-
Tuna Hisi Ngapi?Amkeni!—2003 | Machi 8
-
-
Tuna Hisi Ngapi?
“Sisi hufanya mambo mengi vizuri na kwa urahisi katika mazingira yetu. Ni vigumu kuelewa ile mifumo tata inayotuwezesha hata kuhisi vitu vidogo sana.”—SENSORY EXOTICA—A WORLD BEYOND HUMAN EXPERIENCE.
WAZIA ukiendesha baiskeli katika barabara tulivu ya mashambani. Unaposonga mbele, vipokezi vya hisi kwenye miguu yako vinakuwezesha kukanyaga pedali ipasavyo ili uende kwa mwendo unaotaka. Viungo fulani mwilini vinakusaidia udumishe usawaziko; pua yako inanusa harufu nzuri; macho yako yanatazama mandhari; na masikio yako yanasikia nyimbo za ndege. Unapokuwa na kiu, vipokezi vya hisi katika vidole vyako vinakuwezesha kushika chupa ya kinywaji. Vionjio vilivyo kwenye ulimi wako vinakuwezesha kuhisi ladha ya kinywaji hicho na vipokezi vingine vya hisi vinakusaidia kutambua ikiwa kinywaji hicho ni baridi au moto. Vipokezi vya hisi katika ngozi na nywele vinakuwezesha kufahamu upepo ni wenye nguvu kadiri gani. Vipokezi hivyo pamoja na macho yako vinakuwezesha kutambua unaenda kasi kadiri gani. Ngozi yako pia inakuwezesha kujua hali ya hewa, na uwezo wako wa kutambua wakati unakusaidia kukadiria muda ambao umekuwa ukiendesha baiskeli. Mwishowe, hisi zako za ndani zinakulazimisha upumzike na ule. Ama kweli, uhai unategemea hisi zinazotenda kazi kwa upatano kabisa!
Je, Tuna Hisi Tano Tu?
Ulitumia hisi ngapi ulipokuwa ukiendesha baiskeli? Je, ulitumia zile tano tu za kawaida: kuona, kusikia, kunusa, kuonja, na kugusa? Kulingana na kitabu Encyclopædia Britannica, ile dhana kuhusu hisi tano ilitokana na yule mwanafalsafa wa zamani Aristotle. “Maoni yake yamedumu kwa muda mrefu hivi kwamba mpaka leo watu wengi bado wanafikiri kuna hisi tano tu.”
Hata hivyo, kulingana na kitabu hicho, uchunguzi uliofanywa kuhusu hisi zinazopatikana kwenye ngozi “unadokeza kwamba wanadamu wana zaidi ya hisi tano.” Kwa nini tunasema hivyo? Hapo awali hisi fulani zilidhaniwa kuwa sehemu ya hisi ya kugusa, lakini sasa zinaonwa kuwa hisi tofauti. Kwa mfano, hisi za uchungu zinaweza kutambua na kutofautisha kati ya uchungu unaosikia unapogongwa na kitu na ule unaosikia unapoungua kwa moto au kemikali. Pia kuna hisi zinazotambua mwasho. Uchunguzi unaonyesha kwamba tuna angalau hisi mbili zinazotambua wakati mwili unapofinywa—moja hutuwezesha kutambua tunapofinywa kidogo na nyingine tunapofinywa sana. Miili yetu pia ina hisi nyingi za ndani. Hisi za ndani zinafanya kazi gani?
Hisi za Ndani
Hisi za ndani hutambua mabadiliko yanayotokea mwilini mwetu. Hizo hutusaidia tujue tunapokuwa na njaa, kiu, uchovu, maumivu ndani ya mwili, na tunapohitaji kupumua au kwenda msalani. Hisi hizo hufanya kazi pamoja na uwezo wa mwili wa kutambua wakati. Hivyo, tunahisi uchovu wakati wa jioni au baada ya kusafiri kwa ndege kwa saa nyingi. Watu wengine wamesema kwamba uwezo wa mwili wa kutambua wakati ni mojawapo ya hisi za mwili kwa sababu tunaweza “kuhisi” wakati ukipita.
