Je, Ni Jeni Zetu Ziamuazo Tutakayotenda?
“TULIZOEA kufikiri kwamba ajali yetu huamuliwa na unajimu. Sasa twajua, kwa kiwango kikubwa, ajali yetu inaamuliwa na jeni zetu.” Hivyo ndivyo alivyosema James Watson, aliyenukuliwa mwanzoni mwa kitabu Exploding the Gene Myth, kilichoandikwa na Ruth Hubbard na Elijah Wald. Hata hivyo, chini tu ya mnukuo wa Watson, R. C. Lewontin, Steven Rose, na Leon J. Kamin wananukuliwa wakisema: “Hatuwezi kuwazia juu ya mwenendo wowote wa kijamii wenye maana ulioko kiasili katika jeni zetu katika njia ya kwamba hauwezi kurekebishwa na hali za kijamii.”
Karatasi yenye kufunika kitabu hicho hufupisha baadhi ya yaliyomo ndani yacho na kuanza kwa swali la maana, “Je, mwenendo wa binadamu unaongozwa na jeni?” Yaani, je, mwenendo wa binadamu unaamuliwa kabisa na jeni ambazo hupitisha hulka zenye kurithiwa na vitabia vya kibiolojia vya kiumbe-hai? Je, mwenendo fulani usio wa adili ukubaliwe kwa msingi wa kwamba unaongozwa na jeni? Je, wahalifu washughulikiwe wakiwa wahasiriwa wa msimbo jeni, wakiwa hawawezi kulaumika kwa sababu ya kuelekezwa na jeni?
Hatuwezi kukataa kwamba wanasayansi wamefanya ugunduzi wenye manufaa katika karne hii. Miongoni mwa ugunduzi huu ni DNA yenye kushangaza, iitwayo eti ramani ya mfanyizo wetu wa kijeni. Habari iliyo katika msimbo jeni imeshangaza wanasayansi na watu wa kawaida vilevile. Utafiti katika upande wa jeni umegundua nini hasa? Yaliyopatikana yanatumiwaje kutegemeza fundisho la kisasa la upangaji-kimbele wa kibiolojia au kuamuliwa kimbele yatakayompata mtu?
Vipi Juu ya Ukosefu wa Uaminifu na Ugoni-Jinsia-Moja?
Kulingana na makala iliyotangazwa katika The Australian, utafiti fulani wa kijeni huthibitisha kwamba “yaelekea ukosefu wa uaminifu uko katika jeni zetu. . . . Yaonekana kwamba utu wetu wa kukosa uaminifu wa kingono uliamuliwa kimbele kuwa hivyo.” Fikiria tu jinsi mtazamo huu uwezavyo kuleta uharibifu katika ndoa na familia kwa kufanyiza fursa kwa yeyote asiyetaka kulaumika kwa mtindo-maisha wake wa ngono za ovyo-ovyo!
Kuhusu ugoni-jinsia-moja, gazeti Newsweek lilikuwa na kichwa kikuu “Ni wa Kuzaliwa Nao au wa Kusitawishwa?” Makala hiyo ilitaarifu: “Sayansi na tiba ya kiakili zang’ang’ana kufahamu utafiti mpya unaodokeza kwamba huenda ugoni-jinsia-moja ukawa jambo la tabia za urithi, si wa kukuzwa. . . . Katika jumuiya yenyewe ya wagoni-jinsia-moja, wengi hukubali dokezo kwamba ugoni-jinsia-moja huanza katika chembeuzi.”
Kisha makala hiyo yamnukuu Dakt. Richard Pillard, ambaye alisema: “Ikiwa mapendezi ya mtu kuelekea ngono yanaamuliwa na jeni, basi hilo lamaanisha ‘Hii si kasoro, wala si kosa lako.’” Akiimarisha tetezi hili la “kutokuwa na kosa,” Frederick Whitam, mtafiti wa ugoni-jinsia-moja, aonelea kwamba “kuna mwelekeo wa watu kutweta kwa kuhisi kitulizo, wanapoambiwa kwamba ugoni-jinsia-moja ni wa kiasili. Huondolea familia na wagoni-jinsia-moja hatia. Humaanisha pia kwamba jamii haihitaji kuwa na wasiwasi kuhusu mambo kama vile walimu walio wagoni-jinsia-moja.”
Nyakati fulani, ule uitwao eti uthibitisho kwamba mielekeo ya ugoni-jinsia-moja huamuliwa na jeni huonyeshwa na vyombo vya habari kuwa wa uhakika na wa mkataa badala ya kuwa jambo liwezekanalo na lisilo la mkataa.
