwamba uharibifu wa dini ulikuwa hatua muhimu ya kuweka huru makabwela. Wao walidai kwamba Uatheisti ‘ungeweka huru makabwela kutokana na mzigo wa upendeleo na madanganyo ya wakati uliopita.’ Kufikia 1939, Stalin alikuwa amepunguza idadi ya makanisa ya Othodoksi yaliyokuwa yakitenda katika Muungano wa Sovieti hadi 100, ikilinganishwa na zaidi ya 40,000 kabla ya 1917.
Hitler pia aliona dini kuwa kizuizi katika njia yake kuelekea mamlaka kamili. “Mtu apaswa kuwa ama Mkristo ama Mjerumani. Huwezi kuwa wote wawili,” akatangaza wakati mmoja. Yeye alikusudia kuondosha hatua kwa hatua namna zote za ibada ambazo hakuweza kuzidhibiti. Wakiwa na hilo akilini, Wanazi walianzisha sala zao wenyewe zinazofanana na za kidini, misherehekeo, ubatizo, na hata ibada za maziko. Hitler alikuwa mesiya wao, nayo nchi ilikuwa mungu wao. Ukatili wowote ungeweza kutendwa ikiwa ulikuwa mapenzi ya Hitler.
Je, Ni Siku za Mwisho za Dini?
Wala Stalin wala Hitler hawakufaulu katika kampeni zao za kukandamiza dini. Lakini sasa, yaonekana ubaridi wachukua daraka la kukandamiza dini. Kwa wanafunzi wa Biblia badiliko hili la matukio halishangazi. Mtume Paulo alimwambia Timotheo kwamba katika “siku za mwisho” watu wangekuwa “wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu.”—2 Timotheo 3:1-4.
Je, Biblia yafundisha kwamba katika hizi “siku za mwisho,” zilizo na hali ya kutojali ya kidini, zingekuwa mwanzo wa kukoma kwa dini zote? La. Badala ya kutabiri mwisho wa dini zote, Biblia hueleza kwamba dini isiyo ya kweli—ambayo imepewa jina la mfano Babiloni Mkubwa—itakoma.a Kitabu cha Ufunuo chasema hivi: “Na malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe, kama jiwe kubwa la kusagia, akalitupa katika bahari, akisema, Kama hivi, kwa nguvu nyingi, utatupwa Babeli [“Babiloni,” New World Translation], mji ule mkuu, wala hautaonekana tena kabisa.”—Ufunuo 18:21.
Hata hivyo, kutoweka kwa dini bandia hakutatokeza ulimwengu usiomhofu Mungu. Kinyume na hilo, Zaburi 22:27 hutoa unabii hivi: “Miisho yote ya dunia itakumbuka, na watu watamrejea BWANA; jamaa zote za mataifa watamsujudia.” Ebu wazia tu wakati ambapo “jamaa zote za mataifa” zitakapounganishwa pamoja katika kumwabudu Mungu mmoja wa kweli! Chini ya utawala wa Ufalme wa Mungu, ahadi hiyo nzuri ajabu itapata utimizo mtukufu. (Mathayo 6:10) Wakati huo ujapo, dini—dini ya kweli—itakuwa na umaana mkubwa. Lakini namna gani sasa?
Kujaza Utupu wa Kiroho
Utupu wa kiroho ulioenea sana katika Ulaya leo hufanana na hali katika Milki ya Roma ya karne ya kwanza. Mwanahistoria Will Durant afafanua jinsi Ukristo wa karne ya kwanza ulivyoshughulikia kwa mafanikio uhitaji wa kiroho wa wakati huo: “Katika utupu wa maadili wa upagani uliokuwa ukiisha, katika ubaridi wa Ustoiki na ufisadi wa Uepikureo, katika ulimwengu uliojaa ukali, ukatili, ukandamizaji, na mchafuko wa kingono, katika milki iliyowekwa chini ya utawala ambayo ilionekana kutohitaji tena uwezo wa kiume au miungu ya vita, [Ukristo] ulileta maadili mapya ya udugu, ufadhili, adabu, na amani.”
Utupu wa maadili na kiroho katika maisha ya watu katika wakati wetu waweza kujazwa kwa ujumbe uleule wenye nguvu uliohubiriwa kotekote katika Milki ya Roma na Wakristo wa mapema. Na kuna watu wanaosikia. Watu wengi wa Ulaya, ingawa kwa nje hawaonekani kuwa wa kidini, bado huhisi kwamba Mungu ana fungu muhimu katika maisha zao. Huenda hawahudhurii tena ibada za kidesturi za kanisa, hata hivyo wengine wamejaza utupu wao wa kiroho kwingineko.
Juan José, mwanamume kijana kutoka Palma de Mallorca, Hispania, alielimishwa katika shule ya Kikatoliki na kutumikia akiwa mvulana wa altare hadi alipokuwa na umri wa miaka 13. Yeye alihudhuria Misa kila Jumapili pamoja na familia yake, lakini akaacha kwenda kanisani alipokuwa tineja. Kwa nini? “Kwanza kwenda kwenye Misa kulinichosha,” aeleza Juan José. “Nilikariri sala ya dini. Kila kitu kilionekana kuwa rudio la kile nilichokuwa nimesikia mbeleni. Isitoshe, kasisi wa parishi yetu mara nyingi alitutendea sisi wavulana wa altare kwa ukali. Nami nilifikiria kuwa kosa kwamba watu maskini walipaswa kulipa kasisi ili awafanyie ibada ya maziko.
