Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Mishtuko ya Akili Mfululizo huu wa makala “Kukabiliana na Mshtuko wa Akili” (Februari 8, 1998) ulijibu sala yangu. Mimi na mume wangu tulikuwa tukihudhuria mkusanyiko wa Kikristo miaka michache iliyopita alipopatwa na mshtuko wa akili. Alipokuwa akijaribu kuniandikia habari fulani, mkono wake uliteleza kwenye karatasi; upande wake wote wa kulia ulikuwa umeathiriwa. Makala hiyo ilinisaidia sana kwa njia nisiyoweza kueleza kamwe. Ni vizuri sana kujua kwamba Yehova hajatusahau.
F. S. H., Marekani
Saa chache tu kabla ya kupokea gazeti hili, nilijaribu bila kufanikiwa kumweleza mke wangu jinsi nilivyohisi, lakini sikuweza kujieleza kwa kadiri ambayo ningalitaka kwa sababu ya mshtuko wangu wa akili. Tayari nimelisoma gazeti hili mara tatu. Mke wangu amelisoma pia.
R. Z., Italia
Baba yangu, aliyekuwa mtumishi mwaminifu wa Yehova kwa miaka mingi, alikufa mwaka jana kwa mshtuko wa akili. Makala hiyo ilinisaidia kuelewa tabia aliyodhihirisha kabla ya kifo chake. Ufafanuzi kuhusu mabadiliko ya kihisia-moyo, vilevile kwa nini mtu mwenye mshtuko wa akili hupata ugumu kuwasiliana, ulinisaidia kuelewa kidogo zaidi kile kilichokuwa kikimpata baba.
V. C., Marekani
Nilipatwa na mshtuko wa akili mwaka mmoja uliopita na bado nang’ang’ana na kasoro hii kwenye upande wangu wa kushoto. Makala hizi zitakomesha mafumbo na hofu fulani zinazohusianishwa na mshtuko wa akili. Kusema kwamba mshtuko wa akili huwapata wazee peke yao ni ngano. Nilipopatwa nao nilikuwa na umri wa miaka 47 pekee.
A. A., Uingereza
Makala hii ilinisaidia sana kumwelewa binti yangu Lucia, aliyepatwa na majeraha mabaya sana kichwani katika aksidenti ya gari alipokuwa na umri wa miezi miwili. Hawezi kueleza hisia zake. Hata hivyo, makala hiyo ilinisaidia kuelewa sababu.
N. K., Slovakia
Mimi ni muuguzi aliyesajiliwa ambaye amefuzu katika kutunza wasiojiweza na nimepata uzoefu mkubwa kwa kufanya kazi na wagonjwa wenye mshtuko wa akili. Jambo nililothamini zaidi katika makala hii lilikuwa mfikio wenye hisia-moyo ulioonyeshwa katika kuelezea ugumu unaopata familia zenye mgonjwa wa mshtuko wa akili.
L. C., Marekani
Mama yangu amepatwa na mashambulio ya haraka ya ukosefu wa mtiririko wa damu. Kama ungemwona, ungedhani amepona kabisa. Lakini ana makovu makubwa sana ya kihisia-moyo. Alikuwa mtu mwenye kujitumaini lakini sasa amekuwa dhaifu sana. Asanteni kwa kuonyesha waziwazi madhara ya kisaikolojia yanayoletwa na ugonjwa huu.
R. C., Italia
Miaka miwili iliyopita mama yangu alishikwa na mshtuko wa akili mara mbili. Wa kwanza ulifanya apoteze kumbukumbu lake, na wa pili ukafanya upande wake wa kuume upooze. Nyakati nyingine ninakosa subira naye na kusema mambo yanayomhuzunisha. Makala yenu ilinitia moyo niwe mwenye kuelewa hali zaidi.
R. T. S., Brazili
Unamna-Namna wa Kikristo Natoa shukrani zangu za moyo mweupe kwa mfululizo wa makala “Maoni ya Biblia: Je, Muungano wa Kikristo Huruhusu Kuwe na Unamna-Namna?” (Februari 8, 1998) Kadiri ninavyomjua Yehova zaidi ndivyo nipatapo furaha zaidi kuwa katika tengenezo lake, ambamo twaweza kufurahia nyutu za namna mbalimbali.
I. P., Slovenia
Nina umri wa miaka 15 nami husoma Amkeni! kwa ukawaida. Nilithamini hasa makala hii. Sehemu moja ilizungumzia juu ya Paradiso na namna itakavyokuwa. Nilikuwa nikifikiria namna wanadamu wakamilifu wangekuwa na kama sote tungefanana katika sura na mawazo. Sasa nafahamu kwamba kutakuwako unamna-namna mwingi katika wanadamu na wanyama.
J. C., Marekani