Gazeti New Statesman & Society hukashifu ustadi wenye kuvutia katika kuripoti ugunduzi huo: “Msomaji aliyeduwaa huenda hakuona kwamba huo uthibitisho halisi wa hakika ulikuwa wa kijuu-juu—au, kwa kweli, kutowepo kabisa kwa msingi wa dai lililo wazi la kisayansi kwamba uovyoovyo wa kingono “umepangwa katika ubongo wa mtu wa kiume.’” Katika kitabu chao Cracking the Code, David Suzuki na Joseph Levine huongeza hangaiko lao kuhusu utafiti wa wakati huu wa jeni: “Ingawa yawezekana kutetea kwamba jeni huathiri mwenendo katika maana ya ujumla, ni jambo jingine kabisa kuonyesha kwamba jeni hususa—au jeni 2, au hata jeni 20—kwa hakika hudhibiti mambo hususa ya jinsi mnyama anavyoitikia mazingira yake. Kufikia hapa, ni jambo la haki kuuliza ikiwa kuna mtu yeyote ambaye amepata, katika maana halisi ya kimolekuli ya kutafuta na kubadili, nyuzi zozote za DNA ambazo huathiri mienendo hususa.”
Jeni za Uraibu wa Alkoholi na Uhalifu
Uchunguzi wa uraibu wa alkoholi umeshangaza watafiti wengi wa jeni kwa miaka mingi ambayo imepita. Wengine hudai kwamba uchunguzi umeonyesha kwamba kuwepo au kutowepo kwa jeni fulani ndiko husababisha uraibu wa alkoholi. Kwa kielelezo, jarida The New England Journal of Medicine liliripoti katika 1988 kwamba “katika mwongo uliopita, chunguzi tatu tofauti zimetokeza uthibitisho wenye mkataa kwamba uraibu wa alkoholi ni kitabia cha kurithiwa.”
Hata hivyo, wataalamu fulani katika uwanja wa uraibu sasa wanapinga maoni ya kwamba uraibu wa alkoholi unachochewa kwa sehemu kubwa na visababu vya kiasili. Ripoti moja katika The Boston Globe la Aprili 9, 1996, ilitaarifu: “Haielekei kwamba jeni ya uraibu wa alkoholi itapatikana katika wakati ujao ulio karibu, na baadhi ya watafiti hukubali kwamba kile ambacho huenda wakapata ni kukosa uthabiti kunakofanya watu fulani wanywe kupita kiasi bila kulewa—kitabia kiwezacho kuwafanya wapatwe na uraibu wa alkoholi.”
Gazeti The New York Times liliripoti kuhusu mkutano uliofanywa kwenye Chuo Kikuu cha Maryland uliokuwa na kichwa “Maana na Umuhimu wa Utafiti wa Tabia za Urithi na Mwenendo wa Uhalifu.” Wazo la kwamba kuna jeni yenye kuchochea uhalifu ni sahili sana. Watangazaji wengi wana hamu ya kuunga mkono mwelekeo huo. Mwandikaji wa kisayansi katika The New York Times Magazine alisema kwamba uovu waweza “kuwapo katika mitatio ya chembeuzi ambazo wazazi wetu hutupitishia wakati wa kutungwa mimba.” Makala moja katika The New York Times iliripoti kwamba mazungumzo yenye kuendelea juu ya jeni ya uhalifu hutokeza wazo la kwamba uhalifu una “chanzo kimoja—kasoro ya ubongo.”
Jerome Kagan, mwanasaikolojia wa Harvard, atabiri kwamba wakati utakuja ambapo majaribio ya kijeni yatatambulisha watoto walio na mwelekeo wa kuwa na mwenendo wenye jeuri. Watu fulani hudokeza kwamba huenda kukawa na tumaini la kudhibiti uhalifu kupitia urekebishaji wa kibiolojia badala ya kupitia urekebishaji wa kijamii.
Lugha iliyotumiwa katika ripoti za makisio haya kuhusu msingi wa kijeni kwa mwenendo, mara nyingi si wazi na haina uhakika. Kitabu Exploding the Gene Myth chaeleza juu ya uchunguzi uliofanywa na Lincoln Eaves, mtaalamu wa uvutano wa jeni kwa mwenendo, ambaye alisema kwamba alipata uthibitisho wa kisababishi cha kijeni kwa mshuko-moyo. Baada ya kuchunguza wanawake walioonwa kwamba huelekea kupatwa na mshuko-moyo, Eaves “alidokeza kwamba mtazamo na namna ya kushuka moyo [wa wanawake hao] huenda ulifanya matatizo aina nyingi yaelekee kutokea.” Ni nini hayo “matatizo aina nyingi”? Wanawake waliochunguzwa walikuwa “wamebakwa, kutendwa vibaya, au kufutwa kazi.” Kwa hiyo ni mshuko-moyo uliosababisha matukio haya yenye kufadhaisha? “Huko ni kufikiri kwa aina gani?” chaendelea kitabu hicho. “Wanawake hao walikuwa wamebakwa, kutendwa vibaya, au kufutwa kazi, nao walishuka moyo. Kadiri walivyopatwa na matukio yenye kufadhaisha, ndivyo mshuko-moyo ulivyokuwa mbaya zaidi. . . . Ingestahili kutafuta kiunganishi cha kijeni ikiwa yeye [Eaves] alipata kwamba mshuko-moyo haukuhusiana na ono lolote la maisha.”
Kichapo hicho-hicho chasema kwamba hadithi hizi “zafanana sana na ripoti za wakati huu kuhusu jeni [za kimwenendo], katika vyombo vya habari na vilevile katika majarida ya kisayansi. Yana mchanganyiko wa mambo ya hakika yenye kupendeza, makisio yasiyo na utegemezo, na kuongeza chumvi kusiko na msingi kwa umaana wa jeni katika maisha yetu. Jambo lenye kutokeza kuhusu mwingi wa uandikaji huu ni ukosefu wao wa udhahiri.” Chaendelea hivi: “Kuna tofauti kubwa kati ya kushirikisha jeni na hali zinazofuata kigezo cha urithi cha Mendel na kutumia ‘mielekeo’ ya kijeni ya kinadhariatete kuelezea hali zilizo tata kama vile kansa na msongo wa juu wa damu. Wanasayansi wanafikia mkataa mwingine haraka wanapodokeza kwamba utafiti wa kijeni waweza kusaidia kueleza mienendo ya kibinadamu.”
Hata hivyo, kulingana na yaliyo juu, maswali yatokezwayo mara nyingi bado yabaki: Kwa nini nyakati fulani sisi huona mabadiliko ya vigezo vya kimwenendo maishani mwetu? Na tuna udhibiti gani katika hali kama hizo? Twaweza kupataje na kudumisha udhibiti wa maisha yetu? Makala ifuatayo yaweza kusaidia katika kuandaa baadhi ya majibu ya maswali haya.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]
Tiba ya Jeni—Je, Matazamio Yametimizwa?
Namna gani juu ya tiba ya jeni—kudunga jeni zenye kurekebisha katika wagonjwa ili kuwatibu maradhi ya kijeni waliyozaliwa nayo? Wanasayansi walikuwa na matarajio mazuri miaka michache iliyopita. “Je, tiba ya jeni ni tekinolojia ambayo wakati wayo umefika?” lauliza gazeti The Economist la Desemba 16, 1995, likisema: “Kuamua kulingana na matabibu wayo, taarifa za umma, na kuripotiwa kwingi, huenda ukafikiri hivyo. Lakini kikundi cha wataalamu wenye kuheshimika wa Marekani hukataa. Wanasayansi 14 wajulikanao sana waliombwa na Harold Varmus, mkuu wa Taasisi za Kitaifa za Afya (NIH), wapitie habari hiyo ya tiba ya jeni. Baada ya miezi saba ya kutafakari walisema katika ripoti iliyotangazwa juma lililopita kwamba, ingawa tiba ya jeni ina mataraja mazuri, matimizo yayo hadi wakati huu ‘yametiwa chumvi.’” Majaribio yalifanywa yaliyohusisha wagonjwa 597 wenye kuugua ukosefu wa adenosine deaminase (ADA) au moja ya dazani za maradhi mengineyo yafikiriwayo kuwa yafaa kutibiwa kwa kuongezwa kwa jeni za kigeni. “Kulingana na kikundi hicho,” lasema The Economist, “hakuna mgonjwa hata mmoja ambaye amenufaika kwa wazi kutokana na kushiriki katika jaribio kama hilo.”
[Picha katika ukurasa wa 7]
Licha ya kile ambacho huenda wengine wakadai kuhusu kuamuliwa na jeni watakachofanya, watu wanaweza kuchagua jinsi wanavyotenda