Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Mshtuko wa Akili!
    Amkeni!—1998 | Februari 8
    • Mshtuko wa Akili!

      KISABABISHI kikuu cha kifo na ulemavu wenye kudumu katika ulimwengu wa Magharibi wenye viwanda vingi ni mshtuko wa akili. Maneno yenyewe “mshtuko wa akili” yadokeza hali ya ghafula ambayo “kushambuliwa kwa ubongo” hutokea. Dakika moja, waweza kuwa wajihisi vizuri, na kitambo kidogo, wajihisi kana kwamba umepigwa na umeme wenye radi—mshtuko mkubwa wa akili waweza kubadili maisha yako kwa ghafula na kwa njia ya kutazamisha sana. Ukikulemaza na kukudhoofisha kabisa, waweza kukufanya ushindwe kusema, kuharibu kabisa hisia-moyo zako, kubadilisha utu wako na uwezo wako wa utambuzi, na kukufanya ulazimike kuwa na shindano lionekanalo kutokuwa na mwisho la kurudia maisha ya kawaida ambayo wewe na familia yako mlizoea.

      Mfikirie Ellen Morgan.a Jumatano, alikuwa na umri wa miaka 64 akiwa mtendaji, mwenye afya nzuri. Alhamisi, alipokuwa na mume wake wakinunua vitu madukani, Ellen alipoteza kwa ghafula uwezo wake wa kuongea, na uso wake ukaumbuka. Mwili wake ulidhoofika, na alipepesuka, kana kwamba alikuwa katika hali ya ulevi. Ellen alikuwa amepatwa na mshtuko mkubwa wa akili!

      Baada ya mshtuko wa akili, Ellen alilemazwa sana kiasi cha kushindwa kufanya mambo rahisi kabisa, kama vile kuoga au kujivisha nguo. Akishindwa kuandika, kufuma, au kushona, alikumbwa na vipindi vya kutoa machozi kusikozuilika na uchovu uliomzidi nguvu. Katika mambo yote hayo, uwezo wa kufikiri wa Ellen haukuharibiwa; hata hivyo, hisia za aibu zingetokea wakati alipohisi kwamba labda wengine walimwona kuwa punguani. Baadaye, Ellen alieleza hivi: “Watu wachache hung’amua jinsi ambavyo mshtuko wa badiliko hilo la ghafula humwathiri mtu kihisia-moyo na kiakili. Karibu nihisi kana kwamba ulikuwa mwisho wa maisha yangu nikiwa mtu.”

      Ni nini husababisha mshtuko wa akili? Je, kila mtu ambaye ana mshtuko wa akili huathiriwa katika njia ileile? Waokokaji wamekabilianaje na ugonjwa huo? Familia za waokokaji wa mshtuko wa akili hukabilianaje na hali hiyo? Sisi sote twaweza kufanya nini ili kutegemeza? Amkeni! lachunguza maswali hayo na lakuletea ufahamu wenye kina juu ya maisha ya waokokaji wa mshtuko wa akili na familia zao ambazo hushiriki katika magumu yao.

  • Mshtuko wa Akili—Kisababishi Chake
    Amkeni!—1998 | Februari 8
    • Mshtuko wa Akili—Kisababishi Chake

      “UBONGO ndicho kiungo cha mwili kiwezacho kuharibika kwa urahisi sana,” ataarifu mtaalamu wa elimu ya neva Dakt. Vladimir Hachinski, wa Chuo Kikuu cha Western Ontario katika London, Kanada. Ukiwa na asilimia 2 tu ya uzani wote wa mwili, ubongo una chembe za neva zaidi ya bilioni kumi, ambazo zawasiliana daima ili kutokeza fikira, mwendo, na hisia zetu zote. Ukitegemea oksijeni na glukosi kupata nishati, ubongo hupokea ugavi wa daima kupitia mfumo tata wa ateri.

      Hata hivyo, sehemu yoyote ya ubongo inyimwapo oksijeni hata kwa sekunde chache, utendaji wa nyuroni ziwezazo kuharibika kwa urahisi hudhoofishwa. Hilo likiendelea kwa zaidi ya dakika chache, madhara ya ubongo hutokea, chembe za ubongo zianzapo kufa pamoja na utendaji zinazouongoza. Hali hii huitwa ischemia, ukosefu wa oksijeni hasa usababishwao na kuziba kwa ateri. Madhara zaidi hutokea kwa tishu za ubongo ukosefu wa oksijeni utokezapo maitikio ya kikemikali yenye kutukia kwa mfululizo kwa njia ya kufisha. Tokeo ni mshtuko wa akili. Mshtuko wa akili hutokea pia wakati mishipa ya damu ipasukapo, ikifanya ubongo ufurike kwa damu, jambo ambalo huzuia vijia viunganishavyo. Hili hukatiza mitiririko ya kemikali na ya umeme kwenye misuli na husababisha madhara kwa tishu za ubongo.