Tuna hisi nyingine ndani ya sikio inayotusaidia tutembee kwa usawaziko. Hiyo hutufanya tuhisi nguvu ya uvutano, tuhisi tunapoenda kasi, na tunapozunguka. Mwishowe, tuna hisi inayotuwezesha tujue misuli yetu inapokazika. Hisi hiyo hutuwezesha pia kutambua miguu na mikono yetu inaposonga, na mahali ilipo, hata tukiwa tumefunga macho.
Bila shaka, si wanadamu pekee walio na hisi. Wanyama pia wana hisi nyingi tofauti-tofauti, na nyingine zenye kustaajabisha sana ambazo wanadamu hawana. Tutachunguza baadhi ya hisi hizo katika makala inayofuata. Pia tutajichunguza kwa undani tuone sifa zinazotufanya tuwe viumbe wa kipekee.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 4]
Wanadamu Wana Hisi ya Kugusa Inayostaajabisha
Mkono wa mwanadamu una hisi ya kugusa yenye nguvu sana. Kulingana na gazeti Smithsonian, watafiti waligundua kwamba mkono wa mwanadamu unaweza kuhisi alama ndogo sana ya kituo yenye ukubwa wa mikroni tatu. (Unywele wa mwanadamu una kipenyo cha mikroni 50 hadi 100.) Hata hivyo, “watafiti hao walipofanya uchunguzi kwa kugusa mkwaruzo badala ya alama ya kituo, waligundua kwamba mkono wa mwanadamu unaweza kuhisi mkwaruzo wenye ukubwa wa nanometa 75”—mikroni moja ina ukubwa wa nanometa elfu moja! Uwezo huo wa ajabu unatokana na vipokezi 2,000 vya hisi vilivyo katika ncha za vidole.
Hisi ya kugusa hutusaidia pia kuwa na afya bora na furaha. Gazeti U.S. News & World Report lasema kwamba “mtu anapopapaswa, mwili wake hutokeza homoni ambazo zinaweza kupunguza maumivu na kutuliza akili.” Watu wengine wanaamini kwamba mtoto asipopapaswa kwa upendo, ukuzi wake huathiriwa.
-
-
Viumbe Wana Hisi za AjabuAmkeni!—2003 | Machi 8
-
-
Viumbe Wana Hisi za Ajabu
PANYA anazunguka-zunguka gizani akitafuta chakula huku akihisi yu salama. Lakini hana habari kwamba nyoka aina ya kipiri anaweza kutambua joto linalomtoka mwilini. Ole wake! Samaki aina ya wayo amejificha kabisa mchangani katika kidimbwi chenye papa. Papa mwenye njaa anamwelekea samaki huyo. Ingawa papa hamwoni, kufumba na kufumbua anamrukia yule wayo na kumnyafua papo hapo.
Kipiri na papa ni baadhi ya wanyama wenye hisi za kipekee ambazo wanadamu hawana. Kwa upande mwingine, viumbe wengi wana hisi kama zetu lakini zenye nguvu zaidi au zinazowawezesha kutambua mambo mengi zaidi. Uwezo wa kuona ni mojawapo ya hisi hizo.
Macho Yanayoona Vitu Ambavyo Hatuwezi Kuona
Macho yetu huona rangi chache sana kati ya rangi zote zilizopo. Kwa mfano, macho yetu hayawezi kuona miale inayoitwa infrared. Miale hiyo ni mirefu zaidi kuliko miale ya rangi nyekundu. Lakini aina fulani ya kipiri anaweza kutambua miale hiyo akitumia matundu mawili madogo yaliyo katikati ya macho na pua yake.a Kwa hiyo, anaweza kumshambulia mnyama mwenye damu moto hata akiwa gizani.
Ingawa wanadamu hawawezi kuona miale ya urujuanimno, viumbe wengi kutia ndani ndege na wadudu wanaweza kuiona. Kwa mfano, nyuki huongozwa na jua kutambua mahali wanapoelekea. Hata jua linapofunikwa kidogo na mawingu, wao hutambua mahali lilipo kwa kutafuta anga lililo wazi na kutazama mpangilio wa miale ya urujuanimno. Jua linapoangaza, mimea mingi inayochanua maua hurudisha miale ambayo wanadamu hawawezi kuiona, na mingine hurudisha miale ya urujuanimno kwa njia inayowawezesha wadudu kutambua mahali hususa penye umajimaji mtamu. Vilevile ndege hutambua matunda na mbegu fulani kwa njia hiyo.
Kwa kuwa ndege wanaweza kuona miale ya urujuanimno na kwa sababu miale hiyo hufanya manyoya yao yang’ae zaidi, huenda wao huwaona ndege wenzao wakiwa maridadi zaidi kuliko tunavyowaona. Mtaalamu mmoja anayechunguza ndege alisema kwamba ndege wanaweza kuona “rangi vizuri sana kuliko tunavyoweza kuwazia.” Mwewe na kozi fulani wanaweza kutumia uwezo huo wa kuona miale ya urujuanimno kuwakamata panyabuku. Kwa njia gani? Gazeti BioScience linasema kwamba “mkojo na kinyesi cha panyabuku wa kiume una kemikali ambazo hufyonza miale ya urujuanimno, na panya hao hutia alama kwenye njia wanayopitia kwa mkojo huo.” Hiyo ndiyo sababu ndege wanaweza “kutambua maeneo yenye panyabuku wengi” na kuwinda huko.
Kwa Nini Ndege Huona Vizuri Sana?
Ndege ana uwezo wenye kustaajabisha sana wa kuona. Kitabu All the Birds of the Bible kinasema kwamba “uwezo huo unatokana hasa na utando ulio ndani ya jicho lake unaomfanya aone vizuri. Utando huo una chembe nyingi za kuona kuliko utando wa viumbe wengine. Chembe za kuona zikiwa nyingi, jicho huona vitu vidogo kutoka mbali. Utando wa jicho la mwanadamu una chembe za kuona zipatazo 200,000 kwa kila milimeta ya mraba, ilhali chembe zilizo katika macho ya ndege wengi ni mara tatu ya idadi hiyo. Mwewe, tumbusi, na tai wana chembe milioni moja au zaidi kwa kila milimeta ya mraba.” Isitoshe, ndege fulani wana matundu mawili kwenye utando wa kila jicho ambayo huwawezesha kutambua vizuri umbali na mwendo wa vitu. Vilevile, ndege ambao hunasa wadudu wanaoruka wana uwezo kama huo.
Pia, ndege wana lenzi nyororo sana inayowawezesha kuona vizuri. Ikiwa ndege hawangeweza kuona vizuri, wangekabili hatari nyingi sana hasa wanaporuka msituni au kichakani. Ama kweli, jicho la ndege limebuniwa kwa hekima nyingi sana!b
Uwezo wa Kuhisi Umeme
Kisa kilichotajwa mwanzoni kuhusu samaki aina ya wayo na papa kilitukia wakati wa uchunguzi wa kisayansi kuhusu papa. Watafiti walitaka kujua iwapo papa na samaki aina ya taa wanaweza kuhisi nguvu kidogo za umeme zinazotokezwa na samaki aliye hai.c Walipitisha kiasi kinachofaa cha umeme kwenye mabamba yaliyowekwa mchangani katika kidimbwi chenye papa. Ikawaje? Mara tu papa alipoyakaribia mabamba hayo, aliyashambulia vikali.
Papa wanaweza kuhisi nguvu za umeme kama vile sikio linavyoweza kusikia sauti mbalimbali. Lakini, samaki wengine hutokeza nguvu za umeme. Kama vile popo anavyotoa mlio na kusikiliza mwangwi wake, samaki hao hutokeza mawimbi ya umeme, kisha wakitumia vipokezi maalumu wanaweza kutambua jinsi mawimbi hayo yanavyobadilika yanapogonga kitu fulani.d Kwa kutumia njia hiyo, samaki hao wanaweza kujua mahali penye vizuizi, windo, au hata mwenzi.
Uwezo wa Kujua Njia
Hebu wazia jinsi maisha yangekuwa iwapo ungekuwa na dira mwilini mwako. Hungepotea njia. Wanasayansi wamegundua kwamba viumbe fulani kama vile nyuki na samaki aina ya trauti wana chembe zenye sumaku ndogondogo mwilini mwao. Chembe hizo zimeunganishwa na mfumo wao wa neva. Hiyo inaonyesha kwamba nyuki na trauti wanaweza kuhisi nguvu za sumaku. Nyuki hutumia nguvu za sumaku kutengeneza sega na kujua wanakoelekea.
Watafiti pia wamegundua sumaku katika bakteria fulani zinazoishi kwenye mchanga unaopatikana chini ya bahari. Mchanga huo unapotibuliwa, sumaku zilizo katika bakteria hizo huvutwa na sumaku za dunia ili kusaidia bakteria hizo kurejea kwenye makao yake chini ya bahari. Zisipofanya hivyo, zitakufa.
Huenda wanyama wengi wanaohamahama kama vile ndege, kasa, samaki aina ya salmoni, na nyangumi wanaweza kuhisi nguvu za sumaku. Hata hivyo, inaonekana wanyama hao hawategemei hisi hiyo peke yake, bali wao hutegemea hisi mbalimbali wanapohama. Kwa mfano, huenda salmoni hutumia uwezo wao wa kunusa wenye nguvu ili wafike mahali walipozaliwa. Kwezi fulani huongozwa na jua ili wafike mahali wanapoenda na ndege wengine huongozwa na nyota. Lakini kama alivyosema profesa wa saikolojia Howard C. Hughes katika kitabu chake Sensory Exotica—A World Beyond Human Experience, “ni wazi kwamba itachukua muda mrefu kuelewa mambo hayo na mambo mengine tata kuhusu viumbe.”
Uwezo wa Ajabu wa Kusikia
Wanyama wengi wana uwezo wa ajabu wa kusikia ambao ni bora kuliko wa wanadamu. Ingawa tunaweza kusikia sauti zenye frikwensi ya hezi 20 hadi 20,000 (hezi ni idadi ya mizunguko ya wimbi la sauti kwa sekunde moja), mbwa wanaweza kusikia sauti zenye frikwensi ya hezi 40 hadi 46,000 na farasi hezi 31 hadi 40,000. Tembo na ng’ombe hata wanaweza kusikia sauti za chini zenye frikwensi ya hezi 16 ambazo wanadamu hawawezi kusikia. Kwa kuwa sauti zenye frikwensi ya chini husafiri mbali zaidi, tembo wanaweza kuwasiliana wakiwa umbali wa kilometa nne au zaidi. Watafiti fulani hata wanasema kwamba tunaweza kuwatumia wanyama hao kutambua mapema ishara za matetemeko ya ardhi na hali mbaya ya hewa, kwani matukio hayo huanza kwa sauti zenye frikwensi za chini sana.
Wadudu pia wanaweza kusikia sauti zenye frikwensi tofauti-tofauti, nyingine zenye frikwensi ya juu sana ambazo wanadamu hawawezi kusikia na nyingine zenye frikwensi ya chini sana. Wadudu wachache husikia kupitia viungo vyembamba vilivyo katika sehemu zote za mwili isipokuwa kichwani. Wengine wana nywele nyembamba zinazowasaidia kusikia sauti na vilevile vitu vinavyosonga polepole sana hewani kama vile wakati mkono wa mwanadamu unaposonga. Hiyo ndiyo sababu ni vigumu sana kumgonga nzi.
Wazia ukiwa na uwezo wa kusikia mdudu akitembea! Popo—mnyama pekee anayeweza kuruka kama ndege—ana uwezo huo. Bila shaka, popo wanahitaji uwezo wa kipekee wa kusikia ili kusafiri gizani na kukamata wadudu kwa kusikiliza mwangwi wa sauti yao wenyewe.e Profesa Hughes anasema hivi: “Hebu wazia mfumo wa kupokea mwangwi ulio tata kuliko ule wa nyambizi ya hali ya juu zaidi. Sasa wazia mfumo huo ukitumiwa na popo mdogo sana anayeweza kutoshea katika kiganja cha mkono wako. Ubongo wake ambao ni mdogo kuliko ukucha wa kidole gumba humwezesha kutambua umbali, mwendo, na hata aina ya wadudu anaonuia kukamata!”
