Ile Kolosiamu na Unabii wa Biblia
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA ITALIA
MAANDISHI ya zamani yaliyopatikana kwenye Kolosiamu ya Roma, Italia, yanaweza kwa njia isiyo ya moja kwa moja kuthibitisha unabii wa Biblia juu ya uharibifu wa Yerusalemu. Ni wazi kwamba maandishi hayo yanahusika na kujengwa na kuzinduliwa kwa Kolosiamu hiyo kwenye 80 W.K. Baada ya kujengwa upya na Profesa Géza Alföldy wa Chuo Kikuu cha Heidelberg, Ujerumani, maandishi hayo husomeka hivi: “Maliki Tito Vespiani Kaisari Agusto alisimamisha uwanja-duara huo mpya kwa kutumia nyara.” Nyara zipi?
“Tunazungumza juu ya utekaji nyara mkubwa uliofanywa na Tito katika vita dhidi ya Wayahudi,” asema Alföldy, “na hasa, vile vyombo vya dhahabu” vya hekalu katika Yerusalemu. Hekalu hili liliharibiwa likitimiza unabii wa Yesu. (Mathayo 24:1, 2; Luka 21:5, 6) Alföldy amalizia kwa kusema kwamba ile Kolosiamu—pamoja na Tao la Tito lijulikanalo sana, lenye picha za washindi wa Kiroma wakiwa wamebeba nyara walizoteka katika vita ya Kiyahudi—ni kumbukumbu la ushindi wa kihistoria wa Waroma.