Kuutazama Ulimwengu
Mioto ya Misitu Nchini Mexico
Mfululizo wa mioto ya misitu kufikia katikati ya Aprili ambao ulikuwa umeharibu ekari zipatazo 300,000 nchini Mexico umetajwa kuwa “msiba wa mazingira.” Kulingana na Julia Carabias Lillo, katibu wa serikali ya muungano ya Mexico, mioto ipatayo 6,800 kufikia wakati huo ilikuwa imetokea nchini Mexico katika wakati ulioitwa msimu mbaya zaidi wa mioto katika miaka 57 ambayo imepita. Ingawa hali-joto zilikuwa juu kupita wastani wa kawaida na mvua ilikuwa haba, mioto mingi ilianzishwa na “matendo ya wanadamu—kwa sababu ya kutojua, uzembe, na hata uhalifu,” laripoti gazeti El Universal. Octavio Escobar López, mkurugenzi wa eneo hilo wa Halmashauri ya Mali-asili, alisema: “Itachukua karibu miaka kumi kupata tena mimea na wanyama ambao tumepoteza kwa muda uzidio tu siku tatu.”
Mazoezi na Urefu wa Maisha
“Kutembea haraka-haraka kwa nusu-saa mara sita tu kwa mwezi huonekana kukipunguza kifo cha [mapema] kwa asilimia 44,” laripoti The New York Times kuhusu uchunguzi mmoja wa karibuni juu ya urefu wa maisha. Watafiti nchini Finland walifuatia karibu mapacha 16,000 kwa wastani wa miaka 19 na kupata kwamba hata wenye kufanya mazoezi ya mara kwa mara tu “hawakuelekea sana kwa asilimia 30 kufa kwa kulinganisha na mapacha wao wenye kukaa tu bila mazoezi.” Uchunguzi huo ni muhimu kwa sababu mambo ya chembe za urithi yalitiliwa maanani katika kuamua ubora wa mazoezi. Steve Farrell, mtafiti wa mazoezi ya viungo ambaye hakuhusika na uchunguzi huo, alisema: “Hata kama una chembe za urithi zenye kasoro, uchunguzi huo waonyesha kwa uthabiti kwamba kuongeza utendaji wa kimwili kwaweza kukusaidia kurefusha maisha yako.”
Je, Ni Ndege Wahalifu?
Polisi nchini Afrika Kusini wamegundua magendo ya almasi inayohusu ndege. Polisi wasema kwamba wafanyakazi wa mgodi ambao unamilikiwa na serikali huweka njiwa katika visanduku vya kubebea chakula au katika nguo zao kubwa-kubwa ili kuwaingiza kiharamu ndani ya machimbo. Huko wao huwawekea ndege hao almasi na kisha kuwaachilia wapuruke, laripoti Los Angeles Times. Njiwa hawa wanaweza kusafiri kwa kilometa nyingi wakiwa na hizo almasi. Katika miaka kadhaa ambayo imepita, ndege wanne wameshikwa wakiwa na almasi ya magendo. Katika pindi moja, njiwa mmoja alipatikana amebeba karati sita za almasi ambazo hazijakatwa zikiwa zimefungwa chini ya mabawa yake. Kufikia wakati huu, watu wapatao 70 wameshikwa kwa kutumia mbinu hiyo. Gazeti hilo la habari lilisema kwamba maofisa wa kampuni hiyo wanakadiria kwamba karibu kila almasi 1 kati ya 3 zinazochimbwa huibwa na wafanyakazi wasio wanyofu.
Kubadili Chembe za Urithi
Katika mwongo ambao umepita, wanasayansi wamefanya uvumbuzi mwingi kuhusu chembe za urithi ambazo yasemekana eti zinaongoza tabia na matatizo fulani katika wanadamu. Wanasayansi fulani wametabiri kwamba siku moja jambo hili litawawezesha wanadamu warekebishe chembe za urithi na kuondoa tabia zisizotakikana. Kwa mfano, The New York Times laripoti kwamba Lee Silver, mwanabiolojia kwenye Chuo Kikuu cha Princeton, adai kwamba wazao wetu watakuwa werevu zaidi na wenye kufanya riadha zaidi nao wataishi kwa mamia ya miaka. Lakini, John Horgan, mtungaji wa kitabu The End of Science, asema: “Watafiti wanatumaini kwamba wao wataweza kurekebisha utu wa wanadamu kwa kurekebisha chembe za urithi. Lakini kufikia sasa hakuna hata dai moja leo linalohusianisha chembe za urithi na tabia-tata za wanadamu ambalo limethibitishwa na uchunguzi uliofanywa baadaye.” Kwa hiyo, Horgan aongezea: “Kwa kufikiria mambo ambayo sayansi imeshindwa na vilevile mambo ambayo imetimiza kihalali, labda wanasayansi na waandishi wa habari pia watatoa ripoti zisizopotoa na nyofu zaidi kuhusu matazamio halisi ya sayansi.”
Je, Bidhaa za Shamba Zinazidi Kukosa Lishe?
Je, matunda na mboga zinazidi kukosa lishe leo kwa sababu ya kudhoofika kwa udongo? Kulingana na wanasayansi wa udongo, jibu ni la. Kijarida University of California Berkeley Wellness Letter chasema: “Vitamini katika mimea hutengenezwa na mimea yenyewe.” Basi, ikiwa udongo unakosa madini fulani, mimea haiwezi kumea vizuri. Mmea waweza kukosa kuchanua maua, au unaweza kunyauka tu na kufa. Ili jambo hilo lisitendeke, wakulima hutumia mbolea ili kurudisha madini kwenye udongo. Kijarida hicho cha Wellness Letter chasema: “Ikiwa matunda na mboga unazonunua zinaonekana nzuri, uwe na hakika ya kwamba hizo zinaweza kuwa na lishe inayotakikana.”
Nyumba Zilizojengwa Bila Meko
Inakadiriwa kwamba nchini Australia karibu nusu ya milo yote hailiwi nyumbani. Mwelekeo huo umekuwa na athari kubwa hivi kwamba nyumba fulani katika Sydney zinajengwa bila meko, laripoti The Courier-Mail. Kwa kuongezea, kwa sababu Waaustralia hutumia wastani wa dakika 20 pekee kutayarisha milo, maduka mengi ya Australia yanalazimika kuchunguza aina za chakula ambacho zinauza. Meneja mmoja wa maduka fulani katika Sydney adai kwamba Australia inafuata kigezo kilichowekwa na Marekani, ambako milo mingi huliwa mkahawani.
Uhalifu na Ubaguzi wa Jamii
Ongezeko la uhalifu ambalo limetokea karibuni nchini Ugiriki limesemekana limetokezwa na mmiminiko wa wakimbizi na wahamiaji kutoka Ulaya Mashariki na nchi za Balkani, hasa Albania. Richardos Someritis, mwandikaji wa makala za gazeti la habari To Vima, asema kwamba hangaiko kuhusu ongezeko la uhalifu limesababisha aina fulani ya “chuki kwa wageni na mara nyingi ubaguzi mkubwa dhidi ya” wageni walio katika nchi hiyo. Hata hivyo, imeonyeshwa kwamba wageni hawavunji sheria kuliko Wagiriki wenyewe. Kwa mfano, uchunguzi waonyesha kwamba “visa 96 kati ya 100 vya uhalifu vinafanywa na [Wagiriki],” laripoti hilo gazeti la habari. “Visababishi vya uhalifu ni hali ya kiuchumi na ya kijamii,” adai Someritis, “wala si ‘ubaguzi wa kijamii.’” Pia yeye alaumu vyombo vya habari “kwa kuchochea kwa utaratibu chuki kwa wageni na ubaguzi wa kijamii” kwa sababu haviripoti mambo ya hakika kuhusu uhalifu nchini Ugiriki.
Kidude cha Kompyuta Kilikuwa Kikitazama
Wakimbiaji waliokuwa wakishindana katika mbio za masafa marefu za Boston Marathon walibeba kidude kidogo cha kompyuta kwenye mwendo wote wa meta 42,195. Kulingana na gazeti InformationWeek, ili kuchunguza maendeleo yao, wakimbiaji wote walioorodheshwa walikuwa na kidude cha elektroni kilichoshikanishwa kwenye vazi lao. Vidude hivyo vilitayarishwa ili ‘vipitishe habari kwenye vipokezi vilivyokuwa kwenye vituo vilivyokuwa vimewekwa kila baada ya kilometa tano.” Kisha muda wa wakimbiaji uliwasilishwa kwenye makao makuu, ambako uliingizwa kwenye Internet. Mashabiki wa mbio hizo za masafa marefu hawangeweza tu kufuatia wakimbiaji wanaowashabiki bali pia mkimbiaji yeyote ambaye angejaribu kudanganya kwa kutokimbia mwendo wote alishindwa na tekinolojia hii mpya.
Swala Adimu Agunduliwa Tena China
“Swala-mwekundu wa Tibet ambaye alidhaniwa kuwa ametoweka zaidi ya miaka 50 iliyopita, amepatikana tena katika Mkoa wa Shannan katika Eneo Linalojitawala la Tibet,” laripoti China Today. Kwa miaka mingi idadi ya swala-mwekundu, ambaye huwa na kimo cha futi nne na uzito wa kilogramu 110, ilipunguzwa sana na wawindaji ambao walikuwa wakitaka pembe zake zenye thamani. Vita na mabadiliko ya mazingira pia yamewafanya wafe. Inakadiriwa kwamba swala hao warembo wanaopungua 200 wangali wanaishi, nao wameorodheshwa kuwa aina za wanyama walio hatarini mwa kutoweka.
Michezo ya Kumbukumbu
Washindani katika Mashindano ya Kwanza ya Kitaifa ya Kumbukumbu ya Marekani hivi majuzi walijaribu stadi zao kwa kucheza michezo mitano inayohusu kumbukumbu. Majaribio hayo yalitia ndani kukumbuka nyuso 100 za watu wa kawaida, kukariri shairi lenye mistari 50 (kutia ndani alama za vituo), kukariri nomino 125 za Kiingereza (kwa kufuata utaratibu fulani), kukariri orodha ya nambari zilizopangwa bila utaratibu, na kukariri mfuatano wa karata (ambazo zilichanganywa-changanywa na kuwekwa zikiwa zimeangalia chini). Mshindani mmoja, Wallace Bustello, alivutia washiriki wenzake kwa kukariri tarakimu 109 kwa mfululizo ambazo zilichaguliwa bila utaratibu. Lakini mshindi kwa ujumla alikuwa Tatiana Cooley mwenye umri wa miaka 26. Kulingana na Daily News la New York, yeye pamoja na babake, ambaye hufanya programu za satelaiti katika kampuni moja ya mambo ya angani, walikuwa wamezoea kushindana katika michezo ya kumbukumbu wakiwa nyumbani. “Kwa kawaida nilikuwa nikishinda,” asema Tatiana.
Sherehe Katika Mto Ganges
Mamilioni ya Wahindu walijitumbukiza katika Mto Ganges mnamo Aprili wakati ambapo sherehe ya Kumbh Mela, au sherehe ya gudulia ilifikia upeo. Sherehe hiyo ya Kihindu ya Kumbh Mela huchukua muda wa miezi mitatu nayo huadhimisha zawadi ya kutoweza kufa kwa nafsi. Sherehe hiyo hufanywa kila baada ya miaka mitatu nayo huzunguka katika majiji manne ya India, ambako, kulingana na hekaya, asali ya kutoweza kufa kwa nafsi iliangukia dunia wakati ambapo miungu na roho waovu walipopigana wakiing’ang’ania huko mbinguni. Katika nyakati zilizopita, msongamano wa watu waliotaka kujitosa katika maji hayo matakatifu ya India umesababisha vifo vya wengi.