Ili popo watambue mahali vitu vilipo kwa usahihi, wanahitaji kutoa sauti nzuri. Wao hufanya hivyo kwa kutumia “uwezo wao wa ajabu wa kuinua na kushusha sauti ambao unapita ule wa mwimbaji bora,” chasema kitabu kimoja.f Inaonekana jamii fulani ya popo hutumia viungo fulani vilivyo juu ya pua zao kuelekeza sauti mahali fulani. Kwa kutumia uwezo huo, popo wanaweza kutambua hata vitu vidogo sana kama unywele wa mwanadamu!
Mbali na popo, kuna angalau aina mbili za ndege wanaotumia mwangwi kutambua mahali vitu vilipo. Ndege hao ni mbayuwayu fulani wa Asia na Australia na ndege aina ya oilbird wa Amerika Kusini. Hata hivyo, inaonekana ndege hao hutumia uwezo huo kuwasaidia tu kusafiri katika mapango yao yenye giza.
Kutumia Mwangwi Baharini
Nyangumi wa aina fulani pia hutumia mwangwi kutambua mahali vitu vilipo baharini, hata ingawa wanasayansi hawana uhakika jinsi wanavyotumia uwezo huo. Pomboo hutoa milio tofauti-tofauti ambayo inadhaniwa kuwa hutoka puani wala si kooni. Kiungo fulani chenye mafuta kilicho kwenye kipaji cha uso wa pomboo huelekeza milio hiyo ili kumwezesha kutambua vitu vilivyo mbele yake. Pomboo husikiaje mwangwi wa sauti yao? Inaonekana hawatumii masikio yao moja kwa moja, bali wao hutumia utaya wao wa chini na viungo vingine vilivyounganishwa na sehemu ya ndani ya sikio. Sehemu hiyo ya sikio ina mafuta kama yale yanayopatikana kwenye kipaji cha uso wa pomboo.
Mawimbi ya milio ya pomboo yanafanana sana na wimbi linaloitwa Gabor linalotumiwa katika hesabu. Kulingana na Hughes, wimbi hilo linathibitisha kwamba pomboo hutoa milio “inayokaribia kufanana sana na ile inayotolewa na mifumo ya kupokea mwangwi.”
Pomboo wanaweza kutoa milio ya chini sana au milio ya juu sana yenye kipimo cha desibeli 220. Milio hiyo ni ya juu sana kiasi gani? Muziki wa roki wenye sauti ya juu unaweza kufikia kipimo cha desibeli 120, na mlio wa bunduki desibeli 130. Pomboo wanaweza kutumia mlio mkubwa zaidi kuliko huo kutambua vitu vidogo sana kama mpira wa sentimeta nane ulio umbali wa meta 120. Wanaweza kutambua vitu vilivyo mbali hata zaidi maji yanapokuwa matulivu.
Je, hustaajabishwi na hisi hizo za ajabu za viumbe? Watu wanyenyekevu wenye ujuzi hustaajabishwa nazo. Hilo latufanya tufikirie jinsi tulivyoumbwa. Ni kweli kwamba hisi zetu ni duni sana zinapolinganishwa na zile za wanyama na wadudu fulani. Hata hivyo, ni sisi tu tunaosisimuliwa na maumbile. Kwa nini? Kwa nini tunajitahidi kujifunza kuhusu viumbe na kusudi la kuwapo kwa viumbe hao, na vilevile kujua kusudi letu maishani?
[Maelezo ya Chini]
a Kuna aina 100 hivi za vipiri.
b Wasomaji wanaotaka kujua tofauti iliyopo kati ya dhana ya mageuzi na ubuni wenye hekima wanaweza kusoma kitabu Je, Kuna Muumba Anayekujali?, kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.
c Viumbe wote walio hai, kutia ndani wanadamu, hutokeza kiasi kidogo cha umeme kinachoweza kutambuliwa wanapokuwa ndani ya maji.
d Samaki tunaozungumzia hapa hutokeza nguvu kidogo sana za umeme. Wao ni tofauti na samaki wengine kama vile taa na mkunga, ambao hutokeza nguvu nyingi za umeme ili kushtua adui au kunasa windo. Mkunga hutokeza nguvu nyingi sana za umeme zinazoweza kumuua farasi!
e Kuna aina 1,000 hivi za popo. Tofauti na maoni ya watu wengi, popo wote wanaweza kuona vizuri, lakini si wote wanaoweza kutumia mwangwi wa sauti zao. Baadhi yao, kama wale popo wanaokula matunda, hutumia uwezo wao wa kuona vizuri gizani kupata chakula.
f Popo hutoa mlio wenye frikwensi tofauti-tofauti kuanzia hezi 20,000 hadi hezi 120,000 au zaidi.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]
Enyi Wadudu, Jihadharini!
“Kila siku, wakati wa jioni, jambo la kushangaza sana hutukia chini ya vilima vilivyo karibu na San Antonio, Texas [Marekani],” chasema kitabu Sensory Exotica—A World Beyond Human Experience. “Ukiwa mbali, unaweza kufikiri umeona wingu kubwa la moshi mweusi likipaa kutoka chini ya ardhi. Hata hivyo, si moshi unaofanya anga kuwa jeusi, bali ni popo milioni 20 wenye mikia mirefu ambao wanatoka katika Pango la Bracken.”
Makadirio yaliyofanywa hivi karibuni yanaonyesha kwamba kuna popo milioni 60 katika Pango la Bracken. Popo hao hupaa kufikia meta 3,000 angani ili kutafuta wadudu, kwani hicho ndicho chakula wanachokipenda sana. Ijapokuwa sauti nyingi sana za popo zinasambaa angani wakati wa usiku, hakuna mvurugo wowote unaotokea kwani kila mmoja wa popo hao ana mfumo tata sana unaomsaidia kutambua mwangwi wake.
[Picha]
Pango la Bracken
[Hisani]
Courtesy Lise Hogan
[Picha]
Popo wenye mikia mirefu—husikia mwangwi
[Hisani]
© Merlin D. Tuttle, Bat Conservation International, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Nyuki—huona na hutambua nguvu za sumaku
[Picha katika ukurasa wa 7]
Tai—huona
[Picha katika ukurasa wa 7]
Taa—hutambua nguvu za umeme
[Picha katika ukurasa wa 7]
Kwezi—huona
[Picha katika ukurasa wa 7]
Salmoni—hunusa
[Hisani]
U.S. Fish & Wildlife Service, Washington, D.C.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Kasa—pengine anaweza kutambua nguvu za sumaku
[Picha katika ukurasa wa 7]
Papa—hutambua nguvu za umeme
[Picha katika ukurasa wa 8]
Tembo—husikia sauti za chini sana
[Picha katika ukurasa wa 8]
Mbwa—husikia sauti za juu sana
[Picha katika ukurasa wa 9]
Pomboo—husikia mwangwi
-
-
Zawadi Zinazotufanya Tuwe Viumbe wa KipekeeAmkeni!—2003 | Machi 8
-
-
Zawadi Zinazotufanya Tuwe Viumbe wa Kipekee
‘Wanasayansi huchunguza viumbe kwa sababu wanapendezwa nao, na wanapendezwa nao kwa sababu wanavutia.’—JULES-HENRI POINCARÉ, MWANASAYANSI MFARANSA ALIYE PIA MTAALAMU WA HESABU (1854-1912).
POINCARÉ alipendezwa sana na umaridadi wa viumbe na hasa ule utaratibu na upatano “wa hali ya juu” ambao huwavutia wanasayansi. Lakini si wanasayansi tu wanaofurahia umaridadi na upatano unaotuzunguka. Karibu miaka 3,000 iliyopita, mtunga-zaburi Daudi alivutiwa sana na uumbaji, hasa jinsi ambavyo mwanadamu ameumbwa. Alisali hivi: “Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu, na nafsi yangu yajua sana.”—Zaburi 139:14.