      Matokeo Yake

      Kila mshtuko wa akili ni tofauti, na mishtuko ya akili yaweza kuwaathiri watu mmoja-mmoja kwa njia ambazo karibu hazina mipaka. Ijapokuwa hakuna yeyote apatwaye na kila tokeo liwezekanalo la mshtuko wa akili, matokeo yaweza kutofautiana kuanzia madogo yasiyoonekana wazi hadi makubwa na yenye kuonekana wazi kwa njia yenye kuumiza. Sehemu ya ubongo inayopatwa na mshtuko wa akili huamua ni utendaji upi wa mwili unaodhoofika.

      Taabu ya kawaida ni udhaifu au kupooza kwa miguu na mikono. Kwa kawaida huo huwa upande mmoja tu wa mwili, upande ulio kinyume cha upande wa ubongo ambapo mshtuko wa akili hutukia. Hivyo, madhara ya ubongo wa upande wa kulia hutokeza kupooza kwa upande wa kushoto, na madhara ya ubongo wa upande wa kushoto hutokeza kupooza kwa upande wa kulia. Huenda watu fulani wakaendelea kutumia mikono na miguu yao, ila tu kupata kwamba misuli yao hutetemeka sana hivi kwamba miguu na mikono yao yaonekana kana kwamba kila moja yaelekea upande wake. Mhasiriwa aonekana kana kwamba anajifunza mchezo wa kuteleza akijaribu kudumisha usawaziko wake. Dakt. David Levine, wa Kitovu cha Kitiba cha Chuo Kikuu cha New York, asema: “Wamepoteza namna ya hisia ambayo huwaambia ikiwa mkono au mguu wao unasonga au la na upo katika nafasi gani.”

      Zaidi ya asilimia 15 ya watu waliopatwa na mshtuko wa akili, hupatwa na magonjwa ya ghafula, ikitokeza visa vya misongo isiyodhibitiwa na, hasa, katika vipindi vya kutokuwa na fahamu. Pia, kuhisi maumivu na vilevile badiliko katika hisi ni kwa kawaida. Mtu mmoja aliyepatwa na mshtuko wa akili ambaye hupatwa na ganzi daima katika mikono na nyayo zake asema: “Kuna siku ambazo kitu hugusa miguu yangu na naamka kwa sababu yaonekana kana kwamba napatwa na mishtuo-umeme.”

      Matokeo ya mshtuko wa akili yaweza kutia ndani kuona vitu viwili-viwili na matatizo katika kumeza. Ikiwa vitovu vya hisi vya mdomo na koo vimeharibika, wahasiriwa wa mshtuko wa akili waweza kupatwa na mambo zaidi yenye kuwavunjia heshima, kama vile mate kutoka mdomoni. Yoyote ya hisi tano yaweza kuathiriwa, ikisababisha hitilafu katika kuona, kusikia, kunusa, kuonja, na kugusa.

      Matatizo ya Uwasiliano

      Jiwazie ukifuatwa na watu wawili wakubwa mno usiowajua kwenye barabara ndogo isiyo na mwangaza mwingi. Ukitupa jicho nyuma wawaona wakivuma kasi kukuelekea. Wajaribu kupiga mayowe ili usaidiwe, lakini sauti haitoki! Je, waweza kuwazia jinsi ambavyo ungehisi kukatishwa tamaa katika hali kama hiyo? Hivyo ndivyo wahasiriwa wengi wa mshtuko wa akili huhisi wanapopoteza uwezo wao wa kusema kwa ghafula.

      Kushindwa kupitisha mawazo, hisia, matumaini, na hofu—kwa kitamathali kutengwa na marafiki na familia—ni mojawapo ya matokeo yenye kuangamiza kabisa ya mshtuko wa akili. Mtu mmoja aliyepatwa na mshtuko wa akili alifafanua hali hiyo kwa njia hii: “Kila wakati nilipojaribu kujieleza hakuna lililotoka. Nililazimika kubaki kimya wala sikuweza kufuata mielekezo ya usemi au iliyoandikwa. Maneno yalisikika . . . kana kwamba watu walionizunguka walikuwa wakizungumza lugha ngeni. Sikuweza kufahamu wala kutumia lugha.”

      Ingawa hivyo, Charles alielewa kila kitu alichokuwa akiambiwa. Lakini kwa habari ya kujibu, yeye aandika: “Nilikuwa nikiyapanga maneno niliyotaka kusema, lakini yalitoka yakiwa yamevurugika na kupotoka. Wakati huo nilihisi nikiwa nimenaswa ndani yangu mwenyewe.” Katika kitabu chake Stroke: An Owner’s Manual, Arthur Josephs aeleza: “Misuli tofauti-tofauti zaidi ya mia moja huongozwa na kuambatanishwa wakati wa usemi na kila mmoja ya misuli hiyo huongozwa na wastani wa nyuroni za mwendo zaidi ya mia moja. . . . Kwa kushangaza, zaidi ya matukio ya nyuroni-misuli 140,000 yahitajiwa katika kila sekunde ya usemi. Je, yashangaza kuwa madhara kwa sehemu ya ubongo inayoongoza misuli hii yaweza kutokeza usemi uliopotoka?”