“Bado nilimwamini Mungu, lakini nilifikiri ningeweza kumtumikia katika njia yangu mwenyewe, nje ya mpango wa kanisa. Pamoja na kikundi cha marafiki, nilijaribu kufurahia maisha kwa njia bora kadiri nilivyoweza. Nafikiri ungesema kwamba kitumbuizo kikawa jambo la kwanza maishani mwangu.
“Lakini nilipokuwa na umri wa miaka 18, nilianza kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova. Walikuwa na nini cha kunipa ambacho sikuwa nimepata kanisani? Imani hakika inayotegemea Biblia badala ya desturi na ‘mafumbo’ ambayo sikuweza kuyafahamu. Hata hivyo, itikadi zangu mpya zilimaanisha mabadiliko makubwa kwangu. Badala ya kutumia mwisho-juma nikipanga karamu kwenye majumba ya disko, nilianza kwenda nyumba kwa nyumba ili kushiriki pamoja na majirani wangu imani yangu niliyopata karibuni. Kujihusisha kwa utendaji wa kusaidia wengine kulipatia maisha yangu maana. Kwa miaka saba iliyopita, nimekuwa mhudumu wa wakati wote wa Mashahidi wa Yehova.”
Si vijana tu ambao hutafuta kujaza utupu wao wa kidini. Antonia, mwanamke mzee-mzee kutoka Extremadura, Hispania, alitumia sehemu kubwa ya maisha yake “akimtafuta Mungu,” kama asemavyo. Katika miaka yake ya utineja, alienda kwenye Misa kila siku na hatimaye akaingia makao ya watawa ya Wakatoliki, kwa kuwa aliamini “kwamba ikiwa Mungu hawezi kupatikana katika makao ya watawa, hawezi kupatikana mahali penginepo pote.” Lakini miaka mitatu baadaye aliondoka kwenye hayo makao ya watawa, akihisi akiwa amevurugika hata zaidi na kukosa maana kuliko mbeleni.
Hatimaye, alipokuwa katika miaka yake ya 50, akawa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. “Nilifurahi sana wakati Mashahidi waliponitembelea na kujibu maswali yangu kutoka kwa Biblia yangu mwenyewe,” yeye aeleza. “Tangu niwe mmoja wa Mashahidi wa Yehova, maisha yangu yamekuwa na kusudi. Nina matatizo, lakini naweza kuyakabili kwa sababu sasa nimemjua Mungu wa kweli.”
Hayo si ndiyo mambo yaliyoonwa pekee. Wakikinza mwelekeo wa kidini, idadi zinazoongezeka za watu wanashirikiana na Mashahidi wa Yehova na wamepata kwamba kwa kuishi kupatana na imani yao na kuhubiria wengine kuihusu kunapatia maisha zao maana na kusudi.
Dini ya Kweli Ina Umaana Zaidi ya Wakati Mwingineo Wote
Ingawa twaishi katika wakati ambapo wengi wanakataa dini, halingekuwa jambo la hekima kuhukumu dini zote kuwa zisizofaa. Ni kweli, katika karne ya 20, watu wanaacha desturi zisizo na maana na kanuni za kale na zisizo za kimaandiko, nao hudhihaki kwenda kanisani ambako ni kwa ajili tu ya kuonekana kwa nje. Biblia hasa hupendekeza kwamba tuepuke dini yenye unafiki. Mtume Paulo alitabiri kwamba katika “siku za mwisho,” watu wengine ‘wangekuwa wenye mfano wa ujitoaji kimungu, lakini wakikana nguvu zao.’ Watu kama hao hudumisha wonyesho wa kijuu-juu wa dini, lakini mwenendo wao unakataa uhalali wao. Twapaswa kuitikiaje unafiki huo wa kidini? “Hao nao ujiepushe nao,” akashauri Paulo.—2 Timotheo 3:1, 5, NW.
Lakini Paulo alisema pia kwamba “dini hutokeza faida za juu.” (1 Timotheo 6:6, New English Bible) Paulo hakuwa akizungumza juu ya namna yoyote tu ya dini. Neno la Kigiriki lililotafsiriwa hapa kuwa “dini” lilikuwa eu·seʹbei·a, ambalo lamaanisha “ujitoaji au staha kwa Mungu.” Dini ya kweli, ujitoaji halisi wa kimungu, “unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye.”—1 Timotheo 4:8.
Kama vielelezo vilivyotajwa hapo juu vionyeshavyo, dini ya kweli yaweza kupatia maisha zetu maana na kutusaidia kukabili matatizo kwa uvumilivu. Zaidi ya hilo, dini ya kweli, huhakikisha wakati ujao wa milele. Namna hiyo ya ibada yastahili kufuatiwa, kwa kuwa twahakikishiwa ‘itaijaza dunia’ hatimaye.b (Isaya 11:9; 1 Timotheo 6:11) Hakuna shaka kwamba sasa ndio wakati ambapo dini ya kweli ina umaana kuliko wakati mwingineo wote.
-