Ni wanadamu pekee wanaoweza kuchochewa kumtukuza Mungu jinsi hiyo. Hata mnyama mwenye akili nyingi zaidi hawezi kufanya hivyo. Lakini, hatupendezwi tu na yale tunayoona katika uumbaji. Tangu zamani, watu wenye kufikiri wameuliza hivi: Viumbe hao wa ajabu walitoka wapi? Kwa nini waliumbwa? Kusudi letu maishani ni nini? Hatuwezi kujibu maswali hayo kwa kutumia sayansi au kwa kufuata maoni yetu. Lakini Biblia, ambayo imeandikwa kwa uongozi wa Mungu, inatoa majibu yenye kuridhisha kwelikweli.—2 Petro 1:20, 21.
Kitabu hicho kitakatifu cha kale kinasema kwamba tuna sifa za kipekee kwa sababu tuliumbwa “kwa mfano wa Mungu,” yaani, tunaweza kuiga (ingawaje kwa kadiri fulani) sifa za Muumba wetu. (Mwanzo 1:27) Kwa hiyo, ingawa hatuna macho kama ya tai, tunaweza kutumia hekima kufanya maamuzi mazuri kuhusu wakati ujao. Huenda uwezo wetu wa kusikia ukawa duni sana ukilinganishwa na ule wa popo, lakini sisi hupendezwa na mazungumzo, muziki, na sauti tamu za viumbe. Na ingawa hatuna dira mwilini mwetu, tunaweza kupata mwelekezo bora maishani kwa kuchunguza Neno la Mungu, Biblia Takatifu.—Mithali 3:5, 6.
Kwa kuwa tumeumbwa kwa mfano wa Mungu, ni sisi tu tulio na uhitaji wa kiroho. Yesu alisema hivi: “Binadamu lazima aishi, si kwa mkate pekee, bali kwa kila tamko linalokuja kupitia kinywa cha Yehova.” (Mathayo 4:4) Je, wewe hujilisha matamko hayo yenye kuburudisha kwa kusoma Biblia kwa ukawaida?
Tukisitawisha sifa za kiroho kwa kutumia Neno la Mungu, tunaweza kufahamu mambo mengi zaidi ya yale ambayo hisi zetu zinatuwezesha kutambua. Kwa njia gani? Sifa hizo hujenga imani yetu. Tukiwa na imani thabiti inayotegemea Biblia, tunaweza “kumwona” Mungu asiyeonekana, kama alivyofanya Musa. Pia tunaweza kujua yale ambayo Mungu anakusudia kufanya wakati ujao.—Waebrania 11:1, 27.
Wakati Ujao Mzuri kwa Wale “Wanaomwona” Mungu
Biblia inasema kwamba Muumba, Yehova Mungu, anaipenda dunia na viumbe wote waliomo, na hasa wanadamu wenye kumhofu. Kwa hiyo, ameahidi kuwaharibu waovu wote, kutia ndani wale “wanaoiangamiza dunia” kwa pupa. (Ufunuo 11:18; Zaburi 37:10, 11; 2 Wathesalonike 1:8) Kisha, atawapa wale wanaompenda na kumtii uhai wa milele. Isitoshe, watu hao watasaidia kuigeuza dunia yote iwe paradiso yenye viumbe wengi. Hilo ni taraja lililoje!—Luka 23:43.
Hebu wazia mambo utakayoweza kufanya na kuvumbua utakapoishi milele ukiwa na afya bora! Mwanasayansi mmoja aliandika hivi: “Dunia itaendelea kuwa na viumbe wa aina mbalimbali, walio maridadi na wenye kustaajabisha.” Biblia inasema hivi: “Kila kitu [Mungu] amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho.”—Mhubiri 3:11.
Unawezaje kuwa miongoni mwa wale watakaoishi katika Paradiso inayotajwa katika Biblia? Kwa kujifunza kuhusu kusudi la Mungu sasa na kutenda kupatana na yale unayojifunza. Yesu alisema hivi: ‘Hii yamaanisha uhai udumuo milele, wao kuendelea kutwaa ujuzi juu yako wewe, Mungu pekee wa kweli, na juu ya yule uliyemtuma, Yesu Kristo.’—Yohana 17:3.
-