      Mambo mengi yenye kutamausha katika eneo la usemi hutokezwa na mshtuko wa akili. Kwa kielelezo, huenda mtu asiyeweza kusema akaweza kuimba. Mwingine aweza kusema maneno kwa msukumo lakini si wakati anapotaka kuyasema au aweza, kwa upande ule mwingine, kuzungumza bila kukoma. Wengine hurudia-rudia maneno au fungu la maneno au hutumia maneno isivyofaa, wakisema ndiyo wanapomaanisha la na kusema la wanapomaanisha ndiyo. Wengine hujua maneno wanayotaka kutumia, lakini ubongo hauwezi kuchochea kinywa, midomo, na ulimi kuyasema. Au waweza kupatwa na usemi wenye kukokoteza maneno kwa sababu ya udhaifu wa misuli. Huenda wengine wakakatiza maneno yao kwa vishindo.

      Madhara mengine ya mshtuko wa akili yaweza kuwa kujeruhiwa kwa sehemu ya ubongo ambayo huongoza namna ya sauti yenye hisia-moyo. Tokeo laweza kuwa usemi usio na uchangamshi. Au kwaweza kuwa na ugumu wa kufahamu sauti za wengine zenye hisia-moyo. Vizuizi kama hivi vya uwasiliano na vilivyozungumziwa hapo juu vyaweza kuwatenganisha washiriki wa familia, kama vile mume na mke. Georg aeleza: “Kwa sababu mshtuko wa akili huathiri ishara za uso na za mwili, kwa kweli utu wote mzima, kwa ghafula hatukuelewana kama awali. Kwangu ilionekana kana kwamba nilikuwa na mke mpya kabisa, mtu niliyehitaji kumjua upya tena.”

      Mabadiliko ya Kihisia-Moyo na ya Kiutu

      Kubadilika-badilika kwa hali ya moyoni kusikofaa, kuangua kilio au kicheko, hasira kali, hisi za kushuku zisizo za kawaida, na huzuni nyingi ya kupita kiasi ni sehemu tu ya masumbufu ya kihisia-moyo na ya utu yenye kutia bumbuazi ambayo watu waliopatwa na mshtuko wa akili na familia zao huenda wakalazimika kukabiliana nayo.

      Mhasiriwa wa mshtuko wa akili aitwaye Gilbert aeleza: “Nyakati nyingine nawa mwenye hisia nyepesi, mambo madogo yananifanya ama nicheke ama nilie. Mara kwa mara nichekapo, mtu aweza kuuliza, ‘Mbona unacheka?’ na kwa kweli siwezi kumwambia sababu.” Hili, kutia ndani na matatizo ya usawaziko wa mwili na kuchechemea kidogo, kulimsukuma Gilbert kusema: “Nahisi kana kwamba niko katika mwili mwingine, kana kwamba mimi ni mtu tofauti, si mtu yule niliyekuwa kabla ya kupata mshtuko wa akili.”

      Wakiishi na hali zinazodhoofisha akili na mwili, watu wengi hupatwa na hisia ya mabadiliko ya kihisia-moyo. Hiroyuki, aliyepatwa na hitilafu ya usemi na kupooza kwa sehemu baada ya kupatwa na mshtuko wa akili aeleza: “Hata kadiri muda ulivyopita sikupata nafuu. Niking’amua kuwa singeweza kuendelea na kazi yangu kama awali nilikata tumaini. Nilianza kulaumu vitu na watu nami nikahisi kana kwamba hisia zangu zitalipuka. Sikutenda kama mwanamume.”

      Hofu na hangaiko ni za kawaida kwa wahasiriwa wa mshtuko wa akili. Ellen aeleza: “Ninakuwa na hisia za kukosa usalama wakati ninapopatwa na msongo katika kichwa changu ambao waweza kutoa onyo la kupatwa na mshtuko wa akili siku za baadaye. Ninakuwa mwoga sana ninapojiruhusu kufikiria kwa njia hasi.” Ron aeleza hangaiko analokabiliana nalo: “Kufikia mikataa sahihi wakati mwingine inakuwa kama isiyowezekana kabisa. Kutatua matatizo madogo mawili au matatu wakati mmoja hunitamausha. Nasahau mambo haraka sana hivi kwamba nyakati nyingine siwezi kukumbuka maamuzi yaliyofanywa dakika chache zilizopita. Tokeo ni kwamba, nafanya makosa makubwa sana, na hili laniaibisha mimi na wengine. Nitakuwaje miaka michache ijayo? Je, nitashindwa kuzungumza kwa kutumia akili au kuendesha gari? Je, nitakuwa mzigo wenye kulemea kwa mke wangu?

      Washiriki wa Familia Ni Wahasiriwa Pia

      Basi, yaweza kuonekana kwamba, wahasiriwa wa mshtuko wa akili si wao tu ambao lazima wapigane na matokeo yenye kuangamiza kabisa. Familia zao pia zafanya hivyo. Katika visa fulani lazima wakabiliane na mshtuko mbaya wa kuona mmoja ambaye alikuwa mwenye ufasaha, aliyejiweza wakati mmoja kwa ghafula akididimia machoni pao, akifanywa kuwa kama mtoto mchanga sana mwenye kutegemea wengine kabisa. Mahusiano yaweza kuvurugwa kwani huenda washiriki wa familia wakalazimika kuchukua madaraka wasiyoyazoea.

      Haruko aeleza matokeo yenye kuhuzunisha kwa njia hii: “Mume wangu alipoteza kumbukumbu lake la karibu kila jambo muhimu. Kwa ghafula tulilazimika kuiacha kampuni aliyoisimamia na kupoteza nyumba na mali yetu. Kilichonitaabisha zaidi kilikuwa kutoweza tena kuzungumza kwa uhuru na mume wangu au kumwomba mashauri. Akiwa ametatanika kati ya usiku na mchana, mara nyingi yeye hutoa nepi za kumkinga zihitajikazo usiku. Ijapokuwa tulijua kwamba wakati ungefika ambapo angefikia kiwango hiki, bado ni vigumu kwetu kukubali uhalisi wa hali yake. Hali yetu imetanguka kabisa, hivi kwamba binti yangu na mimi tumekuwa watunzaji wa mume wangu.”

      “Kumtunza mtu aliye na mshtuko wa akili—hata iwe wampenda kadiri gani—kwaweza kukuzidi nguvu nyakati nyingine,” aonelea Elaine Fantle Shimberg katika kitabu Strokes: What Families Should Know. “Misongo na madaraka hayapungui.” Katika visa fulani utunzaji wa hali ya juu ambao washiriki fulani wa familia hutoa waweza kuwa wenye kudhuru kwa afya, hisia-moyo na hali ya kiroho ya mtunzaji. Maria aeleza kwamba mshtuko wa akili wa mama yake ulikuwa na athari kubwa sana katika maisha yake: “Mimi humtembelea kila siku na kujaribu kumjenga kiroho, kusoma na kusali pamoja naye, kisha namwonyesha upendo, namkumbatia, na kumbusu. Ninaporudi nyumbani nakuwa nimechoka kabisa kihisia-moyo—siku fulani kwa kiasi kikubwa hata natapika.”

      Jambo lililo gumu zaidi kwa watunzaji kukabiliana nalo ni badiliko katika tabia. Mwanasaikolojia wa akili Dakt. Ronald Calvanio aambia Amkeni!: “Unapokuwa na ugonjwa unaoathiri utendaji mbalimbali wa juu zaidi wa ubongo—yaani jinsi mtu anavyofikiri, anavyoendesha maisha yake, maitikio yake ya kihisia-moyo—tunashughulika na mtu mwenyewe, kwa hiyo katika njia fulani kuharibika kwa kisaikolojia kunakotokea kwa kweli hubadili maisha ya familia kwa njia kubwa sana.” Yoshiko asimulia: “Mume wangu alionekana kama amebadilika kabisa baada ya ugonjwa wake, akikasirika ghafula kwa sababu ya jambo dogo sana. Nyakati hizi mimi huwa mwenye huzuni sana.”

      Mara nyingi, mabadiliko ya utu huenda yasionekane kwa wale wasio washiriki wa familia. Hivyo, watunzaji fulani hujihisi wakiwa wapweke na huibeba mizigo yao yenye kulemea wakiwa peke yao. Midori aeleza: “Mishtuko ya akili imemwacha mume wangu akiwa hajiwezi kiakili na kihisia-moyo. Ijapokuwa ana uhitaji mkubwa wa kitia-moyo, hatazungumzia hilo na yeyote na huumia akiwa peke yake. Kwa hiyo ni juu yangu kushughulikia hisia-moyo zake. Kutazama hali za moyo za mume wangu kila siku kunanitia wasiwasi na nyakati nyingine hata zaniogopesha.”

      Watu wengi waliopatwa na mshtuko wa akili kutia na familia zao wamekabilianaje na mabadiliko katika maisha yao yaletwayo na mshtuko wa akili? Kila mmoja wetu aweza kuwategemeza katika njia zipi wale wanaoteseka kutokana na madhara ya kulemaza ya mshtuko wa akili? Makala yetu ifuatayo yaeleza.

  • Mshtuko wa Akili—Kisababishi Chake
    Amkeni!—1998 | Februari 8
    • ISHARA ZENYE KUONYA

      • Udhaifu wa ghafula, ganzi, au kupooza kwa uso, mkono, au mguu, hasa upande mmoja wa mwili

      • Kutoona vizuri kwa ghafula, hasa kwa jicho moja; kisa cha kuona vitu maradufu

      • Ugumu wa kuzungumza au kuelewa hata sentensi rahisi

      • Kisunzi au kupoteza usawaziko au upatano wa mwili hasa zinapoungana na ishara nyingine

      Ishara Zisizo za Kawaida Sana

      • Kuumwa kichwa sana kwa ghafula, na kusikoelezeka—mara nyingi hufafanuliwa kuwa “kuumwa kichwa kubaya zaidi”

      • Kichefuchefu cha ghafula na homa—tofauti na ugonjwa uletwao na virusi kwa sababu ya jinsi inavyositawi haraka (ikichukua dakika au saa badala ya siku kadhaa)

      • Kupoteza fahamu kwa muda mfupi au kipindi cha ufahamu uliopunguka (kuzimia, kuvurugika, kufurukuta, kupoteza fahamu)

      Usipuuze Dalili

      Dakt. David Levine ahimiza kwamba wakati dalili zinapotokea, mgonjwa “aende haraka iwezekanavyo kwenye chumba cha dharura cha hospitali. Kuna uthibitisho kwamba ikiwa mshtuko wa akili watibiwa katika saa chache za kwanza, madhara yaweza kupunguzwa.”

      Nyakati nyingine dalili zaweza kutokea kwa kipindi kifupi sana kisha zatoweka. Visa hivi vyajulikana kama TIA, au mashambulio ya haraka ya ukosefu wa mtiririko wa damu. Usizipuuze, kwa vile zaweza kuwa zaonyesha hatari kubwa zaidi ya mshtuko wa akili, na mshtuko wa akili kamili waweza kufuata. Daktari aweza kutibu visababishi na kusaidia kupunguza hatari za kupatwa na mshtuko wa akili baadaye.

      Imetokana na miongozo iliyotolewa na National Stroke Association, Englewood, Colorado, Marekani.

  • Kukabiliana na Matokeo Yake
    Amkeni!—1998 | Februari 8
    • Kukabiliana na Matokeo Yake

      AKIWA amelala katika kitanda cha hospitali mguu na mkono ikiwa imepooza, Gilbert alimwuliza daktari wake: “Je, nitapata kutumia tena mkono na mguu wangu?” Gilbert alisikia jibu hili lenye kuvutia: “Kadiri ufanyavyo bidii, ndivyo utakavyoweza kutumia tena mkono na mguu wako, na ndivyo utakavyotimiza hilo haraka zaidi.” Yeye alijibu: “Niko tayari!” Tibamaungo pamoja na mtazamo chanya ulimsaidia, akiwa na umri wa miaka 65, aache kutumia kiti chenye magurudumu, kisha kitembezi, kisha bakora na hatimaye aliweza kurudi kazini.

      Mingi ya misaada ya kuwezesha kuishi maisha ya kawaida baada ya kupatwa na mshtuko wa akili leo, huunga mkono ile dhana kuwa ikiwa sehemu moja ya ubongo imeharibika, maeneo mengine ya ubongo yaweza kuchukua fungu la tishu zilizojeruhiwa. Kusudi moja la tiba hiyo ni kutokeza uwezekano wa maeneo hayo yasiyohusika na kuyachochea ili kuruhusu ubongo upange upya na kubadilikana,” wasema watafiti Weiner, Lee, na Bell. Hata hivyo, kupona kwategemea mambo mengine pia, kama vile mahali katika ubongo ambapo mshtuko wa akili ulitokea na ukubwa wa mshtuko huo, hali ya jumla ya afya ya mtu huyo, ubora wa utunzaji wa kitiba, na tegemezo la wengine.

      Tegemezo la Familia na Marafiki

      Erikka alishiriki katika mazoezi ya kumsaidia aweze kuishi maisha ya kawaida kwa muda wa miaka mitatu, akijifunza kutembea na kutumia mkono wake wa kulia kufidia mkono wa kushoto uliopooza. Aeleza kilichomsaidia kukabiliana na hali: “Jambo lililokuwa la maana zaidi lilikuwa kwamba mume wangu na marafiki wangu walibaki wakiwa waaminifu-washikamanifu kwangu. Kujua kwamba walinipenda kulinipa nguvu, na waliponitia moyo nisikate tamaa, hilo lilinichochea.”

      Washiriki wa familia hupata kuwa wenzi katika hatua za kupona za mpendwa wao. Wanahitaji kuwauliza maswali watumishi wa kitiba na kuchunguza kwa makini tiba ambazo huenda zikahitaji kuendelezwa nyumbani ili kwamba asipoteze maendeleo ambayo tayari yamefanywa. Subira, fadhili, uelewevu, na shauku zionyeshwazo na washiriki wa familia na marafiki huandaa mazingira ya kihisia-moyo yaliyo salama ya kujifunzia upya usemi, kusoma, na kazi nyingine za maisha ya kila siku.

      Akijaribu kuwa mwenye usawaziko kati ya kulazimisha na kubembeleza, John alifanya bidii kumsaidia mke wake Ellen na mazoezi na tiba. Aelezea jitihada za familia yake: “Hatungemruhusu Ellen ajisikitikie kupita kiasi. Nyakati nyingine tulikuwa wasimamizi wakali, lakini sikuzote tuliangalia vizuizi vyake na kutoa usaidizi. Yeye ni mwenye hisia nyepesi, kwa hiyo huwa najitahidi nisimsababishie mkazo.”

      Kadiri Ellen alivyoendelea kujifunza tena kuzungumza kwa msaada wa mtaalamu wa matibabu ya usemi, John alimsaidia. “Kufanya mambo pamoja kulikuwa kitia-moyo, kwa hiyo tulisoma Biblia pamoja kwa sauti, jambo ambalo lilisaidia kuboresha usemi wake. Pia, pole kwa pole mwanzoni, tulishiriki katika huduma, kwani sisi tu Mashahidi wa Yehova. Kwa njia hii Ellen angeweza kushiriki na wengine tumaini tulilo nalo la wakati ujao. Kufanya hivyo kwenyewe kulikuwa tiba kwa Ellen.” Kufikia mwishoni mwa miaka mitatu, Ellen alikuwa amefanya maendeleo sana.

      Kitia-moyo na nguvu ambazo marafiki waweza kutoa hazipasi kudharauliwa kamwe, kwa sababu zaweza kuwa na athari kubwa kuelekea kupona kwa mtu aliyepatwa na mshtuko wa akili. Jarida la kitiba Stroke liliripoti kwamba “Utegemezo mwingi wa kijamii ulipatikana kuwa unaashiria kupona kwa haraka zaidi na maendeleo makubwa zaidi katika kuweza kufanya mambo, hata miongoni mwa wagonjwa waliokuwa na mshtuko wa akili mbaya sana.”

      Bernie alithamini sana tegemezo ambalo marafiki wake walimpa. Yeye atukumbusha: “Ziara za marafiki husaidia kukabiliana na hali. Sauti yenye kusikitikia na mwelekeo wenye kujali huuchangamsha moyo. Ingawa mtu hapaswi kufikiria sana kutojiweza kwake, kutambua maendeleo yoyote kwatia moyo sana.” Sisi sote twaweza kufanya nini ili kutoa tegemezo kwa wale wanaokabiliana na matokeo ya baadaye ya mshtuko wa akili? “Wapelekee maua,” apendekeza Bernie, “au shiriki nao wazo la Kimaandiko au jambo lililoonwa. Hayo yalikuwa yenye msaada sana kwangu.”

      Melva, mzee-mzee aliyepatwa na mshtuko wa akili aliona kuwa jambo la msaada kwa mmoja wa ndugu zake wa kiroho kusali pamoja naye. Gilbert pia apendekeza hili, akieleza: “Yaonyesha kuwa kwa kweli wajali unaposali pamoja na mtu.” Peter, ambaye mshtuko wa akili ulimwacha akiwa haoni vizuri, huthamini sana wakati ambapo watu wengine wanafahamu kizuizi chake na kuchukua wakati kumsomea.

      Pia kumsaidia mtu kwenda na kutoka mahali pa kumsaidia kuweza kuishi maisha ya kawaida ni ishara ya upendo. Kuhakikisha kwamba nyumba ya mhasiriwa wa mshtuko wa akili ni mahali salama ni muhimu pia. Kuanguka ni tisho la daima wakati usawaziko wa mwili unapokuwa tatizo. Kwa kielelezo, Gilbert, alithamini msaada wenye fadhili wa marafiki ambao, kati ya mambo mengine, walimwekea pao la kujishikilia kwenye bafu yake kwa ajili ya usalama.

      Kujifunza Kutoa Tegemezo

      Mabadiliko ya hali ya moyo na mwelekeo mkubwa wa kulia waweza kuwa wenye kuaibisha mhasiriwa wa mshtuko wa akili, na pia kutatanishwa kwa watu walio kando ambao huenda wasijue jinsi ya kutenda. Hata hivyo, kwa kujifunza kuwa mwenye kutegemeza, marafiki waweza kumwokoa mhasiriwa wa mshtuko wa akili ambaye aweza kujitenga na wengine. Kwa kawaida vipindi vya kulia hupunguka. Lakini machozi yajapo, baki ukiwa mtulivu na ukae na mtu huyo, ukimwambia yale ungependa kusikia ikiwa ungekuwa katika hali yake.

      Zaidi ya yote, kuza upendo wa kimungu kwa wale ambao udhaifu wao huenda ukawa umebadili utu ambao uliujua hapo awali. Wao hutambua unavyohisi, na hilo, nalo, huathiri itikio lao kukuelekea. Erikka aeleza: “Huenda nisipate kuwa mtu yuleyule tena. Lakini hakuna yeyote anayepaswa kudai hilo kutoka kwa mhasiriwa wa mshtuko wa akili. Jamaa na marafiki wapaswa kujifunza kumpenda mtu huyo jinsi alivyo. Wakichunguza kwa uangalifu utu wake, watagundua kuwa sifa nyingi zenye kupendeza za wakati uliopita zingali zipo.”

      Mtu awapo hawezi kuzungumza au kueleweka staha ya kibinafsi hushuka. Kwa kufanya jitihada ya kuzungumza nao, marafiki waweza kuwahakikishia wale ambao usemi wao umedhoofika. Takashi aeleza: “Ninachofikiria na kuhisi moyoni hakijabadilika. Hata hivyo, watu huelekea kuniepuka kwa sababu hawawezi kuwa na mazungumzo ya kawaida nami. Ni vigumu kwangu kuwafikia watu, lakini mtu ajapo kuzungumza nami, huwa ni kitia-moyo kikubwa sana kwangu na hilo hunifurahisha sana sana!”

      Ifuatayo ni miongozo fulani iwezayo kutusaidia sote tuweze kuwategemeza na kuwatia moyo wale wenye udhaifu wa usemi.

      Mishtuko mingi ya akili haiathiri uwezo wa kufikiri. Watu wengi ambao wamepatwa na mshtuko wa akili hubaki wakiwa chonjo kiakili, hata ingawa huenda usemi wao ukawa mgumu kuuelewa. Usiseme nao kwa njia yenye kushusha au kusema kana kwamba wasema na mtoto. Watendee kwa adhama.

      Sikiliza kwa subira. Huenda wakahitaji wakati ili kupanga upya wazo au kumaliza neno, fungu la maneno, au sentensi. Kumbuka kwamba msikilizaji mwenye kujali zaidi hana haraka ya kusikia.

      Usijifanye kuwa waelewa ikiwa huelewi. Kiri kwa ufadhili: “Samahani. Yaonekana sipati kukuelewa. Tujaribu tena baadaye.”

      Sema polepole na waziwazi kwa sauti ya kawaida.

      Tumia sentensi fupi na maneno yajulikanayo.

      Tumia maswali ambayo yanahitaji jibu la ndiyo au la, na umtie moyo kujibu. Kumbuka kwamba huenda wasiweze kufahamu maneno yako.

      Punguza kelele za kando-kando.

      Kukabiliana na Hali, kwa Tegemezo Lenye Upendo la Yehova

      Huku likiwa jambo muhimu kujua kisababishi cha mshtuko wako wa akili, kwani hilo hukuwezesha kuchukua hatua na kupunguza hatari ya kupatwa na mishtuko ya akili wakati ujao, kudhibiti hofu inayoandamana ni kwa muhimu pia. Ellen aeleza: “Maneno ya Mungu kwenye Isaya 41:10 hasa hunitia moyo. Hapo yeye husema: ‘Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.’ Yehova amekuwa wa halisi sana kwangu, akinifanya nisiogope.”

      Biblia pia inamsaidia Anand akabiliane na kukata tumaini anakohisi: “Huniandalia tegemezo kubwa, kwa kuwa huniamsha na kuniburudisha.” Tatizo la Hiroyuki lilikuwa jinsi awezavyo kufaidika kutokana na Maandiko, kwa kuwa hakuweza kukaza fikira. Yeye asema: “Nilipata faraja kutokana na kusikiliza vitabu vya Biblia katika kaseti.”

      Mtume Paulo alitaarifu: “Niwapo dhaifu, ndipo niwapo mwenye nguvu.” (2 Wakorintho 12:10) Ni roho ya Yehova iliyomsaidia Paulo kutimiza yale ambayo hangeweza kwa uwezo wake mwenyewe. Wale watu ambao wamepatwa na mshtuko wa akili pia wanaweza kumtegemea Yehova ili kupata nguvu za kiroho. Erikka aeleza: “Wakati tuna afya na twafanya kila jambo kwa nguvu zetu, huenda tusimpe Yehova fursa nyingi za kutusaidia. Lakini kutojiweza kwangu kumeniwezesha kufanya uhusiano wangu naye uwe wenye nguvu zaidi katika njia ya pekee sana.”

      Watunzaji Wapata Tegemezo

      Watunzaji wahitaji tegemezo katika fungu lao la maana. Wanaweza kugeukia wapi ili kupata tegemezo? Mahali pamoja ni katika familia. Kila mshiriki ahitaji kushiriki mzigo wa kutunza. Yoshiko aeleza jinsi wana wake walivyompa tegemezo la kihisia-moyo: “Walikuwa wakiyasikiliza matatizo yangu kana kwamba yalikuwa yao.” Washiriki wa familia wahitaji kupata habari yote iwezayo kupatikana ili wajifunze jinsi ya kumtunza mhasiriwa wa mshtuko wa akili na pia jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya utu wa mpendwa wao.

      Nani wengine wawezao kutoa tegemezo kwa watunzaji? David na familia yake waliigeukia familia yao ya kiroho ndani ya kutaniko la Mashahidi wa Yehova ili kumtunza Victor: “Waliitikia uhitaji wetu. Wakipokezana zamu, nyakati fulani wao huja na kulala katika nyumba yetu ili kumtunza Victor usiku kucha kwa ajili yetu.”

      Kila mtunzaji apaswa kuhisi upendo wenye joto na tegemezo la familia yake ya kiroho. Lakini wengine waweza kuona vigumu kuomba msaada. Haruko aeleza: “Mara nyingi mimi huambiwa: ‘Ikiwa kuna msaada wowote unaohitaji, usisite kutujulisha.’ Lakini nikijua jinsi kila mtu ni mwenye shughuli nyingi, nasita kuomba msaada. Ningeshukuru sana ikiwa watu wangetoa msaada katika njia hususa: ‘Naweza kukusaidia kusafisha. Ni siku gani iliyo nzuri kwako?’ ‘Naweza kukununulia vitu unavyohitaji, je, ni sawa nikija sasa?’”

      Mke wa Kenji alipatwa na mshtuko wa akili; hata hivyo, Kenji aliweza kuandaa utunzaji ambao mke wake alihitaji. Alipata kwamba kwa sala angeweza kumtwika Yehova mizigo yake yenye kulemea. Hatimaye, mke wake akapoteza uwezo wa kusema, na kwa hiyo, Kenji akampoteza mwenzi wa kuzungumza naye. Lakini yeye husoma Biblia kila siku. Asema: “Hunikumbusha kuhusu utunzaji mwororo wa Yehova kwa wale waliopondeka katika roho, na hilo limenizuia nisishuke moyo au kuwa mpweke.”

      Kutegemea roho ya Yehova kwaweza kutusaidia wakati ionekanapo kana kwamba tunashindwa na hisia-moyo. Yoshiko, akikabiliana na mabadiliko ya utu wa mume wake na hamaki za mara kwa mara baada ya kupatwa na mshtuko wa akili, asimulia: “Nyakati fulani nimehisi nikichochewa na msukumo wa kutaka kupiga yowe kwa sauti kubwa. Katika nyakati hizo nilikuwa nikisali kwa Yehova sikuzote, na roho yake ilikuwa ikiniletea amani.” Akithamini uaminifu-mshikamanifu wa Yehova kumwelekea, haruhusu chochote kuingilia njia yake ya maisha ya Kikristo. Yeye huhudhuria kwa ukawaida mikutano ya Kikristo, hushiriki katika huduma, na hufanya funzo la kibinafsi la Biblia. “Kwa kufanya sehemu yangu,” Yoshiko asema, “Najua kwamba Yehova hataniacha kamwe.”

      Mahangaiko yanaponyemelea, sikuzote Yehova yuko tayari kusikiliza. Midori, ambaye mume wake alipatwa na mshtuko wa akili, hupata faraja kutokana na uhakika wa kwamba, kitamathali, Yehova ameweka machozi yote ambayo amelia katika “chupa” yake. (Zaburi 56:8) Yeye hukumbuka maneno ya Yesu: “Msihangaike kamwe juu ya siku ifuatayo.” Yeye asema: “Nimeamua kuwa mwenye subira hadi ulimwengu mpya ujapo.”—Mathayo 6:31-34.

      Kukabili Vizuizi Vikali

      Ni kweli kwamba katika kujaribu kuishi maisha ya kawaida watu fulani hupata nafuu sana, lakini wengine hufaulu kidogo tu katika kupata tena uwezo mbalimbali waliokuwa nao kabla ya kupatwa na mshtuko wa akili. Ni nini kiwezacho kuwasaidia wenye kufaulu kidogo kukabili ugumu wa vizuizi vyao, ingawa huenda vikawa vikali na vyenye kudumu sana?

      Bernie, ambaye alipoteza uwezo mkubwa wa kusonga kwa sababu ya mshtuko wa akili, ajibu: “Shangwe ya tumaini langu la uhai udumuo milele katika dunia iliyo paradiso na sala kwa Baba yangu wa kimbingu, Yehova, zilinisaidia kukubali vizuizi vyangu kwa utulivu.”

      Tumaini hilo lilimsaidia Erikka na mume wake, Georg, wakubali vizuizi vyake na bado waendelee kuonea shangwe maisha. Georg aeleza: “Tuna ahadi ya Mungu ya kuponywa kabisa siku moja. Kwa hiyo hatukazii fikira kutojiweza huku. Bila shaka, tungali twafanya yote tuwezayo kwa ajili ya afya ya Erikka. Lakini waweza kujifunza kuishi na kutopatana kwa misuli na kukazia fikira mambo yaliyo chanya zaidi.”—Isaya 33:24; 35:5, 6; Ufunuo 21:4.

      Katika visa ambapo kupona ni kwa kadiri ndogo, tegemezo la familia na marafiki ni muhimu hata zaidi. Wanaweza kumsaidia mhasiriwa kukabiliana hadi wakati wa Mungu ufikapo wa kurekebisha taabu zote za afya.

      Kujua kwamba kuna wakati ujao mtukufu kwa ajili ya wahasiriwa wa mshtuko wa akili na familia zao wakati ambapo afya itarudishwa huwawezesha kukabiliana na maisha siku kwa siku. Kwa hiyo wanaweza kungojea kwa subira kitulizo bila kuteseka kote, katika ulimwengu mpya wa Mungu unaokuja karibuni. (Yeremia 29:11; 2 Petro 3:13) Wakati huohuo, wote wanaomgeukia Yehova wanaweza kuwa na uhakika kwamba hata sasa atawasaidia na kuwategemeza katika kukabiliana na matokeo yenye kulemaza ya mshtuko wa akili.—Zaburi 33:22; 55:22.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki