-
Mwalimu Mkuu Atudhihirishia Muumba ZaidiJe, Kuna Muumba Anayekujali?
-
-
Yesu Aliyefufuliwa—Ufunguo wa Maisha Yenye Umaana
Mwanafunzi mpendwa Yohana alimtazama Yesu kwa makini hadi kifo Chake. Isitoshe, Yohana alirekodi ufufuo mkubwa zaidi uliowahi kutokea, tukio ambalo linaweka msingi thabiti wa kuwa na uhai wa milele na wenye umaana.
Maadui wa Yesu walimfanya auawe, akiwa amepigiliwa misumari kwenye mti kama mhalifu tu. Watazamaji—kutia ndani viongozi wa kidini—walimdhihaki alipokuwa akiteseka kwa saa kadhaa. Ajapokuwa na maumivu makali kwenye mti, Yesu alimwona mama yake mwenyewe na kumwambia mamake hivi kumhusu Yohana: “Mwanamke, ona! Mwana wako!” Kufikia wakati huo ni lazima Maria alikuwa mjane, na wale watoto wake wengine bado hawakuwa wanafunzi.e Kwa hiyo, Yesu alikabidhi utunzi wa mamake aliyekuwa akizeeka kwa mwanafunzi Yohana. Jambo hilo pia lilionyesha kufikiri kwa Muumba, ambaye alitia moyo kuwatunza wajane na mayatima.—Yohana 7:5; 19:12-30; Marko 15:16-39; Yakobo 1:27.
Lakini alipokufa, Yesu angetekelezaje fungu lake, akiwa “mbegu” ambaye kupitia kwake ‘mataifa yote yangejibarikia’? (Mwanzo 22:18) Kwa kifo chake, katika alasiri hiyo ya Aprili mnamo 33 W.K., Yesu alitoa uhai wake kuwa msingi wa fidia. Baba yake mwenye kufahamu aliyokuwa akipitia ni lazima alihisi uchungu kwa maumivu makali ya Mwana wake asiye na hatia. Lakini kwa njia hiyo, uandalizi ulifanywa wa kulipa thamani ya fidia iliyohitajiwa ili kuwaondolea wanadamu dhambi na kifo. (Yohana 3:16; 1 Yohana 1:7) Basi msingi ulikuwa umewekwa kwa ajili ya tukio tukufu.
Kwa sababu Yesu Kristo anatimiza fungu kuu katika kutimizwa kwa makusudi ya Mungu, ilikuwa lazima arudie uhai. Ikatokea hivyo, Yohana akashuhudia. Mapema katika siku ya tatu baada ya kifo na kuzikwa kwa Yesu, baadhi ya wanafunzi walienda kwenye kaburi. Lilikuwa tupu. Walishangaa hadi Yesu alipowatokea kadhaa kati yao. Maria Magdalena akaripoti, “Nimemwona Bwana!” Wanafunzi hawakukubali ushahidi wake. Baadaye wanafunzi walikusanyika katika chumba kilichokuwa kimefungwa na Yesu akawatokea tena, hata akazungumza nao. Kwa siku chache, zaidi ya wanaume na wanawake 500 wakajionea ya kwamba kwa kweli Yesu alikuwa hai. Watu wa wakati huo ambao huenda walikuwa wenye kutilia shaka wangeweza kuwahoji mashahidi hao wenye kuaminika na kuthibitisha ushuhuda wao. Wakristo waliweza kuwa na uhakika wa kwamba Yesu alikuwa amefufuliwa na alikuwa hai akiwa kiumbe wa roho kama Muumba. Uthibitisho wa jambo hilo ulikuwa mwingi na wenye kutegemeka hivi kwamba wengi walikabili kifo badala ya kukana kufufuliwa kwa Yesu.—Yohana 20:1-29; Luka 24:46-48; 1 Wakorintho 15:3-8.f
-
-
Mwalimu Mkuu Atudhihirishia Muumba ZaidiJe, Kuna Muumba Anayekujali?
-
-
f Ofisa mmoja Mroma mwenye cheo alisikia ushuhuda wa Petro wa mambo aliyojionea: “Nyinyi mwaijua habari iliyoongewa kotekote katika Yudea . . . Mungu alimfufua Huyu katika siku ya tatu na kumruhusu awe dhahiri . . . Alituagiza sisi tuwahubiri watu na kutoa ushahidi kamili kwamba Huyu ndiye aliyeagizwa na Mungu kuwa hakimu wa walio hai na wafu.”—Matendo 2:32; 3:15; 10:34-42.
-