Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Latvia
    2007 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
    • KUPELEKWA SIBERIA

      Nchini Latvia, kama katika nchi nyingine zilizokuwa chini ya Sovieti, serikali mpya ilianza kufanya taasisi za kitamaduni na za kisiasa ziwe kama za Sovieti. Pia, Wakomunisti walijumuisha mashamba ya watu binafsi ili yasimamiwe na serikali. Kwa sababu ya mradi huo, kulikuwa na visa vingi vya kuwahamisha watu, ambavyo viliisha mwaka wa 1949. Walatvia 100,000 hivi walihamishiwa Urusi Kaskazini, kutia ndani Siberia. Miaka miwili baadaye, Wakomunisti waliwageukia Mashahidi wa Yehova na kuhamisha maelfu kutoka kwenye mashamba, kutia ndani angalau 20 kati ya wahubiri 30 hivi waliobaki Latvia.

      Ingawa hakuwa amebatizwa, Valija Lange, kutoka Ventspils, ni mmoja wa waliokamatwa na KGB (Halmashauri ya Usalama wa Kitaifa ya Sovieti) katika misako ya Septemba 1950. Alipohojiwa usiku wa manane huko Riga, aliulizwa: “Kwa nini unapinga serikali na wewe ni raia wa Muungano wa Sovieti?” Valija akajibu kwa utulivu na heshima: “Ninakusudia tu kumtumikia Yehova Mungu, kuelewa mafundisho yake, na kuwaeleza wengine mafundisho hayo.”

      Jina la Valija, na majina ya Mashahidi 19 wengine, yaliorodheshwa katika hati moja ya Oktoba 31, 1950. Wote walioorodheshwa humo walihukumiwa kifungo na kazi ngumu kwa miaka kumi huko Siberia, na wakanyang’anywa mali yao. Wengine waliruhusiwa kurudi nyumbani lakini wakashtakiwa tena. Kwa mfano, Paulīne Serova alipelekwa tena Siberia kwa miaka mingine minne wakati wenye mamlaka walipogundua anapokea vichapo vya Biblia kupitia posta.

      Akina ndugu waliendelea kuhubiri na kufanya wanafunzi kambini. Mmoja wa wanafunzi hao ni Jānis Garšk̗is. Alibatizwa mwaka wa 1956 na sasa anaishi Ventspils. Anasema: “Nashukuru kwamba Mungu aliacha nipelekwe katika kambi ya kazi ngumu, la sivyo singejifunza kweli.” Huo ni mtazamo mzuri kama nini!

      Tekla Onckule, ambaye ni mzaliwa wa Latvia, alishtakiwa kwa uchochezi wa kisiasa, naye akapelekwa Siberia. Alipokuwa katika jiji la mbali la Omsk, alipata kweli kutoka kwa Mashahidi waliohamishwa. “Sitasahau kamwe siku niliyobatizwa,” Tekla anasema. “Nilibatizwa usiku sana katika mto wenye maji baridi kama barafu. Nilitetemeka sana kwa sababu ya baridi, lakini nilifurahi sana.” Mwaka wa 1954, Tekla aliolewa na Aleksei Tkach, ambaye alibatizwa mwaka wa 1948 huko Moldavia (sasa Moldova) na baadaye akahamishwa mpaka Siberia. Mwaka wa 1969, wenzi hao wa ndoa na Mashahidi wengine wachache walirudi Latvia. Kwa kuhuzunisha, wengi wa wale wengine waliohamishwa kutoka Latvia walikufa kambini.

  • Latvia
    2007 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
    • [Picha katika ukurasa wa 191]

      Orodha ya KGB ya Mashahidi ambao walikamatwa mwaka wa 1950. Wengi wao walihamishiwa Siberia

      [Picha katika ukurasa wa 191]

      Siberia, mapema katika miaka ya 1950

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki