Chembe za Urithi, DNA, na Wewe
HEBU jiangalie sana katika kioo kwa muda fulani. Angalia rangi ya macho yako, umbile la nywele zako, rangi ya uso wako, na umbo la mwili wako. Fikiria vipawa vyako. Kwa nini uko hivyo? Kwa nini una tabia na vipawa hivyo mahususi? Leo, fumbo hilo linafumbuliwa kupitia kwa elimu ya chembe za urithi—elimu ya urithi—na athari za mazingira.
‘Elimu ya chembe za urithi?’ wewe wauliza. ‘Somo hilo lasikika kuwa la kisayansi mno na gumu sana kueleweka!’ Hata hivyo, je, umeshawahi kumwambia mtu fulani kuwa ana macho ya kijani kibichi kama ya baba yake lakini nywele nyekundu na mabakabaka kama ya mama yake? Ikiwa ndivyo, tayari unajua jambo la msingi la elimu ya chembe za urithi—tabia za kiasili hupitishwa kutoka kwa mzazi hadi kwa mtoto. Kwa kuongezea, jambo hilo laweza kukusaidia sana kuelewa namna mwanadamu alivyopata kuwapo—kwa mageuzi au uumbaji. Kwanza, ebu tuone jinsi ambavyo kila mmoja wetu anavyobeba urithi wa vizazi vingi.
Mwili wako umefanyizwa na sehemu hai ndogo-ndogo zinazoitwa chembe—zipatazo angalau trilioni 100, kulingana na kadirio moja. Katika kiini cha kila chembe, kuna maelfu ya chembe za urithi. Hizo ni sehemu mbalimbali za urithi zinazodhibiti chembe na kwa njia hiyo zinaamua baadhi ya tabia zako. Huenda chembe nyingi za urithi zikaamua aina ya damu yako; nyingine, umbile la nywele zako, rangi ya macho yako, na kadhalika. Kwa hiyo kila chembe hubeba maagizo katika chembe za urithi, maagizo yote yanayohitajiwa ili kujenga, kurekebisha, na kuelekeza utendaji wa mwili wako. (Ona mchoro, ukurasa wa 5.) Je, yote haya yaweza kuwa yalitukia kwa aksidenti?
Jinsi Fumbo Hilo Lilivyofumbuliwa
Nadharia ya kwamba tabia hurithiwa kwa damu ilibuniwa na Aristotle katika karne ya nne K.W.K. na kwa ujumla ilikubaliwa kwa zaidi ya miaka elfu moja. Nadharia hiyo iliathiri watu wengi sana hivi kwamba katika lugha ya Kiswahili, watu husema juu ya udugu wa damu.
Katika karne ya 17, yai na shahawa ziligunduliwa, lakini fungu lake lilieleweka vibaya. Watu fulani walidhani kwamba viumbe wadogo wenye umbo kamili walikuwa ama katika yai ama katika shahawa. Ingawa hivyo, kufikia karne ya 18, watafiti walitambua kwa usahihi kwamba yai na shahawa huunganika ili kufanyiza kiinitete. Hata hivyo, ufafanuzi sahihi juu ya urithi ungetolewa baadaye.
Maelezo sahihi hayakutolewa hadi mwaka wa 1866 wakati mtawa Mwaustria anayeitwa Gregor Mendel alipochapisha nadharia sahihi ya kwanza juu ya urithi. Kutokana na majaribio aliyofanyia njegere, Mendel aligundua kile alichokiita “elementi za urithi za kipekee” zilizojificha ndani ya chembe za uzazi, naye alisisitiza kwamba ndizo zinazopitisha tabia. Hizi “elementi za urithi za kipekee” sasa huitwa chembe za urithi.
Mnamo 1910, chembe za urithi zilipatikana katika chembe zinazoitwa kromosomu. Kromosomu hasa ni protini na DNA (deoxyribonucleic acid). Kwa kuwa wanasayansi tayari walijua umuhimu wa protini katika utendaji mwingine wa chembe, walifikiri kwa miaka mingi kwamba protini za kromosomu hubeba habari za urithi. Kisha, mnamo 1944, watafiti wakatokeza uthibitisho wa kwanza wa kwamba chembe za urithi hufanyizwa kwa DNA wala si protini.
Mnamo 1953, mwanadamu alipiga hatua kubwa katika kufumbua fumbo la uhai wakati James Watson na Francis Crick walipogundua muundo wa kemikali wa DNA, molekuli zilizojipinda zinazofanana na nyuzi.