Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 2/8 kur. 4-8
  • Mshtuko wa Akili—Kisababishi Chake

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mshtuko wa Akili—Kisababishi Chake
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Matokeo Yake
  • Matatizo ya Uwasiliano
  • Mabadiliko ya Kihisia-Moyo na ya Kiutu
  • Washiriki wa Familia Ni Wahasiriwa Pia
  • Kukabiliana na Matokeo Yake
    Amkeni!—1998
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1998
  • Mshtuko wa Akili!
    Amkeni!—1998
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1999
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 2/8 kur. 4-8

Mshtuko wa Akili—Kisababishi Chake

“UBONGO ndicho kiungo cha mwili kiwezacho kuharibika kwa urahisi sana,” ataarifu mtaalamu wa elimu ya neva Dakt. Vladimir Hachinski, wa Chuo Kikuu cha Western Ontario katika London, Kanada. Ukiwa na asilimia 2 tu ya uzani wote wa mwili, ubongo una chembe za neva zaidi ya bilioni kumi, ambazo zawasiliana daima ili kutokeza fikira, mwendo, na hisia zetu zote. Ukitegemea oksijeni na glukosi kupata nishati, ubongo hupokea ugavi wa daima kupitia mfumo tata wa ateri.

Hata hivyo, sehemu yoyote ya ubongo inyimwapo oksijeni hata kwa sekunde chache, utendaji wa nyuroni ziwezazo kuharibika kwa urahisi hudhoofishwa. Hilo likiendelea kwa zaidi ya dakika chache, madhara ya ubongo hutokea, chembe za ubongo zianzapo kufa pamoja na utendaji zinazouongoza. Hali hii huitwa ischemia, ukosefu wa oksijeni hasa usababishwao na kuziba kwa ateri. Madhara zaidi hutokea kwa tishu za ubongo ukosefu wa oksijeni utokezapo maitikio ya kikemikali yenye kutukia kwa mfululizo kwa njia ya kufisha. Tokeo ni mshtuko wa akili. Mshtuko wa akili hutokea pia wakati mishipa ya damu ipasukapo, ikifanya ubongo ufurike kwa damu, jambo ambalo huzuia vijia viunganishavyo. Hili hukatiza mitiririko ya kemikali na ya umeme kwenye misuli na husababisha madhara kwa tishu za ubongo.

Matokeo Yake

Kila mshtuko wa akili ni tofauti, na mishtuko ya akili yaweza kuwaathiri watu mmoja-mmoja kwa njia ambazo karibu hazina mipaka. Ijapokuwa hakuna yeyote apatwaye na kila tokeo liwezekanalo la mshtuko wa akili, matokeo yaweza kutofautiana kuanzia madogo yasiyoonekana wazi hadi makubwa na yenye kuonekana wazi kwa njia yenye kuumiza. Sehemu ya ubongo inayopatwa na mshtuko wa akili huamua ni utendaji upi wa mwili unaodhoofika.

Taabu ya kawaida ni udhaifu au kupooza kwa miguu na mikono. Kwa kawaida huo huwa upande mmoja tu wa mwili, upande ulio kinyume cha upande wa ubongo ambapo mshtuko wa akili hutukia. Hivyo, madhara ya ubongo wa upande wa kulia hutokeza kupooza kwa upande wa kushoto, na madhara ya ubongo wa upande wa kushoto hutokeza kupooza kwa upande wa kulia. Huenda watu fulani wakaendelea kutumia mikono na miguu yao, ila tu kupata kwamba misuli yao hutetemeka sana hivi kwamba miguu na mikono yao yaonekana kana kwamba kila moja yaelekea upande wake. Mhasiriwa aonekana kana kwamba anajifunza mchezo wa kuteleza akijaribu kudumisha usawaziko wake. Dakt. David Levine, wa Kitovu cha Kitiba cha Chuo Kikuu cha New York, asema: “Wamepoteza namna ya hisia ambayo huwaambia ikiwa mkono au mguu wao unasonga au la na upo katika nafasi gani.”

Zaidi ya asilimia 15 ya watu waliopatwa na mshtuko wa akili, hupatwa na magonjwa ya ghafula, ikitokeza visa vya misongo isiyodhibitiwa na, hasa, katika vipindi vya kutokuwa na fahamu. Pia, kuhisi maumivu na vilevile badiliko katika hisi ni kwa kawaida. Mtu mmoja aliyepatwa na mshtuko wa akili ambaye hupatwa na ganzi daima katika mikono na nyayo zake asema: “Kuna siku ambazo kitu hugusa miguu yangu na naamka kwa sababu yaonekana kana kwamba napatwa na mishtuo-umeme.”

Matokeo ya mshtuko wa akili yaweza kutia ndani kuona vitu viwili-viwili na matatizo katika kumeza. Ikiwa vitovu vya hisi vya mdomo na koo vimeharibika, wahasiriwa wa mshtuko wa akili waweza kupatwa na mambo zaidi yenye kuwavunjia heshima, kama vile mate kutoka mdomoni. Yoyote ya hisi tano yaweza kuathiriwa, ikisababisha hitilafu katika kuona, kusikia, kunusa, kuonja, na kugusa.

Matatizo ya Uwasiliano

Jiwazie ukifuatwa na watu wawili wakubwa mno usiowajua kwenye barabara ndogo isiyo na mwangaza mwingi. Ukitupa jicho nyuma wawaona wakivuma kasi kukuelekea. Wajaribu kupiga mayowe ili usaidiwe, lakini sauti haitoki! Je, waweza kuwazia jinsi ambavyo ungehisi kukatishwa tamaa katika hali kama hiyo? Hivyo ndivyo wahasiriwa wengi wa mshtuko wa akili huhisi wanapopoteza uwezo wao wa kusema kwa ghafula.

Kushindwa kupitisha mawazo, hisia, matumaini, na hofu—kwa kitamathali kutengwa na marafiki na familia—ni mojawapo ya matokeo yenye kuangamiza kabisa ya mshtuko wa akili. Mtu mmoja aliyepatwa na mshtuko wa akili alifafanua hali hiyo kwa njia hii: “Kila wakati nilipojaribu kujieleza hakuna lililotoka. Nililazimika kubaki kimya wala sikuweza kufuata mielekezo ya usemi au iliyoandikwa. Maneno yalisikika . . . kana kwamba watu walionizunguka walikuwa wakizungumza lugha ngeni. Sikuweza kufahamu wala kutumia lugha.”

Ingawa hivyo, Charles alielewa kila kitu alichokuwa akiambiwa. Lakini kwa habari ya kujibu, yeye aandika: “Nilikuwa nikiyapanga maneno niliyotaka kusema, lakini yalitoka yakiwa yamevurugika na kupotoka. Wakati huo nilihisi nikiwa nimenaswa ndani yangu mwenyewe.” Katika kitabu chake Stroke: An Owner’s Manual, Arthur Josephs aeleza: “Misuli tofauti-tofauti zaidi ya mia moja huongozwa na kuambatanishwa wakati wa usemi na kila mmoja ya misuli hiyo huongozwa na wastani wa nyuroni za mwendo zaidi ya mia moja. . . . Kwa kushangaza, zaidi ya matukio ya nyuroni-misuli 140,000 yahitajiwa katika kila sekunde ya usemi. Je, yashangaza kuwa madhara kwa sehemu ya ubongo inayoongoza misuli hii yaweza kutokeza usemi uliopotoka?”

Mambo mengi yenye kutamausha katika eneo la usemi hutokezwa na mshtuko wa akili. Kwa kielelezo, huenda mtu asiyeweza kusema akaweza kuimba. Mwingine aweza kusema maneno kwa msukumo lakini si wakati anapotaka kuyasema au aweza, kwa upande ule mwingine, kuzungumza bila kukoma. Wengine hurudia-rudia maneno au fungu la maneno au hutumia maneno isivyofaa, wakisema ndiyo wanapomaanisha la na kusema la wanapomaanisha ndiyo. Wengine hujua maneno wanayotaka kutumia, lakini ubongo hauwezi kuchochea kinywa, midomo, na ulimi kuyasema. Au waweza kupatwa na usemi wenye kukokoteza maneno kwa sababu ya udhaifu wa misuli. Huenda wengine wakakatiza maneno yao kwa vishindo.

Madhara mengine ya mshtuko wa akili yaweza kuwa kujeruhiwa kwa sehemu ya ubongo ambayo huongoza namna ya sauti yenye hisia-moyo. Tokeo laweza kuwa usemi usio na uchangamshi. Au kwaweza kuwa na ugumu wa kufahamu sauti za wengine zenye hisia-moyo. Vizuizi kama hivi vya uwasiliano na vilivyozungumziwa hapo juu vyaweza kuwatenganisha washiriki wa familia, kama vile mume na mke. Georg aeleza: “Kwa sababu mshtuko wa akili huathiri ishara za uso na za mwili, kwa kweli utu wote mzima, kwa ghafula hatukuelewana kama awali. Kwangu ilionekana kana kwamba nilikuwa na mke mpya kabisa, mtu niliyehitaji kumjua upya tena.”

