-
Rumania2006 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
Mwishoni mwa miaka ya 1800, Warumania wengi walihamia nchi nyingine ili watafute kazi kwa sababu ya hali ngumu za kijamii na za kiuchumi nchini kwao, na baadhi yao walienda Marekani. Mbali na faida za kimwili, wengine kati yao walipata ujuzi sahihi wa kweli ya Biblia. Károly Szabó na József Kiss ni baadhi yao. Wanaume hao walipendezwa na mambo ya kiroho na walisikiliza hotuba kadhaa za Biblia zilizotolewa na Ndugu Russell.
Ndugu Russell alitambua kwamba wanaume hao wawili walipendezwa kikweli na Biblia naye akajitambulisha na kuongea nao. Walipokuwa wakizungumza aliwapendekezea Károly na József warudi Rumania wakawaeleze watu wao wa ukoo na marafiki wao kuhusu Ufalme. Wote wawili walikubali na wakasafiri kwa meli hadi Rumania mwaka wa 1911. Waliamua kwenda kuishi mjini Tirgu-Mures huko Transylvania.
Alipokuwa safarini kwenda nchini kwao, Ndugu Szabó alisali kwamba angalau mtu mmoja katika jamaa yao angekubali kweli. Alipofika nyumbani alitenda kupatana na sala yake na kuwahubiria watu wake wa ukoo, akiwemo Zsuzsanna Enyedi, ambaye alimkaribisha kukaa nao. Mume wa Zsuzsanna alikuwa mtunza-bustani, naye Zsuzsanna aliuza maua sokoni.
Zsuzsanna aliyekuwa Mkatoliki alihudhuria Misa kila asubuhi kabla ya kwenda kazini, na kila usiku baada ya familia yake kulala alienda bustanini kusali. Károly aliona mambo hayo na usiku mmoja alimwendea bustanini, akaweka mkono begani mwake, na kusema: “Zsuzsanna, wewe una moyo mweupe. Utaipata kweli.” Na kama Ndugu Szabó alivyosema, mwanamke huyo mwenye sifa nzuri alikubali ujumbe wa Ufalme na akawa mtu wa kwanza mjini Tirgu-Mures kujiweka wakfu kwa Yehova. Alikuwa mwaminifu hadi alipokufa akiwa na umri wa miaka 87.
Ndugu Szabó alimhubiria pia Sándor Józsa, mwanamume kijana aliyekuwa mfanyakazi wa familia ya Enyedi. Sándor alihudhuria mikutano yote ambayo ndugu hao wawili waliongoza, na alifanya maendeleo haraka. Punde si punde, kijana huyo mwenye umri wa miaka 18 alianza kuhubiri na kutoa hotuba nzuri za Biblia katika kijiji chao cha Sărăţeni, katika Mkoa wa Mureş. Hatimaye wanaume sita pamoja na wake zao, na watoto wao 24, yaani, wavulana 11, na wasichana 13, wakawa ‘barua zake za kumpendekeza.’—2 Kor. 3:1, 2.
Ndugu Kiss na Szabó walianza kuhubiri mjini Tirgu-Mures na hatimaye wakahubiri katika sehemu zote za Transylvania. Walipokuwa katika kijiji cha Dumbrava, umbali wa kilometa 30 kutoka Cluj-Napoca, walimkuta Mbaptisti Vasile Costea. Vasile alikuwa mtu mfupi na thabiti, na alikuwa mwanafunzi wa Biblia mwenye bidii. Fundisho la Utawala wa Miaka Elfu Moja wa Kristo lilimtatanisha, kwa hiyo alitega sikio József na Károly walipomfafanulia Maandiko. Baada ya kubatizwa, Vasile aliyejua Kihungaria, aliwahubiria kikamili Warumania na Wahungaria walioishi katika mkoa wao. Baadaye, akawa mtumishi wa wakati wote naye akaendelea na utumishi huo hadi alipokufa.
Ndugu Szabó alihubiri habari njema pia katika mji wa Satu-Mare kaskazini-magharibi mwa Rumania. Alipokuwa huko alimkuta Paraschiva Kalmár, mwanamke mwenye kumcha Mungu aliyekubali kweli kwa moyo wote. Paraschiva aliwafundisha watoto wake tisa kumpenda Yehova. Leo, kuna vizazi vitano vya Mashahidi katika familia yake.
-
-
Rumania2006 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
-
-
[Picha katika ukurasa wa 69]
Károly Szabó na József Kiss walirudi nchini kwao mwaka wa 1911, ili wahubiri ujumbe wa Ufalme
-