Mabadiliko ya Kihisia-Moyo na ya Kiutu

Kubadilika-badilika kwa hali ya moyoni kusikofaa, kuangua kilio au kicheko, hasira kali, hisi za kushuku zisizo za kawaida, na huzuni nyingi ya kupita kiasi ni sehemu tu ya masumbufu ya kihisia-moyo na ya utu yenye kutia bumbuazi ambayo watu waliopatwa na mshtuko wa akili na familia zao huenda wakalazimika kukabiliana nayo.

Mhasiriwa wa mshtuko wa akili aitwaye Gilbert aeleza: “Nyakati nyingine nawa mwenye hisia nyepesi, mambo madogo yananifanya ama nicheke ama nilie. Mara kwa mara nichekapo, mtu aweza kuuliza, ‘Mbona unacheka?’ na kwa kweli siwezi kumwambia sababu.” Hili, kutia ndani na matatizo ya usawaziko wa mwili na kuchechemea kidogo, kulimsukuma Gilbert kusema: “Nahisi kana kwamba niko katika mwili mwingine, kana kwamba mimi ni mtu tofauti, si mtu yule niliyekuwa kabla ya kupata mshtuko wa akili.”

Wakiishi na hali zinazodhoofisha akili na mwili, watu wengi hupatwa na hisia ya mabadiliko ya kihisia-moyo. Hiroyuki, aliyepatwa na hitilafu ya usemi na kupooza kwa sehemu baada ya kupatwa na mshtuko wa akili aeleza: “Hata kadiri muda ulivyopita sikupata nafuu. Niking’amua kuwa singeweza kuendelea na kazi yangu kama awali nilikata tumaini. Nilianza kulaumu vitu na watu nami nikahisi kana kwamba hisia zangu zitalipuka. Sikutenda kama mwanamume.”

Hofu na hangaiko ni za kawaida kwa wahasiriwa wa mshtuko wa akili. Ellen aeleza: “Ninakuwa na hisia za kukosa usalama wakati ninapopatwa na msongo katika kichwa changu ambao waweza kutoa onyo la kupatwa na mshtuko wa akili siku za baadaye. Ninakuwa mwoga sana ninapojiruhusu kufikiria kwa njia hasi.” Ron aeleza hangaiko analokabiliana nalo: “Kufikia mikataa sahihi wakati mwingine inakuwa kama isiyowezekana kabisa. Kutatua matatizo madogo mawili au matatu wakati mmoja hunitamausha. Nasahau mambo haraka sana hivi kwamba nyakati nyingine siwezi kukumbuka maamuzi yaliyofanywa dakika chache zilizopita. Tokeo ni kwamba, nafanya makosa makubwa sana, na hili laniaibisha mimi na wengine. Nitakuwaje miaka michache ijayo? Je, nitashindwa kuzungumza kwa kutumia akili au kuendesha gari? Je, nitakuwa mzigo wenye kulemea kwa mke wangu?

Washiriki wa Familia Ni Wahasiriwa Pia

Basi, yaweza kuonekana kwamba, wahasiriwa wa mshtuko wa akili si wao tu ambao lazima wapigane na matokeo yenye kuangamiza kabisa. Familia zao pia zafanya hivyo. Katika visa fulani lazima wakabiliane na mshtuko mbaya wa kuona mmoja ambaye alikuwa mwenye ufasaha, aliyejiweza wakati mmoja kwa ghafula akididimia machoni pao, akifanywa kuwa kama mtoto mchanga sana mwenye kutegemea wengine kabisa. Mahusiano yaweza kuvurugwa kwani huenda washiriki wa familia wakalazimika kuchukua madaraka wasiyoyazoea.

Haruko aeleza matokeo yenye kuhuzunisha kwa njia hii: “Mume wangu alipoteza kumbukumbu lake la karibu kila jambo muhimu. Kwa ghafula tulilazimika kuiacha kampuni aliyoisimamia na kupoteza nyumba na mali yetu. Kilichonitaabisha zaidi kilikuwa kutoweza tena kuzungumza kwa uhuru na mume wangu au kumwomba mashauri. Akiwa ametatanika kati ya usiku na mchana, mara nyingi yeye hutoa nepi za kumkinga zihitajikazo usiku. Ijapokuwa tulijua kwamba wakati ungefika ambapo angefikia kiwango hiki, bado ni vigumu kwetu kukubali uhalisi wa hali yake. Hali yetu imetanguka kabisa, hivi kwamba binti yangu na mimi tumekuwa watunzaji wa mume wangu.”

“Kumtunza mtu aliye na mshtuko wa akili—hata iwe wampenda kadiri gani—kwaweza kukuzidi nguvu nyakati nyingine,” aonelea Elaine Fantle Shimberg katika kitabu Strokes: What Families Should Know. “Misongo na madaraka hayapungui.” Katika visa fulani utunzaji wa hali ya juu ambao washiriki fulani wa familia hutoa waweza kuwa wenye kudhuru kwa afya, hisia-moyo na hali ya kiroho ya mtunzaji. Maria aeleza kwamba mshtuko wa akili wa mama yake ulikuwa na athari kubwa sana katika maisha yake: “Mimi humtembelea kila siku na kujaribu kumjenga kiroho, kusoma na kusali pamoja naye, kisha namwonyesha upendo, namkumbatia, na kumbusu. Ninaporudi nyumbani nakuwa nimechoka kabisa kihisia-moyo—siku fulani kwa kiasi kikubwa hata natapika.”

Jambo lililo gumu zaidi kwa watunzaji kukabiliana nalo ni badiliko katika tabia. Mwanasaikolojia wa akili Dakt. Ronald Calvanio aambia Amkeni!: “Unapokuwa na ugonjwa unaoathiri utendaji mbalimbali wa juu zaidi wa ubongo—yaani jinsi mtu anavyofikiri, anavyoendesha maisha yake, maitikio yake ya kihisia-moyo—tunashughulika na mtu mwenyewe, kwa hiyo katika njia fulani kuharibika kwa kisaikolojia kunakotokea kwa kweli hubadili maisha ya familia kwa njia kubwa sana.” Yoshiko asimulia: “Mume wangu alionekana kama amebadilika kabisa baada ya ugonjwa wake, akikasirika ghafula kwa sababu ya jambo dogo sana. Nyakati hizi mimi huwa mwenye huzuni sana.”

Mara nyingi, mabadiliko ya utu huenda yasionekane kwa wale wasio washiriki wa familia. Hivyo, watunzaji fulani hujihisi wakiwa wapweke na huibeba mizigo yao yenye kulemea wakiwa peke yao. Midori aeleza: “Mishtuko ya akili imemwacha mume wangu akiwa hajiwezi kiakili na kihisia-moyo. Ijapokuwa ana uhitaji mkubwa wa kitia-moyo, hatazungumzia hilo na yeyote na huumia akiwa peke yake. Kwa hiyo ni juu yangu kushughulikia hisia-moyo zake. Kutazama hali za moyo za mume wangu kila siku kunanitia wasiwasi na nyakati nyingine hata zaniogopesha.”

Watu wengi waliopatwa na mshtuko wa akili kutia na familia zao wamekabilianaje na mabadiliko katika maisha yao yaletwayo na mshtuko wa akili? Kila mmoja wetu aweza kuwategemeza katika njia zipi wale wanaoteseka kutokana na madhara ya kulemaza ya mshtuko wa akili? Makala yetu ifuatayo yaeleza.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

ISHARA ZENYE KUONYA

• Udhaifu wa ghafula, ganzi, au kupooza kwa uso, mkono, au mguu, hasa upande mmoja wa mwili

• Kutoona vizuri kwa ghafula, hasa kwa jicho moja; kisa cha kuona vitu maradufu

• Ugumu wa kuzungumza au kuelewa hata sentensi rahisi

• Kisunzi au kupoteza usawaziko au upatano wa mwili hasa zinapoungana na ishara nyingine

Ishara Zisizo za Kawaida Sana

• Kuumwa kichwa sana kwa ghafula, na kusikoelezeka—mara nyingi hufafanuliwa kuwa “kuumwa kichwa kubaya zaidi”

• Kichefuchefu cha ghafula na homa—tofauti na ugonjwa uletwao na virusi kwa sababu ya jinsi inavyositawi haraka (ikichukua dakika au saa badala ya siku kadhaa)

• Kupoteza fahamu kwa muda mfupi au kipindi cha ufahamu uliopunguka (kuzimia, kuvurugika, kufurukuta, kupoteza fahamu)

Usipuuze Dalili

Dakt. David Levine ahimiza kwamba wakati dalili zinapotokea, mgonjwa “aende haraka iwezekanavyo kwenye chumba cha dharura cha hospitali. Kuna uthibitisho kwamba ikiwa mshtuko wa akili watibiwa katika saa chache za kwanza, madhara yaweza kupunguzwa.”

Nyakati nyingine dalili zaweza kutokea kwa kipindi kifupi sana kisha zatoweka. Visa hivi vyajulikana kama TIA, au mashambulio ya haraka ya ukosefu wa mtiririko wa damu. Usizipuuze, kwa vile zaweza kuwa zaonyesha hatari kubwa zaidi ya mshtuko wa akili, na mshtuko wa akili kamili waweza kufuata. Daktari aweza kutibu visababishi na kusaidia kupunguza hatari za kupatwa na mshtuko wa akili baadaye.

Imetokana na miongozo iliyotolewa na National Stroke Association, Englewood, Colorado, Marekani.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki